1,2. Qaaf. Hii ni harufi katika harufi za alifbete iliyo fungulia Sura hii kama ilivyo ada ya Qur'ani katika kufungulia Sura kadhaa wa kadhaa kwa harufi kama hii, ili kuwakabili makafiri kama wanaweza kuleta mfano wake, na pia kuwazindua watu wasikilize yanayo somwa. Ninaapa kwa Qur'ani yenye ubora, na utukufu, na hishima kwamba hakika Sisi tumekutuma wewe, ewe Muhammad, ili uwaonye watu kwa hii. Na watu wa Makka hawakuamini, bali walistaajabu kutokea Mtume miongoni mwa jinsi yao akiwaonya kuwa watafufuliwa. Makafiri wakasema: Jambo hili hatulijui, na la ajabu!

Rudi kwenye Sura

3. Ati baada ya kwisha kufa na tukawa udongo, tutafufuliwa tena? Huko kufufuliwa baada ya kufa ni marejeo yaliyo mbali, hayawi.

Rudi kwenye Sura

4. Sisi hakika tunajua vipi ardhi inavyo vimeza viwiliwili vyao baada ya kufa. Na Sisi tunacho Kitabu kinacho dhibiti na kuhifadhi kila kitu hata kidogo.

Rudi kwenye Sura

5. Wao hawayazingatii aliyo kuja nayo Mtume, bali walimkadhibisha mara tu bila ya kuzingatia na kufikiri. Basi wao wamo katika hali ya kubabaika, hawana utulivu.

Rudi kwenye Sura

6. Wameghafilika hata hawaitazami mbingu ilivyo nyanyuliwa juu yao bila ya nguzo? Vipi tumetengeneza ujenzi wake, na tukaipamba kwa nyota, na haina nyufa za kuitia kombo!
Mbingu ni kote kulio juu yetu, na ndani yake vimo vitu vya namna mbali mbali, vinaogelea katika njia zao, nyota na sayari.  Na hayo ni kwa nidhamu ya uangalizi mkubwa, na mshikamano ulio timia, na vilevile zinafuata kwa mpango wake kuwafikiana na kanuni za mvutano, basi hazitelezi.

Rudi kwenye Sura

7. Na ardhi tumeikunjua na tukaisimamisha milima iliyo kaa imara na kuthibiti kwenda chini. Na tukaijaalia kumea kila namna ya mimea mizuri ya kuwafurahisha watazamao.
Gamba lilio funika ardhi katika mwahali maalumu limetuna, ndio hiyo milima. Na pengine limedidimia ndio sakafu ya chini ya bahari. Na uzani wa vitu hivi vizito vinalingana wenyewe kwa wenyewe. Na ni katika uwezo wa Mwenyezi Mungu na hikima yake kupatikana kulingana huku kwa uzani, na ukawa umethibiti kwa kupenya madda za ardhi zilizo fanyika hilo gamba jembamba chini ya mat'abaka ya juu juu. Na hayo ni kutoka kuliko kuwa kuzito kwendea kuliko kwepesi.

Rudi kwenye Sura

8. Tumejaalia hayo aone na akumbuke kila mja mwenye kurejea kwa Mola wake Mlezi, akafikiri Ishara za uwezo wake.

Rudi kwenye Sura

9. Na kutoka mbinguni tukateremsha maji yenye kheri nyingi na baraka, na kwa hayo tukaotesha mabustani yenye miti, na mauwa, na matunda, na tukatoa kwa hayo nafaka za makulima ya kuvunwa.

Rudi kwenye Sura

10. Na mitende mirefu mirefu, yenye makole ya tende yaliyo pandana kwa wingi.

Rudi kwenye Sura

11. Tumeotesha hiyo ili iwe ni riziki kwa waja wetu, na tukaihuisha kwa maji ardhi iliyo kauka mimea yake. Hali kadhaalika ndivyo kufufuliwa wafu kutoka makaburini.

