Sura hii iliteremka Makka kabla ya Hijra, kuhamia Mtume s.a.w. Madina. Imeitwa
Al-Faatih'a, yaani Kifungulio kwa kuwa ndiyo sura ya mwanzo katika mpango wa Msahafu
Mtukufu, nayo ni sura ya mwanzo iliyo teremka kwa utimilivu wake. Na sura hii
inakusanya jumla ya yaliyomo katika Qur'ani na kama kwamba huu ni mukhtasari wake,
na baadaye yatakuja mambo kwa tafsili, babu-babu.
Na makusudio ya Qur'ani ni: Kubainisha Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu; na kubainisha
ahadi na bishara kwa Muumini mtenda mema; na kubainisha ahadi na onyo kwa kafiri
na mtenda maovu; na kubainisha ibada; na kubainisha njia ya kufanikiwa duniani
na Akhera; na hadithi za walio mt'ii Mwenyezi Mungu wakafuzu, na hadithi za walio
muasi wakaangamia.
Sura Al-Faatih'a inakusanya kwa ufupi na kwa kuashiria makusudio haya, na kwa
hivyo ndio ikaitwa pia "Ummul Kitaab" yaani "Msingi wa Kitabu".
1. KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. 1
2. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote; 2
3. Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu; 3
4. Mwenye Kumiliki Siku ya Malipo. 4
5. Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada. 5
6. Tuongoe njia iliyo nyooka, 6
7. Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea. 7
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com