mecca_1.jpgFIQHI ILIYOWEPESISHWA: SALA

Farouk Abdalla Al-Barwani

SALA

Nini Sala?

Kilugha, kuomba du'a ya kheri, kama ilivyo kwenye Qauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: " , na uwaombee rehema. ". (Tawba : 103).

Kisharia, maneno na vitendo vyenye kuanzwa kwa "takbiir na kumalizwa kwa "salaam" .

Kuwajibika Sala Tano Kwa Siku - Mchana na Usiku

Kuthibiti kuwajibika Sala kumekuja kwa Qauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, Hadithi za Mtume s.a.w. na kukubaliana Wanazuoni wote. Mwenye kukanya kuwajibika Sala au mwenye kufanya istihzai na maskhara juu ya Sala, huyo huwa ni kafiri na murtadi,

yaani alietoka kwenye Uislam. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na shikeni Sala ". (Al Baqara : 110).

Na Hadithi za Mtume s.a.w. juu ya Sala ni nyingi, miongoni mwa hizo ni hizi:

"Amefaridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya umati wangu Lailati Israai, Sala khamsini; sikuwacha kumrejelea (Mwenyezi Mungu Mtukufu) na kumuomba kupunguziwa mpaka Akazijaalia tano kwa kila siku - mchana na usiku ". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Na qauli ya Mtume s.a.w. alipomtuma Mu'adh r.a. Yaman:

"Waambie kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amefaridhisha juu yao Sala tano kila siku - mchana na usiku".

Na kuthibiti kubainishwa Sala tano kila siku - usiku na mchana - ni kwa Qauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Basi Subhanallah! Mtakaseni Mwenyezi Mungu jioni na asubuhi, Na sifa zote njema ni Zake katika mbingu na ardhi, na alasiri na adhuhuri". (Arrum 17-18).

Amesema Ibnu 'Abbas kwamba inakusudiwa Sala ya Magharibi na Sala ya 'Isha, na inakusudiwa Sala ya Alfajiri; na inakusudiwa Sala ya Alasiri, nainakusudiwa Sala ya Adhuhuri. Hizi ndizo Sala tano za fardhi na ndizo zenye kulazim kusaliwa kila siku, mchana na usiku.

Nyakati za Sala Tano

Kujua nyakati za Sala ni muhim na dharura mno, kwani kwa kujua wakati wa Sala ndio utajua kuingia na kutoka kwa Sala hio. Kuthibiti kwa nyakati za Sala tano kumekuja kwa Qauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na Hadithi za Mtume s.a.w. na kwa kukubaliana Wanazuoni. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

". Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu". (Annisai : 103).

Na Mtume s.a.w. amesema:

"Amenisalisha Jibril a.s., yaani alikuwa Imam wangu, kwenye Msikiti wa Makka mara mbili. Siku ya mwanzo alisali nami Sala ya adhuhuri wakati jua lilipotenguka na ikawa kivuli urefu (kuinuka kwa juu) wa kiatu cha ndara, na akasali na mimi Sala ya laasiri wakati kivuli kilikuwa urefu wa kitu chenyewe, na akasali na mimi Sala ya magharibi wakati wa kufuturu mwenye kufunga, na akasali na mimi Sala ya 'isha wakati ulipopotea wekundu wa mwangaza wa jua; na akasali na mimi Sala ya alfajiri wakati ulioharimishwa kula na kunywa kwa mwenye kufunga. Ilipofika siku ya pili, alisali na mimi (Jibril a.s.) Sala ya adhuhuri wakati kivuli kilikuwa urefu wa kitu chenyewe, na akasali na mimi Sala ya laasiri wakati kivuli kilikuwa mara mbili ya urefu wa kitu chenyewe, na akasali na mimi Sala ya magharibi wakati wa kufuturu mwenye kufunga; na akasali na mimi Sala ya 'isha (wakati) baada ya sehemu moja ya sehemu tatu za usiku, na akasali na mimi Sala ya alfajiri wakati kumeingia umanjano wa kukaribia kuchomoza jua. Baada ya hapa akanielekea na akasema: "Ewe Muhammad (s.a.w.), huu ndio wakati (wa Sala) wa Mitume ya kabla yako, na wakati wa kila Sala ni baina ya nyakati mbili za kila Sala". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy na Ibnu Khuzaima na Al Haakim wameipa darja ya Hadithi sahihi).

Kasema Al Tirmidhy r.a. kuwa amesema Al Bukhary r.a. ya kwamba hivi ndivyo ilivyo sahihi mno kukhusu nyakati za Sala tano. Kivuli chenye kukusudiwa hapa ni kile cha baada ya kutenguka jua kuelekea uchejua.

Kutokana na Hadithi hii ya Mtume s.a.w. nyakati za Sala ni kama hivi:

1. Sala ya Adhuhuri, inaingia kwa kivuli cha kutenguka jua, nacho ni kuwa na urefu (kuinuka kwa juu) wa mfano wa kiatu cha ndara, yaani ni kivuli kidogo kabisa. Huendelea wakati wa Sala ya adhuhuri mpaka kivuli kuwa na urefu sawa na kitu chenyewe, ziyada na kivuli cha kutenguka jua; hapo huwa ndio mwisho wa wakati wa Sala ya adhuhuri na huingia awali ya wakati wa Sala ya laasiri.

2. Sala ya Laasiri, inaingia kwa kivuli kuwa na urefu wa kitu chenyewe na kuzidi kidogo, yaani kwa kutoka Sala ya adhuhuri. Huendelea wakati wa Sala ya laasiri mpaka kivuli kuwa na urefu mara mbili wa kitu chenyewe. Huu unaitwa wakati wa khiari; haipendezi kuiakhirisha Sala mpaka kufika wakati huu. Huendelea wakati wa Sala ya laasiri mpaka kuingia Sala ya magharibi.

3. Sala ya Magharibi, inaingia kwa kutuwa juwa na kuingia wakati wa kufuturu. Wakati wa Sala ya magharibi huendelea kwa muda wa kiasi cha mtu kutia udhu, kuadhiniwa Sala, kuqimiwa na kusali raka'a saba - mbili za kabla ya magharibi, tatu za fardhi ya magharibi na mbili za baada ya magharibi. Kwa qauli ya Mtume s.a.w. wakati wa Sala ya magharibi hautoki mpaka upotee mwangaza mwekundu wa kutuwa jua.

4. Sala ya 'Ishaa, inaingia kwa kutoka Sala ya magharibi, huendelea wakati wa Sala ya 'ishaa mpaka kupita sehemu moja ya sehemu tatu za usiku, kama ilivyo kwenye Hadithi hii. Vile vile kuna Hadithi ya Mtume s.a.w. yenye maana kwamba Sala ya 'ishaa inamalizika kwa kupita nusu ya usiku: "" "Wakati wa Sala ya 'ishaa unaendelea mpaka nusu ya usiku".

