mecca_1.jpgFIQHI ILIYOWEPESISHWA: SALA

Farouk Abdalla Al-Barwani

 

Sunna za Sala Kabla ya Kuingia Kwenye Sala

Sunna za Sala kabla ya kuingia kwenye Sala ni adhana na iqama, na maana ya hizi ni kujuulisha kuingia wakati wa Sala na kuwa tayari Sala kusaliwa. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na mnapo adhinia Sala wao wanaichukulia maskhara na mchezo . " (Al Maida : 58).

Na kwa Qauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ". Ikiadhiniwa Sala". (Al Jumu'a : 9). Na kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Ikifika (wakati wa) Sala, naadhini mmoja wenu na asalishe mkubwa wenu". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Kwa Hadithi ya Mtume s.a.w. kwamba hata akisali mtu peke yake, basi pia aadhini na aqimu, kwani yeye s.a.w. alimwambia Aba Saeed Al Khudry r.a.:

"Hakika mimi ninakuona unapenda jangwani na kwenye mbuzi (wako), basi unapokuwa jangwani (kwako) au kwenye mbuzi wako na ukaadhini kwa Sala, basi inua sauti yako kwenye adhana, kwani kila inapofika sauti ya adhana na akaisikia jini na binaadam na chochote kile isipokuwa wata/vitakushuhudia kwa adhana hio Siku ya Qiyama". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Mwenye kuadhini anatakiwa aadhini naye amesimama na kuelekea qibla na inapendekezwa awe 'taahir na mwenye sauti nzuri, na asimame juu kitu kilichoinuka au mlangoni pa msikiti, hivi ikiwa haadhini kwa kikuza sauti. Anapoadhini akifika pakusema: aelekeze uso wake upande wa mkono wa kulia na akisema aelekeze uso wake upande wa mkono wa kushoto na aadhini kwa sauti hata kama anasali peke yake, hivi kama ilivyo kwenye Hadithi ya Mtume s.a.w. hio hapo juu, alipomfunza Aba Saeed Al Khudry r.a.".

Sharti ya kufaa mwenye kuadhini ni awe Muislam, mwenye kufahamu, mwenye akili timam na ni mwanamume. Kuadhini hakuhitaji idhini ya Imam, ni juu ya muadhini kuhakikisha kuingia wakati wa Sala, aadhini. Ama kuqim Sala ni kwa idhini ya Imam, yaani muadhini atamtaka idhini Imam ili aqim Sala.

Kushari'ishwa Adhana na Iqama

Imehadithiwa kwamba Abdullah bin Zaid r.a. amesema: "Alipoamrisha Mtume s.a.w. kengele ili waitiwe watu kwenye Sala, alinipitia nami nimo usingizini mtu amechukua kengele mkononi mwake, nikamwambia: "Ewe mtumwa wa Mwenyezi Mungu, unaiuza hio kengele"? Akaniuliza: "Unaitaka ya nini"? Nikamjibu: "Ninaitaka tuitiane kwenye Sala". Akasema: "Kwani unataka nikujuulishe kitu ambacho ni bora zaidi kuliko hivyo"? Nikamwambia: "Hapana shaka". Akasema: "Sema:

Akasita kidogo, (yule mtu aliemuona yeye Bwana Abdullah bin Zaid r.a. usingizin) kisha akasema: "Ukiqimu Sala sema hivi:

Ameendelea Bwana Abdullah bin Zaid r.a. kueleza: "Kulipokucha asubuhi nikenda kwa Mtume s.a.w. nikamueleze nilioyaona usingizini". Akasema Mtume s.a.w."

"Hio ni ndoto ya kweli Inshaallah, inuka pamoja na (Sayyidna) Bilal (r.a.) umsomee ulivyoota kisha aadhini kama hivyo, kwani yeye (Bilal) ni mbora wa sauti ya weye". Akasema Bwana Abdullah bin Zaid r.a.: "Nikasimama pamoja na Bilal r.a. nikawa ninasema na huku yeye anaadhini". Akaisikia adhana hii (Sayyidna) 'Umar r.a. nae yuko nyumbani kwake akaja mbiombio huku anasema: "Na kwa aliekuleta kwa haqi, nimeota kama hivi". Akasema Mtume s.a.w. , yaani kuhimidiwa ni Kwake Yeye Mwenyezi Mungu. (Imehadithiwa na Imam Ahmad).

Kwenye adhana imesuniwa kurejea mara mbili unaposema:

, na unaposema: yaani useme:

Hivi ni kama ilivyopokewa kutoka kwa Abi Mahdhuuri:

"Kwamba Mtume s.a.w. amemfundisha (Aba Mahdhuura) adhana yenye maneno kumi na tisa". (Imehadithiwa na wapokezi wa tano wa Hadithi).

Imesuniwa kwenye adhana ya Sala ya asubuhi (alfajir) baada ya kusema:

aseme:

Amesema Abu Mahdhuura: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu"! "Nifunze sunna ya adhana". Mtume s.a.w. akasema: "Ikiwa Sala ya asubuhi sema:

Vile vile imesuniwa kwa mwenye kumsikia muadhini aitikie kama vile anavyosema muadhini, isipokuwa kwenye kusemwa:

na . aitikie kwa kusema:

Hivi ni kama vile ilivyopokewa kutoka kwa Sayyidna 'Umar r.a. kwamba Mtume s.a.w. amesema:

Mwisho wa Hadithi hii anasema Mtume s.a.w. ya kwamba atakaesema hivi kutoka moyoni mwake basi ataingia Peponi.

Pia ni sunna katika kuadhini kusimama kwa: (sekne). Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.: , yaani ukiadhini adhini polepole, si mbiombio. (Imehadithiwa na Muslim). Amesema Muhammad bin Abdul Rahman r.a. katika Sharh Al Tirmidhy: Hadithi hii inafahamisha kwamba muadhini aseme kila neno miongoni mwa maneno ya adhana kwa upumzi mmoja. Na ameeleza Al Tirmidhy r.a. kwamba Mtume s.a.w. alimwambia Sayyidna Bilal r.a.: "Ukiadhini, adhini kwa utaratibu (polepole) na ukiqimu, qimu upesiupesi".

Imependekezwa anaposema muadhini:

Maana yake ni kama hivi: "Sala ni bora kuliko usingizi, Sala ni bora kuliko usingizi".

Mwenye kumsikia aseme: Maana yake ni kama hivi: "Umesema kweli na umetoka makosani".

Pia imependekezwa baada ya kumaliza adhana kumsalia Mtume s.a.w. na kumuombea Mwenyezi Mungu Mtukufu . Hivi kwa alivyopokea Abdullah bin 'Umar r.a. kwamba amemsikia Mtume s.a.w. akisema:

"Mukimsikia muadhini semeni kama anavyosema, kisha munisalie mimi; kwani anaenisalia mara moja, Mwenyezi Mungu Mtukufu humsalia yeye mara kumi; kisha muniombee "alwasiila", kwani hayo ni makaazi Peponi ambayo hayapati isipokuwa mja mmoja miongoni mwa waja Wake, na mimi naomba niwe ndio huyo mja Wake wa kupata makaazi hayo, basi mwenye kuniombea "alwasiila" utamhalalikia uombezi wangu". (Imehadithiwa na Muslim).

