mecca_1.jpgFIQHI ILIYOWEPESISHWA: SALA

Farouk Abdalla Al-Barwani

 

Ya Kusemwa Baada ya Sala

Kwanza, inasuniwa mtu akimaliza kusali apanguse kipaji chake cha uso na aseme:

"Ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba hapana Mola anaepasa kuabudiwa kwa haqi isipokua Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu; Mwenyezi Mungu, niondolee mmahaniko na huzni".

Au apanguse kichwa chake na aseme:

"Hapana Mola anaepasa kuabudiwa kwa haqi isipokua Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu; Mwenyezi Mungu, niondolee mmahaniko na huzni".

Pili, aseme mara tatu: yaani naomba maghfira kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kisha aseme:

Maana ya Hadithi, du'a hii ni kama hivi:

"Mwenyezi Mungu, Wewe ndio Salama, na kutokana na Wewe ndio Salama, Umetukuka Ewe Mwenye Utukufu na Mwingi wa Ukarim". (Imehadithiwa na jamaa isipokuwa Al Bukhary r.a.).

Tatu, kisha aseme:

Maana yake ni kama hivi:

"Mwenyezi Mungu, niwezeshe kukutaja sana na kukuabudu vyema". Hivi ni kutokana na qauli ya Mtume s.a.w.:

"Nnakuusia Ewe Mu'adh, usiwache baada ya kila Sala kusema : "Mwenyezi Mungu, niwezeshe kukutaja sana na kukuabudu vyema". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Nissaai na Ibnu Khuzaimah na Al Haakim)

Nne, kisha aseme:

Maana Hadithi, duá hii ni kama hivi:

"Hapana Mola anaepasa kuabudiwa kwa haqi isipokua Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni Yeye Pekee, hana mshirika, Ufalme na Shukrani zote ni zake Yeye, na Yeye ni muweza wa kila kitu. Mwenyezi Mungu, hapana wakuzuia kwa unachokitoa, wala hapana mwenye kutoa kwa unachokizuia, wala haunufaishi ukarimu zaidi ya Ukarimu Wako". (Imehadithiwa na Ahmad na Al Sheikhan).

Tano, kisha asome yaani ni: na , na . Hivi ni kutokana na alivyoeleza 'Uqbat bin 'Amir r.a. :

"Ameniamrisha Mtume s.a.w. nisome baada ya kila Sala yaani na (Imehadithiwa na Ahmad na Abu Daud na Al Tirmidhy na Al Nissaai).

Sita, kisha asome: (Ayat Al Kursi). Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Mwenye kusoma baada ya kila Sala ya fardhi, hakitamzuilia kuingia Peponi ila mauti, (yaani kuwa bado hajafa)". Imehadithiwa na Al Nissaai na Ibnu Hibbaan).

Saba, kisha asabbih, ahimidi na akabbir; hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

Mwenye kumsabbih Mwenyezi Mungu Mtukufu: mara thalathini na tatu, na akamhimidi mara thalathini na tatu na takabbir mara thalathini na tatu, baada ya kila Sala. Hizo ni tisiini na tisa, kisha akasema: Kutimia mia: "Hapana Mola anaepasa kuabudiwa kwa haqi isipokua Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni Yeye Pekee, hana mshirika, Ufalme na Shukrani zote ni zake Yeye, na Yeye ni Muweza wa kila kitu; ataghufiriwa makosa yake hata yakiwa wingi wa mapovu ya mawimbi ya bahari. (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Sheikhan).

Vilevile kwa qauli ya Mtume s.a.w. kuwa asabbih, ahimidi na akabbir mara kumi kumi:

"Kheri mbili akizidumisha mtu zitamtia Peponi, nazo ni nyepesi; na ni wachache watakaozitenda". Wakasema Masahaba r.a. kumuuliza s.a.w.: "Ni zipi hizo Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu"? Akasema s.a.w.: "Umhimidi Mwenyezi Mungu na umkabbir na umsabbih baada ya kila Sala ya fardhi mara kumi kumi, na unapotaka kulala umsabbih Mwenyezi Mungu na umkabbir na umhimidi mara mia, hivyo itakua mia mbili na khamsini kwa kuzitamka na ni elfu mbili na mia tano kwenye mizani. Nani miongoni mwenu atakaefanya maovu elfu mbili na mia tano katika mchana na usiku"? Wakauliza Masahaba r.a. kumuuliza Mtume s.a.w.: "Na vipi hivyo kuwa ni wachache wataotenda hivyo?