Kasema Imam Al Nawawy r.a. hii ni Hadithi sahihi na katika upokezi mwengine amesema Mtume s.a.w.:

" " "Lau kama haitakuwa kuwafanyia uzito Umma wangu, ningaliiakhirisha Sala ya 'ishaa mpaka nusu ya usiku".

Huendelea kujuzu kusali Sala ya 'ishaa mpaka kutokeza alfajiri ya pili, (yaani kuingia wakati wa Sala ya alfajiri), hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:

"Tambua! Hakuna katika kulala kupindukia kiasi, lakini kupindukia kiasi ni kwa yule ambae hakuisali Sala ilipoingia mpaka ukafika wakati wa Sala nyengine". (Imehadithiwa na Muslim).

Hadithi hii ni dalili ya kwamba wakati wa kila Sala huendelea mpaka kuingia wakati wa Sala nyengine, isipokuwa Sala ya alfajiri; kwani Sala ya alfajiri wakati wake si wenye kuendelea mpaka kuingia wakati wa Sala ya adhuhuri, hivi ndivyo wanavyo kubaliana Wanazuoni wote; bali wakati wa Sala ya alfajiri humalizika kwa kuchomoza jua. Na hivi ndivyo ilivyo katika hii Hadithi ya Mtume s.a.w. ya kusalishwa na Sayyidna Jibril a.s.

Ama katika miji ambayo haupotei mwangaza wa kupambazuka au kutua jua, basi wao hukisia kwa nchi iliokaribu nao.

Kuna Hadithi ya Mtume s.a.w. iliopokewa na Abu Birza Aslamy r.a. kwamba Mtume s.a.w. alikuwa hakipendezewa kulala kabla ya Sala ya 'ishaa na hakipendezewa na mazungumzo baada ya Sala ya 'ishaa, isipokuwa ikiwa ni mazungumzo ya kheri:

" "Alikuwa (s.a.w.) akichukia kulala kabla ya kusali Sala ya 'ishaa na akichukia mazungumzo baada ya Sala ya 'ishaa". (Imehadithiwa na Muslim).

5. Sala Ya Asubuhi (Alfajiri), inaingia kwa kuchomoza alfajiri ya kweli, nayo ni ile ambayo mwangaza wake huenea kila upembe. Na wakati wa khiari huendelea mpaka kuanza kuchomoza umanjano wa kutoka jua. Huu wakati wa khiari huendelea na kufuatiwa na wakati wa kujuzu ambao huendelea mpaka kuchomoza jua, kama alivyobainisha Mtume s.a.w.:

"Mwenye kuipata katika Sala ya asubuhi raka'a moja kabla ya kuchomoza jua, basi ameipata Sala ya asubuhi". (Imehadithiwa na Muslim).

Huu wakati wa khiari una hukmu mbili, moja ni khiari bila ya karaha; nao ni ule wakati toka kuingia alfajiri ya kweli mpaka kuanza wekundu wa kuchomoza jua. Ukiingia wekundu wa kuchomoza jua humalizika wakati wa khiari bila karaha na huingia wakati wa karaha kusali, huu huendelea mpaka kuchomoza jua. Haijuzu kuakhiarisha Sala mpaka kuingia wakati wa karaha isipokuwa kwa udhuru wa kisharia.

Shuruti za Kuwajibikiwa Kusali

Shuruti za kuwajibikiwa mtu kusali ni kuwa, Muislam, kesha baalegh, mwenye akili timam, na awe hana janaba, wala hayumo kwenye siku za hedhi au damu ya uzazi. Haimuwajibikii Sala kafiri wa tangu awali (sio murtadi), kuwajibika kwa hapa duniani, kwani Sala haisihi kwa kafiri, Hukmu hii ndiyo ilivyo juu ya kafiri wa asili kukhusu mambo yote ya Kiislam. Ama murtadi, yaani akitoka kwenye Uislam, inamuwajibikia Sala, hivi ni kwa vile alipokuwa Muislam ikimuwajibikia Sala, kwa hivyo, kwa kutoka kwenye Uislam hakuondoki kuwajibikiwa kwake na hukmu zote za Kiislam, Sala na nyenginezo. Mtumzima, yaani baalegh, si mtoto mdogo; mtoto mdogo, yaani kabla ya kubalegh haimlazim juu yake Sala. Mgonjwa wa akili - kwa hali yoyote ile - yeye haimlazim juu yake Sala. Hivi ni kwa Hadithi ya Mtume s.a.w. kuwa aliomo usingizini, mtoto mdogo, na mtu asiekuwa na akili; hawa hawahisabiwi.

"Imeondoshwa kalamu (kuhisabika Kisharia) kwa watu watatu: alielala mpaka aamke, na mtoto mdogo mpaka abalegh, na mgonjwa wa akili mpaka apate akili". (Imehadithiwa na Abu Daud).

Inampasa mzee/mlezi wa mtoto akiwa kesha kuwa na fahamu amfundishe hukmu za 'tahara, na amuamrishe kusali akifika umri wa miaka saba; akifika umri wa miaka kumi akiwacha kusali, apigwe (kwa kiasi); hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Waamrisheni wenenu kusali wakifika umri wa miaka saba, na wapigeni kwa kuwacha kusali wakifika umri wa miaka kumi, na walazeni mbali mbali (khasa baina ya watoto wanaume na watoto wanawake)".

Shuruti za Kusihi Sala

Shuruti za kusihi Sala ni tano:

Kwanza, kuwa na 'tahara kutokana na hadathi kubwa, kama vile janaba, damu ya hedhi au damu ya uzazi, na kuwa na 'tahara kutokana na hadathi ndogo; yaani uwe una udhu. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Na kwa qauli ya Mtume s.a.w.: na hii Hadithi ya Mtume s.a.w. zimetangulia kutajwa kwenye Mlango wa Udhu).

Pili, kutokuwa na najsi (uchafu) kwenye mwili, nguo na mahala pakusalia. Ama kutokuwa na najsi mwilini ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na yaliyo machafu yahame"! (Al Muddathir : 5).

Yaani uchafu (najsi) jiepushe nayo, na kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Ukipatwa na damu ya hedhi basi usisali, na ikiondoka jikoshe damu na usali". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Kukhusu hukmu ya damu ya hedhi na damu ya uzazi tumetangulia kuzitaja katika mlango wa najsi. Kukhusu kujiepusha na najsi kwenye nguo kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: , yaani na nguo zako zisafishe, zisiwe na uchafu. Na kwa Hadithi ya Mtume s.a.w. alipofundisha kukhusu nguo ikipatwa na damu ya hedhi: yaani "kisha ikoshe kwa maji". Ama kukhusu kutokuwepo uchafu (najsi) mahali pakusalia ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. pale Bedui alipokojoa msikitini akaamrisha s.a.w. kumiminiwa maji hapo pahala alipokojoa huyo Bedui.