Na imepokewa kutoka kwa Jabir r.a. kwamba Mtume s.a.w. amesema:

Maana ya Hadithi hii, ambayo ni du'a; ni kama hivi: "Mwenye kusema anapomsikia muadhini: "Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa huu wito uliotimia, na Sala iliosimamishwa, mpe Muhammad "alwasiila" (makaazi ya juu kabisa Peponi), na umpe fadhila Zako na umuweke mahala patukufu ambapo Umemuahidi", basi huyo humhalalikia uombezi wangu Siku ya Qiyama". (Imepokewa na Al Bukhary).

Imependekezwa pia kuomba du'a baina ya adhana na kuqimiwa Sala, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.; "Hairejeshwi du'a baina ya adhana na iqama".

Wakasema Masahaba r.a. kumuuliza Mtume s.a.w., nini tuseme Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Akasema s.a.w.:

"Muombeni Mwenyezi Mungu msamaha na afiya duniani na Akhera".

Vilevile inapedekezwa kwa mwenye kusikia Sala inaqimiwa aseme kama vile anavyosema yule mwenye kuqimu Sala, (na kama anavyosema anapomsikia muadhini), lakini anaposema mwenye kuqimu Sala:

yeye aseme: , yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu aisimamishe na aidumishe. Hivi ni kwa vile Mtume s.a.w. alimsikia Sayyidina Bilal r.a. akisema: , akasema s.a.w.:

Sunna za Sala Baada ya Kuingia Kwenye Sala

Sunna za Sala baada ya kuingia kwenye Sala ni mbili, nazo:

Ya Kwanza, tahiyatu ya mwanzo; hivi ni kwa alivyopokea Abdullah bin Maalik bin Buhainah r.a. kwamba Mtume s.a.w.:

"Alisimama (Mtume s.a.w.) kwenye Sala ya adhuhuri na hakukaa tahiyatu ya mwanzo, alipomaliza Sala yake s.a.w. alisujudi sijda mbili (sajida za kusahau)". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Hii ni dalili ya kwamba lau kama tahiyatu ya mwanzo ni waajibu basi Mtume s.a.w. angelirejea ili kukaa na asingaliiwacha, hivi ikaonesha kuwa tahiyatu ya mwanzo ni sunna si waajibu. Katika kikao cha tahiyatu ni bora kukaa kwa kukalia mguu wa kushoto na kuusimamishia mguu wa kulia kwa matumbo ya ncha za vidole huku vidole vimeelekea qibla.

Ya Pili, kunuti katika Sala ya asubuhi; na katika witri ya nusu ya mwisho ya Ramadhani. Dalili ya kunuti ya katika Sala ya asubuhi ni Hadithi alioieleza Anas r.a. kuwa:

"Hakuwacha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. anakunuti kwenye Sala ya asubuhi mpaka ameifariki dunia". (Imehadithiwa na Imam Ahmad na wengineo).

Kunuti ni du'a, na du'a nzuri ya kunuti ni hii:

Maana ya Hadithi, du'a hii ni kama hivi:

"Mwenyezi Mungu Mtukufu tuongowe miongoni mwa uliowaongowa, na utu'afu miongoni mwa uliowa'afu, na ututawilie mambo yetu miongoni mwa uliowatawalia na utubarikie katika vile ulivyotupa, na utukinge na shari uliokwisha ihukumia, kwani hakika Wewe unahukumu wala huhukumiwi, na hakika hadhiliki uliemtukuza, wala hatukuki aliefanya uadui Kwako, umetukuka Mola wetu Mlezi na kuwa juu ya kila kitu, zinasitahiki kwako kuhimidiwa kote na zinastahiki kwako shukrani zote kwa uliotune'emesha, na Rehma za Mwenyezi Mungu zimshukie Mtume Sayyidna Muhammad (s.a.w.) na Ahli zake na Masahaba zake, na amani juu yao iwe". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy na Al Nissaai na wengineo kwa upokezi sahihi).

Imam anapoomba du'a huomba kwa dhamiri ya wote (yaani sisi), si kwa dhamiri yake pekee (yaani mimi). Ni karaha kwa Imam kujiombea du'a peke yake, daima aombe kwa watu wote. Hivi ni kwa Hadithi ya Mtume s.a.w.: "Mja (hawi imam) haongozi wenziwe akajiombea du'a yeye mwenyewe peke yake, akifanya hivyo basi amewakhini wenziwe". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy).

Sunna wakati wa kukunuti kuinua mikono, ama kupangusa uso baada ya du'a ya kunuti haijatajwa kufanya hivyo. Kupangusa kifuani hili wanazuoni walisema kuwa ni karaha.

Dalili ya kuthibiti kunuti katika nusu ya pili ya Ramadhani ni kwa alivyopokea Imam Al Tirmidhy r.a. kutoka kwa Sayyidna 'Ali r.a. na Abi Daud kutoka kwa Ubayi bin Ka'ab.

Haiati za Sala

Haia ya Sala ni kitu ambacho ukikiwacha haiwi kosa, wala hakiungwi kwa sijda ya kusahau. Kitu ambacho ni haia ukikifanya utapata ujira, na ni chini ya sunna kwa daraja. Tunaweza kulitarjimu hili neno: kwa maana ya karibu kuwa ni "pambo", wingi wake ni: yaani mapambo. Haiati za Sala ni kumi na tano.

Miongoni mwa haiati (mapambo) ya Sala ni:

La Kwanza, kuinua mikono wakati wa kupiga takbiiratu-l-ihrAam (takbiir ya kuingia kwenye Sala), yaani unaposema: na wakati wa kuruku'i, na unapoinuka kutoka kwenye kuruku'i, na wakati unapoinuka kutoka kwenye tahiyatu ya mwanzo. Kuinua mikono ni kwa kuelekeza viganja viwili takriba kuelekea qibla na kunyoosha vidole vya viganja viwili mpaka kufika vidole vya gumba sawa na mabega baina ya shingo na masikio. Kufanya hivi ni sawa ikiwa katika Sala ya fardhi au sunna au ya mwenye kusimama, kukaa au kwa katika hali yoyote ile, na sawa kwa mwanamume au mwanamke, imam au maamuma.

Kuinua mikono wakati wa kupiga takbiir ya kuingia kwenye Sala kumekuja kwa dalili ya kitendo cha Mtume s.a.w.:

"Alikuwa (Mtume s.a.w.) anainua mikono yake kufika sawa na mabega yake anapofungua Sala".(Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Kuinua mikono wakati wa kuruku'i na kuinuka kutoka kwenye ruku'i kumekuja kwa dalili ya kitendo cha Mtume s.a.w. alivyoeleza Ibnu 'Umar r.a.:

"Alikuwa Mtume s.a.w. akiingia kwenye Sala huinua mikono yake mpaka kuwa sawa na mabega yake, kisha akakabbir , akitaka kuruku'i huinua mikono yake kama hivyo huku akikabbir na akiinua kichwa kutoka kwenye ruku'i huinua mikono yake kama hivyo, huku akisema:

"Amemsika Mwenyezi Mungu Mtukufu aliemshukuru, Mola wetu Mlezi ni Kwako shukarani". (Imehadithiwa na Al Sheikhan na Al Baihaqy).

