mecca_1.jpgFIQHI ILIYOWEPESISHWA: SALA

Farouk Abdalla Al-Barwani

 

Nyakati Ambazo ni Karaha Kusali

Nyakati zenye kukatazwa kusali ndani yake ni tano, tatu katika hizo zinakhusiana na wakati, nazo ni:

Kwanza, linapochomoza juwa mpaka lifike juu kiasi cha urefu wa mkuki.

Pili, linapokuwa juu sawa na utosi, mpaka litenguke kidogo.

Tatu, linapopiga juwa umanjano wa kutua mpaka likamilie kutua.

Haya yametolewa dalili kwa Hadithi aliopokea Imam Muslim r.a. kutoka kwa Qubat bin 'Aamir r.a.

  "Katika nyakati tatu Mtume s.a.w. alikuwa akitukataza kusali au kuzikana, likianza jua kuchomoza mpaka liinuke, na jua linapokuwa katikati ya adhuhuri mpaka litenguke, na jua linapoinamia kutuwa mpaka lituwe kamili".

Sababu ya karaha hii ni vile kwa qauli yake Mtume s.a.w. aliposema:

"Jua linapochomoza huwa pamoja na wapambe wa She'tani, linapoinuka huliwacha; linapokuwa sawa na utosi huliambata tena, linapotenguka huliwacha; linapoingia kutuwa huliambata tena, linapokamilika kutua huliwacha". (Imehadithiwa na Imam Shafi'ii r.a.).

Wapambe wa She'tani ni wale wa qaumu yake, nao ni wale wenye kuabudu juwa, ambao husujudia juwa katika nyakati hizi zilizotajwa hapa. Na inasemekana kuwa She'tani hukaribisha kichwa chake kwenye juwa katika nyakati hizi ili iwe wale wenye kusujudia juwa wanamsujidia yeye She'tani wakati huo huo.

Ama nyakati mbili miongoni mwa nyakati tano zenye kukatazwa kusali ndani yake, hizi zina khusiana na kitendo; nazo ni:

Kwanza, baada ya Sala ya laasiri mpaka jua lituwe.

Pili, baada ya Sala ya alfajiri mpaka jua lichomoze.

Dalili ya haya ni walivyopokea Sheikhan kutoka kwa Abi Huraira r.a

"Imekatazwa (na Mtume s.a.w.) Sala baada ya laasiri (Sala ya laasiri)

mpaka juwa lituwe, na baada subhi (Sala ya asubuhi) mpaka juwa lichomoze".

Imevuliwa kutoka katika nyakati tatu zenye kukatazwa kusali, wakati linapokuwa juwa sawa na utosi; siku ya Ijumaa. Imesemwa kuvuliwa karaha kusali juwa linapokuwa utosini siku ya Ijumaa kwamba iko Hadithi juu ya suala hili; pia imesemwa sababu ni kwamba wakati huu mtu mara nyingi hushikwa na usingizi, kwahivyo akijishughulisha na Sala ni afadhali, badala ya kukaa akachukuliwa na usingizi, akatokwa na udhu ikabidi akiuke watu kwenda kutia udhu. Vilevile imevuliwa karaha ya kusali wakati juwa liko utosini ikiwa ni kwenye Bait-l-haram, yaani Msikiti wa Makka, hivi ni kwa utukufu wa pahala. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Enyi Bani Abdul Manaafi! Mwenye kutawalishwa miongoni mwenu chochote kile miongoni mwa mambo ya watu, basi asimkataze yeyote yule mwenye ku'tufu kwenye Nyumba hii na akasali saa yoyote ile, ikiwa usiku au mchana". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy na wengineo).

Ama Sala yenye sababu iliotangulia, si karaha kusali katika nyakati tano tulizozitaja hapo juu. Kama vile kulipa Sala ya fardhi iliompita au sunna ambayo inafuatana na Sala, au sunna ambayo ameijaalia mtu dasturi kuisali. Hivi ni kwamba Mtume s.a.w. alisali raka'a mbili baada ya Sala ya laasiri, akasema hizi ni raka'a mbili za sunna ya baada ya Sala ya adhuhuri. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Vilevile si karaha kusali katika nyakati tano tulizozitaja hapo juu Sala yenye sababu ilioambatana kama vile Sala ya maiti, na sujudi ya kisomo, na sujudi ya shukra, au Sala ya kupatwa mwezi, au Sala ya kupatwa juwa, au Sala ya kuomba mvua. Ama Sala zenye sababu zilioakhirika hizo ni karaha kusaliwa katika nyakati tano tulizozitaja hapo juu, kama vile Sala ya istikhara, yaani kuomba kuoneshwa lenye kheri, au raka'a mbili za ihraam.

Sala ya Jama'a

Kushari'ishwa Sala ya jama'a kumethibiti kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, qauli ya Mtume s.a.w. na itifaqi ya wanazuoni. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 "Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe………". ( Annisaai : 102 ).