Ikiwa itatokea mtu kusali na najsi na hali kuwa hajui, yaani hakuiona kabla ya kusali, sawa sawa ikiwa najsi hio imemuingia mwilini mwake au nguoni au mahala pakusalia, akaiona baada ya kusali; basi itamlazim ailipe Sala hio, kwani 'tahara ni sharti ya kusihi Sala. Wanazuoni wengine wamesema kuwa hailazim kuilipa Sala hio, hivi ndivyo wanavyofuata Ibnu Al Mundhir r.a. na vile vile Imam Al Nawawi r.a. katika "Sherhe Al Muhadhab". Ikiwa atajuwa kuwa, kwa mfano nguo yake ina najsi, kisha akasahau na akasali na nguo hio yenye najsi; itamlazim ailipe Sala hio, kwa vile kuwacha kuikosha najsi wakati ule ule alipojua kua nguo yake ina najsi.

Tatu, kusitiri mwili wake kwa nguo ilio 'taahir, hata kama atasali mbali na watu au kizani, hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada,.....".(Al 'Araaf:31).

Maana ya Aya hii ni kusitiri mwili katika kila Sala. Na Mtume s.a.w. ametwambia:

"Hakubali Mwenyezi Mnngu Mtukufu Sala ya mtumzima mpaka awe amejisitiri mwili wake". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).

Kulazimika kujistiri wakati wa kusali, huwa kwa mwenye kuweza kufanya hivyo; akiwa hawezi kujistiri kwa sababu yoyote ile yenye kukubalika na Sharia, basi atasali hivyo hivyo bila ya kujistiri na hatalazimika kulipa hio Sala. Sharti ya kutimia huku kujistiri ni kuvaa nguo yenye kustiri isionekane rangi ya mwili, haifai nguo nyepesi. Ikiwa hakupata nguo, basi hata kwa kujifunika majani au udongo itajuzu. Kujistiri vile vile iwe kwa nguo yenye kustiri tangu juu na pembezoni mwa mwili. Ikiwa nguo aliojistiria akiruku'i au akisujudi sehemu yake ya siri itabainika, basi haitafaa; kwahivyo itabidi avae nguo kama vile seruni/kikoi au suruali, au aitie kitu kama vile kifungo au aipige fundo, muhim ipatikane kuendelea hivi kustirika hata katika wakati wa kurukui na kusujudi. Imepokewa kutoka kwa Salamata bin Al Akwa'iy r.a. kwamba alimuuliza Mtume s.a.w. kuwa anaweza kusali na amevaa kanzu? Mtume s.a.w. akamjibu kwa kumwambia:

"Na'am, ifunge sehemu ya chini japo kwa mwiba". (Imehadithiwa na Imam Al Bukhary).

Ikiwa hakupata isipokuwa nguo yenye uchafu (najsi), atasali kwa nguo hio hio na itamlazim alipe Sala atakayoisali kwa nguo yenye uchafu (najis). Na kwa qauli nyengine ya wanazuoni ni kwamba atasali bila ya nguo na haitamlazimu kuilipa hio Sala atakayoisali bila ya nguo. Ikitokea akafungwa mahala pachafu (penye najsi) na asipate nguo ya kutosha kumstiri sehemu inayopasa kustiriwa kwa ajili ya Sala na mahala 'taahir pakusali, basi atasali hivyo hivyo, na bila ya nguo na haitamlazim kuilipa hio Sala alioisali katika hali hio. Ni karaha kwa mwanamke kujifunika uso wakati anaposali ila ikiwa anasali msikitini na wamo watu wa mbali - si mahaarim zake - na ambao hawatazuilika kumtizama na akachelea fitna.

Katika hali hio itamlazimu avae kitu cha kumfunika uso na itakuwa haramu kwake kuwacha uso wake wazi..

Nne, kujua kuingia wakati wa Sala; kwani haisihi Sala bila ya kuingia wakati wake, akiwa hakujua; itabidi ajitahidi kujua kwani hivyo ndivyo inavyoamrishwa. Kujitahidi huwa kwa uradi wake wa kawaida ambao huusoma na huumaliza kwa muda maalumu. Au darsa maalum anayosoma au anayosikiliza, au kwa kusikia sauti ya jogoo aliemzoea kuwa akiwika wakati maalum ndio kuingia wakati wa Sala maalum, kama vile akiwika alfajiri ndio kuingia wakati wa Sala ya alfajiri. Au kwa kumsikia muadhini, ikiwa ni siku ambayo hakuna mawingu, ikiwa kuna mawingu na hakuna njia yenye kuaminika kujuulisha kuingia wakati wa Sala (kama vile saa), basi hatamfuata muadhini, kwani itakuwa muadhini ametumia jitihada kujuwa kuingia wakati wa Sala, kwahivyo haitafaa mujitahidi (asiekuwa na hakika) kumfuata mujitahidi (asiekuwa na hakika). Ikiwa baada ya kujitahidi kwa kila njia ili ajue kuingia wakati wa Sala, akaona kuwa umeingia wakati wa Sala atasali, ikiwa baadae itambainikia kuwa amesali katika wakati khaasa wa hio Sala, au amesali baada ya kutoka wakati wa hio Sala; itakuwa Sala yake imesihi. Lakini ikimbainikia kuwa ameisali hio Sala kabla ya kuingia wakati wake, itamlazim aisali tena Sala hio, kwani ameisali kabla ya kuingia wakati wake, na shuruti ya kusihi Sala ni kuingia wakati wake. Kwa mwenye uwezo wa kujua kuingia wakati wa Sala, haijuzu kwake yeye kufanya jitihada iwapo hanauwezo, akipata mtu mwenye kuaminika, akamwambia kuingia wakati wa Sala, atamfuata qauli yake. Ikiwa mwenye elimu ya falaki - elimu ya falaki ni kujua hisabu za mwendo wa jua, mwezi na nyota - atajuwa kuingia wakati wa Sala kwa hisabu ya falaki, basi atafuatwa. Watu wa elimu ya falaki wenye kukubalika sio wale wenye kupiga ramli, wenye kupiga ramli hawakubaliki katika Sharia kwani ni haraam kitendo cha kupinga ramli. Amesema Mtume s.a.w:

"Mwenye kumwendea mpiga ramli haikubaliwi Sala yake muda wa siku arubaini".

Na katika alivyopokea Imam Muslim r.a.: "Mwenye kumwendea mpiga ramli akamuuliza kitu kisha akakisadiki".

