mecca_1.jpgFIQHI ILIYOWEPESISHWA: UTANGULIZI

Farouk Abdalla Al-Barwani

 

UTANGULIZI
(Imam Shafi'ii r.a.)

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuongoza kwa haya, na lau kuwa si kuongozwa na Yeye s.w.t. basi tusingalipata uwongofu. Na ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba hakuna Mola anaejuzu kuabudiwa isipokuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, wala hana mshirika Nae. Ufalme wote ni wake Yeye na kuhimidiwa kote kunastahiki kwake Yeye. Na Yeye ni muweza wa kila kitu; na ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba Sayyidna Muhammad s.a.w. ni Mtumwa na Mjumbe wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni kipenzi na mteule wake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amempeleka Mtume wake s.a.w. Rehma kwa walimwengu, na nuru na mwongozo kwa wenye kuemewa. Rehma na amani zimshukie yeye Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na Ahli zake na Masahaba zake r.a., nuru za uwongofu, na chemchem za rehma, na shina la Waumini wa kweli. Ama baada ya haya, hakika kujishughulisha katika mambo ya elimu ni alama ya kufanikiwa duniani na Akhera na ni dalili za heshima, khasa ikiwa elimu hio itakufikisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ukapokelewa kwa ridhaa Zake, na ikawa kinga baina yako na ghadhabu Zake s.w.t., na ukaepukana na adhabu kali za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hakika katika tukufu mno ya elimu na yenye daraja kubwa zaidi, na yenye kunufaisha zaidi, na yenye wingi wa baraka; ni elimu ya Fiqhi na hukumu zake. Hivyo kwa sababu kutokana na elimu ya Fiqhi ndio hujuulikana na kutambulikana baina ya halali na haramu, na baina ya uwovu na wema, na baina ya mwema na muwovu, na baina ya ibada iliyokamilika na ile iliyofisidika, pia kwa elimu ya Fiqh hujuulikana baina ya mu'amala (vitendo) uliyotengenea na ule uliyoharibika, kwa hivyo, kwa elimu ya Fiqhi utaweza kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ujuzi na hakika. Na kwa elimu ya Fiqhi utaweza kujikurubisha kwa Mola wako Mlezi katika hali ya kujua na kufahamu, na utaweza kuishi na kuingiliana na watu kwa njia ya uwongofu, utaweza kutendeana nao vile unavyopenda wewe utendewe. Ukishafika katika kiwango hiki cha ilimu na fahamu, basi moyo wako utatua juu ya vitendo vyako, na wema wa ibada zako; na hapo nafsi yako itastarehe na itasalimika kwa vile kuwa mbali na maafa ya ujinga na wasiwasi wa mashe'tani, na katika hali hii utaweza kufuata mwenendo wa watu wema miongoni mwa Mitume a.s.w. na 'Siddiqiina, na Shuhadaai r.a. na watu wema kwa jumla. Na utambue kuwa Maimam wote - Mwenyezi Mungu Mtukufu awe radhi juu yao wamo katika uwongofu na kheri, kwani wao wote ni wenye kushikamana na Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa yale aliyokuja nayo; na sisi hatubaguwi wala kutengua yeyote baina ya Maimam hao watukufu. Mwenyewe Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa hikma na uadilifu wake amewafadhilisha baadhi yao zaidi ya baadhi yao, kama vile alivyo wafadhilisha baadhi ya Mitume a.s.w. zaidi ya baadhi yao. Na sisi, kwa vile ni wenye kutafuta ukweli na faida; ni waajibu wetu kuchukua kila zuri na jema mno zaidi, hivi ili tuweze kupata faida zaidi na wazidi kuongezeka wenye kujitahidi katika kutafuta ukweli na kuufuata kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, wala si kwa ajili ya lolote lile jengine -

Amin.