Sala ya jama'a imeamrishwa hata katika vita, kwahivyo katika hali ya amani ni zaidi amri yake. Sala ya Ijuma'a ni fardhi 'aini, yaani fardhi kwa kila mtu nafsi yake. Ama kulazimika Sala ya jama'a kuna qauli tafauti, qauli yenye kutegemewa, yaani qauli sahihi ni kwamba Sala ya jama'a ni sunna yenye kutiliwa nguvu . Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w

   "Sala ya jama'a ni afadhali kuliko Sala ya mtu peke yake kwa daraja ishirini na saba". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Hii qauli ya Mtume s.a.w. ya kufadhilishwa Sala ya jama'a zaidi ya Sala ya mtu peke yake ni dalili ya kujuzu hali mbili, yaani ya jama'a na ya mtu peke yake. Ingalikuwa ni hali moja tu ndio yenye kujuzu, isingaliletwa hivi kufadhilishwa; kufadhilishwa huwa penye zaidi ya hali moja. Na wamesema baadhi ya wanazuoni kwamba Sala ya jama'a ni fardhi kifaya. Fardhi kifaya ni ile ambayo wakifanya baadhi huanguka faradhia yake juu ya wengine, na wakiwacha kufanya wote hupata iqabu wote. Kama vile yale yote yenye kulazim kufanyiwa maiti.

Wanazuoni wenye kusema kuwa Sala ya jama'a ni fardhi kifaya wanatoa dalili kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Hawawi watu watatu, ikiwa mtaani au jangwani wasisimamishe Sala isipokuwa hutawaliwa na She'tani, basi dumisheni Sala ya jama'a kwani mbwa mwitu humla yule mbuzi alioko mbali na wenziwe". (Imehadithiwa na Abu Daud na Ahmad na Al Nissaai na Ibnu Hibbaan na Al Haakim).

Na wanazuoni wengine wamesema kuwa Sala ya jama'a ni fardhi 'ain, yaani ni fardhi kwa kila mtu juu yake mwenyewe. Wao wametolea dalili qauli ya Mtume s.a.w.:

  "Nilitaka niamrishe iqimiwe Sala kisha nimuamrishe mtu asalishe, kisha nitoke pamoja na watu na mizigo ya kuni kupita kwenye nyumba za watu waliokuwa hawakwenda kusali jama'a nizichome moto nyumba zao na wao wamo humo". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Imepokewa kwamba haya yalikuwa yanakhusiana na munaafiqiina, na Mtume s.a.w. hakuwachomea moto nyumba zao, basi ilikuwa ni kutaka kufanya hivyo.

Ikiwa mtu atakuta Imam yuko kwenye ruku'i na akajuwa kuwa akifuata jama'a hii atawahi raka'a (japo moja) katika wakati wa Sala, (kwa hivyo Sala yake itakuwa kaisali ndani ya wakati) basi atafuata jama'a hii. Na kufuata jama'a huwa ni haram, ikiwa atakuta Imam yuko kwenye tahiyatu ya mwisho na akajuwa kuwa akifuata jama'a hii hatawahi raka'a katika wakati wa Sala, (kwa hivyo Sala yake haitakuwa kaisali ndani ya wakati) katika hali hii hafuati jama'a, atasali peke yake ili awahi kuisali Sala yake ndani ya wakati.

Sala ya jama'a hupatikana hata mtu akisali nyumbani kwake na mkewe au na watu wake wa nyumbani, lakini jama'a ya msikitini ni afadhali; na kila jama'a ikiwa kubwa kwenye msikiti ni afadhali zaidi. Ikiwa msikiti wa karibu nae jama'a yake ni ndogo, na mbali nae una jama'a kubwa basi atakwenda kwenye ule wenye jama'a kubwa; isipokuwa kwa sababu mbili - ikiwa kwa kuuwacha msikiti wa karibu nae, jama'a ita'a'tilika, au ikiwa Imam wa huo msikiti wa mbali ana ila ya Kisharia yenye kujuulikana; basi atasali kwenye msikiti wake wa karibu japo kuwa jama'a ya msikiti huo ni ndogo.

Mwenye kumuwahi Imam kabla hajatoa salam, basi atapata fadhila ya jama'a, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:  

"Akija mmoja wenu kwenye Sala na sisi tumo kwenye sujudi, basi naasujudi na sisi wala asiirejee; mwenye kuwahi (kumuwahi Imam kwenye) ruku'i basi ameiwahi (ameipata) raka'a". Kuipata raka'a kwa kumuwahi Imam kwenye ruku'i ni uruku'i na ipatikane kutulia kwenye ruku'i kwa muda wa kiasi cha kuwahi kusema:  ikiwa si hivi hatakuwa kaipata raka'a.