Tano, kuelekea qibla kwa mwenye kuweza; ikiwa hawezi kuelekea qibla kwa udhuru wowote wenye kukubalika Kisharia atasali bila ya kuelekea qibla. Kuelekea qibla katika Sala ya sunna ikiwa yumo safarini, safari ya halali, basi kuelekea qibla si lazima. Huku kuelekea qibla ni kama ilivyokuja kwenye Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

". Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; ". (Al Baqara : 144).

Kuelekea qibla hakulazimiki isipokuwa katika Sala, kwa hivyo hivi kutakiwa kuelekea qibla ni kwa wakati wa kuingia kwenye Sala; imebainishwa kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Unapotaka kusali, tia vyema udhu; kisha elekea qibla". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Kulazimika kukielekea qibla chenyewe khaasa ni kwa waliopo karibu na hicho qibla, walioko mbali nacho wao ni kuelekea huo upande wa qibla.

Mwenye kusali Sala ya fardhi, anatakiwa atulie mahala pamoja, asielekee huku na huku; isipokuwa akiwa ndani ya chombo kama vile meli na vya mfano wake, au katika gari au ndege. Kkatika hali hii haimlazimikii kuelekea qibla kutokana na uzito wa kuweza kufanya hivyo; na kutowezekana kuteremka kutoka chomboni kwa kila Sala.

Venye kujuilisha upande wa qibla ni ama kwa maelezo - maneno - au kwa ishara/alama. Ikiwa mtu hakupata mtu au kitu cha kumjuilisha upande wa qibla, ikiwa ni mwenye uwezo wa kujitahidi yeye mwenyewe ili ajuwe upande wa qibla atafanya hivyo na atachukua vile anavyoona (anavyo dhani) kuwa ndio upande wa qibla na kusali kwa kuelekea huko anakoona ndiko qibla.

Kujuzu Kutoelekea Qibla

Inajuzu kutoelekea qibla katika hali mbili:

Kwanza, wakati wa khofu kubwa na kuwemo vitani; katika hali hii watu husali wakiwa wako kwenye kipando au wanakwenda kwa miguu, husali wakielekea qibla au bila ya kuelekea qibla; yote hutegemea hali ya vita ilivyo. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Ikiwa mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. .........". (Al Baqara : 239).

Ruhusa hii imetolewa kwa Sala ya fardhi pia, sio ya sunna tu; kwa sababu huweza kutokea hali ambazo zitafanya mtu asiweze kuelekea qibla, kama wakati wa vita. Katika hali kama hizo hailazim kuelekea qibla hata katika kuhirimia (kufunga) Sala, bali atahirimia na huku anakwenda, ama kawa miguu au kwenye kipando na bila ya kuelekea qibla; wala haitakuwa juu yake kulipa Sala atakazozisali katika hali hii. Muhim ni kwamba haitakiwi kuakhirisha kusali, ni muhim kusali katika wakati wake; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

". Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu". ( Annisaai : 103 ).

Inatakiwa kufuata wakati wa Sala hata katika hali kama hii ya vitam. Vilevile inapasa kujizuia kupiga makelele, kwani hapana haja ya kufanya hivyo. Sala katika hali kama hii ambayo khasa imejuzishwa katika hali ya vita baina ya Waumini na makafiri, pia inajuzu katika vita vya kupigana na madhaalim.Au wakata njia (maharamia) na katika hali ya kujilinda mtu nafsi yake dhidi ya maadui au kulinda ahli zake, au mali yake, au katika hali ya kukimbia maafa yoyote yale, kama vile moto, mafuriko na kadhaalika.

Pili, kwenye Sala ya sunna katika hali ya safarini, ikiwa kwenye kipando au kwenda kwa miguu. Kukhusu kujuzu kwa mwenye kuwa juu ya kipando ni kwa qauli ya Ibni 'Umar r.a.:

"Alikuwa Mtume s.a.w. akiwa safarini anasali juu ya kipando chake upande kinakoelekea". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Na kwa alivyohadithia Imam Bukhary r.a. kuwa: "Akisali (Mtume wetu Mmpenzi s.a.w.) juu ya mgongo wa kipando chake kokote kinakoelekea". Hadithi mbili hizo hapo juu zinakhusu Sala ya sunna, ama anapotaka s.a.w. kusali Sala ya fardhi huteremka kutoka kwenye kipando chake; hivi ni kwa Hadithi alioipokea Jaabir r.a.:

"Alikuwa Mtume s.a.w. akisali juu ya kipando chake kule kinakoelekea, akitaka kusali Sala ya fardhi huteremka kutoka kwenye kipando chake akasali kwa kuelekea qibla".

Ingalikuwa mtu akiwa safarini anakalifishwa kuelekea qibla wakati anaposali, kwa kukalifishwa huko kungalipelekea mtu kuwacha nyiradi zake na kuwacha kusali Sala za sunna au kuwacha kupigia mbio maisha.

Ama kuruhusiwa kusali bila ya kuelekea qibla kwa msafiri anaekwenda kwa miguu, kumekuja kwa kulinganishwa na mwenye kupanda. Haya yote tuliojaaliwa kuyataja ni kwa yule ambae hawezi kuelekea qibla kwa sababu zenye kukubalika Kisharia, ikiwa ataweza kuelekea qibla itamlazim aelekee upande wa qibla; hivi ikiwa yeye ndie mwenye amri ya huo msafara au kwa makubaliano ya wasafiri wenyewe au mnyama wake si mkaidi. Haya yametolewa hoja ya kwamba Mtume s.a.w. :

"Ilikuwa (Mtume s.a.w.) akiwa safarini na akataka kusali Sala za sunna, huelekea qibla kwa (juu ya) ngamia wake na akakabbir na akasali upanade anaoelekea mnyama wake aliopanda". (Imehadithiwa na Abu Daud).

Ilivyo ni kwamba kule anakoelekea mtu aliomo safarini, basi huko ndio qibla chake, na ikiwa atageuka akaacha kuelekea kule anakokwenda basi itaba'tilika Sala yake. Na anaposali katika hali hii nae yuko juu ya kipando, basi ataruku'i kwa kuinama kidogo na atasujudi kwa kuinama zaidi kidogo kuliko aliporuku'i ili ipambanuke baina ya kuruku'i na kusujudi.

Ama kwa yule anaekwenda kwa miguu, yeye ataruku'i kama kawaida na atasujudi juu ya ardhi kama kawaida; ama tahiyatu (shahada), ikiwa ni ya kwanza au ya pili; ataisoma huku anakwenda. Msafiri katika chombo cha baharini, kama vile jahazi na cha mfano wake; yeye haimjuzii kusali hata Sala za sunna bila ya kuelekea qibla, kwani huwezekana kwake yeye kuelekea qibla nae yumo ndani ya hicho chombo. Ikiwa haimkiniki, atasali kama inavyoyumkinika.