Kuinua mikoni wakati wa kutoka kwenye tahiyatu ya mwanzo kumekuja kwa dalili iliopokewa kutoka kwa Nafi'i r.a. kutoka kwa Ibini 'Umar r.a. kuwa yeye s.a.w. alikuwa akitoka kwenye tahiyatu ya mwanzo, huinua mikono yake huku akikabbir: ; Ibinu 'Umar r.a. amesema kuwa hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Mtume s.a.w. (Yamehadithiwa haya na Al Bukhary na Abu Daud na Al Nissaai).

La Pili, kufunga mikono kwa kuweka (kwa kukamata) kiganja cha mkono wa kulia juu ya kiganja cha mkono wa kushoto. Imepokewa kutoka kwa Qubaisa bin Halab r.a. kutoka kwa baba yake akisema:

"Mtume s.a.w. alikuwa akitusalisha hushika (kiganja cha mkono) wa kushoto kwa (kiganja cha mkono) wa kulia". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).

Na amesema Mtume s.a.w.:

"Miongoni mwa akhalaaq za Mitume (a.s.w.s) katika Sala ni kuweka kiganja cha mkono wa kulia juu ya kiganja cha mkono wa kushoto". (Imehadithiwa na Al Sheikhan, Al Nissaai na Al Haakim).

Kufunga mikono chini ya kitovu au juu ya kitovu, vyote ni sawasawa, kwani hali zote hizo mbili zimepokewa na Masahaba (r.a.) zake Mtume s.a.w.

La Tatu, kujisalimisha , (tawajuhi) kwa kusema baada ya takbbiir ya kuingia kwenye Sala, yaani baada ya kusema 9?5; 8 " "aseme :

Maana ya du'a hii ambayo imenasibishwa kwa Sayyidna 'Ali r.a.

kutokana na Mtume s.a.w. ni kama hivi:

"Nimeelekeza na kusalimisha uso wangu na nafsi yangu kwa Alieumba Mbingu na Ardhi, mimi ni mwenye kuamini na kusilim kwa dhati, wala mimi si katika washirikina. Hakika ya Sala yangu, na u'tiifu wangu na kuishi kwangu, na kufa kwnagu ni kwa ajili ya Mola Mlezi wa Ulimwengu, hana mshirika naye; na kwa hayo ndivyo nilivyo amrishwa na mimi ni miongoni mwa waliosilim". (Imehadithiwa na Muslim).

Ikiwa atawacha kuisoma hii du'a ya kuingilia kwenye Sala na akaingia kusoma Al Faatih kabla ya kuisoma hii dua ya "iftitaah", kuingilia kwenyea Sala; basi hatarejea kwa kuisoma hii dua, kwani itakuwa ishapita mahala pake. Mahala pake ni mara tu baada ya kuingia kwenye Sala, yaani baada ya kusema na kabla ya kusoma Alhamdu.

Amehadithia Abu Huraira r.a. kuwa Mtume s.a.w. alikuwa akisha kabbir kuingia kwenye Sala husita kidogo kabla ya kusoma Alhamdu, yaani Alfaatiha, akasema (yeye Abu Huraira r.a.): "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa nafsi ya baba yangu na mama yangu kwa ajili yako, kimya chako baina ya takbiir na kisomo; unasema kitu gani? Akasema Mtume s.a.w

"Nnasema Mwenyezi Mungu niweke mbali baina yangu na baina ya makosa yangu kama ulivyoweka mbali baina urejua na uchejua, Mwenyezi Mungu nitakase kutokana na makosa yangu kama inavyotakaswa nguo nyeupe kutokana na uchafu; Mwenyezi Mungu nioshe kutokana na makosa yangu kwa theluji na maji na baridi". (Imehadithiwa na Al Sheikhan na wanazuoni wa Hadithi, isipokuwa Imam Al Tirmidhy).

Ya Nne, kusoma: , yaani kujilinda na She'tani. Hivi ni kwa Qauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na ukisoma Qur'ani muwombe Mwenyezi Mungu akulinde na She'tani maluuni". (An Nah'l : 98).

Na imepokewa kutoka kwa Jubeir bin Mu't'am r.a. kwamba Mtume s.a.w.:

"Alikuwa (Mtume s.a.w.) akifunga Sala husema: Mwenyezi Mungu Mkubwa kuliko wakubwa wote, na kuhimidiwa Kwake Yeye ni kwingi na ametakasika Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni. (husema hivi mara tatu). Mwenyezi Mungu, mimi ninajilinda nawe na She'tani mal'uuni na najilinda na wazimu alionao na kibr na mpulizio wake". (Imehadithiwa na Ibnu Hibbaan).

Kujilinda na Mashe'tani huwa kwa tamko lolote lile lenye kutaja kujilinda.

Na lenye kupendeza mno ni : . Na amesema Ibnu Al Mundhir r.a. kutokana na Mtume s.a.w. kwamba:

Inapendezwa kusoma hii awali ya kila raka'a kwa vile kuwepo uwazi baina ya visomo viwili na ikawa unajilinda na She'tani kila unaposoma hivi kutaka Mwenyezi Mungu Mtukufu akulinde nae huyu She'tani mal'uuni ni vyema.

Ya Tano, kusoma kwa kutoa sauti au bila ya kutoa sauti, kwa mujib wa kila Sala. Wamekubaliana Wanazuoni kujuzu kusoma kwa sauti katika Sala ya: Asubuhi, Sala ya Ijumaa, Sala za Iddi mbili, Sala ya Taraweh na Sala ya witri katika mwezi wa Ramadhani, na katika raka'a mbili za mwanzo katika Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa. Ikiwa mtu anasali peke yake basi pia atasoma hivyo hivyo kama ilivyo hapo juu, kwani yeye hajatakiwa asikilize inaposomwa Quar'ani akiwa yumo kwenye Sala, hivyo ni sawa na Imam. Maamuma (mwenye kusalishwa) yeye husoma kimyakimya hata katika Sala zenye kutakiwa kusoma kwa sauti.

Imesuniwa kuisoma na hii Bismillah kwa sauti katika kila Sala yenye kusomwa kwa sauti, kwani hivi ndivyo ilivyopokewa kutoka kwa Sayyidna 'Ali na Ibni 'Abbaas na Ibni 'Umar na Abi Hurira na Sayyidana 'Aisha, Mwenyezi Mungu Mtukfu awe radhi kwao wote; kwamba Mtume s.a.w.:

"Alikuwa (s.a.w. ) akisoma kwa sauti kwenye Sala anayoisali katika wakati wake".

Ikiwa atasali Sala iliompita, ikiwa ni ya Sala ya usiku; kama vile magharibi au 'ishaa na akaisali usiku, basi huisali kwa kudhihirisha sauti.