Shuruti ya kuipata jama'a ni kunuia kuwa unamfuata Imam pamoja na kuleta takbbiir ya kuingia kwenye Sala  Inajuzu mtu mzima, huru kumfuata Imam mtoto au sio huru. Dalili ya kujuzu huru kusalishwa na aliekuwa sio huru ni kwa Hadithi ya Imam Al Bukhary r.a. kwamba Sayyidah 'Aisha r.a. alisalishwa na mtumwa wake mwanamume. Dalili ya kujuzu kusalishwa na mtoto ni Hadithi iliopokewa kwamba 'Aamri bin Salamah r.a. alikuwa anasalisha watu wake na yeye umri wake ni miaka sita au saba. (Imehadithiwa na Bukhary).

Haisihi mwanamume kusalishwa na mwanamke, hivi ni kutokana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  "Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, ……." (Annisaai : 34).

Na amesema Mtume s.a.w.:

  "Msiwatangulize wanawake kwa vile alivyokuwa hakuwatanguliza Mwenyezi Mungu Mtukufu". Na kwa Hadithi ya Mtume s.a.w.:

   "Tambueni, mwanamke asiwe Imam wa wanaume". (Imehadithiwa na Ibnu Maajah).

Hivi ni kwa sababu mwanamke maumbile yake ni wasitara, na kuwa mbele ya wanaume akiwa ni Imam (mkuu) ni sababu za fitna; na kusalisha ni kuchukuwa dhamana, ni kutawalia dhima na jukumu la anaowasalisha.

Kukhusu suala la kusalishwa na mtu mwenye kusoma vyema Qur'ani na mtu ambae hakuhifadhi Qur'ani, kuna qauli mbili; yenye nguvu ni ile kuwa haisihi, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:    "Asalishe qaumu yule mbora wao wa kusoma (Qur'ani)".

Kwa vile Imam ndie mwenye kuchukua dhima na jukumu la Sala za maamuma wake, hata kama ataingia mtu na kuunga Sala na Imam yuko kwenye ruku'i basi yeye Imam huchukua dhima ya Sala ya maamuma huyo, asiehifadhi Qur'ani hatofaa kuchukua dhima ya Sala za wenziwe. Asio hifadhi Qur'ani anaweza kusalisha Sala za kimyakimya, yaani zile ambazo hazisomwi kwa sauti na haitalazim kumchungua. Asiohifadhi Qur'ani inajuzu kumsalisha asiohifadhi Qur'an, kama vile inavyojuzu mwanamke kumsalisha mwanamke mwenziwe.

Shuruti za kusihi kumfuata Imam ni kuijua Sala ya Imam, ama kwa kuwa unamuona yeye Imam, au kwa kumsikia sauti yake, au sauti ya mubaligh. Vilevile haijuzu maamuma kumtangulia Imam, maamuma daima awe nyuma ya Imam kwa qauli na kwa vitendo. Ama kwenye Al Ka'aba, wale wenye kuizunguka Al Ka'aba inajuzu kuwa karibu zaidi na qibla kuliko Imam, lakini wale ambao hawaizunguki Al Ka'aba haijuzu wao kuwa karibu zaidi na qibla kuliko Imam.

Sala ya Jama'a inaweza kuwa katika Hali Tatu

Ya Kwanza, Imam na maamuma wote wamo msikitini. Katika hali hii jama'a husihi hata kama safu zitakuwa hazikuungana au hata kama kuna kizuizi baina ya Imam na maamuma, au hata kama Imam yuko juu ya membari ya msikiti na maamuma wako chini, muhim wote wamo kwenye jengo la msikiti.

Ya Pili, Imam yumo ndani ya msikiti na maamuma wako nje ya msikiti. Katika hali hii jama'a husihi ikiwa masafa baina ya Imam na maamuma hayazidi dhira'a mia tatu takriban kuanzia mwisho wa msikiti mpaka alipo maamuma. Hivi ni kwa sharti kuwa maamuma atazijua harakati zote za Imam, za kisoma na za vitendo; kama vile, akisoma Alhamdu, akisoma Sura, akiruku'i, akisujudi, wakati akiwa kwenye tashahudi na nyenginezo, zote hizi maamuma azijuwe kwa ukamilifu.

Ya Tatu, Imam na maamuma wote wako nje ya msikiti. Katika hali hii, ikiwa Sala inasaliwa uwanjani - nje ya jengo - jama'a husihi ikiwa masafa baina ya Imam na maamuma hayazidi dhira'a mia tatu takriban. Masafa haya inakisiwa ya maamuma kuweza kumsikia Imam katika pahali palipo pawazi, kama vile uwanjani, uwandani na kadhaalika. Ama ikiwa Sala inasaliwa kwa hali ya kuwa Imam yumo ndani ya jengo jingine na maamuma wamo kwenye jengo jingine, katika hali hii jama'a husihi kwa sharti ikiwa itakuwepo itisali (mawasiliano) ya kuendelea yanayouganisha baina ya Imam na maamuma na kutokuwepo kizuizi baina ya Imam na maamuma. Kwa hivi kuwa Imam na maamuma wamo kwenye majengo mbali mbali uwezekano wa kukosekana mawasiliano ya kuendelea wakati wa Sala na kuwepo kizuizi baina ya Imam na maamuma, hivyo ndivyo imewekwa shuruti hizi.