Muhimu asiwache wakati wa Sala ukampita bila ya kusali.

Nguzo za Sala

Nguzo za Sala ni kumi na saba:

Kwanza, nia; nayo ni kukusudia kitendo pamoja na kukifanya, mahala pake moyoni. Kuitamka sio lazima, lakini wakati unapotia nia uwe moyo wako uko katika hilo unalolinuwilia kulifanya na kufuatiliwa na "takbiiratul- ihraam", yaani takbiir ya kufunga Sala, yaani . Dalili ya kuwajibika nia ni Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, .". (Al Bayyinah : 5).

Na Mtume s.a.w. ametwambia: "Hakika ya kila kitendo ni kwa nia yake". Kutokana na haya, mtu anapotaka kusali Sala yoyote ile ya fardhi, ni lazima unuwie moyoni kuwa anaingia kwenye Sala, na anuie ni Sala ipi, ya adhuhuri au ya laasiri, pia anuie kuwa ni Sala ya fardhi na abainishe idadi ya raka'a za hio Sala. Kwa hivyo basi, atanuwia kama hivi: " "Nina nuwia kusali Sala ya fardhi ya adhuhuri raka'a nne Lillah Ta'ala".

Kama tulivyosema hapo mwanzo kuwa nia si lazima kutamkwa, bali ni moyoni na ifuatane na kitendo chenyewe. Kwa mtoto kabla ya baalegh nia si lazima, kwani hio Sala hata kama ni ya fardhi kwake yeye huwa ni sunna; kwa vile yeye bado hajawajibika na Sharia.

Pili, kusimama kwa mwenye kuweza kusimama; asieweza kusimama atasali kitako, asieweza kwa kitako; atasali kwa kulala chali. Hivi ni kwa Hadithi alioipokea 'Imran bin Hussain r.a.:

"Nilikua nina bawasiri nikamuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w., akanambia: "Sali hali ya kuwa umesimama, ikiwa huwezi, kwa kukaa, ikiwa huwezi kwa kulalia ubavu". (Imehadithiwa na Al Bukhary).

Ameongeza Al Nassaai kwa kusema:

"Ikiwa huwezi (Sali) kwa kulala chali, Mwenyezi Mungu Mtukufu hamkalifishi mja wake ila kwa uwezo wake".

Kwa mwenye kuweza kusali kwa kusimama, kusimama kwake kuwe kwa kunyoosha mgongo vyema. Ikiwa ataweza kusimama, lakini hawezi kuruku'i au/na kusujudi kama vile akiwa ana ugonjwa wa mgongo, au ugonjwa wowote ule; basi atasimama na wakati wa kuruku'i na/au kusujudi atafanya anavyoweza, kama vile kukaa juu ya kiti na kuashiria ruku'i na sujudi, kwa kuinama. Kutokuweza sio lazima kwa sababu ya maradhi, bali kwa sababu nyengine yoyote ile yenye kukubalika Kisharia, kama vile akikhofu kizunguzungu ikiwa yumo melini au kwenye kipando chochote kile. Au akikhofu kupata maradhi au kuzidiwa na maradhi ikiwa atasimama au ataruku'i au atasujudi kidasturi. Muhim ni kwamba Mola wetu Mlezi s.w.t. hatukalifishi waja Wake ila kwa uwezo wetu. Kusali kwa ubavu, huwa kwa kulalia ubavu wa kulia na kuelekea qibla, akiwa hawezi atalala chali na uso wake uelekee qibla, na ataashiria kwa kuinamisha kichwa upande wa qibla kwa ruku'i na sujudi, atainamisha kichwa zaidi kwa kusujudi kuliko kwa ruku'i ili kutafautisha baina ya viwili hivi. Akiwa hawezi hata kufanya hivi basi ataashiria kwa macho na nia moyoni kuwa sasa anaruku'i na sasa anasujudi. Akifika hata kushindwa kufanya hivi, basi ataipitisha Sala moyoni mwake; katika hali hii ikiwa ataweza kutamka takbiiratu-l-ihram, yaani (Allaahu Akbar) na kusoma japo (Alhamdulillah) atafanya, ikiwa hawezi basi ataipitisha moyoni Sala yote kama anavyoweza. Tena, Mwenyezi Mungu Mtukufu hamkalifishi mja wake zaidi ya uwezo wake. Muhim ni kwamba binaadam hatakiwi kuiwacha Sala katika hali yoyote ile na katika ugonjwa wowote ule madam bado akili yake inafanyakazi. Na mwenye kusali katika hali hii haimlazim kulipa Sala alizozisali katika hali hii. Ametolea hoja Imam Al Ghazali r.a. haya kwa qauli ya Mtume s.a.w.: "Nikikuamrisheni kitu, basi kitendeni katika kitu hicho; kile mnachokiweza".

Na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: " Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini". (Al Hijr : 99).

Na muhim mno miongoni mwa ibada ni Sala, kwa hivyo inapasa kusali mpaka ufikwe na mauti madam akili inafanyakazi vyema.

Tatu, Takbiiratu-l-ihraam, yaani (Allaahu Akbar), hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:

"Ufunguo wa Sala ni udhu, na ihraam yake ni Takbiir na kutoka katika Sala ni kwa kutoa salaam". (Imehadithiwa na Abu Daud).

Na qauli ya Mtume s.a.w. wakati akitufundisha Sala kwa kupitia kwa Bwana alieikosea Sala yake, Mtume s.a.w. alisema hivi:

"Ukitaka kusali, tia udhu vyema, kisha elekea qibla na ukabbir". Kukabbir ni kusema: (Allaahu Akbar). Mtume s.a.w. alikuwa:

"Akifungua (Mtume s.a.w.) Sala huelekea qibla na akainua mikono yake miwili na akasema:

(Allaahu Akbar)". (Imehadithiwa na Ibun Maajah na Ibnu Hibbaan).

Hivi kuleta takbiir kwa Kiarabu ni kwa yule mwenye kujuwa Kiarabu, ikawa hajui Kiarabu basi atakabbiri kwa lugha yake na itamlazim kwa haraka ajifundishe ili aweze kutamka kwa Kiarabu. Huku kujifundisha ikiwa anaweza itakuwa hata kwa kusafiri kwa mahala karibu atakapopata kujifunza. Huku kusafiri itakuwa ni waajibu juu yake kwa sababu huku kujifunza ni waajibu, na kwa vile lenye kuambatana na waajibu nalo ni waajibu, kwa hivyo kusafiri kwa ajili ya kujifunza la waajibu ni waajibu.