Na ikiwa iliompita ni Sala ya mchana kama vile adhuhuri au laasiri, na akaisali mchana; basi huisali bila sauti. Ama ikiwa akiilipa Sala ya mchana, kama vile adhuhuri au laasiri, na akailipa usiku, au Sala ya usiku, kama vile magharibi au 'ishaa, na akailipa mchana; basi huchukuliwa ule wakati inapolipwa hii Sala iliompita katika wakati wake, ikiwa inalipwa wakati wa usiku, basi husaliwa kwa sauti, ikiwa inalipwa wakati wa mchana, husaliwa bila ya sauti.

Ya Sita, kuitikia &?) "Amin" ; hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

 

"Akisema Imam: , semeni Amin, kwani itakae wafiqia (sadifiana) qauli yake hii ya kuitikia "Amin" na qauli ya Malaika hughufiriwa makosa yake yaliotangulia".(Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Kwenye Sala ya kudhihirisha sauti huitikia . Amin kwa sauti imam na maamuma, vile vile anaesali peke yake, hivi ni kwa Hadithi:

"Alikuwa Mtume s.a.w. akimaliza kusoma Alhamdu huinua sauti na husema: Amin. (Imehadithiwa na Darqu'tny). Amesema Imam Shafi'ii r.a. kuwa ameambiwa na Muslim bin Khalid r.a.

kutokana na Ibni Jariih r.a. kuwa amesema 'A'taai kwamba alikuwa akiwasikia maimam - Ibna Al Zubair r.a. na waliokuja baada yake, wakiitikia . Amin na walioko nyuma yao, yaani wenye kusalishwa, wanaitikia Amin mpaka msikiti mzima hujaa sauti.

Ya Saba, kusoma Sura baada ya Alhamdu katika Sala ya Asubuhi, Sala ya Ijumaa, Sala za Idi mbili na katika raka'a mbili za mwanzo za Sala zote za fardhi. Kwenye Sala ya maiti haisomwi Sura baada ya Alhamdu.

Hivi ni kwa alivyopokea Abu Qataada r.a.:

"Alikuwa Mtume s.a.w. kwenye Sala ya adhuhuri katika raka'a mbili za mwanzo akisoma Alhamdu na Sura, na katika raka'a mbili za mwisho akisoma Alhamdu bila ya kusoma Sura, wakati mwengine s.a.w. husoma na sisi kusikia Aya anazozisoma. Alikuwa s.a.w. akirefusha kwenye raka'a ya mwanzo kuliko kwenye raka'a ya pili, hivi hivi ndivyo alivyokuwa akifanya kwenye Sala ya laasiri na Sala ya asubuhi". (Imehadithiwa na Al Sheikhan). Kuhusu kusoma Sura baada ya Alhamdu, unaweza kusoma Sura yoyote ile, unaweza kusoma Sura yote kaamil au unaweza kusoma sehemu ya Sura, vyote hivi inafaa.

Mtume s.a.w. alikuwa akirefusha kwenye raka'a ya mwanzo kuliko raka'a ya pili ya Sala ya asubuhi na katika kila Sala. Ama kurefusha kwenye Sala ya asubuhi huwa zaidi kwa vile kisomo cha Qur'ani alfajiri kinashuhudiwa la Malaika, au hushuhudiwa na Malaika wa usiku na Malaika wa mchana. Hivi pia kwa vile Sala ya asubuhi ni yenye raka'a kidogo kuliko Sala nne ziliobaki, kwahivyo basi, hivi kurefusha katika kusoma Sura ni badili ya vile kupungua raka'a zake.

Vilevile ni kwa vile kuwa hii Sala ya asubuhi inasaliwa baada ya watu kuwa wemepumzika usiku na bado hawajaingia kwenye mbio za maisha na ndio msingi na ufunguzi wa kuingia kwenye maisha, ndio imepewa muhimu zaidi na kurefushwa. Mtume s.a.w. alikuwa akisoma kwenye Sala ya asubuhi kiyasi ya Aya sitini mpaka mia, na ameisali Sala ya asubuhi kwa kusoma Surat (Qaaf), na pia ameisali kwa kusoma Surat (Ar-Rum) , na ameisali Sala ya asubuhi vilevile kwa kusoma , na wakati yuko safarini aliisali Sala ya asubuhi kwa kusoma . Na alikuwa Mtume s.a.w. wakati akisalisha akisikia sauti ya mtoto, hufupisha Sala kwa kumrehem mtoto na mama wa mtoto. Katika Sala ya Ijumaa alikuwa s.a.w. akisali kwa kusoma Surat na Surat . Akisoma Sura mbili hizi zote kaamili, wala haikupokewa kuwa s.a.w. alisoma sehemu ya Sura hizi bila ya kukamilisha Sura kaamili kama vile wanavyofanya baadhi ya watu hii leo, kufanya hivyo ni kinyume na mwenendo wa Mtume s.a.w. Hikma katika kuzisoma Sura mbili hizi kaamili ni kwa yale yalimo kwenye Sura mbili hizi, nayo ni kutajwa mwanzo na mwisho na kuumbwa Adam, na kuingia Peponi na kutajwa juu ya adhabu ya Moto na mengine ambayo ni uzinduzi kwa Umma kukhusu matokeo ya Siku ya Qiyama na onyo na mawaidha.

Ama Sala ya adhuhuri alikuwa Mtume s.a.w. mara nyingine akirefusha na mara nyengine huwa katinakati, amesema Abu Saeed r.a.:

Maana ya haya ni kama hivi:

"Ilikuwa Sala ya adhuhuri inasaliwa na mtu huwahi kwenda nje kufanya haja yake kisha akenda nyumbani kwake, akatia udhu na akarejea msikitini akakuta Mtume s.a.w. yuko kwenye raka'a ya kwanza kwa jinsi s.a.w. alivyoirefusha". (Imehadithiwa na Muslim).

Kwenye Sala ya adhuhuri Mtume s.a.w. alikuwa akisoma Surat na Surat , na wakati mwengine s.a.w. akisoma Surat na Surat Ama katika Sala ya laasiri huwa nusu ya Sala ya adhuhuri akiwa amerefusha na kiyasi ya hivyo akiwa amefupisha. Kwenye Sala ya magharibi imepokewa kuwa Mtume s.a.w. amesali kwa kusoma katika raka'a mbili Surat na mara nyingine kwa Surat na mara nyingine amesali kwa kusoma Surat pia s.a.w. amesali magharibi kwa kusoma Surat pia s.a.w. amesali magharibi kwa kusoma Kwenye Sala ya 'ishaa amesali Mtume s.a.w. kwa kusoma Surat na amesali s.a.w. Sala ya 'ishaa pia kwa kusoma Surat

Kwenye Sala ya Ijumaa, Mtume s.a.w. alikuwa akisali kwa kusoma Surat na Surat au Surat na Surat kaamili, au akisoma Surat na Ama kufupisha kwa kusoma mwisho tu wa Sura hizo, hivyo hakupata kufanya s.a.w., kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mwenendo wa Mtume s.a.w.

Kwenye Sala za Idi mbili alikuwa Mtume s.a.w. akisoma Surat yote na Surat na mara nyengine s.a.w. alikuwa akisoma Surat na Surat . Huu ndio mwenendo aliokwenda nao Mtume s.a.w. mpaka akafika kwa Mola wetu Mlezi, na wakaufuata Makhalifa wake na Maimam wanazuoni wote.