Akaeleza s.a.w.: Atamjia mmoja wenu She'tani kwenye Sala yake amkumbushe haja hii na hii (akimbilie kuondoka) asifanye uradi huu, na atamjia She'tani wakati wa kulala amlaze (upesiupesi) asifanye uradi huu". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy).

Imesuniwa kwa Hadithi ya Mtume s.a.w.:

"Mwenye kusema mara kumi kabla hajaondoka na kukunjua mguu wake kutoka kwenye Sala ya magharibi na Sala ya asubuhi: "Hapana Mola anaepasa kuabudiwa kwa haqi isipokua Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni Yeye Pekee, hana mshirika, Ufalme na Shukrani zote ni zake Yeye, Kwake Yeye ndio ziko kheri zote, anahuisha na anafisha, na Yeye ni Muweza wa kila kitu, huandikiwa kwa kila moja mema (thawabu) kumi na hufutiwa maovu (dhambi) kumi na hupandishwa cheo kwa daraja kumi, na huwa ni kinga kwake kwa kila ovu na kinga ya She'tani mlaanifu wala haitakuwepo dhambi itakayo muangamiza isipokuwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na atakua miongoni mwa watu bora mno, isipokuwa kwa yule atakaesema bora zaidi ya hivi alivyosema yeye". (Imehadithiwa na Ahmad).

Vilevile imesema Mtume s.a.w.:

"Ukimaliza kusali Sala ya asubuhi kabla hujasema na mtu yeyote, sema mara saba: Mwenyezi Mungu niepushe na Moto, kwani ukifa katika siku hii Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuandikia kuepukana na Moto. Na ukimaliza kusali Sala ya magharibi, kabla hujasema na mtu yeyote, sema mara saba: Mwenyezi Mungu, mimi ninakuomba Pepo. Mwenyezi Mungu niepushe na Moto, kwani ukifa katika usiku huu Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuandikia kuepukana na Moto". (Imehadithiwa na Ahmad na Abu Daud).

Amehadithia Abu Haatim kwamba Mtume s.a.w. alikuwa akisema baada ya kumaliza Sala yake:

"Mwenyezi Mungu nisalihishie (niongolee) dini yangu ambayo ndio mwongozi wa mambo yangu, na nisalihishie dunia yangu ambayo umejaalia ndani yake ndio maisha yangu. Mwenyezi Mungu mimi ninajikinga adhabu yako kwa ridhaa yako, na ninajikinga naqama yako kwa msamaha wako, na ninajikinga Kwako kwa nafsi Yako. Mwenyezi Mungu, hapana wakuzuia kwa unachokitoa, wala hapana mwenye kutoa kwa unachokizuia, wala haunufaishi ukarimu zaidi ya Ukarimu Wako".

Yenye Kutafautiana Baina ya Mwanamume na Mwanamke

Mambo yenye kutafautiana kutendwa katika Sala baina ya mwanamume na mwanamke:

Mosi, imependekezwa mwanamume anaporuku'i asigandishe vifundo vya mikono yake na mbavu zake, kwani Mtume s.a.w. alikuwa hagandishi vifundo vya mikono yake na mbavu zake. Mwanamke hugandisha vifundo vyake vya mikono na mbavu zake, kwani hivyo ndio stara kwake.

Pili, imependekezwa mwanamume awache nafasi (asigandishe) vifundo vyake vya mikono na mbavu zake anaposujudi. Hivi ni kwa vile Mtume s.a.w. ilikuwa akisujudi hutengesha mikono yake (mbali na mbavu zake) mpaka huonekana weupe wa kwapa zake. Mwanamke hugandisha mikono yake na mbavu zake, kwani hivyo ndio stara kwake.