Vilevile kusihi jama'a ni kutotafautiana mfumo wa Sala, kwa mfano Sala ya dasturi na Sala ya maiti. Lakini inasihi jama'a ikiwa Imam anasali Sala ya wakati na maamuma akasali Sala ya kulipa au/na kinyume chake, au Imam anasali fardhi na maamuma akasali sunna, au/na kinyume chake. Au Imam anasali adhuhuri na maamuma anasali laasiri, na kinyume chake. Au Imam anasali Sala ya alfajiri (anailipa wakati wa adhuhuri), maamuma ikasali nae Sala ya adhuhuri, akimaliza Imam kutoa salam maamuma atainuka na kukamilisha Sala yake. Hivi ni kwa vile Sala zote hizi mfumo wake wa kusali ni mmoja, tafauti na Sala ya maiti.

Vilevile shuruti ya kusihi jama'a maamuma asimtangulie Imam kwa takbbiir ya ihraam, yaani  na asimtangulie kwa nguzo ya kisomo wala ya kitendo; wala asiakhirike nae kwa nguzo mbili za vitendo bila ya udhuru. Akiwa atafanya hivi na hali anajuwa kuharimishwa kufanya hivi, basi Sala yake itaba'tilika; itamlazim aisali upya. Ama ikiwa atamkhalif Imam wake kama hivyo tulivyosema hapo juu na hali ya kuwa hajui kuharimishwa hivyo au amesahau kumfuata Imam wake, Sala yake haitaba'tilika lakini hii raka'a haitahisabiwa; kwahivyo itamlazim airejee kuisali raka'a hii baada ya Imam kutoa salam.

Kwenye Sala ya jama'a ni sunna maamuma awe nyuma kidogo ya Imam; asisimame nae bega kwa bega. Maamuma atasimama mkono wa kulia wa Imam nyuma yake kidogo, akija mtu mwengine atafunga Sala nyuma ya Imam. Hapa tena ama Imam atasogea mbele kiyasi ya khatuwa au maamuma alioko mkono wa kulia atarejea nyuma kiyasi ya khatuwa na kufanya mstari mmoja nyuma ya Imam pamoja na huyu aliejiumga hivi baadae nyuma ya Imam. Akija mtu mwengine (maamuma wa tatu) kuingia kwenye Sala atasimama mkono wa kulia wa maamuma (wawili) mwenziwe, akija mwengine (maamuma wa nne) atasimama mkono wa kushoto na hivyo hivyo. Kwenye Sala ya jama'a hupangika mstari kwa kusimama watu-wazima wanaume, kisha watoto wanaume, kisha nyuma yao husimama khuntha, kwa uwezekano wa kuwemo kwenye uwanauke, kisha nyuma kabisa husimama wanawake.

Kwenye jama'a ya wanawake kwa wanawake, sunna Imam asimame katikati ya maamuma wake. Ikiwa wanawake wanasalishwa na mwanamume, basi Imam atasimama mbele. Ni karaha maamuma kusimama peke yake kwenye safu, kwahivyo ataingia kwenye mstari, ikiwa hamna nafasi atamuashiria kwa kumvuta kwa utaratibu alioko kwenye safu ili asimame na yeye. Ni sunna kwa yule anaeashiriwa kurejea nyuma na kuungana na mwenziwe ili asiwepeke yake, amsaidie mwenziwe kwa kurejea polepole na kusimama kwenye safu yao mpya.

Inajuzu mtu alietie udhu kwa kutawadha - kutumia maji - kusalishwa na mtu alietayamam ambae kwa tayamam yake hio halazimiki kulipa Sala yake, au kusalishwa na mtu aliomo kwenye ruhusa ya kuvaa khuffu mbili. Vilevile inasihi jama'a ya Imam kakaa na maamuma wamesimama. Mtume s.a.w. katika maradhi yake alisalisha nae amekaa kitako na Sayyidna Abu Bakar na Masahaba wengine r.a. wamesimama nyuma yake s.a.w. Vilevile inajuzu mtu mwema kusalishwa na mtu muovu, wamesimulia Al Sheikhan kuwa Ibnu 'Umar r.a. alikuwa akisali nyuma ya Hajaj ambae akijuulikana kwa uovu wake hata Imam Shafi'ii r.a. akautaja uovu wa Hajaj.

Kufupisha Sala za Raka'a Nne

Kusafari aghalab yake ni njia ya kuepuka maovu au kutafuta mema. Na safari aghlab yake ina mashaka, kutokana na hivi, Muweka Sharia - Nmwenyezi Mungu Mtukufu. - amejaalia njia ya kupunguza mashaka ya safari, akajaalia kufupisha katika Sala za raka'a nne kusaliwa raka'a mbili wakati wa safari. Kufupisha huku kumekuja kwa Qauli yake Mola wetu Mlezi na qauli ya Mtume s.a.w. na itifaqi ya wanazuoni. Kufupisha huku kumeruhusiwa kwa sharti kuwa ni katika safari ya halali na ndefu, si katika safari ya ma'asi wala safari fupi.