Na kwa vile hivyo ndivyo yalivyo madhehebu ya Imam Shaafi'ii r.a., ndipo mimi nikajitegemeza zaidi katika madhehebu ya Imam Shafi'ii. Na kujitegemeza katika madhehebu ya Imam Shafi'ii ni ndivyo kabisa, kwani haya ndiyo madhehebu ambayo ni maadilifu zaidi na mepesi mno na ndio yaliyo karibu mno katika kufahamika, hivi ndivyo walivyoqiri wenye uadilifu na ufikirifu mwongofu. Amesema Imam Al'alaama - mwenye kuhuisha sunna za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na mwenye kunusuru haqi - Abu Shama Al Shafi'ii; Rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu ziwe juu yake, amesema katika risala yake : maneno yenye maana kama hii: "Ilikuwa katika siku zilizopita, Umma mujtahidiina (wenye kujitahidi katika elimu ya Ijtihaad) wakishughulikia kueneza elimu ya Ijtihaadi sehemu zote za ulimwengu. Wao katika juhudi zao hizi walikuwa katika fani mbali mbali, wako miongoni mwao waliokuwa wamezama katika elimu ya Qur'ani Tukufu, wako waliokuwa ni bahri katika elimu ya Hadithi. Na kati yao waliokuwa wamebobea katika elimu ya lugha ya Kiarabu, na wengine miongoni mwao walikuwa elimu yao zaidi kwenye fani ya kukusanya na kubainisha hukmu za Sharia (Fiqhi) kutokana na Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Kidogo mno ilikuwa kupatikana waliokusanya vyema ilimu ya fani hizi tafauti; lakini basi, ikawa aliekusanya na kufahamu vyema fani hizi zote ni Imam wetu, Abu Abdulla Al Qurashy Al Mu'taliby Al Shafi'ii, Mwenyezi Mungu Mtukufu awe radhi juu yake - Amin. Imam Al Shafi'ii amekusanya fani hizo, na kwa kutokana na nasaba iliyo 'taahir na kwa elimu iliyozagaa juu yake na wingi wa aliyojaaliwa kuyapata, kwa kusikia na kwa kuona; amekuwa ni mwingi wa mengi ya fakhari na utukufu. Kutokana na hali hii, ikawa Imam Shafi'ii ana utukufu uliomfadhilisha kati ya wengi wa Maimam watukufu. Haya yamethibitishiwa juu yake Imam Al Shafi'ii na kila mjuzi wa katika kila fani. Amesema Al Maziny kwamba amemsikia Imam Shafi'ii akisema kuwa amehifadhi Qur'ani nae ni mtoto wa miaka saba, na amehifadhi "Almau'tia" (hiki ni kitabu cha Hadithi za Mtume wetu Mpenzi s.a.w.) nae ana umri wa miaka kumi. Na amesema Yunis bin Abdula'alaa kuwa: "Ilikua Imam Shafi'ii akiingia katika tafsiri ya Qur'ani Tukufu, utaona kama kwamba alikuwepo ilipoteremshwa". Na amesema Ahmed bin Muhammad Ibn bint Shafi'ii kwamba amewasikia baba yake na 'ami yake wakisema: "Alikuwa Sufiyan bin 'Aiyana kikimjia kitu katika tafsiri ya Qur'ani Tukufu au kitu cha kutakiwa fatwa, hugeukia upande aliopo Imam Shafi'ii r.a. na husema: "Muulizeni huyu", yaani Imam Shafi'ii r.a.". Na amesema Muslim bin Khalid r.a. (Sheikh wake Imam Shafi'ii r.a.) wakati yeye ni Mufti, Makka: "Ewe Aba Abdulla! Towa fatwa, imewadia kwako kutowa fatwa". Wakati huo yeye Imam Shafi'ii umri wake ni miaka kumi na tano. Na amesema Arrabi'i kwamba Imam Shafi'ii akitowa fatwa nae ni mtoto wa miaka kumi na tano, na akidumisha ibada za usiku mpaka kufa kwake. Na amesema Abu Na'im Al Haafidh: "Nimemsikia Suleiman bin Ahmed akisema: "Nimemsikia Ahmed bin Muhammad bin Ibn bint Shafi'ii akisema: "Ilikuwa vikao vya fatwa kwenye Msikiti wa Makka, kwanza chini ya Ibni 'Abbas, kisha vikawa chini ya 'Atai bin Rabaah, kisha Abdulla bin Jariih, kisha vikawa chini ya Muslim bin Khaalid, kisha Said bin Salim, na baada yake vikao hivyo vikawa chini ya Muhammad bin Idris Al Shafi'ii, nae wakati huo ni kijana. Amesema Ibnu Mahdy kwamba amemsikia Imam Malik r.a. akisema: "Hanijii Qurashy mwenye kufaham zaidi ya kijana huyu". Anakusudia Imam Shafi'ii r.a. Na amesema Abu 'Ubaid bin Salaam: "Sijapata kuona katu mtu mwenye akili, wala uchaungu, wala fasaha kuliko Al Shafi'ii". Vilevile amesema Hilal bin Ala'alaa Arraqy: "Watu wa Hadith ni wadeni wa Imam Shafi'ii, amewafungulia kufuli". Amesema Is-haq bin Rahwiya kwamba alikutana na Imam Ahmed bin Hambal r.a. Makka, akamwambia: "Njoo nikuoneshe mtu halijaona jicho lako mfano wake". Akanionesha Imam Shafi'ii. Akasema (Is-haq): "Tukapitia kutizama wanazuoni wa elimu ya Hadithi, sikuona alie na elimu zaidi yake yeye Imam Al Shafi'ii, tukapitia kutizama wanazuoni wa Fiqh, sikuona alie na elimu ya Fiqh zaidi yake yeye Imam Shafi'ii, kisha tukapitia kutizama katika Qur'ani, sikuona aliomzidi Imam Shafi'ii, kisha tukapitia kutizama katika fani ya lugha (lugha ya Kiarabu), nikamuona Imam Shafi'ii ni nyumba ya lugha. Wala macho yangu hayakuonapo mfano wake". Akasema (Is-haq) tulipowachana nae, alinambia jamaa kati ya watu wenye kuifahamu Qur'ani kuwa yeye (Imam Shafi'ii) aliwapita wengi wa wanazuoni wa zama zake katika kufahamu maana ya Qur'ani, na kwamba Imam Al Shafi'ii alipewa kipaji cha kuifahamu Qur'ani Tukufu.

