* 1. Sura inaanza kwa Jina la Mwenyezi Mungu ambaye hapana
anayefaa kuabudiwa ila Yeye aliye sifika kwa kila sifa za ukamilifu, na
ametakasika na kila la upungufu. Yeye ndiye Mwenye rehema ambaye ananeemesha
kwa neema kubwa na ndogo, na za kuwapa wote, na za kuwapa walio khusika.
Na Yeye ndiye mwenye kusifika kwa sifa ya Rehema yenye kudumu. (Kauli ya
mwanzo aliyo semezwa Mtume s.a.w. na kuamrishwa na Mwenyezi Mungu ni "Iqra`
bismi Rabbika", yaani: "Soma kwa jina la Mola wako Mlezi!" Naye Mtume s.a.w.
amesema: "Jambo lolote lisilo anziwa kwa Bismillahi ni pungufu." Kila Sura
ya Qur'ani, isipo kuwa Sura Attawba, imeanziwa kwa Bismillahi Rrahmani
Rrahim.)
Rudi kwenye Sura
* 2. Sifa njema za namna yote na katika kila hali ni za Mwenyezi Mungu
pekee. Na tunamsifu Yeye kwa sifa zote kwa sababu Yeye ndiye mwenye kuviumba
viumbe vyote na mwenye kuviangalia na kuvilea. (Neno Rabb, kwa Kiarabu,
lina maana ya Ubwana na Ulezi na Utengenezaji. Ndiyo tukatumia Mola Mlezi.
Neno Baba lina upungufu.)
Rudi kwenye Sura
* 3. Na Yeye ndiye Mwenye rehema ya kudumu, na rehema inatokana naye.
Ananeemesha kwa neema zote ndogo na kubwa. (Arrahman ni jina lake Mwenyezi
Mungu tu, na hafai mtu kuitwa hivyo.)
Rudi kwenye Sura
* 4. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye kumiliki Siku ya Malipo na Hisabu,
yaani Siku ya Kiyama, anafanya atakavyo wala hapana mwenye kushirikiana
naye walau kwa kuonekana tu.
Rudi kwenye Sura
* 5. Hatumuabudu yeyote ila Wewe tu, wala hatutaki msaada kwa yeyote
ila kwako tu.
Rudi kwenye Sura
* 6. Tunakuomba utuwafikishe kuendea Njia ya haki, na kheri na mafanikio.
Rudi kwenye Sura
* 7. Na njia hiyo ndiyo ya waja wako ulio wawezesha kukuamini Wewe,
na ukawajaalia neema ya uwongofu na radhi, sio njia ya walio stahiki kupata
ghadhabu zako na wakaiwacha njia ya haki na kheri, kwa sababu hao wameitupa
imani kukuamini Wewe na kuelekea kwenye uwongofu wako.
(Hapana katika Vitabu vyote vitakatifu, vya dini zote, dua inayo lingana
na hii kwa uzuri wake, na utimilivu wake. Baada ya kumsifu Mwenyezi Mungu
kwa Rehema yake isio na ukomo wala kipimo, na kumshukuru Mola Mwenye kuviumba
na kuviangalia na kuvilea kwa huruma viumbe vyote, na kuhakikisha kuwa
tunajua kuwa hapana Mungu ila Yeye tu wa kuabudiwa na kuombwa msaada, na
kuwa hapana wa kumuingilia katika Ufalme wake na Uwezo wake wa kulipa hisabu
kwa kila alitendalo mtu, hapo tena ndio tunaomba. Na tunaomba nini? Si
mkate wa kula, wala riziki yoyote, wala jambo lolote la manufaa ya kimwili
duniani, bali tunaomba Uwongofu kwenye Njia Iliyo Nyooka, Njia ya kumwendea
Yeye Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema. Tunaomba tusiendee njia waliyo ifuata
wale walio kasirikiwa na Mwenyezi Mungu, kwa kuwa walifunzwa wakajua, lakini
kwa chuki na jeuri wakakataa kuongoka, wala sio njia ya wale ambao labda
kwa ujinga wamepotea. Hiyo kwa mukhtasari ndiyo Dua ambayo Waislamu, wanafunzwa
waiombe, na wanaiomba mara kadhaa wa kadhaa katika Sala zao, na katika
kila fursa inapo tokea.)
Rudi kwenye Sura