Tatu, mwanamume akisujudi hutengesha tumbo lake na magoti yake. Hivi ni kwa vile Mtume s.a.w. ilikuwa akisujudi huwacha mwanya. (Imehadithiwa na Muslim r.a.). Na amehadithia Abu Daud r.a. kuwa Mtume s.a.w. alikuwa akisujudi lau kama mtoto wa mbuzi angalitaka kupenya angaliweza kupenya. Mwanamke yeye hugandisha mikono yake na sehemu yake ya tumbo, yaani hajitandazi; kwani hivyo ndio stara kwake.

Nne, mwanamume husoma kwa sauti mwahala mwa kusoma kwa sauti, mwanamke ikiwa anasalisha wanawake wenziwe au anasali peke yake na mbali na wanaume wasiokuwa mahaarim zake, hapo atasoma kwa sauti; lakini si kwa sauti (kubwa) kama mwanamume; ikiwa wapo watu wa mbali basi hatosoma kwa sauti, atasoma kimoyomoyo.

Tano, mwanamume akitaka kunabihisha kitu nae yumo kwenye Sala, kama vile kumzindua imam au kumzindua kipofu, au kama anasali nyumbani akaitwa au mtu akapiga hodi, basi atasabbih kwa sauti: mwanamke yeye atapiga ukofi. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Mwenyekuzindua kitu katika Sala yake, basi na asabbih; kwani akisabbih itazindua. Mwanamke yeye atapiga ukofi". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Na amepokea Imam Al Bukhary r.a.:

"Mwenye kunabihisha kitu kwenye Sala yake, basi naaseme, . Hivi kusabbih (kwa mwanamume) na kupiga ukofi (kwa mwanamke) kwa ajili ya kuzindua inatakikana anapofanya hivyo atie nia ya kufanya hivyo kwa sababu ya kuzindua. Na mwanamke hupiga ukofi kwa kupiga kwa tumbo la kiganja cha mkono wa kulia juu ya mgongo wa kiganja cha mkono wa kushoto. Kuzindua kwa kusabbih au kwa kupiga ukofi, inajuzu kufanya hivyo kwa mara zinazotokea dharura kufanya hivyo.

Utupu wa Mwanamume na Utupu wa Mwanamke

Utupu wa mwanamume - huru au aliemilikiwa - ni baina ya kitovu na magoti. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Na mmoja wenu akimuozesha mtumwa au mtumishi wake kijakazi chake, basi huyo kijakazi asitizame utupu wa huyo mwanamume alieozeshwa. Na utupu ni baina ya kitovu na magoti". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).

Na imehadithiwa kwamba Mtume s.a.a alimwambia Jarhad:

"Funika paja lako kwani paja ni utupu". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).

Imepokewa kuwa Mtume s.a.w. alimwambia Sayyidna 'Ali r.a.:

"Usiwachewazi paja lako wala usitizame paja, la aliehai au la maiti". (Imehadithiwa na Abu Daud na Ibnu Maajah na Al Haakim).

Kitovu na magoti si utupu japokuwa ni waajibu kufunika sehemu yake, hivi ni kwa vile kuwa kinacholazim kupatikana ili utime waajibu; nacho huwa ni waajibu.

Mwanamke huru mwili wake wote ni utupu isipokuwa uso na viganja, ikiwa yumo kwenye Sala au 'Tawafi au kwenye Ihraam. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

" Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. .........". (Al Ahzaab : 59).

Na imesemwa kuwa uso na viganja si utupu kwa hali yoyote ile, japokuwa imeharamishwa kuvitazama. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ".. , wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unao dhihirika..". (Nuur : 31).

Wamesema Wafasiri wa Qur'ani Tukufu na Ibnu 'Abbaas na Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba unao dhihirika inakusudiwa uso na viganja. Vilevile kwa qauli ya Mtume s.a.w. kumwambia Asma bint Abi Bakar r.a. alipomkuta emevaa nguo nyepesi:

"Ewe Asma, mwanamke akishabalegh si halali kuonekana isipokuwa hiki na hiki, akiashiria (s.a.w.) uso wake na viganja vyake".