Nne, kusoma Alhamdulillah yote yaani mpaka mwisho wake; hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Hana Sala asiesoma Surat Al-Fatiha, Alhamdulillah (yote)". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Na katika upokezi mwengine: "Haijuzu Sala kwa asiesoma Surat Al-Fatiha Alhamdulillah". (Imehadithiwa na Darqu'tny na Ibnu Hibbaan na Ibnu Khuzaima).

Na hili ni sawa kwa mwanamume na kwa mwanamke. Na amepokea Imam Shafi'ii r.a. kukhusu mafunzo ya Mtume s.a.w. kwetu sisi kupitia Bwana aliekosea Sala yake kwamba Mtume s.a.w. alisema:

"Kabbir, kisha soma Umu-l-Kitaab" . Umu-l-Kitaab ni " Al-Fatiha, yaani Alhamdulillah. Na katika riwaya nyengine:

"Mwenye kusali asisome Umu-l-Kitaab, Al-Fatiha (Alhamdulillah), basi hio (Sala) ni kasoro, haikutimia; akasema mmoja wa Masahaba: "Hakika sisi tunakuwa nyuma ya Imam". Akasema s.a.w.: "Isomeni moyoni mwenu". (Imehadithiwa na Muslim kutoka kwa Abi Huraira).

Hakika ni kwamba (Bismilaahir Rahmaanir Rahym), ni Aya kaamili ya mwanzo wa Sut-l-faatiha (Alhamdu); dalili ya qauli hii ni kwamba Mtume s.a.w.:

"(Mtume s.a.w.) ameihisabu Alfaatiha (kuwa ina) Aya saba, na akaihisabu Bismillahi kuwa ni Aya miongoni mwa hizo Aya saba". (Ameyataja haya Imam Al Bukhary r.a. katika taarikh yake). Na kwa qauli yake Mtume s.a.w.:

"Mukisoma (Alhamdu), basi someni na (Bismilaahir Rahmaanir Rahym), kwani hio (Alhamdu) ni Ummu-l-Qur'ani, na ni Ummu-l-Kitaab, na ni Saba'a Almathany (yaani ni yenye Aya saba), na (Bismilaahir Rahmaanir Rahym) ni moja miongoni mwa Aya zake". (Imehadithiwa na Darqu'tny).

Tunaona hapa kwenye Hadithi hii ya kwamba Surat-l-Faatiha imetajwa na Mtume s.a.w. kwa majina matatu tafauti, imetajwa kwa jina la Umm-l-Qur'an, na ikatajwa kwa jina la Ummu-l-Kitaab, na ikatajwa kwa jina la Saba'a-l-Mathaany; yote haya ni majina ya Surat Al Faatiha (Alhamdu). Na kutoka kwa Ummu Salamah r.a:

"Kwamba Mtume s.a.w. ameihisabu ni miongoni mwa Aya za Surat Al Faatiha". (Imehadithiwa na Ibnu Khuzaima).

Amesema Imam Abu Nasri Al Muadib r.a.Kuwa : "Wamewafiqiana wasomaji Qur'ani wa Al Kufa na wanazuoni wa Fiqhi wa Madinat-al- Munawwara kwamba, ni Aya miongoni mwa Aya za Surat-l-Faatiha. Ikiwa utasema kuwa katika kitabu "Sahih Muslim" kutokana na Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba Mtume s.a.w. alikuwa anafungua Sala kwa takbiir na anafungua kusoma Sura kwa Alhamdulillah Rabbi Al 'Aalamin", iIkiwa utasema hivyo; basi jawabu ni kwamba inavyo kusudiwa ni kuwa yeye s.a.w. husoma Sura yenye kujuulikana kwa jina la: (Alhamdu). Ikiwa itasemwa kuwa huku ndio kukhitalifiana kuliko dhaahir, jawabu itakuwa kutaka dalili.

Kusoma Alfaatiha huwa wakati uko kwenye kusimama au mahala pake, na kulazimika kusoma Alfaatiha ni kwa wote, yaani kwa anaesalisha na anaesalishwa, na anaesali peke yake; ikiwa kwenye Sala ya kudhihirisha kusoma, au kwenye Sala si ya kudhihirisha kusoma. Haifai kuitarjim Alfaatiha kwa lugha yoyote ile, hivi ni kwa vile kutowezekana kutarjimika ilivyo. Kusoma Alfaatiha ni waajibu. Kusoma Alfaatiha iwe kwa kuzisoma vyema Aya zake na kutia 'irabu zake vyema, pakutia shadda utie shadda na pakutia kisra utie kisra; na pakutia dhumma, utie dhumma. Lau kama ataacha herufi au akaacha shadda, au akabadilisha herufi kwa herufi nyengine; basi kusoma kwake hakutasihi, kwa hivyo Sala yake haitasihi.

Na ikiwa atasoma kwa kuvuta mno herufi na 'irabu zake, au kama atasoma kwa kughani mpaka ikabadilika maana kama vile kutia irabu ambayo si ya mahala pake mpaka ikabadilika maana haifai kufanya hivi, na Sala yake hubatilika. Ikiwa amefanya hivyo makusudi na itamlazim ailipe Sala yake, ikiwa hakufanya makusudi; basi ataisoma tena kwa njia iliosahihi. Yote haya tulioyaeleza ni kwa yule mwenye kuweza kusoma Alfaatiha, ama asieweza, yaani hajui kuisoma Alfaatiha kwa moyo itamlazim ajifunze au aisome kutoka kwenye mas-hafu, au kijuzuu, au popote pale ilipoandikwa; ikiwa hatoweza basi atasoma Aya saba za Qur'ani kama ilivyo kwenye qauli ya Mtume s.a.w.:

"Ukiwa unacho chochote cha Qur'ani, basi soma; kama huna basi muhimidie Mwenyezi Mungu Mtukufu na umtakase na umtukuze".

Imetajwa kusoma Aya saba (zozote zile za Qur'ani) kuwa ndio badala ya Alfaatiha kwa yule asiejuwa kuisoma Alfaatiha kwa moyo na hata kwa kwenye maandishi. Ikiwa hata hivyo hawezi, yaani hajui; basi badala yake ndio amhimidie Mwenyezi Mungu Mtukufu na amtakase na amtukuze. Hivi ni kama ilivyopokewa kutoka kwa Ibni Hibbaan r.a. kwamba bwana mmoja alikwenda kwa Mtume s.a.w. akamwambia s.a.w. kuwa yeye, yaani huyo bwana; hawezi kujifunza kusoma Qur'ani (kwa umri wake au kwa sababu nyengine yoyote ile); na badala yake afunzwe kitakachofidia badala ya Qur'ani, Mtume s.a.w. akamwambia aseme

Maneno hayo hapo juu ni uradi, na ndio anayotakiwa mtu ayaseme akiwa hajui kitu chochote katika Qur'ani. Atafanya hivyo na huku anafanya kila jitihada kujifunza Qur'ani, hata ikiwa kwa kusafiri kufuatia wa kumfunza. Maneno hayo tutayatajrim kama hivi ifuatavyo, hii sio maana yake khasa; bali ni kuweza kujua tu kwa uchache ni nini yanakusudia. "Ametakasika Mwenyezi Mungu, na Shukrani zote ni Zake Yeye Mwenyezi Mungu, na hapana mwenye kufaa kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Yeye Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa, na hapana hila wa nguvu isipokuwa ni kutokana kwake Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alie Tukuka". Kwa yule asiejua lugha ya Kiarabu, basi anaweza kusema kwa lugha yake, ikiwa Kiswahili au lugha nyengine; muhim iwe kwenye maana kama hio hapo juu. Lakini basi, ni dharura na muhim ajifunze Qur'ani kwa haraka kama atakavyoweza. Huu ni waajibu wake.