Rudi kwenye Sura

12,13,14. Kabla ya hawa,  kaumu nyingi ziliwakadhibisha Mitume- kaumu ya Nuhu, na kaumu nyengine iliyo kuwa  ikiitwa  "Watu wa Rassi", na wa Thamudi, na wa A'di, na wa Firauni, na kaumu Lut'i, na kaumu iliyo kuwa maarufu kwa jina la "Watu wa Machakani", na kaumu ya Tubbaa' - wote hao waliwakadhibisha Mitume wao. Kwa hivyo wakastahiki maangamizo niliyo waahidi.

Rudi kwenye Sura

15. Kwani kutaka kwetu kulipungua, au uwezo wetu ulitetereka, hata tukashindwa kwa kule kuumba kwa mara ya kwanza, tusiweze tena kuwarejeza? Hasha! Hatukushindwa, nao wanatambua hayo. Bali wao wana shaka tu na wanadanganyikiwa na huku kuumbwa kupya baada ya kufa.

Rudi kwenye Sura

16. Ninaapa: Bila ya shaka tumemuumba mtu, na Sisi tunajua hata anayo semezwa na nafsi yake. Na Sisi kwa kuzijua hali zake zote, ni karibu kuliko mshipa wake wa damu ulioko shingoni mwake. Na hicho ndicho kitu kilicho karibu mno naye.

Rudi kwenye Sura

17. Watakapo kutana Malaika wawili walinzi, mmoja anakaa kuliani, na mwingine anakaa upande wa kushoto, wakiviandika vitendo vyake.

Rudi kwenye Sura

18. Halimtoki neno ila yuko karibu naye Malaika  tayari kuandika neno lake.

Rudi kwenye Sura

19. Na yatapo kuja machungu ya  kukata roho, kwa haki isiyo na shaka ndani yake, hilo ni jambo la kweli ulilo kuwa ukilikimbia.

Rudi kwenye Sura

20. Na baragumu litapulizwa kwa mpulizo wa kuwafufua watu. Kupulizwa huko kutakuwa siku hiyo ya kuteremka adhabu waliyo ahidiwa.

Rudi kwenye Sura

21. Na kila nafsi njema na mbaya, itakuja na pamoja nayo wa kuichunga kuipeleka kwenye mkusanyo, na wenye kuwatolea ushahidi wa vitendo vyao

Rudi kwenye Sura

22. Wataambiwa, kumtisha huyo mwenye kukadhibisha: Hakika wewe huko duniani ulikuwa umeghafilika kabisa na haya unayo sononeka nayo hivi sasa. Basi Sisi tumekuondolea pazia lilio kuwa likikuzuia usiyaone mambo ya Akhera. Basi jicho lako hii leo linaona kwa nguvu.

Rudi kwenye Sura

23. Na Shetani wake aliye kuwa mwongozi wake duniani, atasema: Kafiri huyu alioko kwangu yuko tayari kuingia Jahannamu kwa kupotezwa nami.

Rudi kwenye Sura

24,25. Malaika wawili wataambiwa: Watieni katika Jahannamu kila aliye pita mipaka kwa ukafiri, na aliye pita mipaka kwa inadi, na akaacha kuifuata Haki, na akapita mipaka kuzuia kheri, mwenye kudhulumu akaipindukia Haki, mwenye kumtilia shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu na aliyo yateremsha.

Rudi kwenye Sura

26. Aliye mfanya mungu mwengine wa kumuabudu pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni huyo katika adhabu yenye mwisho wa ukali.

Rudi kwenye Sura

27. Shetani atasema kumrudi yule kafiri: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi siye niliye mfanya awe mwenye kua'si, lakini yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali na haki. Na mimi nilimsaidia tu kwa kumpotoa.

Rudi kwenye Sura

28. Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaambia makafiri na wenzi wao: Msigombane mbele yangu hapa pahala pa hisabu na malipo. Na Mimi nilikuleteeni mbele duniani onyo juu ya kukufuru kwenu kuukataa Ujumbe wangu niliyo utuma kwenu. Nanyi hamkuamini.

Rudi kwenye Sura

29. Hapana la kugeuza kauli ilioko kwangu na onyo langu kuwatia makafiri Motoni, wala Mimi si Mwenye kuwadhulumu waja. Kwani simuadhibu mja yeyote bila ya makosa.