Yenye Kuba'tilisha Sala

Mambo kumi na moja huba'tilisha Sala:

La Kwanza, kusema kwa kukusudia lenye kufahamika, sawa ikiwa ni kwa maslaha ya Sala, kama kusema: "usisimame", au "kaa". Au hata ikiwa lililosemwa halifahamiki, hivi ni kwa alivyoeleza Zaid bin Arqam r.a. kwamba walikuwa wakizungumza kwenye Sala mpaka walipokatazwa baada ya kuteremshwa: "na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea). (Al Baqara : 238).

Na vilevile kwa alivyopokea Ibnu Masoud: yaani hakika kwenye Sala ni shughuli (haingizwi ndani yake shughuli nyengine). Vilevile kwa qauli yake Mtume s.a.w. kwa Mu'aawiya bin Al Haakim Al Salmy wakati alipomuombea Rehma mtu aliekwenda chafya nao wamo kwenye Sala:

"Hakika ya hii Sala haijuzu ndani yake chochote cha maneno ya binaadam, hakika ya hii Sala ni kusabbih na kukabbir na kusoma Qur'ani". (Imehadithiwa na Muslim).

Ikiwa kasema kwa kusahau, au kwa kutojua kuharimishwa kwake, kwa vile kuwa ni karibuni kuingia kwenye Uislam, au maneno yakamponyoka bila ya kukusudia, au kicheko kikamzidi; hivyo Sala yake haitaba'tilika, kwani yote haya yametokea bila ya yeye kukusudia. Hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:

"Hawatahisabiwa Umma wangu katika hali tatu, kukosea, kusahu na kwa lile walilolazimishwa".(Imehadithiwa na Al 'Tibraany).

Ikiwa atazidiwa na kikohozi, au chafya haitaba'tilika Sala yake hata kama itadhihiri harufi mbili, kwani si makusudi yake. Wala asijikohoze kama vile mtu mwenye balagham, khasa kwenye Sala ya kusoma kwa sauti.

La Pili, kufanya vitendo vingi kwa mfululizo, kama vile kwenda khatuwa tatu za mfululizo au kupiga kofi. Hivi ndivyo walivyokubaliana wanazuoni, na kwa sababu vitendo hivi huvunja mpango na utaratibu wa Sala. Ama ikiwa atafanya kwa sababu na haja, kama vile kwenda khatuwa moja kisha akasita kidogo kisha akenda tena; hivi hakutaba'tilisha Sala yake. Vilevile inaruhusiwa kama vile kumzuia mtu asipite mbele yako kwa kunyoosha mkono wako mbele yake, au kuuwa kidudu chenye kudhuru kama vile nnge, nyoka au mbu. Vitendo vyote hivi vinaruhusiwa kwa udhuru na kwa uchache. Sala inatakiwa khushu'u (unyenyekevu) ya moyoni na utulivu wa viungo, utulivu wa viongo ni dalili ya khushu'u ya moyoni.

La Tatu, kutokwa na udhu, kwa kufusa, kujamba, (au hata kutokwa na tone la mkojo); hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

. "Akifusa mmoja wenu katika Sala, basi naatoke (kwenye Sala) akatie udhu kisha asali tena". (Imehadithiwa na Abu Daud).

La Nne, kupatwa na najsi (uchafu) kwenye nguo yake, au mwilini mwake au pahala anaposalia, hivi ni kwa vile 'tahara ya mwili, nguo na pahala pakusalia ni miongoni mwa shuruti za kusihi Sala. Ikiwa itamfika najsi na akaiondoa hapo hapo na ikaondoka kikamilifu bila ya kubakia laa harufu walaa rangi walaa ladha, basi Sala haitaba'tilika; ikiwa si hivyo Sala itaba'tilika. Kujichora mwili ni haraam, kwa hivyo ikiwa kajichora lazima afute michoro hiyo. Ikiwa atakhofia kwamba katika kuiondoa michoro hiyo itasababisha michuniko kufika kuwa hataweza kutia udhu kwa kutumia maji, yaani ni kwa kutayamam tu; basi atasamehewa kuiondoa katika hali hio, atasali hivyo hivyo na michoro yake na Sala yake itakubaliwa, yaani si baa'til; na atafaa hata kuwa imam akasalisha. Ikiwa amekuwa na kijaraha na kwa dharura akatia dawa ambayo inayo kitu cha najsi ndani yake, au akafunga kitata kwa kitu cha najsi, kama vile mfupa; haitamlazim kufungua, atasali hivyo hivyo na Sala yake itakubaliwa, yaani si baa'til.