Ametwambia Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na mnapo safiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha Sala, iwapo mnachelea wasije wale walio kufuru wakakuleteeni maudhi…..". (Annisai : 101).

Hivi kuambatishwa (kutiwa sharti) na kuwemo kwenye hali ya khofu hakutumiki katika hukmu ya kufupisha Sala. Imepokewa kutoka kwa Bwana Ya'ali bin Umayah r.a. kuwa alimwambia Sayyidna 'Umar r.a. kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "iwapo mnachelea wasije wale walio kufuru wakakuleteeni maudhi". Akasema Sayyidna 'Umar r.a. kuwa na yeye pia lilimshughulisha hili na akamtajia Mtume  s.a.w., akasema s.a.w.:   "Ni sadaqa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenu, basi ipokeeni sadaqa Yake".

Na amesema Ibnu Masoud r.a.:

"Nimesali na Mtume s.a.w. raka'a mbili mbili, (na nimesali) na pamoja na Abi Bakar r.a. raka'a mbili, (na nimesali) na pamoja na 'Umar r.a. raka'a mbili". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Na imehadithiwa na Ibnu 'Umar r.a. kuwa alisafiri na Mtume  s.a.w. na Abi Bakar r.a. na 'Umar r.a. na wakawa wanasali Sala ya adhuhuri na Sala ya laasiri raka'a mbili mbili.

Kufupisha Sala hairuhusiwi isipokuwa kwa Sala za raka'a nne nne, nazo ni, Sala ya adhuhuri, Sala ya laasiri na Sala ya 'ishaa. Ama Sala ya alfajiri na Sala ya magharibi hata katika safari husaliwa kaamili, yaani raka'a mbili Sala ya alfajiri na raka'a tatu Sala ya magharibi.

Shuruti za Safari

Inashurutishwa kwa safari yenye kujuzu kufupisha Sala:

Kwanza, isiwe safari ya ma'asi; kwa hivyo hukubalika safari ya kutekeleza waajibu, kama vile kwenda kuhiji, kwenda kulipa deni, na ya mfano wake. Pia inaingia safari ya kwenda kutekeleza sunna, kama vile kwenda kufanya hija ya sunna, yaani kwa mtu aliekwisha hiji ya fardhi, au kwenda kufanya 'Umra. Pia inaingia safari ya kwenda kuwaona wazee, pia huingia safari ya kwenda kutekeleza jambo la mubah, kama vile kwenda kufanya biashara; pia huingia safari yenye sababu yenye kukirihishwa kisharia, kama vile kusafiri kwa kujitenga na rafiki. Ama safari yenye ma'asi ndani yake, kama vile safari ya ujambazi; biashara ya haraam, kama vile kuuza/kununua ulevi, madawa ya kulevya na ya mfano wake, katika hali hizi haijuzu Sala ya safari. Vilevile safari ya mwanamke bila ya ruhusa ya mumewe, safari ya mwenye kudaiwa na hali anao uwezo wa kulipa, akasafiri bila ya ruhusa ya anaemdai. Wote hawa na wa mfano wao kwa vile safari zao ni za ma'asi, basi hawaruhusiwi kufupisha Sala, vile vile hawaruhusiwi kuchanganya Sala, wala hawaruhusiwi kusali sunna juu ya kipando, wala hawaruhusiwi kupangusa juu ya khuffu mbili, wala hawaruhusiwi kula maiti (mzoga) kwa dharura; yote haya kwa sababu safari yao msingi wake ni haraam. Amesema Sufiyan Al Thauriy r.a. lau akikutikana dhaalim porini au jangwani (peke yake) hana maji wala chakula, basi hapewi maji wala chakula; kwani akifa itastarehe miji, na watastarehe binaadam na miti na wanyama pia watastarehe kwa kufa huyo dhaalim.

Pili, iwe ni safari ndefu; na safari ndefu nyenye kukubalika ni isiyopungua mwendo wa miguu wa siku mbili kwa mwendo wa kawaida, hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:

  "Haifupishwi Sala ikiwa ni safari ya chini ya burudi nne - baina ya Makka na 'Asfaan". 'Asfaan ni mwendo wa miguu wa siku mbili kutoka Makka, kwa kipimo cha kilomita (km) ni km 84. Na inampasa msafiri kubainisha sababu ya safari yake, haitoshi kutia nia ya kusafiri tu; bila ya kubainisha sababu ya safari; hata ikiwa safari yake ni ndefu.

