SURA hii ni ya Makka isipo kuwa Aya hizi: 20, 23, 91, 93, 114, 141, 151, 152, na 153. Na Aya zake ni 165. Iliteremka baada ya Sura Al-Hijr. Na Sura hii tukufu imekusanya maana zilizo wekwa mbali mbali kama ifuatavyo:
Imewazindua watu wauzingatie ulimwengu na dalili ziliomo ndani yake zenye kuonyesha Ubora wa aliye uumba, na Utukufu wake na Umoja wake wa pekee, na kuwa Yeye hashirikiani na yeyote, la katika kuumba, wala katika kuabudiwa, wala katika dhati yake.
Na imekusanya visa vya baadhi ya Manabii, na ikaanza kwa kisa cha Ibrahim a.s. kwa kubainisha kuwa alichukua maana ya ibada na Tawhidi kwa kuuchungua ulimwengu, na kufuata yaliyomo ndani yake. Naye alianza kwa kupeleleza nyota, kisha mwezi, kisha jua, na akamalizia kwa kufuata ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake.
Na ikapelekea macho yaangalie ajabu za uumbaji na vipi mambo yanavyo kuwa. Ikabainisha vipi kilicho hai kinyevu kinatokana na kisicho kuwa na uhai kikavu; na vipi mbegu inavyo pasuka na ukachipua mmea.
Na Sura hii imezitaja sifa za wapinzani, na vipi wanavyo shikilia ndoto zao zinazo watenga na Haki, na zinazo wapotosha.
Na ndani ya Sura hii umebainishwa uhalali wa vyakula alivyo halalisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na upotovu wa Washirikina walivyo jiharimishia wenyewe bila ya kutegemea dalili yoyote, na vipi wanavyo mnasibishia kuharimisha huko Mwenyezi Mungu Aliye Takasika.
Na ndani yake yamebainishwa mambo haya, ambayo ndio mukhtasari wa Uislamu na tabia njema za kusifika. Mambo yenyewe ni:- kuharimisha ushirikina, uzinzi, kuuwa mtu, kula mali ya yatima, waajibu wa kutimiza vipimo na mizani, kutimiza uadilifu, kutekeleza ahadi, kuwatendea wema wazazi, na kukataza kuwazika watoto wa kike nao wahai.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, na akafanya
giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya wengine sawa na
Mola wao Mlezi. ***
2. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha akakuhukumieni ajali, na muda
maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi mnatia shaka. ***
3. Na Yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani yenu na
ya nje yenu. Na anajua mnayo yachuma. ***
4. Na haiwafikii hata ishara moja katika ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa
wenye kuipa nyongo. ***
5. Wameikanusha Haki ilipo wajia. Basi zitawajia khabari za yale waliyo kuwa
wakiyakejeli. ***
6. Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla yao? Tuliwaweka katika
nchi tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi na tukaifanya mito inapita
chini yao. Mwishoe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha baada yao kizazi
kingine. ***
7. Na lau tungeli kuteremshia kitabu cha karatasi, wakakigusa kwa mikono yao,
wangeli sema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uchawi dhaahiri. ***
8. Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama tungeli teremsha Malaika,
basi bila ya shaka ingesha hukumiwa amri, tena hapo wasingeli pewa muhula. ***
9. Na kama tungeli mfanya Malaika bila ya shaka tungeli mfanya kama binaadamu,
na tungeli watilia matatizo yale wanayo yatatiza wao. ***
10. Na hakika Mitume walio kabla yako walifanyiwa kejeli, lakini walio wafanyia
kejeli wakaja kuzungukwa na yale yale waliyo kuwa wao wanayafanyia kejeli. ***
11. Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha. ***
12. Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi
Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika atakukusanyeni Siku ya
Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri wenyewe hawaamini. ***
13. Na ni vyake vilio tulia usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye
kujua. ***
14. Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye
Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa
niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina. ***
15. Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku kubwa hiyo ikiwa nitamuasi Mola wangu Mlezi. ***