Rudi kwenye Sura

30. Siku tutapo iambia Jahannamu kwa kuwatia kiwewe makafiri: Je! Umejaa? Nayo Jahannamu iseme kwa kuwaghadhibikia: Wapo wengine zaidi wa kuwaongeza katika hawa wenye kudhulumu?

Rudi kwenye Sura

31. Na Pepo iliyo pambwa italetwa karibu kwa ajili ya wenye kumcha Mola wao Mlezi, kwa kufuata amri zake na kuyaepuka makatazo yake, iletwe pahala pasipo kuwa mbali nao.

Rudi kwenye Sura

32. Haya ndiyo malipo ya kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu, aliye mwingi wa kuhifadhi sharia zake.

Rudi kwenye Sura

33. Mwenye kukhofu adhabu ya Mwenyezi Mungu ambaye rehema yake imeenea juu ya kila kitu, na Yeye haonekani, na akaja Akhera na moyo wa aliye kwisha rejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Rudi kwenye Sura

34. Itasemwa kwa hishima yao: Ingieni Peponi kwa amani. Hiyo siku mtakapo ingia Peponi ndiyo siku ya kubakia milele isiyo na mwisho.

Rudi kwenye Sura

35. Hao wachamngu watapata kila wakitakacho huko Peponi. Na Sisi tunazo neema za kuzidi kuliko yanayo mpitikia mtu kuyawaza.

Rudi kwenye Sura

36. Na wengi tumekwisha wateketeza kabla ya hawa wanao kadhibisha katika mataifa yaliyo kwisha pita. Wao walikuwa na nguvu na madaraka zaidi kuliko hawa. Wakaizunguka miji wakishughulika kuchungua na kutafuta. Je! Walipata pa kukimbilia wasiangamizwe?

Rudi kwenye Sura

37. Hakika kwa waliyo tendewa hao wa kaumu zilizo kwisha pita ni mawaidha kwa mwenye moyo wa kufahamu hakika ya mambo, au akasikiliza uwongofu naye akili zake anazo.

Rudi kwenye Sura

38. Ninaapa: Hakika tumeziumba mbingu na ardhi na viumbe viliomo baina yao katika siku sita. Na hatukupata kuchoka.
Rejea mambo yaliyo khusu maana ya neno "Siku" za uumbaji katika maelezo ya kitaalamu juu ya Aya za idadi 9 mpaka 12 katika Sura ya "Fuss'ilat". 41:9-12

Rudi kwenye Sura

39,40. Ikiwa haya yamebainika, basi, ewe Mtume, yastahamilie hayo wayasemayo hao wanao kanusha, ya uwongo na uzushi kukhusu Utume wako. Nawe mtakasishe, Msabbih,  Muumba wako na Mlezi wako na kila upungufu, ukimhimidi wakati wa alfajiri, na wakati wa alasiri, kwani ibada nyakati hizo ni jambo kuu. Na pia mtakasishe, Msabbih, katika saa za usiku, na baada ya Sala.

Rudi kwenye Sura

41,42. Na sikiliza khabari ninazo kwambia katika hadithi za Kiyama kwani shani yake ni kubwa. Siku atapo nadi Malaika wa kunadi kutoka pahala pa karibu na hao wanao itwa. Siku watapo sikia mpulizo wa pili wa Haki, nao ni wa kufufuliwa watu. Hiyo ndiyo siku ya kutoka kwenye makaburi.

Rudi kwenye Sura

43. Hakika Sisi, peke yetu, ndio tunao huisha viumbe vyote, na tunavifisha duniani. Na kwetu Sisi, peke yetu, ndio marejeo Akhera.

Rudi kwenye Sura

44. Siku itakapo wapasukilia ardhi, na watoke humo mbio mbio wakikimbilia mkutanoni...Hilo jambo kuu la kuwakusanya wote ni dogo na jepesi kwetu.

Rudi kwenye Sura

45. Sisi tunajua kuliko yeyote hayo wayasemayo ya uwongo juu yaliyo khusu Utume wako. Wala wewe hukutumwa uwalazimishe kwa unayo yataka. Ila wewe ni mwonyaji basi mkumbushe kwa Qur'ani Muumini mwenye kuiogopa adhabu yangu ili ukumbusho umfae..

Rudi kwenye Sura