Tatu, iwe Sala ya rakaá nne - adhuhuri, laasiri, au Sala ya ‘íshaa, iwe anaisali katika wakati wake; si Sala ya/za kulipa. Ikiwa ni Sala ya/za kulipa itakuwa katika hali nne kama hivi:

Ya Kwanza, ikiwa Sala itampita wakati yumo safarini, na ikawa anailipa nae bado yumo safarini; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya msafiri, yaani atafupisha.

Ya Pili, ikiwa Sala ilimpita wakati hayumo safarini, yaani muqim; kisha ikawa anailipa wakati yumo safarini, yaani msafiri; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya muqim, yaani hatafupisha; kwani hivyo ndivyo asili ya hukmu juu yake.

Ya Tatu, ikiwa Sala itampita wakati yumo safarini, kisha ikawa anailipa wakati hayumo safarini; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya muqim, yaani hatafupisha, kwani hivyo ndivyo asili ya hukmu juu yake.

Ya Nne, ikiwa itamjia shaka, kuwa Sala ilimpita wakati ni muqim au msafiri; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya muqim, yaani hatafupisha; kwani hivyo ndivyo asili ya hukmu juu yake.

Shuruti za Kufupisha Sala

Shuruti za kufupisha Sala ni tano:

Kwanza, kutia nia kuwa anasali Sala ya safari na kubainisha sababu ya safari yake katika huku kutia nia, asipotia nia ya kusali Sala ya safari itafunganika takbiira yake ya kuingia kwenye Sala kuwa ni Sala ya kawaida, kwani hivyo ndivyo asili ya Sala.

Pili, iwe tangu awali ya Sala mpaka mwisho wa Sala inaendelea juu yake shuruti za kujuzu kusali Sala ya safari. Hivi ni kama ilivyokuja kwenye hii Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuainisha kuwemo kwenye safari  kwahivyo isiekuwemo kwenye safari hatofupisha Sala.

Tatu, kujua kujuzu msafiri kufupisha Sala, asiejuwa kujuzu msafiri kufupisha Sala haitajuzu kwake kufupisha. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:   "……. Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.". (Annahal : 43).

Nne, asimfuate mwenye kusali Sala kaamili, au kutimiza Sala yake; akiwafata hawa atatimiza Sala yake pamoja na Imam kwani haifai kumuwacha Imam na weye umo ndani ya Sala. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. alipoulizwa na Ibnu 'Abbaas r.a.: "Nini inakuwa kwa msafiri anaposali raka'a mbili (yaani kafupisha Sala), anaposali peke yake; na akasali raka'a nne akimfuata mwenye kusali Sala ya muqim? Akasema s.a.w. kujibu:  Đáß ÇáÓäÉ  hio ni sunna”. (Imehadithiwa na Ahmad).

Tano, iwe ni Sala ya raka'a nne, yaani iwe ni Sala ya adhuhuri au Sala ya laasiri au Sala ya 'ishaa; kwani hakuna kufupisha Sala kwa Sala ya alfajiri walaa Sala ya magharibi.

Lini Msafiri Anafupisha Sala

Msafiri hajuziwi kufupisha Sala mpaka atoke kwenye majengo ya mji alioondokea. Amesema Ibnu Al Mundhir: "Sijui kwamba Mtume  s.a.w. amepata kufupisha Sala katika safari zake ila baada ya kutoka nje ya mji. Na hufupisha Sala muda anaokuwa kwenye safari, akitua kwa kungojea kutekeleza haja yoyote ile, huendelea kufupisha Sala kwa muda wa siku nne, akiendelea kuwepo hapo baada hizo siku nne na ikiwa hio haja imekwisha au haijesha, husali Sala ya muqim, yaani Sala kaamili bila ya kufupisha. Imethibiti kwa ilivyopokewa kwamba Mtume s.a.w.:

"(Mtume s.a.w.) aliingia Makka taarikh nne ya mfunguo tatu, akakaa hapo hio taarikh nne, na taarikh tano, na taarikh sita na taarikh saba, na akasali alfajiri ya taarikh nane kisha akenda Mina". Mtume s.a.w. alipokaa hapo Makka siku nne alifupisha Sala, na hivi kuazimia kwake s.a.w. kukaa hapo Makka kwa muda maalum katika kutekeleza vitendo vya Hija, ni dalili kwamba mwenye kuazimia kukaa mahala kwa muda maalum (nje ya kwake) wakati yumo safarini, atafupisha Sala zake kwa siku nne, baada ya hapo atasali Sala ya muqim. Hivi ni kufuata alivyofanya Mtume s.a.w. Kwa qauli ya Imam Shafi'ii r.a. kwamba msafiri anaruhusiwa kufupisha Sala zake kwa muda wa siku kumi na tisa au siku kumi na nane, hivi ni kutokana na alivyopokea Imam Bukhary r.a. kutoka kwa Ibni 'Abbaas r.a.:

"Mtume s.a.w. amekaa kwenye baadhi ya safari zake muda wa siku kumi na tisa anasali raka'a mbili, yaani anafupisha Sala; na sisi tukikaa (nje ya kwetu) muda wa siku kumi na tisa tunasali raka'a mbili, yaani tunafupisha Sala; na tukikaa zaidi ya muda huo, tunasali Sala ya muqim".