Mtume s.a.w. hakuwa akichagua Sura maalum katika Sala, isipokuwa kwenye Sala ya Ijumaa na Sala za Idi mbili na Sala ya asubuhi siku ya Ijumaa; bali imepokewa kuwa akisalisha kwa kusoma Sura fupi na Sura ndefu bila ya kuchagua. Haikupokewa kuwa Mtume s.a.w. akichanganya Sura mbili katika raka'a moja, isipokuwa kwenye Sala za sunna, ama katika Sala za fardhi haikupata kupokewa kuwa akichanganya Sura mbili kwenye raka'a moja..

Ya Nane na Tisa, kusema wakati wa kuinama kwenda kwenye ruku'i, na kusema wakati wa kuinuka kutoka kwenye ruku'i, na kusema ukishafika kwenye kusimama kaamili kutoka kwenye rukuí. Hivi ni kama alivyoeleza Abu Hureira r.a.:

"Alikuwa Mtume s.a.w. anapoingia kwenye Sala hukabbir, yaani husema , na hukabbir wakati anaporuku'i, na anapoinuka kutoka kwenye ruku'i husema: akifika juu kutoka kwenye ruku'i na kunyooka mgongo wake sawasawa husema ; kisha hukabbir wakati anapoinama kwenda kwenye kusujudi, kisha hukabbir wakati anapoinua kichwa kutoka kwenye kusujudi. Hufanya hivi kwenye Sala yake yote. Pia Mtume s.a.w. alikuwa hukabbir anapoinuka kutoka tahiyatu ya mwanzo". (Imehadithiwa na Bukhary na Muslim).

Ya Kumi, kusabbih wakati uko kwenye kuruku'i na kwenye kusujudi. Amehadithia Abu Daud kwamba Mtume s.a.w. ilipoteremka Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: alisema Mtume s.a.w.: yaani ijaalieni iwe kwenye kuruku'i kwenu, na ilipoteremka Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

alisema s.a.w.: yaani ijaalieni iwe kwenye kusujudi kwenu. Na amepokea Imam Muslim r.a. kutoka kwa Hudhaifa r.a.:

"Hakika ya Mtume s.a.w. alikuwa akisema hivyo". Imesuniwa kusema mara tatu tatu, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Unaporuku'i sema nawe umo kwenye ruku'i: mara tatu, na hivi ndio uchache wake, na unaposujudi sema nawe umo kwenye kusujudi: mara tatu, na hivi ndio uchache wake".

Uchache wa kusabbih kwenye ruku'i na kwenye kusujudi ni hivyo, yaani kusabbih mara tatu-tatu, ukamilifu wake ni kusabbih mara tisa au mara kumi na moja. Amesema Al Mawridy r.a. ya kwamba hizi tasbiih tatu-tatu ndivyo inavyotakiwa kwa Imam, yaani mwenye kusalisha; ama mtu akiwa anasali mwenyewe peke yake basi naarefushe kwa tasbiih na du'a vile anavyotaka. Amesema Mtume s.a.w.:

"Mja huwa karibu mno na Mola wake Mlezi wakati yumo kwenye sujudi, basi zidisheni du'a wakati mumo kwenye sujudi". Kuzidisha tasbiih kwenye kusujudi na du'a hata Imam anaweza kufanya hivyo iwapo watu anaowasalisha wanaridhia hivyo.

Mtume s.a.w. alikuwa anafanya mno katika kusujudi kwake na katika kuruku'i kwake du'a na nyiradi. Imepokewe kutoka kwa Sayyidah 'Aisha, Mama wa Waumini r.a.:

"Hakika Mtume s.a.w. alikuwa hufanya mno kusema nae yumo kwenye kuruku'i na kwenye kusujudi: Umetakasika Mola wetu Mlezi, Na kwa Sifa Zako Njema zote ninakuomba unighufirie". (Imehadithiwa na Al Sheikhan na Ahmad na wengineo).

Na imepokewa kutoka kwa Sayyidah 'Aisha r.a. vilevile kwamba Mtume s.a.w. alikuwa akisema kwenye kuruku'i na kwenye kusujudi

Maana ya du'a hii:"(Mola wangu Mlezi) Umetakasika na Mwenye kutokana na kila lisilolingana na Utukufu Wako, Mola Mlezi wa Malaika na Jibriil". Na imepokewa kutoka kwa Sayyidna 'Ali r.a. kwamba Mtume s.a.w. alikuwa akisema katika ruku'i:

"Mwenyezi Mungu wangu Mtukufu, kwa ajili yako ninaruku'i, na Kwako ninaamini, na Kwako nimesalim; Wewe ndio Mola wangu Mlezi, yananyenyekea masikio yangu, macho yangu, ubongo wangu, mifupa yangu na mishipa yangu na kilichobeba miguu yangu Kwako Wewe Mola Mlezi wa viumbe wote". (Imehadithiwa na Ahmad na Muslim na Abu Daud na wengineo).

Ya Kumi na Moja, kuweka viganja juu ya magoti wakati uko kwenye tahiyatu ya kwanza na ya pili. Kuweka viganja huwa kwa kukunjuwa kiganja cha mkono wa kushoto, mkono wa kulia hufumba vidole vyote isipokuwa kidole cha shahada, (kidole cha shahada ni baada ya kidole gumba), kidole cha shahada hukinyoosha na amekilaza juu ya goti lake.

Ameeleza Ibnu 'Umar r.a. kutokana na Mtume s.a.w., ni sunna anapofika kwenye kusema: , kuinua kidole chake cha shahada, hivi inakuwa imepatikana kushuhudia kwake kuwa hakuna Mola anaepasa kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kushuhudia kwa qauli na kwa kitendo. Kwa qauli ni vile kutamka , na kwa kitendo ni vile kuinua kidole chake cha shahada anapofika kwenye qauli . Imependekezwa anapokiinua kidole chake cha shahada akiinue kwa juu kidogo, iwe kama kakipindia juu kidogo. (Imehadithiwa na Ibnu Hibban katika kitabu chake).

Imepokewa kutoka kwa Al Zubair r.a. kuwa amesema:

"Alikuwa Mtume s.a.w. akikaa kwenye tahiyatu huweka kiganja chake cha kulia juu ya goti lake la kulia na kiganja cha kushoto juu ya goti la kushoto na akaashiria kwa kuinua kidole cha shahada, na kuashiria kwake hakupindukii macho yake". (Imehadithiwa na Ahmad na Muslim na Al Nissaai).