16. Siku hiyo yule atakaye epushwa nayo adhabu hiyo atakuwa Mwenyezi Mungu amemrehemu.
Na huko ndiko kufuzu kulio wazi. ***
17. Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea
hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila
kitu. ***
18. Naye ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, na ndiye Mwenye hikima na Mwenye
khabari zote. ***
19. Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye
shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni
nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi
Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu
mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha. ***
20. Wale Tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto wao. Wale
walio zikhasiri nafsi zao hawaamini. ***
21. Na nani dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na akazikanusha
Ishara zake? Hakika madhaalimu hawafanikiwi. ***
22. Siku tutapo wakusanya wote pamoja, kisha tuwaambie walio shirikisha: Wako
wapi washirikishwa wenu mlio kuwa mnadai? ***
23. Kisha hautakuwa udhuru wao ila ni kusema: Wallahi! Mola wetu Mlezi! Hatukuwa
washirikina. ***
24. Tazama jinsi wanavyo jisemea uwongo wenyewe. Na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua. ***
25. Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza; na tumezitia pazia nyoyo zao wasije
kuyafahamu. Na upo uziwi masikioni mwao, na wakiona kila Ishara hawaiamini. Hata
wakikujia kwa kujadiliana nawe, wanasema walio kufuru: Hizi si chochote ila hadithi
za watu wa kale. ***
26. Nao huwazuia watu, na wao wenyewe wanajitenga nayo. Nao hawaangamizi ila
nafsi zao tu, wala wao hawatambui. ***
27. Na unge ona watakapo simamishwa kwenye Moto, wakawa wanasema: Laiti tungeli
rudishwa, wala hatutakanusha tena Ishara za Mola wetu Mlezi, na tutakuwa miongoni
wa Waumini. ***
28. Bali yamewadhihirikia waliyo kuwa wakiyaficha zamani. Na kama wangeli rudishwa
bila ya shaka wange yarejea yale yale waliyo katazwa. Na hakika hao ni waongo. ***
29. Na walisema: Hakuna mengine ila maisha yetu haya ya duniani, wala sisi hatutafufuliwa. ***
30. Na lau ungeli ona watavyo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, akawaambia:
Je, si kweli haya? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola Mlezi wetu ni kweli.
Yeye atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya vile mlivyo kuwa mnakataa. ***
31. Hakika wamekhasirika walio kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, mpaka ilipo
wajia Saa kwa ghafla, wakasema: Ole wetu kwa tuliyo yapuuza! Nao watabeba mizigo
yao juu ya migongo yao. Ni maovu hayo wanayo yabeba. ***
32. Na maisha ya dunia si chochte ila ni mchezo na pumbao tu. Na hakika nyumba
ya Akhera ni bora zaidi kwa wanao mcha Mungu. Basi, je, hamtii akilini? ***
33. Tunajua ya kwamba yanakuhuzunisha wanayo yasema. Basi hakika wao hawakukanushi
wewe, lakini hao madhaalimu wanazikataa Ishara za Mwenyezi Mungu. ***
34. Na hakika walikanushwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia kule kukanushwa,
na kuudhiwa, mpaka ilipo wafikia nusura yetu. Na hapana wa kubadilisha maneno
ya Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka zimekujia baadhi ya khabari za Mitume hao. ***
35. Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi kama unaweza kutafuta njia
ya chini kwa chini ya ardhi, au ngazi kwendea mbinguni ili uwaletee Ishara --
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa angeli wakusanya kwenye uwongofu. Basi usiwe