La Tano, kukashifika utupu; ikiwa kukashifika huku kwa makusudi, basi Sala yake itaba'tilika. Ama ikiwa kukashifika kwa sababu ambayo si ya makusudi, kama vile nguo kupeperuka kwa upepo au kwa kuinama au kukunjika na akajistiri hapo-hapo, yaani upesi-upesi; basi Sala yake haitaba'tilika.

La Sita, Sala huba'tilika kwa kuondoa nia; kwa mfano akinuwia kutoka kwenye Sala, hivi ni kwa vile kuwa nia ni miongoni mwa nguzo za Sala, na kuendelea kubakia nia ni shuruti ya nia yenyewe. Pia Sala huba'tilika kwa kubadilisha nia, kwa mfano alinuwia kusali Sala ya adhuhuri, wakati yumo kwenye Sala akaona asali Sala ya laasiri, akanuwia kusali Sala ya laasiri, kwa kufanya hivi itaba'tilika ile ya adhuhuri na haitasihi hii ya laasiri. Ikiwa anasali peke yake Sala ya fardhi, kama vile Sala ya adhuhuri, mara ikaqimiwa Sala ya jama'a, basi anaweza kuinuwia (kubadilisha nia) Sala yake hii ya fardhi kuwa sunna (bila ya kubainisha ni sunna gani), akatoa salam baada ya raka'a ya pili kisha akajiunga na hio Sala ya jama'a ilioqimiwa/inayosaliwa. Lakini basi, katika hali hii haitajuzu kuibadilisha Sala yake ya fardhi kwa Sala ya sunna maalum, kwa mfano kunuwia kutoka kwenye Sala ya adhuhuri na kuingia kwenye Sala ya dhuhaa, hivi ni kwa sababu nia haikukamilia vifungu vyake, miongoni mwa vifungu vya nia ni kubainishwa tangu mwanzo ni Sala gani inayokusudiwa kusaliwa, hili limekosekana kwa kuwa haikunuwiwa tangu mwanzo kusaliwa Sala ya dhuhaa. Vilevile Sala huba'tilika ikiwa ataazimia kutoka kwenya Sala, hivi ni kwa vile kuondolewa kuendelea nia ambako ni sharti ya nia yenyewe. Vilevile Sala huba'tilika kwa kutia shaka (kutaradad) kuwa aikate Sala au asiikate. Ikiwa ni mtu mwenye wasi-wasi, ikamjia kuwa aikate Sala au asiikate, katika hali hii Sala yake haitaba'tilika.

La Saba, kuelekea nje ya qibla kwa sehemu ya kifua chake bila ya udhuru wenye kukubalika Kisharia; hivi ni kwa sababu kuelekea qibla ni miogoni mwa nguzo za Sala.

La Nane na Tisa, kula au/na kunywa; Sala huba'tilika kwa kula au kunywa hata kama ni kitu kidogo kabisa. Ikiwa mtu ndio kwanza kaingia kwenye Uislam au ameishi katika nchi au mitaa mbali kabisa na penye elimu, ikawa hakujua kuwa kula au kunywa kunaba'tilisha Sala, ikiwa kula au kunywa huko ni kidogo mno, basi Sala haitaba'tilika, ama kukiwa kwingi kutaba'tilisha Sala yake.

La Kumi, kujikohoza au kucheka kwa makusudi. Ikiwa atazidiwa na kikohozi au kicheko kidogo tu, hivyo havitaba'tilisha Sala, ama ikiwa makusudi au vikiwa kwa wingi, Sala itabaa'tilika.

La Kumi na Moja, kuritadi; yaani kutoka kwenye Uislam, hivi ni kwa sababu miongoni mwa nguzo za Sala ni kuwa Muislam.

Sijda ya Kusahau

Kusahu kilugha maana yake ni kusahau kitu kwa muda au kwa ghafla.