Ya Kumi na Mbili, kukaa tahiyatu; kikao cha tahiyatu mara zote huwa kwa kukunja miguu na kukalia mguu wa kushoto na kuunyosha mguu wa kulia na kuzisimamisha ncha za vidole (vya mguu wa kulia) huku umevipinda vidole na vinaelekea upande wa qibla. Mara nyingi hivi huwa kwenye tahiyatu ya mwanzo na ya mwisho pia. Lakini basi, kwenye tahiyatu ya mwisho inapendekezwa kukaa mkao wa "". Mkao wa (tawaruk), mkao huu ni kukalia matako mawili na mguu (unyayo) wa mguu wa kushoto kuulaza (kwa kuunyosha) mpaka ikawezekana mguu wa kulia ambao umesimamishiwa juu ya ncha za vidole kukaa juu ya unyayo wa mguu wa kushoto, hivi huwa umekaa kwa hali ya kuwa nyonga imepindika kidogo. Kukaa namna hivi kumethibiti katika Hadithi ziliomo kwenye Sahiihaini. Na alivyoeleza Imam Bukhary r.a.: "Anapokaa (Mtume s.a.w.) kwenye tahiyatu ya mwanzo hukalia mguu wa kushoto na kuusimamishia mguu wa kulia ncha za vidole, na akikaa kwenye tahiyatu ya mwisho huuweka mbele mguu wa kushoto na kuusimamishia vidole mguu wa kulia na kukalia matako".

Ya Kumi na Tatu, kuomba du'a baina ya sijida mbili. Hivi ni kwa vile Mtume s.a.w. alikuwa baina ya sijida mbili akisema: . Maana ya du'a hii ni kama hivi:

"Mola wangu Mlezi nighufirie, Mola wangu Mlezi nighufirie". (Imehadithiwa na Al Nissaai na Ibnu Maajah).

Na imepokewa kutoka kwa Ibni 'Abbas r.a. kwamba Mtume s.a.w. alikuwa akisema baina ya sijida mbili:

"Mwenyezi Mungu Mtukufu nighufirie na unirehemu na uniafu, na uniongowe na uniruzuku". (Imehadithiwa na Abu Daud), na katika upokezi wa Al Tirmidhy badala ya imekuja . "" maana yake ni niunge; kutokana na kuvunjika.

Ya Kumi na Nne, kikao kidogo baada ya kukamilisha sijida mbili za raka'a ya mwanzo na kabla ya kuinuka kwenda raka'a ya pili, vilevile baada ya kukamilisha sijida mbili za raka'a ya tatu na kabla ya kuinuka kwendea raka'a ya nne. Imethibiti kuwa hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Mtume s.a.w. na ni moja ya Hadithi mbili zilizopokewa na Imam Ahmad r.a.

Ya Kumi na Tano, kuomba du'a baada ya tahiyatu ya mwisho; yaani baada ya kumaliza Sala. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Masoud r.a. kuwa Mtume s.a.w. aliwafundisha du'a ya kusoma kwenye tahiyatu, kisha akasema s.a.w.: yaani kisha aombe du'a anayotaka. (Imehadiathiwa na Muslim).

Na imepokewa kutoka kwa Sayyidna 'Ali r.a. kuwa Mtume s.a.w. akiwemo kwenye Sala alikuwa baina ya tashahudi, yaani du'a ya tahiyatu na kutoa salam ya kutoka kwenye Sala, alikuwa s.a.w. akisema:

Maana ya Hadithi na du'a hii ni kama hivi:

"Mwenyezi Mungu nighufirie makosa yangu yaliopita na yanayokuja, na ya siri na ya dhaahiri na niliopindukia na yale ambayo Wewe unayajua kuliko mimi, Wewe ni mwenye kutanguliza na mwenye kuakhirisha, hakuna mungu isipokuwa ni Wewe Mola wangu Mlezi". (Imehadithiwa na Muslim).

Na imepokewa kutoka kwa Abdullah bin 'Amri r.a. kwamba Sayyidna Abu Bakar r.a. alisema kumwambia Mtume s.a.w.:

"Nifundishe du'a niiombe kwenye Sala yangu. Akasema Mtume s.a.w.: "Sema: "Mwenyezi Mungu, hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu dhulma nyingi, na wala hakuna mwenye kughufiria makosa isipokuwa ni Wewe, ninakuomba unijaalie maghfira kutoka Kwako, na unirehemu kwani Wewe Mwingi wa maghfira na Mwingi wa rehema" . (Iimekubaliwa na wapokezi wa Hadithi).

Na imepokewa kutoka kwa Abi Huraira r.a. kuwa Mtume s.a.w. kasema:

Maana ya Hadithi na du'a hii ni kama hivi:

"Akimaliza mmoja wenu tashahudi ya mwisho, basi naajilinde kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na mambo manne, naaseme: "Mwenyezi Mungu, hakika mimi ninajilinda na Wewe na adhabu ya Jahannam, na adhabu ya kaburi, na fitna ya uhai na mauti, na shari ya fitna ya masihi dajjaal". (Imehadithiwa na Muslim).

Ya Kumi na Sita, kutoa salam ya pili, yaani ya upande wa mkono wa kushoto.

Sala za Sunna Zenye Kufuatana za Sala za Fardhi

Sala za sunna zenye kufuatana na Sala za fardhi ni raka'a kumi na nane, pamoja na raka'a moja ya witri; ni raka'a kumi na tisa; nazo ni:

Sala Ya Fardhi

Raka'a Za Sunna Za Kabla Ya Sala Ya Fardhi

Raka'a Za Sunna Za Baada Ya Sala Ya Fardhi

Alfajiri

2

 

Adhuhuri

4

2

Laasiri

4

 

Magharibi

2

2

'Ishaa

 

2 +1 (witri)

Jumla

12

7

 

Na miongoni mwa hizi Sala za sunna, zimetiliwa nguvu raka'a kumi, na hivyo ndivyo Mtume s.a.w. alivyodumisha kufanya aghlab; nazo ni:.

Sala Ya Fardhi

Raka'a Za Sunna Za Kabla Ya Sala Ya Fardhi

 

Raka'a Za Sunna Za Baada Ya Sala Ya Fardhi

 

Alfajiri

2

 

Adhuhuri

2

2

Laasiri

-

 

Magharibi

-

2

'Ishaa

-

2

Jumla

4

6

 

Imetolewa dalili ya haya kwa Hadithi ya Ibni 'Umar r.a.:

"Nimesali pamoja na Mtume s.a.w. raka'a mbili kabla ya Sala ya adhuhuri, na raka'a mbili baada ya Sala ya adhuhuri, na raka'a mbili baada ya Sala ya magharibi, na raka'a mbili baada ya Sala ya 'ishaa. Na amenambia Sayyidah Hafsa bint 'Umar r.a. kuwa Mtume s.a.w. alikuwa akisali raka'a mbili khafifu baada ya

kutokeza alfajiri". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Wenye kusema juu ya kusali raka'a nne kabla ya Sala ya adhuhuri, dalili yao ni Hadithi aliyopokea Imam Bukhary r.a. kutoka kwa Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba Mtume s.a.w.: "Alikuwa (Mtume s.a.w.) hawachi kusali raka'a nne kabla ya Sala ya adhuhuri".

Na wenye kusema juu ya kusali raka'a nne kabla ya Sala ya laasiri, dalili yao ni Hadithi aliopokea Imam Al 'Tirmidhy kutoka kwa Sayyidna 'Ali r.a. kwamba Mtume s.a.w.:

"Alikuwa (Mtume s.a.w.) akisali raka'a nne - mbili mbili - kabla ya Sala ya laasiri".