miongoni mwa wasio jua. ***
36. Hakika wanao kubali ni wale wanao sikia. Na ama wafu Mwenyezi Mungu atawafufua,
na kisha kwake Yeye ndio watarejeshwa. ***
37. Na wamesema: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi?
Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuteremsha muujiza. Lakini wengi wao
hawajui. ***
38. Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anaye ruka kwa mbawa zake mbili,
ila ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao
Mlezi watakusanywa. ***
39. Na walio kanusha Ishara zetu ni viziwi na mabubu waliomo gizani. Mwenyezi
Mungu humwachia kupotea amtakaye, na humweka katika Njia iliyo nyooka amtakaye. ***
40. Sema: Mwaonaje ikikujieni adhabu ya Mwenyezi Mungu, au ikakufikieni hiyo
Saa - mtamwomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni wakweli? ***
41. Bali Yeye ndiye mtakaye mwomba, naye atakuondoleeni mnacho mwombea akipenda.
Na mtasahau hao mnao wafanya washirika wake. ***
42. Na kwa yakini tulipeleka Mitume kwa kaumu zilizo kuwa kabla yako, kisha tukazitia
katika dhiki na mashaka ili zipate kunyenyekea. ***
43. Kwa nini wasinyenyekee ilipo wafika adhabu yetu? Lakini nyoyo zao zilikuwa
ngumu, na Shet'ani akawapambia waliyo kuwa wakiyafanya. ***
44. Basi walipo sahau walio kumbushwa tuliwafungulia milango ya kila kitu. Mpaka
walipo furahia yale waliyo pewa tuliwashika kwa ghafla, na mara wakawa wenye kukata
tamaa. ***
45. Ikakatwa mizizi ya watu walio dhulumu - na wa kuhimidiwa ni Mwenyezi Mungu,
Mola Mlezi wa viumbe vyote. ***
46. Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu akanyakua kusikia kwenu, na kuona kwenu, na
akaziziba nyoyo zenu, ni mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni
hayo tena? Angalia vipi tunavyo zieleza Ishara, kisha wao wanapuuza. ***
47. Sema: Mwaonaje, ikikufikieni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla, au kwa
dhaahiri, jee wataangamizwa isipo kuwa walio dhulumu? ***
48. Na hatuwatumi Mitume ila huwa ni wabashiri na waonyaji. Na wenye kuamini
na wakatenda mema haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika. ***
49. Na walio kanusha Ishara zetu itawagusa adhabu kwa walivyo kuwa wakipotoka. ***
50. Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui
mambo yaliyo fichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika. Mimi sifuati ila
yanayo funuliwa kwangu. Sema: Je, wanakuwa sawa, kipofu na mwenye kuona. Basi
hamfikiri? ***
51. Na waonye kwayo wanao ogopa kuwa watakusanywa kwa Mola wao Mlezi, hali kuwa
hawana mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye, ili wapate kuchamngu. ***
52. Wala usiwafukuze wanao mwomba Mola Mlezi wao asubuhi na jioni kwa kutaka
radhi yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata
kidogo, hata uwafukuze na uwe miongoni mwa wenye kudhulumu. ***
53. Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili waseme: Ni hao ndio Mwenyezi
Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanao shukuru? ***
54. Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum! Amani
iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakaye fanya uovu
miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea, basi hakika
Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. ***
55. Na ndio hivi tunavyo zieleza Ishara ili ibainike njia ya wakosefu. ***
56. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu.