Kisharia hapa ni kusahau kitu cha Sala. Na sijda mbili, sijda ya kusahau kumeshari'ishwa ili kufidia ule upungufu uliotokea kwenye Sala kwa kusahau. Sababu za sijda ya kusahau ni, ama kwa kutenda kwa kusahau kitu ambacho hakitakiwi kutendwa kama vile kuongeza kisimamo, au ruku'i au kusujudi zaidi ya mara mbili kwenye raka'a moja, au kukaa kitako mahala si pakukaa kitako. Pia sijda ya kusahau huwa kwa kuacha kwa kusahau nguzo ya Sala, kama vile kusahau kuruku'i, au kusujudi, au kisimamo, au kusahau kusoma Alhamdu, au kusahau tashahudi (tahiyatu) ya mwisho. Sijda ya kusahau huwa kwa kukumbuka alichosahau baada ya kupita mahala pa alichokisahau nae bado yumo kwenye Sala, ndivyo hufaa kusujudi sijda ya kusahau. Ikiwa kakumbuka nae keshatoa salam, yaani hayumo tena kwenya Sala; lakini kakumbuka mara tu baada ya kutoa salam, yaani baada ya muda mdogo tu; katika hali hii, hapo-hapo atakifanya kile alichokisahau kisha atasujudi sijda ya kusahau. Hii hali ya katika muda mfupi ni sawa-sawa ikiwa kawahi kukenguka kamili mbali na qibla au kazungumza au katoka msikitini, katika hali zote hizi, madhali bado yumo katika hali ya muda mfupi; anaruhusiwa kukifanya kile alichokisahau na kisha akasujudi sijida ya kusahau. Kiasi cha kuhukumiwa kama muda mdogo au muda mrefu kuna qauli mbili, ya kwanza wanasema ni kukisiwa kwa 'ada, qauli ya pili wanasema ni muda usiozidi kiasi ya kusali raka'a moja fupi kabisa. Ikiwa kakumbuka baada ya kutoa salam baada ya muda mrefu, itamlazim aisali upya Sala yote. Haya yote ni vile ikiwa amekuwa na hakika kuwa amesahua moja miongoni mwa nguzo za Sala, ama ikiwa keshatoa salam ikamjia shaka au wasi-wasi kuwa amesahau au hakusahau nguzo ya Sala; katika hali hii haitahitaji kufanya kile anachoshaka kuwa kakiwacha walaa kusujudi sijda ya kusahau walaa kumlazim kuirejea Sala; katika hali ya shaka kama hivi Sala yake itakuwa sahihi. Ama ikimjia shaka nae bado yumo ndani ya Sala atachukua cha hakika na kutenda la asili, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Ikiwa atatia shaka mmoja wenu nae yumo kwenye Sala, asijue amesali raka'a ngapi tatu au nne - ataacha shaka na kutumia hakika, hapa lenye hakika kwake ni kuwa amezisali raka'a tatu, kwahivyo atasali raka'a moja kukamilisha raka'a nne; kisha atasujudi sijida mbili za sijda ya kusahau. Ikiwa imekuwa amesali raka'a tano itakuwa ni maombezi kwa Sala yake, ikiwa imekuwa amesali raka'a nne itakuwa ni idhlali kwa She'tani". (Imehadithiwa na Muslim).

Haya tulioyataja hapo juu, hukmu yake ni sawa-sawa juu ya imam na mwenye kusali peke yake. Ama mwenye kusali jamaa, yaani maamuma; yeye akisahau hasujudi sijda ya kusahau, sahau yake huchukuliwa na imam. Ikiwa maamuma atayaqinisha naye yuko kwenye tashahudi kuwa amesahau nguzo miongoni mwa nguzo za Sala, kama vile kusoma Alhamdu au kuruku'i ataendelea na Sala yake pamoja na imam, atapomaliza imam kutoa salam yeye atainuka na kulipa kile alichokiwacha wala hatasujudi sijida ya kusahau, sahau yake huchukuliwa na imam. Ikiwa amesahau kitu cha sunna - si nguzo - miongoni mwa sunna za Sala, kama vile akisahau kukaa tahiyatu ya mwanzo, au kusoma qunuti au kumsalia Mtume s.a.w. kwenye tashahudi; katika hali kama hizi haitatakiwa kulipa hivi alivyokuwa hakuvifanya kwa kusahu, yeye itamlazim basi kusujudi sijda mbili za sijida ya kusahau.