Na imepokewa vilevile kwamba:

"Mtume s.a.w. alikaa Makka muda wa siku kumi na nane baada ya Ufunguzi wa Makka, kwani alitaka kuifungua Hunaina, lakini haikuwa; baada ya hapo akawa anasali Sala za muqim, yaani bila ya kufupisha".

Kuchanganya Sala Mbili

Inajuzu kwa msafiri kuchanganya Sala ya adhuhuri na laasiri na kuchanganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa kwa kutanguliza na kuzisali katika wakati wa Sala ya mwanzo. Kuchanganya namna hivi kunaitwa:

  (jam'u taqdiim), yaani kuchanganya kwa kutanguliza. Na inajuzu vilevile kuchanganya Sala ya adhuhuri na Sala ya laasiri na inajuzu vilevile kuchanganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa kwa kuakhirisha na  kuzisali katika wakati wa Sala ya pili. Kuchanganya namna hivi kunaitwa : "  (jam'u taakhiir), yaani kuchanganya kwa kuakhirisha.

Dalili ya kujuzu hivi ni vile alivyoeleza Mu'adh bin Jabal r.a.:

"Tulikuwa pamoja na Mtume s.a.w. kwenye vita vya Tabuk, akawa s.a.w. anachanganya kusali Sala ya adhuhuri pamoja na Sala ya laasiri, na anasali Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa, akapumzika; kisha akatusalisha Sala ya adhuhuri na Sala ya laasiri zote pamoja, akapumzika, kisha akatusalisha Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa zote pamoja".

Kwa ilivyoelezwa ni kwamba hivi vyote ilikuwa ni kusali  (jam'u taqdiim), yaani kuchanganya kwa kutanguliza. Hivi kusali jam'u taqdiim kuna shuruti tatu:

Ya Kwanza, kusali Sala ya mwanzo, kwa mfano kuchanganya Sala ya adhuhuri na Sala ya laasiri; ukifika wakati wa Sala ya adhuhuri, ataadhini, ataqim; atasali Sala ya adhuhuri raka'a mbili atatoa salam, atainuka kwa kusali Sala ya laasiri, ataqim (bila ya adhana), atasali Sala ya laasiri raka'a mbili; atatoa salam. Kuchanaganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa; ukifika wakati wa Sala ya magharibi, ataadhini, ataqim; atasali Sala ya magharibi bila kufupisha, yaani rakaa tatu, atatoa salam, atainuka kwa kusali Sala ya íshaa, ataqim (bila ya adhana), atasali Sala ya 'ishaa rakaa; mbili atatoa salam.

Ya Pili, kutia nia (moyoni) tangu awali ya kuingia kwenye Sala ya mwanzo (adhuhuri), kuwa anasali Sala ya adhuhuri pamoja na Sala ya laasiri. Atasali kila moja mbali mbali, yaani kila moja ataisali kwa iqama yake, nia yake na takbiir yake. Ataadhini mwanzo, mara moja tu; kuqim ndio ataqim kwa kila Sala.

Ya Tatu, mfululizo baina ya Sala ya mwanzo na Sala ya pili, yaani akishasali Sala ya adhuhuri hapo hapo atainuka kwa kusali Sala ya laasiri, ataqim (hatoadhini) atasali Sala ya laasiri. Na kwa kuchanganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa ni vile vile, akimaliza kusali Sala ya magharibi hapo hapo atainuka kwa kusali Sala ya íshaa, ataqim (bila ya adhana) atasali Sala ya 'ishaa. Imethibiti ya kwamba Mtume s.a.w. alipokuwa Namra alisali Sala ya safari, akachanganya baina ya adhuhuri na laasiri na akaamrisha iqama baina ya Sala mbili hizo, yaani imeqimiwa kwa Sala ya adhuhuri kumaliza kusali Sala ya adhuhuri, ikaqimiwa kwa Sala ya laasiri.

Vilevile kwa  (jam'u taakhiir), kuchanganya kwa kuakhirisha; anatakiwa atie nia ndani ya wakati wa Sala ya adhuhuri kuwa anaakhirisha kusali Sala ya adhuhuri na ataisali pamoja na Sala ya laasiri katika wakati wa Sala ya laasiri. Katika hali hii, inajuzu kusali kwanza Sala ya adhuhuri kisha akasali Sala ya laasiri, au akasali kwanza Sala ya laasiri kisha akasali Sala ya adhuhuri. Muhim ahakikishe kuwa wakati wa Sala ya laasiri haumpiti. Hivi hivi ndivyo atavyofanya kwa kuakhirisha Sala ya magharibi na kuisali pamoja na Sala ya 'ishaa, katika wakati wa Sala ya íshaa. Inajuzu kwa muqim, yaani si msafiri kwa sababu ya mvua kuchanganya Sala, kwa kusali Sala ya adhuhuri - raka'a nne na Sala ya laasiri - raka'a nne wakati wa Sala ya adhuhuri, na akachanganya kwa kusali Sala ya magharibi - raka'a tatu na Sala ya 'ishaa - raka'a nne wakati wa Sala ya magharibi. Hivi ni kwa alivyo hadithia Imam Al Bukhary na Muslim r.a. kutoka kwa Ibni ‘Abbaas r.a. kwamba Mtume s.a.w.:

