Surat Al Anfaal hii imeteremka Madina. Aya zake ni 75. Mwenyezi Mungu aliye takasika
na kutukuka, amebainisha katika Sura hii baadhi ya hukumu za vita, na mambo yanayo
pelekea vita, na sababu za ushindi, na makamo ya nguvu za moyo zinazo pelekea
kushinda, na hukumu za ngawira za vita, na wakati gani kuchukua mateka. Na Mwenyezi
Mungu kwa hikima yake amekusanya humu hukumu za kisharia. Sura hii inaeleza kisa
cha Vita vya Badri, na baadhi ya yaliyo kuwa kabla yake, na kuashiria sababu zilizo
sabibisha hivyo vita, nazo ni kutoka makafiri washirikina Makka kumwendea Nabii
s.a.w.. Na humu Mwenyezi Mungu anataja kujitayarisha kwa vita, na kupasa kuelekea
salama na amani ikiwa maadui wanaelekea kutaka salama. Na Sura hii tukufu inamalizikia
kubainisha urafiki wa Waumini, wao kwa wao; na kuwawajibikia Waumini kuihama nchi
inayo waonea na kuwafanya wanyonge, ili wende kuwaunga mkono Waumini wenzao katika
juhudi ya kutukuza Uislamu na Waislamu.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU
1. Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi
mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mt'iini Mwenyezi Mungu
na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini. ***
2. Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu,
na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi. ***
3. Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale tunayo waruzuku. ***
4. Hao kweli ndio Waumini. Wao wana vyeo, na maghfira, na riziki bora, kwa Mola
wao Mlezi. ***
5. Kama Mola wako Mlezi alivyo kutoa nyumbani kwako kwa Haki, na hakika kundi
moja la Waumini linachukia. ***
6. Wanajadiliana nawe kwa jambo la Haki baada ya kwisha bainika, kama kwamba
wanasukumwa kwenye mauti nao wanaona. ***
7. Na Mwenyezi Mungu alipo kuahidini kuwa moja katika makundi mawili ni lenu.
Nanyi mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na Mwenyezi Mungu anapenda ahakikishe
Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri. ***
8. Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangachukia wakosefu. ***
9. Mlipo kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini
Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wanao fuatana mfululizo. ***
10. Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe.
Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye nguvu, na Mwenye hikima. ***
11. Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na akakuteremshieni
maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shet'ani,
na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu. ***
12. Mola wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi
watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru. Basi wapigeni
juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole. ***
13. Hayo ni kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumuasi
Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu. ***
14. Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka makafiri wana adhabu ya Moto. ***
15. Enyi Mlio amini! Mkikutana na walio kufuru vitani msiwageuzie mgongo. ***
16. Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo - isipo kuwa kwa mbinu za vita
au kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na
pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu. ***
17. Hamkuwauwa nyinyi lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye wauwa. Na wewe hukutupa,
walakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye tupa, ili awajaribu Waumini majaribio mema
yatokayo kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Msikizi na Mjuzi. ***
18. Ndio hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kudhoofisha vitimbi vya makafiri. ***
19. Kama mnataka hukumu basi hukumu imekwisha kujieni. Na mkiacha itakuwa ndio
kheri kwenu. Na mkirejea Sisi pia tutarejea. Na jeshi lenu halitakufaeni kitu,
japo likiwa kubwa. Kwani hakika Mwenyezi yu pamoja na Waumini. ***
20. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye,
nanyi mnasikia. ***
21. Wala msiwe kama wale wanao sema: Tumesikia, na kumbe hawasikii. ***
22. Hakika vinyama viovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni vile viziwi na bubu visio
tumia akili zao. ***
23. Na Mwenyezi Mungu angeli jua wema wowote kwao ange wasikilizisha, na lau
ange wasikilizisha wangeli geuka wakapuuza. ***
24. Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo
la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu
na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa. ***
25. Na jikingeni na Fitna ambayo haitowasibu walio dhulumu peke yao kati yenu.
Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu. ***
26. Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, mkionekana wanyonge katika nchi, mnaogopa
watu wasikunyakueni, naye akakupeni pahala pazuri pa kukaa, na akakutieni nguvu
kwa nusura yake, na akakupeni riziki nzuri ili mpate kushukuru. ***
27. Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msikhini
amana zenu, nanyi mnajua. ***
28. Na jueni ya kwamba mali zenu na wana wenu ni Fitna (mtihani), na kwamba kwa
Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa. ***
29. Enyi mlio amini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atakupeni kipambanuo, na atakufutieni
makosa, na atakusameheni, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa. ***
30. Na walipo kupangia mpango walio kufuru wakufunge, au wakuuwe, au wakutoe.
Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye
mbora wa mipango. ***
31. Na wanapo somewa Aya zetu, wao husema: Tumesikia. Na lau tungeli penda tunge
sema kama haya. Haya si chochote ila hadithi za watu wa kale tu. ***
32. Na walipo sema: Ee Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni kweli itokayo kwako basi
tunyeshee mawe kutoka mbinguni, au tuletee adhabu yoyote iliyo chungu. ***
33. Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu nawe umo pamoja nao, wala Mwenyezi
Mungu si wa kuwaadhibu na hali ya kuwa wanaomba msamaha. ***
34. Lakini wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu, na hali ya kuwa wanawazuilia
watu Msikiti Mtakatifu? Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake, bali walinzi wake
hawakuwa ila wacha-Mngu tu. Lakini wengi katika wao hawajui. ***
35. Na haikuwa ibada yao kwenye hiyo Nyumba (Al Kaaba) ila ni kupiga miunzi na
makofi. Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru. ***
36. Hakika wale walio kufuru hutoa mali yao ili kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu.
Basi watayatoa, kisha yatakuwa juu yao majuto, na kisha watashindwa. Na wale walio
kufuru watakusanywa kwenye Jahannam. ***
37. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwa pambanua walio waovu na walio wema, na kuwaweka
waovu juu ya waovu wengine, na kuwarundika wote pamoja, na kuwatupa katika Jahannam.