Sema: mimi sifuati matamanio yenu. Hivyo nitakuwa nimepotea, na sitakuwa miongoni
mwa walio ongoka. ***
57. Sema: Mimi nipo kwenye sharia iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu Mlezi, nanyi
mnaikanusha. Mimi sinacho hicho mnacho kihimiza. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi
Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa kuhukumu kuliko wote. ***
58. Sema: Lau kuwa ninacho hicho mnacho kihimiza, ingeli kwisha katwa shauri
baina yangu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu anawashinda wote kuwajua madhaalimu. ***
59. Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua
kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika
giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinacho bainisha. ***
60. Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlicho fanya mchana. Kisha
Yeye hukufufueni humo mchana ili muda ulio wekwa utimizwe. Kisha kwake Yeye ndiyo
marejeo yenu, na tena akwambieni mliyo kuwa mkiyafanya. ***
61. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja wake. Na hukupelekeeni
waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha, nao hawafanyi
taksiri. ***
62. Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki. Hakika, hukumu ni
yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu. ***
63. Sema: Ni nani anaye kuokoeni katika giza la nchi kavu na baharini? Mnamwomba
kwa unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa
miongoni mwa wanao shukuru. ***
64. Sema: Mwenyezi Mungu hukuokoeni kutoka hayo, na kutoka kila mashaka, na kisha
nyinyi mnamshirikisha! ***
65. Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini
ya miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na kuwaonjesha baadhi yenu jeuri
ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili wapate kufahamu. ***
66. Na watu wako wameikanusha, nayo ni Haki. Sema: Mimi sikuwakilishwa juu yenu. ***
67. Kila khabari ina kipindi chake. Nanyi mtakuja jua. ***
68. Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie
mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi
usikae pamoja na watu madhaalimu. ***
69. Wala wamchao Mungu hawana jukumu lolote kwao, lakini ni kukumbusha, asaa
wapate kujiepusha. ***
70. Waachilie mbali walio ifanya dini yao ni mchezo na pumbao, na uhai wa dunia
ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi ikaangamizwa kwa sababu ya iliyo
yachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila Mwenyezi Mungu. Na ingatoa kila fidia
haitokubaliwa. Hao ndio walio angamizwa kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Wao
watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa, na adhabu chungu. ***
71. Sema: Je, tumuombe asiye kuwa Mwenyezi Mungu ambae hatufai wala hatudhuru,
na turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuhidi? Tuwe kama ambao mashet'ani
wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki wanao mwita ende kwenye uwongofu,
wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio Uwongofu.
Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote, ***
72. Na mshike Sala, na mcheni Yeye, na kwake Yeye ndiko mtako kusanywa. ***
73. Naye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na anaposema: Kuwa! Basi
huwa. Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku litapo pulizwa barugumu,
Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye ndiye Mwenye hikima na Mwenye
khabari. ***
74. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni
miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu ulio wazi. ***
75. Na kadhaalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe
miongoni mwa wenye yakini. ***
76. Na ulipo muingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola Mlezi wangu.
Ilipo tua akasema: Siwapendi wanao tua. ***
77. Alipo uona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Ulipotua
akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu walio potea. ***
78. Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu
mkubwa kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo
mnayo fanyia ushirikina. ***
79. Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliye ziumba mbingu na ardhi,
wala mimi si miongoni mwa washirikina. ***
80. Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu, na
hali Yeye ameniongoa? Wala siogopi hao mnao washirikisha naye, ila Mola wangu
Mlezi akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya kila kitu. Basi je,
hamkumbuki? ***
81. Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi
mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia uthibitisho. Basi
kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua? ***
82. Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma - hao ndio watakao
pata amani na wao ndio walio ongoka. ***
83. Na hizo ndizo hoja zetu tulizo mpa Ibrahim kuhojiana na watu wake. Tunamnyanyua
kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye hikima na Mwenye ujuzi. ***
84. Na tukamtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila mmoja wao tulimwongoa. Na
Nuhu tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake tulimwongoa Daud na Suleiman na
Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wafanyao wema. ***
85. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyas. Wote walikuwa miongoni mwa watu wema. ***
