SURA HII NI ya Makka, na idadi ya Aya zake ni 69. Lakini Aya 1 mpaka 11 ziliteremka
Madina. Sura hii imeanzia kwa kubainisha kwamba hapana budi ila Imani ya Waumini
itiwe mitihanini kwa misukosuko na jihadi kwa ajili ya kulinda dola ya Haki na
Imani. Na binaadamu ameusiwa kwa wazazi wake pamoja na amri ya jihadi, ili ukusanyike
wema na jihadi, na baina ya watu wa namna mbali mbali na Imani. Na imeelezwa kwamba
miongoni mwao yupo anaye sema kwa ulimi wake kwamba ameamini na hali moyo wake
haukukubali. Kisha Sura hii imetaja khabari za Nuhu na kaumu yake, na kadhaalika
imeeleza kisa cha Ibrahim katika wito wake. Na ikabainisha mafunzo hayo kwa ajili
ya Mtume s.a.w. Kisha ikasimulia jawabu ya watu wa Ibrahim. Na ikaeleza khabari
za Lut'i na kisa cha kaumu yake, na kuteremka kwa Wajumbe Malaika wa Mwenyezi
Mungu kuja kuwahiliki, na wakaokoka ahali zake isipo kuwa mkewe. Kisha Subhanahu
akaashiria kisa cha Shuaibu pamoja na Madyana, na cha Hud na A'di, na Saleh na
Thamud, na kudanganyikiwa kwa Qaruni na Firauni na Hamani na matokeo ya mwisho
wao. Na Yeye Subhanahu amebainisha kwamba kuabudu masanamu kwa washirikina kunategemea
hoja iliyo kuwa dhaifu kabisa kuliko jumba la buibui. Na kwamba mifano kama hii
hawaielewi ila wale wanao tumia akili zao. Na baada ya hayo Mwenyezi Mungu akamuamrisha
Nabii wake asijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia nzuri. Na Yeye Subhanahu
akaashiria kwamba Nabii s.a.w. hajui kusoma wala kuandika, na hayo yanazidi kuonyesha
Utume wake. Na pia Subhanahu ametaja ukaidi wa washirikina katika kutaka kwao
waletewe miujiza ya kuiona, nayo wataikataa kama walivyo ikataa kaumu ya Musa
na wengineo. Na akagusia kule kuhimiza kwao kuteremshiwa adhabu. Naye amewabainishia
adhabu itakayo wapata. Naye Subhanahu akataja malipo ya Waumini na Makafiri Siku
ya Kiyama, na akataka watu watazame baada ya hayo ulimwengu na neema za Mwenyezi
Mungu Mtukufu ziliomo ndani yake. Kisha akataja thamani ya uhai wa duniani ukilinganisha
na wa Akhera, na hali ya washirikina katika unyonge wao na kumkimbilia kwao Mwenyezi
Mungu wanapo kuwa katika khofu, na wanapo kuwa na nguvu na wakawa katika usalama
wanavyo mshirikisha Mwenyezi Mungu. Kisha akaeleza neema zake anazo wapa katika
Nyumba Takatifu ya Makka, na wanavyo zikanya neema hizo. Kisha Mwenyezi Mungu
akabainisha fadhila za wanao pigana Jihadi.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Alif Lam Mim (A.L.M.) ***
2. Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe? ***
3. Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha
walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo. ***
4. Au wanadhani wanao tenda maovu kwamba watatushinda? Hukumu mbaya hiyo wanayo
hukumu. ***
5. Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi
Mungu itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. ***
6. Na anaye fanya juhudi basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi
yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu. ***
7. Na walio amini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na tutawalipa
bora ya waliyo kuwa wakiyatenda. ***
8. Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia
unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi ndio
marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda. ***
9. Na walio amini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawatia miongoni mwa watu
wema. ***
10. Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapo
pewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu kama ni adhabu
ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika
sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu? ***
11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio amini, na atawatambulisha
wanaafiki. ***
12. Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba
makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni
waongo. ***
13. Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao.
Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua. ***
14. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka
khamsini. Basi tufani liliwachukua, nao ni madhaalimu. ***
15. Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na tukaifanya kuwa ni Ishara
kwa walimwengu wote. ***
16. Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na mcheni
Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua. ***
17. Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi.
Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote.
Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake
Yeye ndio mtarudishwa. ***
18. Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla yenu zilikwisha kadhibisha.
Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi. ***
19. Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha uumbaji, na kisha akarudisha
tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. ***
20. Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha
Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza
juu ya kila kitu. ***
21. Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa. ***
22. Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika mbingu. Wala nyinyi
hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. ***
23. Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye, hao ndio wenye
kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata adhabu chungu. ***
24. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto!
Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao
amini. ***
25. Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa
mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Kiyama mtakataana
nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makaazi yenu ni Motoni.
Wala hamtapata wa kukunusuruni. ***
26. Lut'i akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye
ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. ***
27. Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika dhuriya
zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika
Akhera bila ya shaka ni katika watu wema. ***
28. Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao
hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo. ***
29. Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu
mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo
adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli. ***
30. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa! ***
31. Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi hapana
shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu. ***
32. Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo
humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe aliye miongoni
mwa watao kaa nyuma. ***
33. Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa ajili yao, na moyo uliona
dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa
wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa watao kaa nyuma. ***
34. Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa
sababu ya uchafu wanao ufanya. ***
35. Na tumeacha katika mji huo Ishara ilio wazi kwa watu wanao tumia akili zao. ***
36. Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu!
Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msende katika ardhi
mkifisidi. ***
37. Lakini walimkanusha basi ukawatwaa mtikiso wa ardhi, wakapambazukiwa ndani
ya nyumba zao nao wamefudikia. ***
38. Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana na maskani
zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa
wenye kuona. ***
39. Na pia Qaruni na Firauni na Hamana! Na Musa aliwajia kwa Ishara waziwazi,
lakini walijivuna katika nchi, wala hawakuweza kushinda. ***
40. Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao wapo tulio
wapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walio nyakuliwa na ukelele;
na kati yao wapo ambao tulio wadidimiza katika ardhi; na kati yao wapo tulio wazamisha.
Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu
nafsi zao. ***
41. Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui
alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui,
laiti kuwa wanajua. ***
42. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanacho kiomba badala yake Yeye.
Na Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima. ***
43. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu ila wenye ilimu. ***
44. Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Kwa hakika katika hayo ipo
Ishara kwa Waumini. ***
45. SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia
mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa
kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda. ***
46. Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo
kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa
kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi
ni wenye kusilimu kwake. ***
47. Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa
Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo
watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri. ***
48. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa
mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka wavunjifu. ***
49. Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya walio pewa ilimu.
Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu. ***
50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema:
Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha
tu. ***
51. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanacho somewa?
Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao amini. ***
52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua
yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na wakamkataa Mwenyezi
Mungu, hao ndio walio khasiri. ***
53. Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana wakati maalumu
ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea kwa ghafla, na hali wao
hawana khabari. ***
54. Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa hakika imewazunguka
makafiri! ***
55. Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na
atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda! ***
56. Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni
Mimi peke yangu. ***
57. Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu. ***
58. Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao, ***
59. Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi. ***
60. Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi Mungu anawaruzuku
hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. ***
61. Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua na mwezi kuti'ii
amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanako geuzwa? ***
62. Mwenyezi Mungu humkunjulia, na humdhikishia, riziki amtakaye katika waja
wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. ***
63. Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha
ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu
Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao hawafahamu. ***
64. Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo. Na nyumba ya
Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua! ***
65. Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut'iifu.
Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha. ***
66. Wapate kuyakanya tuliyo wapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja jua! ***
67. Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine
wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu, na neema za Mwenyezi
Mungu wanazikataa? ***
68. Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu au
anaye kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya
makafiri? ***
69. Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu.
Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema. ***
Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com