Na imepokewa ya kwamba Mtume s.a.w. alisema:

"Mwenyezi Mungu amemrehemu mja mwenye kusali raka'a nne kabla ya Sala ya laasiri".

Amesema Imam Al Tirmidhy r.a. kuwa Hadithi hii ni "hasan" na Ibnu Hibbaan r.a. kaipa daraja ya Hadithi sahihi. Ama dalili ya kusali raka'a mbili kabla ya Sala ya magharibi ni kutokana na Hadithi ya Imam Bukhary r.a.:

"Salini kabla ya Sala ya magharibi, salini kabla ya Sala ya magharibi, mara ya tatu akaongeza, kwa mwenye kutaka".

Na amehadithia Imam Muslim r.a. kwamba walikuwa wanakimbilia kusali sunna ya kabla ya Sala ya magharibi kwa wingi hata mtu akiingia msikitini hufikiri kuwa Sala ya magharibi ishasaliwa (na watu wanasali sunna ya baada magharibi), kwa wingi wa wenye kusali hii sunna ya kabla ya Sala ya magharibi.

Sunna ya Kabla ya Sala ya Alfajiri

(Ilivyoelezwa Kwenye Fiqh Sunna)

Kuna Hadithi nyingi za Mtume wetu s.a.w. kukhusu fadhila za hii Sala ya sunna ya kabla ya Sala ya alfajiri, na juu ya sunna yenyewe kwa jumla. Hapa tutataja baadhi ya Hadithi hizo, kukhusu fadhila ya sunna hii, na juu ya kujuzu kukidhiwa (kulipwa); yaani kusaliwa nje ya wakati.

Fadhila za Sunna ya Kabla ya Sala ya Alfajiri

Miongoni mwa Hadithi za Mtume s.a.w. juu ya fadhilia ya Sala ya sunna ya kabla ya Sala ya Alfajiri ni:

"Ameeleza Sayyidah 'Aisha - Mama wa Waumini - r.a., kuwa amesema Mtume s.a.w. kukhusu raka'a mbili za sunna ya kabla ya Sala ya alfajiri: "Hizo ni bora zaidi kwangu kuliko dunia yote". (Imehadithiwa na Ahmad na Muslim na Al Tirmidhy).

Ameeleza Abu Huraira r.a. kwamba Mtume s.a.w. amesema:

"Musiwache raka'a mbili za kabla ya Sala ya subhi hata mukifukuzwa na farasi".

Imeelezwa ya kwamba makusudio ya Hadithi hii ni kuhimizwa kutowacha kusali sunna ya kabla ya Sala ya asubuhi hata katika hali ya vita kupamba moto. Hii yote ni kuthibitisha darja ambayo Mtume s.a.w. ameipa hii Sala ya sunna ya kabla ya Sala ya alfajiri.

Na ameeleza vilevile Sayyidah 'Aisha r.a

"Hakuwa Mtume s.a.w. katika mambo ya sunna mwenye kudumisha mno kuliko alivyo dumisha sunna ya raka'a mbili za kabla ya Sala ya asubuhi (alfajiri)". (Imehadithiwa na Al Sheikhan na Ahamad na Abu Daud).

Kuilipa Sala ya Sunna ya Kabla ya Sala ya Alfajiri

Imepokewa kutoka kwa Ibi Huraira r.a. kwamba Mtume s.a.w. amesema: " " "Asiewahi kusali raka'a mbili za (sunna) ya kabla ya alfajiri mpaka likachomoza jua, basi naazisali". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).

Na ameeleza Qais bin 'Umar r.a. kwamba alikwenda kusali Sala ya asubuhi (msikitini), akamkuta Mtume s.a.w. yumo kwenye Sala, akaingia kusali fardhi pamoja na Mtume s.a.w (hakusali sunna ya alfajiri). Baada ya kumaliza hii fardhi akasimama na kusali sunna ya kabla ya Sala ya alfajiri, akapita (hapo alipokuwepo) Mtume s.a.w. akamuuliza (akaulizwa Sayyidna Qais r.a.) "Sala ipi hii"? Akamueleza, Mtume s.a.w. akanyamaza bila ya kusema kitu.

(Yamehadithiwa haya na Ahmad na Ibnu Khuzaimah na Ibnu Hibbaan).

Na wameeleza Al Sheikhan na Ahmad kutokana na 'Imraan bin Hu'sain kwamba walikuwa kwenye msafara pamoja na Mtume s.a.w. wakachukuliwa na uzingizi, wakaikosa Sala ya alfajiri katika wakati wake. Wakaamka kwa ujoto wa jua, wakangoja kidogo mpaka jua likapanda juu kidogo, kisha hapo Mtume s.a.w. akaamrisha iadhiniwe, akasali s.a.w. raka'a mbili za sunna ya kabla ya Sala ya alfajiri, (hapana shaka na Masahaba nao pia walisali sunna hii) kisha ikaqimiwa na kusaliwa Sala ya alfajiri. Kutokana na Hadithi hii ni kwamba hii sunna ya kabla ya Sala ya alfajiri inajuzu kulipwa, sawa ikiwa imempita mtu kabla ya kuchomoza jua, au baada ya kuchomoza jua; ikiwa kwa udhuru au bila ya udhuru, na sawa imempita hii sunna tu, au imempita sunna na fardhi yenyewe, yaani Sala ya alfajiri.

(Mwisho wa kunukulu kutoka Fiqhi Sunna).

Sunna Zilizotiliwa Mkazo

Sala za sunna zilizotiliwa mkazo ni Sala tatu, Sala za usiku, Sala ya dhuha na Sala ya taraweih. Sala za sunna za usiku husaliwa baada ya mtu kusali Sala ya witri akalala na kuamka baada ya nusu ya usiku, hapo ndipo husali Sala za usiku, na pia huitwa Sala ya tahajjud , pia huitwa Sala ya qiyamu-l-lail Wamekubaliana wanazuoni kwa kupendeza kusali Sala hii kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na amka usiku kwa ibada, ni ziada ya sunna khasa kwako wewe............". (Al Israai : 79).

Na kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Walikuwa wakilala kidogo tu usiku". (Adh-dhaariyaat : 17).

Na kwa Qauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na kutumaini, ". (Assajdah : 16 ).

Sala ya qiyamu-llayl mwanzo ilikua ni Sala ya waajibu, baadae ikafutwa kuwa waajibu, ikabakia kuwa ni sunna iliotiliwa mkazo. Na katika Hadithi, Mtume s.a.w. ameusia Sala za usiku:

"Jilazimisheni Sala za usiku kwani hivyo ndivyo walivyodumisha watu wema (wachamngu) wa kabla yenu, na ndizo zitakazo kufanyeni muwe karibu na Mola wenu Mlezi, na ndizo zenye kupatisha maghfira na ni kinga ya maasi". (Imehadithiwa na Al Haakim).

Na katika Hadithi nyengine amesema Mtume s.a.w.:

"Mwenye kusali Sala ya usiku akasoma Aya mia za Qur'ani Tukufu basi hatoandikwa miongoni mwa wenye kughafilika, na mwenye kusali Sala ya usiku akasoma Aya mia mbili za Qur'ani Tukufu basi ataandikwa miongoni mwa wenye kum'tii Mwenyezi Mungu Lillah". (Imehadithiwa na Al Haakim).