"(Mtume s.a.w.) alisali nae yuko Madina raka'a nane na raka'a saba zote pamoja, yaani alisali Sala ya adhuhuri rakaá nne na  akasali Sala ya laasiri raka'a nne, wakati wa Sala ya adhuhuri; na akasali Sala ya magharibi raka'a tatu na akasali Sala ya ‘ishaa raka'a nne, wakati wa Sala ya magharibi". Hivi kuchanganya Sala katika hali hizi, haiwi kuzisali kwa kufupisha Sala, kwa sababu si Sala ya safari, ni Sala ya muqim; lakini imeruhusiwa kuchanganya kwa sababu ya mashaka yaliopo kwa ile hali ya kuendelea kunyesha mvua katika wakati wa Sala hizi. Na katika upokezi wa Imam Muslim r.a. amesema:  yaani bila ya khofu wala safari. Hii ni dalili kuchanganya huku kunajuzu bila ya sababu ya khofu au safari. Miongoni mwa shuruti za kujuzu kuchanganya hivi ni kama vile zilivyo kwenye Sala ya  (jam'u taqdiim), yaani kuchanganya kwa kutanguliza. Vilevile miongoni mwa shuruti zake ni kuendelea kuwepo hio sababu - kunyesha mvua - tangu awali ya Sala ya mwanzo na awali ya Sala ya pili. Vilevile iwe hizi Sala zinasaliwa kwenye mahala ambapo mtu akienda kufuatia kusali atarowa kwa mvua inayonyesha.

Na wamesema wanazuoni miongoni mwao as-haabu Imam Shafi'ii r.a. na wengineo kujuzu kuchanganya Sala kwa sababu ya ugonjwa. Na imesemwa kwamba Mtume s.a.w. amefanya hivyo, yaani amechanganya Sala kwa sababu ya ugonjwa.

Kulipa Sala

Kuwacha Sala, kwa 'udhru au bila ya 'udhru. Mwenye kuwacha Sala bila ya 'udhru huwa amemuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu na ameingia kwenye madhambi makubwa,  inampasa atubie upesi na azilipe Sala alizoziwacha. Kufanya hivyo, yaani kuzilipa kwa haraka hizo Sala alizoziwacha ni waajibu wake; asipofanya ni waajibu wa Mkuu wa Nchi kumpiga vita, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

"Nimeamrishwa niwapige vita watu mpaka waseme: "Hapa Mola anaefaa kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Yeye Mwenyezi Mungu, na wasimamishe Sala, na watoe Zaka na wende kuhiji - Makka, na wafunge Ramadhani, mwenye kufanya hivyo imehifadhika damu yake na mali yake, isipokuwa kwa haqi yake Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu". Kwa hivyo basi, mwenye kuacha Sala akitubu na akitekeleza inatuwajibikia kumuwachilia, hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

  "... Lakini wakitubu, wakashika Sala, na wakatoa Zaka, basi waachilieni....". (Tawba:5).

Ikiwa kuwacha Sala ni kwa 'udhru wa kulala au kusahau, huwa hana kosa juu ya hili; itamlazim kuilipa kwa taratibu. Na imesemwa kuwa huzisali kuwa zimo kwenye wakati wake, yaani wakati wake ni pale ulipoondoka huo 'udhru, ikiwa kulala au kusahau. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

 "Mwenye kulala au akasahau ikampita Sala, basi wakati wa Sala hio ni pale atapokumbuka".

Imesuniwa azipange katika kuzisali, baina ya Sala zilizompita na baina ya Sala iliompita na ile Sala ya wakati wake ambayo wakati wake haujaanza kuwa dhiki, kukaribia kutoka; asikose japo raka'a moja katika wakati. Ikiwa ataingia kulipa Sala iliompita, katika Sala akatambua kuwa akikamilisha kuilipa hii Sala iliompita hatopata katika Sala ya wakati hata raka'a moja, hapo ataikatiza hii Sala anayoilipa au atainuia kuwa ni sunna ili akimbilie kusali Sala ya wakati, hivi ili isije na hii ya wakati ikampita pia.

 

 

 

__________________________________________________

© Haki za Uchapishaji zimehifadhiwa na Mtungaji

Farouk Abdalla Al-Barwani, P.O. Box 828, Ruwi, P.C.112 Sultanate of Oman

e-mail: umojabaraka@yahoo.co.uk