mecca_1.jpgFIQHI ILIYOWEPESISHWA: Neno la Mwandishi

Farouk Abdalla Al Barwani

Neno la Mwandishi

Amesema Mwandishi - Mwenyezi Mungu Amrehem: Himidi zote ni zake yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alieumba kila kitu kutoka giza la kutokuwepo chochote kwa nuru ya kuwezesha kuwepo na akajaalia hayo ni dalili ya Upweke wake mpaka siku ya Mi'aadi (Siku ya Qiyama) kwa wale wenye uwezo wa kuona na kutambua, na akashari'isha Shari'a alioichaguwa Yeye mwenyewe s.w.t., na akaiteremsha katika Kitabu chake, Qur'ani Tukufu na akamleta Bwana wa viumbe, Sayydina Muhammad s.a.w. kutufafanulia yale ambayo hayako bayani kwetu sisi, na akasema: "Hii njia ya uwongofu". Rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu zimshukie Mtume wetu Mpenzi, Sayydina Muhammad s.a.w. na Ahli zake r.a. na jamii ya wafuasi wake - Amin.

Ama baada ya haya, hakika nafsi takatifu hazijaacha jitihada katika kutafuta elimu ya Shari'a, na miongoni mwa hayo ni kujua matawi ya elimu ya Fiqhi, kwani kwa hivyo ndio huweza kujikinga kutokana na wasiwasi wa mashe'tani. Na hivyo yatasihi mambo ya maingiliano na mambo ya ibada yenye kuridhiwa na Mola wetu Mlezi s.w.t. Na inakutosheleza kuwa ni sharaf kwako kuwa nayo ilimu ya Fiqhi, hayo ni maneno ya Bwana wa viumbe - waliotangulia na wanaofuatia Mtume wetu Mpenzi s.a.w. pale aliposema: "Mwenyezi Mungu Mtukufu anae mtakia kheri humfundisha mambo ya dini, (yaani Fiqhi)". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Vilevile amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "Hajapatapo kuabudiwa Mweneyezi Mungu Mtukufu kwa kitu bora kuliko kwa kujifunza mambo ya dini, (yaani Fiqhi)". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy). Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Mukipita kwenye mabustani ya Peponi kaeni hapo mstarehe na mfaidike, wakauliza Masahaba r.a.: "Nini hizo bustani za Peponi, Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu"? Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "Vikao vya dhikri". (Imehadithiwa na Ahmad na Al Tirmidhy na Al Baihaqy). Amesema 'A'taa: vikao vya dhikri ni vikao vyenye kufundishwa humo halali na haram, namna ya kuuza na kununua, vipi kusali, vipi kufunga na hukmu zake, hukmu na shuruti za Hija, hukmu za ndoa na 'talaqa, na kadhaalika, yaani Ilimu ya Fiqhi. Na amesema Sufiyan bin 'Aiyana: "Hajapewapo mtu baada ya utume kitu bora kuliko elimu na Fiqhi". Na akasema Abu Huraira r.a. na Abu Dhari r.a.: "Mlango wa elimu tunaousoma ni bora zaidi kwetu kuliko raka'a elfu za sunna".

Aya za Qur'ani Tukufu, na Hadithi za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. juu ya suala hili, yaani kutafuta elimu ya Fiqhi ziko nyingi.

Kwa vile kuwa Fiqhi iko kwenye daraja ya utukufu kiyasi hiki katika Shari'a, inakuwa kushughulikia suala hili kuna daraja kubwa na sharaf kuu kwa kuutumia wakati katika haya, bali kuutumia umri katika suala hili; kwani njia inayoendea juhudi na matunda ya haya ni njia ya Peponi.

Na kujishughulisha katika suala hili ni kinga na uwokozi wa kutokana na adhabu ya Moto. Lakini haya husihi kwa yule mwenye kutenda hivyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu - Lillahi Ta'aala - si kwa ajili ya jina, pato au fakhari ya kilimwengu.

Amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Mwenye kujifunza ilimu ambayo inatakiwa iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yeye asijifunze kwa ajili ya hivyo; bali ikawa anajifunza kwa ajili ya kujipatia manufaa ya kilimwengu, basi hatainusa harufu ya Pepo Siku ya Qiyamah". (Imehadithiwa na Abu Daud).

Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Mwenye kutafuta ilimu ili apate kujadiliana na kushindaniana na masafihi, na ili apate kuongeza kwa elimu yake hio idadi ya wanazuoni, au ili apate nyuso za watu zimuelekee yeye (kwa kusemwa kuwa ni mwanazuoni); basi na ajiandalie kibao chake Motoni". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).

Jua kwamba wenye kutafuta elimu wanakhitalifiana kwa vile yanavyo khitalifiana makusudio yao, na yale yenye kuwashughulisha yanakhitalifiana kwa kukhitalifiana vyeo vyao. Huyu huzamia bahari na mfano wake akitaka apate mtiririko mkubwa wa mali yaliomo humo baharini, na huyu anaqinai kwa kichache chake. Kisha hivi kuqinai kunakuwa kwa aina mbili, aina ya kwanza ni yule mwenye watoto na nguvu za juhudi zimemwisha; na wa aina ya pili ni yule anamuelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa dhati na juhudi. Si wa awali anaweza kujidumisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wa pili amejishughulisha na yale alionayo; usiku na mchana pamoja na nafsi yake kuwemo katika mashaka. Kutokana na haya, nikamtakia raha kila mmoja wao kwa kubakia katika hali aliyo na aache kila mmoja wao kupigia mbio anayoyahitajia. Ninatarajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu wepesi wa kufahamika haya, kwani Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwenye kutarajiwa na kila mwenye kutaraji, na ni mwenye kuwapa nguvu na utukufu walio dhaifu na walio wanyonge.

Nimekipanga kitabu hiki nikakiita (Al Fiqhu al Muyassar) (Fiqhi Iliyowepesishwa) Nina muomba Mwenyezi Mungu Mtukufu anisamehe mimi na vipenzi vyangu na aniepushe na makri na ghadhabu Zake na aniepushe na adhabu ya Moto, hakika Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni muweza wa kila kitu na kila alitakalo; na ni Mwingi wa kuitikia maombi ya viumbe vyake.

 

__________________________________________________

Haki za Uchapishaji zimehifadhiwa na Mtungaji

Farouk Abdalla Al-Barwani, P.O. Box 828, Ruwi, P.C.112 Sultanate of Oman

e-mail: umojabaraka@yahoo.co.uk