Amesema Imam Ahmad bin Hambal r.a.: "Walikuwa wanazuoni wa Fiqhi na wanazuoni wa Hadithi ni mfano wa wajuzi wa elimu ya madawa, akaja Imam Shafi'ii akiwa ni dakitari na mjuzi wa elimu ya madawa (kakusanya yote mawili), hayajapata macho kuona mfano wake. Na akasema: "Hakika, Mwenyezi Mungu Mtukufu kila baada ya miaka mia anawawekea waja Wake 'aalim wakuwafundisha Hadithi za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na kuukanya uwongo anaozuliwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Tukagundua kuwa katika kilele cha miaka mia alikuwa ni Omar bin Abdul Azizi r.a., na katika kilele cha miaka mia mbili alikuwa Imam Shafi'ii r.a. Na akasema (Ahmad bin Hambal): "Nikiulizwa kitu ambacho sijui khabari zake, hurejelea kwa Imam Shafi'ii; kwani yeye ni Imam 'aalim mwenye kutokana na Maquraishi".

Na imepokewa kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alisema:

Maana ya Hadithi hii ni kama hivi:"'Aalim wa Kiquraishi ataijaza ardhi ilimu". Na amesema Imam Ahmad r.a.: "Maneno ya Imam Shafi'ii juu ya lugha ni hoja". Na amesema Abu Othman Al Maaziny: "Imam Shafi'ii kwetu sisi ni hoja juu ya nahaw". Na amesema Abu Thaur Ibrahim bin Khalid: "Alikuwa Imam Shafi'ii kutokana na maadeni ya Fiqhi na mahiri wa uteuzi wa utumizi wa maneno na upekuzi wa maana ya maneno".Amesema Al Hassan bin Muhamad bin Al 'Sabbah Al Za'afarani: "Walikuwa wanazuoni wa Hadithi wamelala mpaka alipokuja Imam Shafi'ii akawaamsha, wakaamka. Matukufu yake Imam Shafi'ii r.a. ni mengi, yameweza, na yanaweza; kutungiwa vitabu kadhaa wa kadhaa".