Hao ndio walio khasirika. ***
38. Waambie wale walio kufuru: Wakikoma watasamehewa yaliyo kwisha pita. Na wakiyarudia
basi imekwisha pita mifano ya wa zamani. ***
39. Na piganeni nao mpaka isiwepo fitna na mateso, na Dini yote iwe kwa ajili
ya Mwenyezi Mungu. Lakini wakiacha, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayo
yatenda. ***
40. Na kama wakigeuka basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola
Mwema na Msaidizi Mwema. ***
41. NA JUENI ya kwamba ngawira mnayo ipata, basi khums (sehemu moja katika tano)
ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na
wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo yateremsha kwa mja
wetu siku ya kipambanuo, siku yalipo kutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu
ni Muweza wa kila kitu. ***
42. Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao
wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini yenu. Na ingeli kuwa mmeagana
mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Mwenyezi Mungu atimize
jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili
zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. ***
43. Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache - na lau
angeli kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli zozana katika
jambo hilo. Lakini Mwenyezi Mungu kakuvueni. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yalio
vifuani. ***
44. Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni wachache, na akakufanyeni
nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa liwe.
Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu. ***
45. Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi
Mungu sana ili mpate kufanikiwa. ***
46. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na
zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri. ***
47. Wala msiwe kama wale walio toka majumbani mwao kwa fakhari na kujionyesha
kwa watu, na wakawazuilia watu Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka
yote wanayo yafanya. ***
48. Na pale Shet'ani alipo wapambia vitendo vyao, na akawaambia: Hapana watu
wa kukushindeni hii leo, na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipo onana majeshi mawili,
akarudi nyuma, na akasema: Mimi si pamoja nanyi. Mimi naona msiyo yaona. Mimi
namwogopa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu. ***
49. Na walipo sema wanaafiki, na wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao: Watu hawa dini
yao imewadanganya. Na Mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu Ametukuka, na Mwenye hikima. ***
50. Na laiti ungeli ona Malaika wanapo wafisha wale walio kufuru wakiwapiga nyuso
zao na migongo yao, na kuwaambia: Ionjeni adhabu ya Moto! ***
51. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyo kwisha tangulizwa na mikono yenu, na hakika
Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja. ***
52. Kama ada ya watu wa Firauni na walio kuwa kabla yao - walizikataa Ishara
za Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa sababu ya madhambi yao.
Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na mkali wa kuadhibu. ***
53. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizo waneemesha
watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Mwwnyezi Mungu
ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. ***
54. Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao - walizikanusha Ishara
za Mola wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi yao. Na tukawazamisha watu
wa Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu. ***
55. Hakika vinyama vilio viovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao kufuru,
basi hao hawaamini; ***
56. Wale ambao miongoni mwao umepatana nao ahadi, kisha wanavunja ahadi yao kila
mara, wala hawamchi Mungu. ***
57. Basi ukiwakuta vitani wakimbize walio nyuma yao ili wapate kukumbuka. ***
58. Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie ahadi yao kwa usawa. Hakika
Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini. ***
59. Wala wasidhanie wale walio kufuru kwamba wao wametangulia mbele. La, wao
hawatashinda. ***
60. Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari,
ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo ambao hamwajui,
lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu
mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa. ***
61. Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye
ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. ***
62. Na wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu atakutosheleza. Kwani Yeye ndiye
aliye kuunga mkono kwa nusura yake na kwa Waumini. ***
63. Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli
weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika
Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima. ***
64. Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea wewe na Waumini walio kufuata. ***
65. Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani. Wakiwapo kati yenu ishirini wanao
subiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo kati yenu mia watawashinda elfu moja
katika walio kufuru. Kwa sababu wao ni watu wasio fahamu. ***
66. Sasa Mwenyezi Mungu amekupunguzieni, na anajua kuwa upo udhaifu kwenu. Kwa
hivyo wakiwa wapo watu mia moja kati yenu wenye kusubiri watawashinda mia mbili.
Na wakiwapo elfu moja watawashinda elfu mbili, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri. ***
67. Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika
nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu
ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima. ***
68. Lau isingeli kuwa hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu
ingeli kupateni adhabu kubwa kwa vile mlivyo chukua. ***
69. Basi kuleni katika mlivyo teka, ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu. ***
70. Ewe Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi akiona kheri
yoyote nyoyoni mwenu atakupeni bora kuliko vilivyo chukuliwa kwenu, na atakusameheni.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. ***
71. Ikiwa wanataka kukufanyia khiana, wao walikwisha mfanyia khiana Mwenyezi
Mungu kabla yake, na Yeye akakuwezesha kuwashinda. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kujua Mwenye hikima. ***
72. Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu
kwa mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa kukaa, na wakanusuru, hao
ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walio amini lakini hawakuhama, nyinyi
hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada
kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo
mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda. ***
73. Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipo fanya hivi itakuwako
fitna katika nchi na fisadi kubwa. ***
74. Na walio amini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu,
na walio toa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata
msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema. ***
75. Na watakao amini baadaye na wakahajiri, na wakapigana Jihadi pamoja nanyi,
basi hao ni katika nyinyi. Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe
zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua
kila kitu. ***
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@yahoo.com