86.Na Ismail, na Al Yasaa, na Yunus, na Lut'. Na wote tuliwafadhilisha juu ya
walimwengu wote. ***
87. Na kutokana na baba zao, na vizazi vyao na ndugu zao. Na tukawateuwa na tukawaongoa
kwenye Njia iliyo nyooka. ***
88. Hiyo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo humhidi amtakaye katika waja wake.
Na lau wangeli mshirikisha yangeli waharibikia waliyo kuwa wakiyatenda. ***
89. Hao ndio tulio wapa Vitabu na hukumu na Unabii. Ikiwa hawa watayakataa hayo,
basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasio yakataa. ***
90. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewahidi. Basi fuata hidaya yao. Sema: Mimi
sikuombeni ujira. Haya hayakuwa ila ni mawaidha kwa walimwengu wote. ***
91. Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri yake, walipo sema: Mwenyezi
Mungu hakumteremshia mwanaadamu chochote. Sema: Nani aliyo teremsha Kitabu alicho
kuja nacho Musa, chenye nuru na uwongofu kwa watu, mlicho kifanya kurasa kurasa
mkizionyesha, na mengi mkiyaficha. Na mkafunzwa mlio kuwa hamyajui nyinyi wala
baba zenu? Sema: Mwenyezi Mungu. Kisha waache wacheze katika porojo lao. ***
92. Na hiki ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa, chenye kuhakikisha
yaliyo tangulia, na ili uuwonye Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na wenye
kuamini Akhera wanakiamini hichi, nao wanazihifadhi Sala zao. ***
93. Nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzuliya uwongo Mwenyezi Mungu, au
anaye sema: Mimi nimeletewa wahyi; na hali hakuletewa wahyi wowote. Na yule anaye
sema: Nitateremsha kama alivyo teremsha Mwenyezi Mungu. Na lau ungeli waona madhaalimu
wanavyo kuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia:
Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyasema
juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo ya haki, na mlivyo kuwa mkizifanyia kiburi Ishara
zake. ***
94. Nanyi mlitujia wapweke kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza. Na mkayaacha
nyuma yenu yote tuliyo kupeni, na wala hatuwaoni hao waombezi wenu, ambao mlidai
kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenu. Yamekatika makhusiano baina yenu, na
yamekupoteeni mliyo kuwa mkidai. ***
95. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa, zikachipua. Humtoa aliye
hai kutoka maiti, naye ni mtoaji maiti kutokana na aliye hai. Huyo ndiye Mwenyezi
Mungu. Basi vipi mnageuzwa? ***
96. Ndiye anaye pambazua mwangaza wa asubuhi; na ameufanya usiku kwa mapumziko
na utulivu, na jua na mwezi kwenda kwa hisabu. Hayo ndiyo makadirio ya Aliye tukuka
Mwenye nguvu, Mwenye ujuzi. ***
97. Na Yeye ndiye aliye kuwekeeni nyota ili mwongoke kwazo katika kiza cha bara
na bahari. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu wanao jua. ***
98. Na Yeye ndiye aliye kuzalisheni kutokana na nafsi moja. Pako pahali pa kutulia
na pa kupita njia. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu wanao fahamu. ***
99. Na Yeye ndiye anaye teremsha maji kutoka mbinguni; na kwayo tunatoa mimea
ya kila kitu. Kutokana na baadhi yao tukatoa mimea ya majani, tukatoa ndani yake
punje zilizo pandana; na kutokana na mitende yakatoka kwenye makole yake mashada
yaliyo inama; na bustani za mizabibu na mizaituni, na makomamanga, yaliyo fanana
na yasiyo fanana. Angalieni matunda yake yanapo zaa na yakawiva. Hakika katika
hayo pana Ishara kwa watu wanao amini. ***
100. Bado wamemfanyia Mwenyezi Mungu majini kuwa washirika wake, na hali Yeye
ndiye aliye waumba. Na wakamzulia, bila ya ujuzi wowote, kuwa ana wana wa kiume
na wa kike. Subhanahu, Ametakasika na ametukuka juu ya hayo wanayo mbandikiza
nayo! ***
101. Yeye ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi bila ya ruwaza. Itakuwaje awe na
mwana naye hakuwa na mke? Naye ndiye aliye umba kila kitu. Naye ni Mwenye kujua
kila kitu. ***
102. Huyo ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu, hapana mungu ila Yeye,
Muumba wa kila kitu. Basi muabuduni Yeye tu. Naye ni Mtegemewa wa kila kitu. ***
103. Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho. Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari. ***
104. Zimekwisha kukujieni hoja wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi anaye ona
ni kwa faida yake mwenyewe, na anaye pofuka basi ni khasara yake. Nami si mtunzaji