Na nimechagua miongoni mwa hivi vitabu vilivyo tungwa katika Fiqhi Shafi'ii, kitabu kinachoitwa: cha Imam Taqi Diin Abi Bakr Muhammad Al Husainy Addimishqy, miongoni mwa wanazuoni wa karne ya tisa Hijria. Nilikipitia mbio mbio ukurasa baada ya ukurasa, kikanivutia kwa ubora wa utunzi wake na utamu wa mwenendo wake, na uzito wa madda yenyewe; zimewadhihika hukmu zake ambazo yeye Imam Taqi Diin - Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehem amezitegemeza juu ya Qur'ani Tukufu na Sunna za Mtume wetu Mpenzi s.a.w., na Ijtima'a (makubaliano) ya wanazuoni. Kisha nikakisoma mara baada ya mara; nikazichambua baadhi ya 'ibara ziliomo humo ili iwe wepesi kukubalika na kufahamika maana, isiwemo ndani yake mizunguko wala mazonge.

Pia niliongeza ndani yake yale ambayo hayanabudi kuwemo na siyakukosekana kuwemo, hivi ili kutimiza faida yenye kutarajiwa na kutarajia thawabu; pia nikatoa yale ambayo yanaweza kutoleka ili kufupisha pamoja na kubakia kiini cha faida. Katika chapa hii nimeongeza kukhusu hukmu za Kishari'a juu ya kupasuliwa maiti na rai za wanazuoni juu ya suala hili. Vile vile nimeongeza kukhusu hukmu za Kishari'a juu ya bima ya uhai (life insurance) na rai za wanazuoni juu ya suala hili. (Haya yamo kwenye Juzuu ya pili, yaani . Na nikakiita kitabu hiki yaani "Fiqhi Iliyowepesishwa", na nikakijaalia kimekusanya mambo ya ibada, kama vile Sala, Saumu, Zaka, Hija na 'Umra; na mambo ya mu'amalaati, yaani maingiliano baina ya binaadamu; kama vile kuuza na kununua, ndoa na 'talaka, kudai na kudaiwa; na kadhaalika. Mu'amalaati ni miongoni mwa hukmu za Sharia ambazo ni waajibu juu ya kila Muislam kuzisoma na kuzijua na kuzifuata, bali na kuzitekeleza; hivi ni kwa vile kulazimika kulioko juu yake hakuna kasoro ya kulazimika kulioko juu ya hukumu za Kisharia kukhusu mambo ya ibada, bali huenda baina ya hali na hali ikazidi kulazimika juu ya mambo ya mu'amalaati. Hivi ni kwa sababu mambo ya ibada yanamkhusu mtu mwenyewe binafsi, na matunda yake humrejelea (leo) na yatamrejelea (Kesho) yeye mwenyewe; ama mambo ya mu'amalaati (maingiliano) yanamrejelea yeye mwenyewe na mujtama'a (watu) anaoishi nao. Kwa hivi hali kuwa hivyo, ndio ikawa utafiti juu ya mu'amalaati na kubainisha hukmu zake Kisharia ni katika mambo muhimu na ya dharura katika Dini ya Kiislam, na hivyo ndivyo walivyo yashughulikia wanazuoni wa Fiqhi na watafiti katika elimu hii tangu hapo zamani mpaka hii leo. Kutokana na hali hii, ndio na mimi nikaingia katika utafiti juu ya mambo ya mu'amalaati (maingiliano) na nikaweka wazi natija ya utafiti wangu kadiri ya uwezo ili niulete kama vile nilivyoleta natija ya utafiti wangu juu ya mambo ya ibada, nikayaweka katika mpango mzuri na ibara nyepesi na wepesi wa kufahamika. Na uchambuzi wangu katika kubainihsa hukmu za Kisharia nimetegemeza juu ya Qur'ani Tukufu, Sunna za Mtume wetu mpenzi s.a.w. na makubaliano ya wanazuoni.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu yawafae haya viumbe, na yaongoe upotofu, na yaingie katika vitendo vyangu vyema, na kuendelea kukumbukwa; na yataqabaliwe, kwani Yeye ni Mola Mlezi Mwema na Mola Msaidizi Mwema, Amin.

 

Ahmad 'Isa 'Aashuur

 

 

__________________________________________________

Haki za Uchapishaji zimehifadhiwa na Mtungaji

Farouk Abdalla Al-Barwani, P.O. Box 828, Ruwi, P.C.112 Sultanate of Oman

e-mail: umojabaraka@yahoo.co.uk