Fadhila ya Surat-l-Faatiha (Alhamdu)

Amehadithia Abu Saeed Al Khudry r.a. kuwa alikuwa akisali akaitwa na Mtume s.a.w., asiende wakati ule ule kwa vile yumo ndani ya Sala; baada ya kumaliza kusali akamwendea s.a.w. akasema kwa utiifu, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu hakika yangu nilikuwa nikisali! Mtume s.a.w. akamwambia:

"Kwani hakusema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele?" (Al Anfaal : 24). Kisha akasema s.a.w. : "Kwani si kufunzi Sura tukufu mno kwenye Qur'ani kabla hujatoka hapa msikitini"?

Ameendelea Abu Saeed Al Khudry r.a. kueleza ya kwamba alipotaka kutoka msikitini alisema kwa unyenyekevu: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu hakika yako ulisema kuwa utanifundisha tukufu mno ya Sura katika Qur'ani, akasema s.a.w.:

"Al-Hamdulillaahi Rabbi-l-'Aalamiin, hio ni Sab'u-l-Mathaani; (Sura yenye Aya saba) ambayo nimepewa na Qur'ani Tukufu". (Imehadithiwa na Al Bukhary na Abu Daud).

Na kutoka kwa Ubay bin Ka'abi r.a. amesema kuwa amesema Mtume s.a.w.:

"Ninataka usitoke msikitini mpaka nikufundishe Sura ambayo haimo kwenye Taurat wala kwenye Injiil, wala hamna mfano wake kwenye Qur'ani, Saba'a-l-Mathaany, Mfungua Kitabu". (Imehadithiwa Al Haakim).

Tano, kuruku'i; imethibiti hili kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na qauli za Mtume s.a.w. na kukubaliana Maimam na wanazuoni wote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, ". (Al Hajj : 77).

Na amesema Mtume s.a.w. wakati akitufunza Sala kwa kupitia Bwana aliekosea Sala yake:

"Kisha ruku'i mpaka utulie hali umeruku'i".

Sita, kutulia kwenye ruku'i; kama ilivyo kwenye hio Hadithi hapo juu. Uchache wa kuruku'i ni kuinama kwa mwenye kuweza mpaka viganja vyake viwili vifike kwenye magoti yake mawili. Ikiwa hawezi, kwa sababu ya ugonjwa au sababu yoyote ile; basi ataruku'i kama atavyoweza, ikiwa hawezi ataashiria. Ukamilifu wa ruku'i ni kuinama mpaka mgongo unyooke hali ya kuwa ameinama, na shingo inyooke na viganja vya mikono vikamate magoti na huku umepapachua vidole vya viganja vyako viwili kwenye magoti yako hali umevielekeze qibla, hivi ndivyo ilivyokuja kuwa ni sunna kwa mwenye kusali kasimama. Ama mwenye kusali kitako, uchache wa kuruku'i kwake ni kuinamisha uso wake mbele ya magoti yake ambayo yamethibiti juu ya ardhi. Ukamilifu wa kuruku'i kwa anaesali kitako ni kuinamisha uso wake na kuelekeza kipaji chake cha uso mahala anaposujudia. Ama uchache wa kutulia kwenye ruku'i ni kusubiri mpaka viungo vitue katika hali ya kuruku'i na ipambanuke baina ya kuinama (kuruku'i) na kuinuka. Ikiwa atafika kwenye kuruku'i, kisha akainuka kwa harakati zilizofuatana, hatapata kutulia kwenye ruku'i kunakotakikana. Kutulia kwenye ruku'i kuna kisiwa kwa uchache wa muda wa kusema:

Saba, kuinuka na kutulia wima baada kutoka kwenye ruku'I; hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. wakati akitufunza Sala kwa kupitia Bwana aliekosea Sala yake: , yaani kisha inuka mpaka usimame hali umenyooka sawa. Kuinuka na kutulia wima baada ya kutoka kwenye ruku'i ni kurejea katika hali ya kabla ya kuruku'i. Inapasa kuwa kuinuka huku kusiwe kwa makusudio mengine bali ni kwa kutimiza nguzo ya Sala. Iwapo kwa mfano yuko kwenye ruku'i akaona kitu cha kutisha, akainua mgongo wake ghafla hio haitakuwa kuinuka kwenye kuwajibika, kwa hivyo atarejea kwenye ruku'i kisha atainuka kwa kutimiza nguzo ya Sala kama inavyotakiwa.

Nane, kutulia wima baada ya kuinuka kutoka kwenye ruku'I; hii pia imethibiti kwa qauli ya Mtume s.a.w. wakati akitufunza Sala kwa kupitia Bwana aliekosea Sala yake. Kutulia kwenye kutakiwa ni kubaki kwa muda mdogo baada ya kutoka kwenye ruku'i na kabla ya kusujudi kwa kadiri ya kusema:

Tisa, kusujudi; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, ". (Al Hajj : 77).

Na kwa qauli ya Mtume s.a.w. wakati akitufunza Sala kwa kupitia Bwana aliekosea Sala yake:

"Kisha usujudu mpaka utulie kwenye kusujudi".

Ya Kumi, kutulia kwenye kusujudi; hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. wakati akitufunza Sala kwa kupitia Bwana aliekosea Sala yake, kama ilivyo hapo juu. Na uchache wa kusujudi ni kuweka kipaji cha uso kwenye pahala pakusujidia (ardhi, msala, na kadhaalika) huku unakididimiza kidogo kiasi ambacho ikiwekwa pamba chini yake itabonyea na kuonesha athari ya kubonyea huko. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Ukisujudi kithibitishe kipaji chako cha uso juu ya ardhi wala usidonowe (kama anavyodonowa kuku)". (Imehadithiwa na Ibnu Hibbaan).