Dalili ya kuwa tashahudi ya awali ni sunna, ni kitendo cha Mtume s.a.w. kama ilivyohadithiwa na Abdullah bin Buhaina r.a. kwamba Mtume s.a.w.:

, yaani Mtume s.a.w. aliwacha kukaa tahiyatu ya mwanzo akasujudi kabla ya kutoa salam. Amesema Imam Ghazali r.a. kwenye kitabu kwamba: "Hayo ni katika mambo yaliowazi yenye kukhusiana na Sala. Lau kama ataacha moja ya sunna, kama vile akiwacha tashahudi ya awali na akainuka mpaka kwenye qiyam (kisimamo), au akawa yuko karibu zaidi kwenye kisimamo kuliko kwenye kitako, basi haijuzu kwenda kwenye kitako kwa ajili ya kuleta hio tashahudi ya awali alioiwacha kwa kusahau, ikiwa atakwenda kwenye kitako basi itaba'tilika Sala yake ikiwa amefanya hivyo kwa kukusudia na hali ya kujuwa kuwa imeharimishwa kufanya hivyo. Ama ikiwa amefanya hivyo kwa kusahau au kwa kutojua kukatazwa kwake, kama kwa vile yeye ni mpya kwenye Uislam, basi Sala yake haitaba'tilika, na atasujudi sijda ya kusahau. Ama ikiwa kakumbuka na yeye yupo karibu zaidi na kwenye kitako kuliko kisimamo, basi atakaa na kuleta hio tashahudi na kabla ya kutoa salam atasujudi sijda mbili za kusahau. Hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:

"Ikiwa mmoja wenu atainuka kutoka kwenye kitako (kusujudi) nae amesahu kukaa tahiyatu ya awali, ikiwa yuko karibu zaidi na hali ya kitako, basi atakaa. Ama ikiwa yuko karibu zaidi na hali ya kusimama, basi hatarejea kwa kwenda kwenye kitako, bali ataendelea kwenye kisimamo; kisha kabla ya kutoa salam atasujudu sijda mbili za sijda ya kusahau". (Imehadithiwa na Ahmad na Abu Daud na Ibnu Maajaah).

Ikiwa atasahau kusoma qunuti, akenda kwenye kusujudi moja-kwamoja, haijuzu kurejea kwenda kwenye kisimamo kwa ajili ya kusoma qunuti; kisha akaleta sijda mbili za kusahau, ikiwa atafanya hivyo makusudi na hali ya kuwa anajuwa kuharimishwa kwake, basi Sala yake itaba'tilika. Ikiwa qunuti alioiwacha ni ya Sala ya alfajiri au Sala ya taraweih. Ama ikiwa ni qunuti za Sala za yaani Sala za kuomba rehema kwa kuteremkiwa na kitisho cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama vile kupatwa juwa, au kupatwa mwezi au kuadimika mvua, hatosujudi sijda ya kusahau, sawa-sawa ikiwa kuacha huko ni kwa makusudi au si kwa makusudi. Vilevile ikiwa ameacha "haia" ya Sala, kama vile akiwacha du'a ya kuingilia kwenye Sala; au akiwacha kabla ya Alhamdu, yaani akiacha kusoma hatosujudi sijda ya kusahau, sawa-sawa kuwacha huko ikiwa ni kwa makusudi au kwa kusahau. Sijda ya kusahau, husujidiwa sijda mbili baada ya kukamilisha tashahudi (tahiyatu) na kabla ya kutoa salam, hivi ni kama ilivyopokewa kwenye Hadithi zilizotangulia kutajwa hapo juu.

 

 

 

__________________________________________________

Haki za Uchapishaji zimehifadhiwa na Mtungaji

Farouk Abdalla Al-Barwani, P.O. Box 828, Ruwi, P.C.112 Sultanate of Oman

e-mail: umojabaraka@yahoo.co.uk