wenu. ***
105. Na namna hivyo tunazisarifu Aya, na wao wakwambie: Umesoma. Na ili tuyabainishe
kwa watu wanao jua. ***
106. Fuata uliyo funuliwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Hapana mungu ila Yeye.
Na jitenge na washirikina. ***
107. Na lau Mwenyezi Mungu angeli penda, wasingeli shiriki. Na Sisi hatukukufanya
wewe uwe mtunzaji wao. Wala wewe si mlinzi juu yao. ***
108. Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije na wao
wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo tumewapambia kila
umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia
waliyo kuwa wakiyatenda. ***
109. Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao, kuwa ikiwafikia Ishara
wataiamini. Sema: Ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na nyinyi hamjui kuwa zitapo
kuja hawato amini. ***
110. Nasi twazigeuza nyoyo zao na macho yao. Kama walivyo kuwa hawakuamini mara
ya kwanza, tunawaacha katika maasi yao wakitangatanga. ***
111. NA LAU kuwa tungeli wateremshia Malaika, na maiti wakazungumza nao, na tukawakusanyia
kila kitu mbele yao, bado wasingeli amini, ila Mwenyezi Mungu atake. Lakini wengi
wao wamo ujingani. ***
112. Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashet'ani wa kiwatu, na kijini,
wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupamba-pamba, kwa udanganyifu. Na angeli
penda Mola wako Mlezi wasingeli fanya hayo. Basi waache na wanayo yazua. ***
113. Na ili nyoyo za wasio amini Akhera zielekee hayo, nao wayaridhie na wayachume
wanayo yachuma. ***
114. Je, nimtafute hakimu ghairi ya Mwenyezi Mungu, naye ndiye aliye kuteremshieni
Kitabu kilicho elezwa waziwazi? Na hao tulio wapa Kitabu wanajua ya kwamba kimeteremshwa
na Mola wako Mlezi kwa Haki. Basi usiwe katika wanao tia shaka. ***
115. Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye
kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua. ***
116. Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Mwenyezi
Mungu. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema uwongo tu. ***
117. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio potea Njia
yake, na ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio hidika. ***
118. Basi kuleni katika walio somewa jina la Mwenyezi Mungu, ikiwa mnaziamini
Aya zake. ***
119. Na kwa nini msile katika walio somewa jina la Mwenyezi Mungu, naye amekwisha
kubainishieni alivyo kuharimishieni, isipo kuwa vile mnavyo lazimishwa? Na hakika
wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya kuwa na ilimu. Hakika Mola wako Mlezi
ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua wanao pindukia mipaka. ***
120. Na acheni dhambi zilizo dhaahiri na zilizo fichikana. Hakika wanao chuma
dhambi watalipwa kwa waliyo kuwa wakiyachuma. ***
121. Wala msile katika wale wasio somewa jina la Mwenyezi Mungu. Kwani huo ni
upotofu. Na kwa yakini mashet'ani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi. Na
mkiwafuata basi hapana shaka nyinyi mtakuwa washirikina. ***
122. Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru inakwenda naye
mbele za watu, mfano wake ni kama aliyoko gizani akawa hata hawezi kutoka humo?
Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyo kuwa wakiyafanya. ***
123. Kadhaalika katika kila mji tumewajaalia wakubwa wa wakosefu wao wafanye
vitimbi ndani yake. Na wala hawafanyii vitimbi isipo kuwa nafsi zao, nao hawatambui. ***
124. Na inapo wajia Ishara, wao husema: Hatutoamini mpaka tupewe mfano wa walio
pewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote kujua wapi
anaweka ujumbe wake. Itawafikia hao walio kosa udhalili na adhabu kali kutoka
kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo kuwa wakivifanya. ***
125. Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumhidi humfungulia kifua chake
kwa Uislamu. Na anaye taka apotee hukifanya kifua chake kina dhiki, kimebana,
kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu anajaalia uchafu juu
ya wasio amini. ***
126. Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka. Tumezipambanua Aya kwa
watu wanao kumbuka. ***
127. Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye ndiye Rafiki Mlinzi
wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda. ***
128. Na ile Siku atapo wakusanya wote awaambie: Enyi makundi ya majini! Hakika
nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu. Na marafiki zao katika wanaadamu
waseme: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana sisi na wao. Na tumefikia ukomo wetu ulio
tuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto ndio makaazi yenu, mtadumu humo, ila
apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye hikima, na Mwenye kujua. ***
129. Ndio kama hivi tunawaelekeza madhaalimu wapendane wao kwa wao kwa sababu
ya waliyo kuwa wakiyachuma. ***
130. Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakukujieni Mitume kutokana na nyinyi
wenyewe wakikubainishieni Aya zangu, na wakikuonyeni mkutano wa Siku yenu hii.