Tutambuwe kwamba kati ya usiku ni afadhali (kwa ibada) kwa Qauli yake Mtume s.a.w. alipoulizwa Sala gani ni bora baada ya Sala ya fardhi? Akasema s.a.w.: yaani, " Sala ya kati ya usiku". Hivi ni kwa sababu kufanya ibada wakati kama huo ni kitu kizito na kughafilika na kuona tamu ya usingizi na raha zake ndio mno. Na nusu ya pili ya usiku ni afadhali zaidi, kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira". (Adh-dhaariyaat : 18).

Huu wakati wa nusu ya pili ya usiku ni wakati ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu huteremsha Rehma Zake na Qudra Zake. Ama kusimama usiku wote kwa ibada, hivi imekatazwa, ni karaha, kwani kufanya hivyo ni kudhuru nafsi. Vievile imekuja kwenye Hadithi ya Mtume s.a.w. kwamba ni karaha kwa yule aliekuwa na dasturi ya Sala za usiku kisha baadae akaacha sunna hii, amesema s.a.w. kumwambia Abdullah bin 'Amr bin l'Aas r.a.:

"Ewe Abdullah! (Ewe Mtumwa wa Mwenyezi Mungu). Usiwe kama fulani, alikuwa anasali Sala za usiku, kisha akawacha". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Kuthibiti sunna ya Sala ya dhuha kumekuja kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye". ('Saad : 18).

Amesema Ibnu 'Abbaas r.a. inakusudiwa Sala ya dhuha. Na kutokana na Hadithi aliohadithia Abu Dharr r.a., kuwa amesema:

"Ameniusia kipenzi changu (khaliili), yaani Mtume s.a.w. mambo matatu: Kufunga siku tatu katika kila mwezi, na raka'a mbili za Sala ya dhuhaa, na nisali Sala ya witri kabla ya kulala". Na akaongeza Al Bukhary: "Nisiyawache".

Sala ya dhuha uchache wake ni raka'a mbili, na wingi wake ni raka'a kumi na mbili, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. akimwambia Aba Dharr r.a.:

"Ukisali Dhuha raka'a kumi na mbili, Mwenyezi Mungu Mtukufu atakujengea nyumba Peponi". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).

Amesema Imam Annawawy r.a.: "Wingi wake ni raka'a nane".

Wakati wa Sala ya dhuha ni tangu kuchomoza jua urefu wa mkuki mpaka kuwa katikati. Sala ya taraweih haina shaka kuthibiti sunna yake kwa kukubaliana na wanazuoni; imekuja kwenye Hadithi:

"Mwenye kusimama Ramadhani (kwa kusali taraweih) kwa imani na kwa ajili ya ridhaa ya Mwenyezi Mungu, basi ataghufiriwa makosa alioyafanya".

Na amesema Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba Mtume s.a.w.:

"Mtume s.a.w. amesali Sala ya taraweih, na wakaisali pamoja nae, kisha akaisali nyumbani kwake katika sehemu ya mwezi iliobakia; na akasema s.a.w.: "Hakika mimi nnachelea kujafaridhishwa juu yenu kisha ikajakukushindeni". Na Mtume s.a.w. aliendelea hivyo, na vilevile Sayyidna Abu Bakar r.a.; na ikaendelea katika khilafa ya Sayyidna 'Umar r.a. Kisha Sayyidna 'Umar akaona watu wanasali msikitini taraweih mmoja mmoja, na wengine wawili wawili, na wengine watatu watatu. Alipoona hivi (Sayyidna 'Umar r.a.) akawakusanya chini ya uimamu wa Ubaiya bin Ka'ab r.a. na akawadumisha kusali kwa raka'a ishirini. Sayyidna 'Umar r.a. amefanya hivi, yaani kuendelea yeye kutosali taraweih msikitini na badala yake akaendelea kumueka Sayyidna Ubaiyya r.a. kuisalisha, Sayyidna 'Umar r.a. alifanya hivi vilevile na yeye kuchelea kuja faridhishwa hii Sala ya taraweih.

Sala ya taraweih ni sunna kwa wanaume na kwa wanawake, kutokana 'Arfajah: "Alikuwa Sayyidna 'Ali r.a. anaamrisha kusaliwa Sala ya taraweih na huweka imam wa wanaume na imam wa wanawake, mimi nilikuwa imam wa wanawake".

Sala ya taraweih husaliwa baada ya Sala ya 'ishaa na kabla ya Sala ya witri na huendelea muda wa kujuzu kusali tarweih mpaka mwisho wa usiku. Sala ya taraweih husaliwa raka'a mbili mbili.

Sala ya taraweih ni bora kusaliwa raka'a nane kufuata alivyokuwa akifanya Mtume s.a.w. Amepokea Ibnu Khuzaima na Ibnu Hibbaan kutoka kwa Jaabir r.a.:

"Mtume s.a.w. aliwasalisha raka'a nane na witri, kisha wakamngoja baadae (siku nyengine); hakuwajia".

Ameeleza Abu Ya'alaa na 'Tabraany kwamba alikwenda Ubaiya bin Ka'ab kwa Mtume s.a.w. akamwambia: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hakika kimenitokezea mimi jana kitu, Mtume s.a.w. akamuuliza: "Ni nini hicho ewe Ubaiyya"? Akajibu: "Wanawake nyumbani kwangu walisema kuwa wao hawasomi Qur'ani, basi tutasali kwa Sala yako. Nikasali nao raka'a nane na witri. Ikawa hii ni sunna kwa ridhaa ya Mtume kwa kutosema kitu. Hii ikawa ni dalili ya kusaliwa taraweih raka'a nane, kwa kitendo na kukiri kwake Mtume s.a.w. Na imeelezwa na Sayyidah 'Aisha r.a.:

"Hakika Mtume s..a.w. hakuwa akizidisha raka'a kumi na moja, (za Sala za sunna); ikiwa Ramadhani au si Ramadhani". (Imehadithiwa na jamaa, wapokezi wa Hadithi).

Ama cha kusoma kwenye Sala ya taraweih haijaja kubainisha Sura au kiasi maalum, lakini kuwa katinakati ni bora; isiwe kusoma mpaka kuwachokesha wanosalishwa. Imam anaweza kurefusha kwa watu kushauriana na kukubaliana. Ameeleza Abu Dharr, tulisimama na Mtume s.a.w., yaani aliwasalisha; mpaka tukaogopa isitupite wakati wa daku. Na ni bora katika mwezi isipungue kusoma khitma nzima, hivi ili watu wapate kuisikia Qur'ani yote katika huu mwezi mtukufu wa Ramadhan; na isizidi khitma, kuchelea kuwachokesha maamuma.

 

 

 

__________________________________________________

Haki za Uchapishaji zimehifadhiwa na Mtungaji

Farouk Abdalla Al-Barwani, P.O. Box 828, Ruwi, P.C.112 Sultanate of Oman

e-mail: umojabaraka@yahoo.co.uk