Lau kama atasujudi kwa pua yake, au juu ya kilemba chake au juu ya mkono wa kanzu yake; haitafaa; hivi ni kwa Hadithi alioihadithia Imam Muslim r.a.:

"Tulimshtakia Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. joto la Al Ramdhai, hakutuondolea mashtaka yetu". Na akaongeza Al Baihaqy: "Kwenye vipaji vyetu vya uso na viganja vyetu vya mikono".

Hadithi hii inaonesha kuwajibika kusujudu na kugusa chini kipaji cha uso na viganja vya mikono miwili. Na kwa qauli ya Mtume s.a.w. kuwa ameamrishwa kusujudu kwa viungo saba:

"Nimeamrishwa nisujudu juu ya vifupa saba: kipaji cha uso, viganja viwili vya mikono, magoti mawili, na ncha za vidole vya miguu miwili". (Imekubaliwa na Maimam wapokezi wa Hadithi).

Inavyotakiwa katika kusujudi kuweka matumbo ya viganja na ncha za vidole vya miguu na kutopanua mikono miwili na kutoibana mbavuni.

Vilevile anaposujudi asiilaze mikono yake chini, bali ainue kwa kiasi; pia ainue sehemu yake ya kiuno. Hivi ni kwamba Bwana Al Barai. bin 'Aazib r.a. aliinua sehemu yake ya nyuma (kiuno) na akasema:

"Kama hivi alikuwa Mtume s.a.w. akisujudu". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Nassaai na Ibnu Hibbaan).

Lau kama ikiwa ana jaraha juu ya kipaji na amefunga bendeji au plasta na akasujudu juu yake, basi itajuzu wala haitamlazim kuzilipa Sala atazosali katika hali hio. Ikwa kwa ugonjwa hataweza kusujudia kipaji cha uso, basi ataashiria kwa kichwa, akishindwa ataashiria kwa kupepesa au kwa nyusi. Hakuna kujikalifisha kwenye Dini, Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. : " "Nikikuamrisheni kitu, basi fanyeni katika kitu hicho, kile mnachoweza kukifanya".

Kumi na Moja, kukaa baina ya sijda mbili; hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. wakati akitufunza Sala kwa kupitia Bwana aliekosea Sala yake:

"Kisha inua kichwa mpaka ukae kitako sawasawa". Na katika upokezi mwengine: "Mpaka utulie kwenye kitako, kisha fanya hivyo hivyo kwenye Sala yako yote". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Na imepokewa vilevile kuwa Mtume s.a.w. akiinua kichwa chake hasujudi (sijda ya pili) mpaka akae kitako sawasawa.

Kumi na Mbili, kutulia katika kitako cha baina ya sijda mbili.

Kumi na Tatu, Kumi na Nne na Kumi na Tano, kitako cha tahiyatu ya mwisho; kusoma tahiyatu ya mwisho na kumsalia Mtume s.a.w. kwenye tahiyatu ya mwisho. Zote hizi tatu kila mmoja ni nguzo miongoni mwa nguzo za Sala. Kukhusu du'a ya tahiyatu ziko riwaya mbili na zote ni sahihi, riwaya ya Ibni Masoud r.a. na riwaya ya Ibni 'Abbaas r.a. Amesema yeye Ibnu 'Abbaas kuwa Mtume s.a.w. alikuwa akiwafunza du'a ya tahiyatu kama anawafunza Qur'ani na alikuwa akisema:

"Maamkio yenye barka, Sala njema ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Salam, Rehma na Barka Zake Mwenyezi Mungu Mtukufu zikufikie weye Mtume s.a.w. Salama itufikie sisi na waja wema wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba hapana mungu isipokuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba Muhammad ni Mtumwa na Mjumbe Wake Mwenyezi Mungu Mtukufu". (Imehadithiwa na Al Shafiíi na Muslim na Abu Daud na Al Nissaai).

Amesema Imam Shafi'ii r.a. kuwa zimepokewa Hadithi mbali mbali kukhusu du'a ya tahiyatu, na hii ndio ninayoipenda zaidi, kwani hii ndio iliokamilika kuliko zote. Akasema Al Hafidh: "Ameulizwa Imam Shafi'ii r.a. sababu ya kuichaguwa du'a ya tahiyatu ya Ibni 'Abbaas". Akasema Imam Shafi'ii r.a. kuwa hii ndio nilioiona yenye kuenea zaidi na nimeisikia vyema kutoka kwa Ibni 'Abbaas. Akaendelea Imam Shafi'ii r.a. kuwa yeye alikuwa anayo du'a iliokusanya zaidi na yenye maneno mengi zaidi, nikachukua hii bila ya uzito, kwani mtu kuchukua kutoka kwa mwenziwe kiliocho bora zaidi ndivyo inavyofaa. Na du'a ya tahiyatu ya ukamilifu zaidi ni kuongeza ziada ya tuliotaja hapo juu, aongeze:

"Mwenyezi Mungu Mtukufu msalie Muhammad na Ahli zake Muhammad kama ulivyomsalia Ibrahiim na Ahli zake Ibrahiim, na mbaarik Muhammad na Ahli zake Muhammad, kama ulivyombaarik Ibrahiim na Ahli zake Ibrahiim, hakika Yako ni Mwingi wa kushukuriwa, na Mwingi wa mazuri".

Ama kuwajibika kumsalia Mtume s.a.w. kwenye Sala ni kwa ilivyopokewa kuwa Mtume s.a.w. aliulizwa vipi tukusalie wakati tumo kwenye Sala zetu, akasema s.a.w.:

"Semeni, Mwenyezi Mungu Mtukufu, msalie Muhammad na Ahli zake Muhammad". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Kumi na Sita, kutoa salam ya mwanzo; hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.: , yaani na kutoka kwenye Sala ni kwa kutoa salam. Uchache wa salam ni: , yaani amani juu yenu. Amesema Imam Al Nawawi r.a. kuwa zimesihi Hadithi kuwa Mtume s.a.w. alikuwa akisema: , na alikuwa mara nyingi akisema: , yaani amani na rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu.

Ya Kumi na Saba, kufanya kwa mpango huu nguzo zote hizi za Sala ili kufuatana na Hadithi ya Mtume s.a.w.: "Salini kama mnavyoniona mimi ninasali".

Na Mtume s.a.w. amesali kwa mpango kama ilivyotajwa humu katika hizi nguzo za Sala, na yeye Mtume s.a.w. ndio pekee ruwaza yetu. Ametwambia Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana". (Al Ahzaab : 21).

 

__________________________________________________

Haki za Uchapishaji zimehifadhiwa na Mtungaji

Farouk Abdalla Al-Barwani, P.O. Box 828, Ruwi, P.C.112 Sultanate of Oman

e-mail: umojabaraka@yahoo.co.uk