Nao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na yaliwadanganya maisha ya dunia.
Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri. ***
131. Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi hakuwa wa kuiangamiza miji kwa
dhulma, hali wenyewe wameghafilika. ***
132. Na wote wana daraja mbali mbali kutokana na yale waliyo yatenda. Na Mola
wako Mlezi si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda. ***
133. Na Mola wako Mlezi ndiye Mkwasi, Mwenye rehema. Akipenda atakuondoeni na
awaweke wengine awapendao badala yenu, kama vile alivyo kutoeni kutokana na uzazi
wa watu wengine. ***
134. Bila ya shaka hayo mnayo ahidiwa yatafika tu, wala nyinyi hamtaweza kuyaepuka. ***
135. Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezayo, na hakika mimi nafanya. Mtakuja
jua nani atakuwa na makaazi mema mwishoni. Hakika madhaalimu hawatafanikiwa. ***
136. Na wamemwekea sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea na wanyama alio umba, nao
husema: Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu - kwa madai yao - na hii ni ya miungu
tunao washirikisha. Basi vile walivyo wakusudia miungu yao havimfikii Mwenyezi
Mungu, na vilivyo kuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia miungu yao. Ni uovu kabisa
hayo wanayo yahukumu. ***
137. Na kadhaalika hao washirika wao wamewapambia wengi katika washirikina kuwauwa
watoto wao ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu
angeli penda wasinge fanya hayo. Basi waache na hayo wanayo yazua. ***
138. Nao husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko. Hawatokula ila wale tuwapendao
- kwa madai yao tu. Na wanyama hawa imeharimishwa migongo yao kupandwa. Na wanyama
wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao. Wanamzulia uwongo tu Mwenyezi
Mungu. Atawalipa kwa hayo wanayo mzulia. ***
139. Na husema: Waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya wanaume wetu
tu, na wameharimishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa nyamafu basi wanashirikiana.
Mwenyezi Mungu atawalipa kwa maelezo yao hayo. Hakika Yeye ni Mwenye hikima, Mwenye
kujua. ***
140. Hakika wamekhasirika wale ambao wamewauwa watoto wao kwa upumbavu pasipo
kujua, na wakaharimisha alivyo waruzuku Mwenyezi Mungu kwa kumzulia Mwenyezi Mungu.
Hakika wamepotea, wala hawakuwa wenye kuongoka. ***
141. Na Yeye ndiye aliye ziumba bustani zenye kutambaa juu ya chanja, na zisio
tambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbali mbali, na mizaituni na mikomamanga
inayo fanana na isiyo fanana. Kuleni matunda yake inapo zaa, na toeni haki yake
siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye hawapendi watumiayo
kwa fujo. ***
142. Na katika wanyama amekujaalieni wenye kubeba mizigo na kutoa matandiko.
Kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, wala msifuate nyayo za Shet'ani.
Hakika yeye ni adui yenu dhaahiri. ***
143. Amekuumbieni namna nane za wanyama: Wawili katika kondoo, na wawili katika
mbuzi. Sema je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni
mwa majike yote mawili? Niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema kweli. ***
144.Na wawili katika ngamia, na wawili katika ng'ombe. Sema: Je, ameharimisha
yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa yote majike? Au,
nyinyi mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuusieni haya? Basi ni nani dhaalimu mkubwa
kuliko yule aliye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa ajili ya kuwapoteza watu bila
ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawahidi watu madhaalimu. ***
145. Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho harimishwa kwa
mlaji kukila isipo kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika, au nyama ya nguruwe,
kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi
Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka,
basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. ***
146. Na wale walio fuata dini ya Kiyahudi tumewaharimishia kila mwenye kucha.
Na katika ng'ombe na kondoo na mbuzi tumewaharimishia shahamu yao, isipo kuwa
ile iliyo beba migongo yao au matumbo yao, au iliyo gandamana na mifupa. Tuliwalipa
hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na bila ya shaka Sisi ndio wasema kweli. ***
147. Wakikukanusha basi wewe sema: Mola Mlezi wenu ni Mwenye rehema iliyo enea.
Wala haizuiliki adhabu yake kwa watu wakhalifu. ***
148. Watasema walio shirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu ange taka tusingeli shiriki
sisi, wala baba zetu; wala tusingeli harimisha kitu chochote. Vivi hivi walikanusha
walio kuwa kabla yao mpaka walipo onja adhabu yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu
mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila uwongo tu. ***
149. Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye hoja ya kukata. Na kama angeli penda
angeli kuhidini nyote. ***
150. Sema: Leteni mashahidi wenu watao shuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameharimisha
hawa. Basi wakishuhudia, wewe usishuhudie pamoja nao. Wala usifuate matamanio
ya walio zikanusha Ishara zetu, wala hawaiamini Akhera, na ambao wanamlinganisha
Mola Mlezi wao na wengine. ***
151. Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola wenu Mlezi. Nayo ni kuwa,
msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema. Wala msiwauwe
watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao. Wala msikaribie
mambo machafu, yanayo onekana, na yanayo fichikana. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi
Mungu ameharimisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini. ***
152. Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya wema kabisa, mpaka afikilie
utu-uzima. Na timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu. Sisi hatumkalifishi mtu
ila kwa kadiri ya uwezo wake. Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa.
Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni. Hayo amekuusieni ili mpate kukumbuka. ***
153. Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni, wala msifuate
njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya amekuusieni ili mpate kuchamngu. ***
154. Tena tulimpa Musa Kitabu kwa kumtimizia (neema) aliye fanya wema, na kuwa
ni maelezo ya kila kitu, na uwongofu na rehema, ili wapate kuamini mkutano wao
na Mola wao Mlezi. ***
155. Na hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa. Basi kifuateni,
na mchenimngu, ili mrehemewe. ***
156. Msije mkasema: Hakika mataifa mawili kabla yetu yameteremshiwa Kitabu; na
sisi tulikuwa hatuna khabari ya waliyo kuwa wakiyasoma. ***
157. Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu tungeli kuwa waongofu zaidi
kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu,
na rehema. Basi nani aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kanusha Ishara
za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa wanao jitenga na Ishara zetu
adhabu kali kabisa kwa sababu ya kujitenga kwao. ***
158. Wanangoja jengine ila wawafikie Malaika, au awafikie Mola wako Mlezi, au
zifike baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi? Siku zitakapo fika baadhi ya Ishara
za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu, ikiwa hakuwa ameamini kabla
yake, au amefanya kheri katika Imani yake. Sema: Ngojeni, nasi pia tunangoja. ***
159. Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna ukhusiano nao
wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale
waliyo kuwa wakiyatenda. ***
160. Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila
sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa. ***
161. Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka,
Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliye kuwa mwongofu, wala
hakuwa miongoni mwa washirikina. ***
162. Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu,
ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. ***
163. Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa kwanza
wa Waislamu. ***
164. Sema: Je nitafute Mola Mlezi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ndiye
Mola Mlezi wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na habebi mwenye
kubeba mzigo wa mwenziwe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi, naye atakuambieni
mliyo kuwa mkikhitalifiana. ***
165. Naye ndiye aliye kufanyeni makhalifa wa duniani, na amewanyanyua baadhi
yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa, ili akujaribuni kwa hayo aliyo kupeni.
Hakika Mola Mlezi wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika Yeye ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu. ***
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@yahoo.com