1. Alif Lam Mim Ra - Kwa kuanzia harufi hizi ni kunabihisha
muujiza wa Qur'ani, juu ya kuwa imeundwa kwa harufi hizi hizi zinazo tumiwa
kwa kusemea. Na pia kuwazindua watu waisikilize. Haya yaliyo tajwa katika
Sura hii ni Kitabu kilicho teremshwa kwako wewe, Muhammad, kutokana nasi,
ili uwatoe watu wote kwenye kiza cha ukafiri na ujinga waendee kwenye nuru
ya Imani na ilimu, kwa kusahilishiwa na Mola wao Mlezi. Na nuru hiyo ndiyo
Njia ya Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kwa kuadhibisha, na Mwenye kuhimidiwa
kwa kuneemesha.
Rudi kwenye Sura
2. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Mwenye kuumba na kumiliki
kila kiliomo mbinguni na kwenye ardhi. Ikiwa hii ndiyo hali ya Mungu wa
Haki, basi makafiri, wenye kukanya, watahilikika kwa adhabu iliyo kali.
Rudi kwenye Sura
3. Hao ndio walio khiari uhai wa duniani kuliko Akhera, na wanawazuia
watu wasifuate Sharia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotoa Sharia katika
macho ya watu ili wapate kuikataa. Hao ndio wanao elezwa katika yaliyo
tajwa kuwa wamepotelea mbali na Haki.
Rudi kwenye Sura
4. Na Sisi hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako, ewe Nabii, ila kwa
lugha ya kaumu yake ile tuliyo mtumia, ili apate kuwafahamisha aliyo kuja
nayo, na wao wayafahamu, na wayaelewe kwa wepesi. Wala si juu yake yeye
kuwa lazima waongoke. Mwenyezi Mungu Mwenyewe ndiye humwacha apotee anaye
mtaka kwa kuwa huyo si tayari kuitaka Haki. Na humwongoa amtakaye kwa kuwa
kajitayarisha vyema kufuata Haki. Naye Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu
ambaye hashindiki kwa atakalo, na ambaye anayapanga mambo yote kwa mahala
pao. Basi haachi kupotea wala haongoi ila kwa hikima yake.
Rudi kwenye Sura
5. Na tulimtuma Musa na tukamuunga mkono kwa miujiza yetu. Tukamwambia:
Watoe watu wako, Wana wa Israili, kwenye kiza cha ukafiri na ujinga uwapeleke
kwenye nuru ya Imani na ilimu, na uwakumbushe vituko na nakama aliyo wapelekea
Mwenyezi Mungu kaumu za kabla yao. Hakika katika kukumbusha huko zipo dalili
kubwa za kuthibitisha Upweke wa Mwenyezi Mungu, zinamlingania kwenye Imani
kila mwenye kuthibiti kuwa na ukamilifu wa kuweza kuvumilia balaa, na kushukuru
neema. Na hii ni sifa ya Muumini.
Rudi kwenye Sura
6. Ewe Nabii! Wakumbushe watu wako, huenda wakazingatia, wakati Musa
alipo waambia watu wake kwa kufuata amri ya Mola wako Mlezi: Kumbukeni
neema ya Mwenyezi Mungu kwenu, pale alipo kuvueni kutokana na kaumu ya
Firauni, nao wakikupatilizeni kwa adhabu ovu kabisa. Wakikufanyisheni kazi
ngumu, wakiwachinja watoto wenu wa kiume, na wakiwaacha wa kike na kuwaweka
katika unyonge na udhalili bila ya kuwauwa. Na mateso yote yaliyo tajwa
na kuokoka ni mtihani mkubwa unao toka kwa Mwenyezi Mungu, ili upate kudhihiri
uwezo wa kusubiri na kushukuru.
Rudi kwenye Sura
7. Na kumbukeni, enyi Wana wa Israil, pale Mola wenu Mlezi alipo
kufunzeni, na akasema: Wallahi! Mkishukuru kwa neema niliyo kupeni ya kukuvueni,
na mengineyo, kwa kuthibiti juu ya Imani na ut'iifu, basi hapana shaka
nitakuzidishieni neema yangu. Na mkiikanya neema yangu kwa ukafiri na maasi,
basi hakika nitakuadhibuni kwa adhabu ya kutia uchungu. Kwani adhabu yangu
ni kali kwa wanao kanya.
Rudi kwenye Sura
8. Na Musa aliwaambia watu wake walipo mpinga na kumkanya: Mkizikanya
neema za Mwenyezi Mungu, wala msishukuru kwa Imani na ut'iifu, nyinyi na
wote waliomo duniani, basi hakika hayo hayatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote.
Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, hahitajii shukra za wanao shukuru.
Yeye ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa dhati yake, bila ya yeyote kumhimidi.
Rudi kwenye Sura
9. Je! Haijakufikilieni khabari za walio tangulia kabla yenu? Kaumu
ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na kaumu nyenginezo zilizo kuja baada yao,
ambao hapana anaye wajua ila Mwenyezi Mungu kwa wingi wao. Hao walijiwa
na Mitume wao kwa hoja zilizo wazi kuthibitisha ukweli wao. Na hao wakaweka
mikono yao kwenye vinywa vyao, kwa mastaajabu na kukanya. Wakawaambia Mitume:
Sisi tunaikataa miujiza na ishara mlizo kuja nazo. Na hakika sisi tuna
shaka na hayo mnayo tuitia, mambo ya Imani na Tawhidi, ya kuwa Mungu ni
mmoja. Sisi hatukuyakinika na chochote, na tuna shaka nayo!
Rudi kwenye Sura
10. Mitume wakawaambia watu wao, kwa mastaajabu, kuvunja shaka zao
za kuwepo Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye ni Mmoja peke yake: Hivyo katika
kuwepo Mwenyezi Mungu Mmoja peke yake ipo shaka yoyote, na hali Yeye ndiye
Muumba mbingu na ardhi bila ya kuwepo mfano wa kuigiza? Na Yeye anakuiteni
apate kukusameheni baadhi ya madhambi mliyo yatenda kabla hamjaamini, na
anakuakhirisheni mpaka umalizike muda wenu! Hao watu wakawaambia Mitume
wao kwa kuudhi: Nyinyi si chochote ila ni watu tu, wanaadamu, kama sisi.
Hamna ubora wowote wa kukufadhilisheni juu yetu hata mpewe Utume. Mnataka
kwa huo wito wenu mtuzuie tusiabudu walio kuwa wakiabudu baba zetu! Basi
tuleteeni hoja iliyo wazi katika tunazo kwambieni.
Rudi kwenye Sura
11. Mitume wao wakawaambia: Sisi si chochote ila ni watu kama nyinyi,
kama mlivyo sema. Walakini Mwenyezi Mungu huwateua awatakaye miongoni mwa
waja wake akawapa Unabii na Utume. Wala hatuna sisi uwezo wa kukuleteeni
hoja mnayo taka ila Mwenyezi Mungu apendavyo. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu
tu peke yake ndio wategemee Waumini, na wamtegemee kwa kustahamilia inda
zenu na upinzani wenu.
Rudi kwenye Sura
12. Na sisi tuna udhuru gani wa kuacha kumtegemea Mwenyezi Mungu,
na Yeye ndiye aliye tuongoza kila mmoja wetu kwenye njia yake na maelekeo
yake aliyo mwekea, na akamlazimisha afuate katika Dini? Na hakika sisi
tunatilia mkazo tegemeo letu kwa Mwenyezi Mungu; na hapana shaka tutayavumilia
maudhi yenu ya inadi na kutaka miujiza. Na juu ya Mwenyezi Mungu peke yake
ndio humtegemea wanao tegemea.
Rudi kwenye Sura
13. Wakuu wa makafiri majabari wenye madaraka wakaazimia watumie
nguvu walipo shindwa wote kupambana kwa hoja na dalili. Wakawaambia Mitume
wao: Na liwe moja ya mawili. Ama tukutoeni katika nchi yetu, au muingie
katika dini yetu. Mwenyezi Mungu akawafunulia Mitume kwa wahyi: Tutawateketeza
hao makafiri kwa dhulma yao!
Rudi kwenye Sura
14. Na baada ya kuwateketeza tutakuwekeni nyinyi katika ardhi yao.
Na huko kuwekwa kwa Waumini ni kweli, hakika, kwa mwenye kukhofu kusimama
mbele yangu kwa ajili ya hisabu, na akakhofu ahadi yangu ya adhabu. Kwani
mwenye kuingia na khofu huwa mt'iifu.
Rudi kwenye Sura
15. Hao Mitume waliomba nusura wawashinde hao watu wao wanao wapinga,
baada ya kukata tamaa kuwa hawataamini tena. Mwenyezi Mungu aliwanusuru,
na wakafuzu, na akakhasiri kila mwenye kiburi, akakataa kumt'ii Mwenyezi
Mungu, akawa shadidi wa upinzani. (Haya yaliyo wapata Mitume huwapata watu
wa Mungu wote wanao wania Haki hata katika zama zetu. Ushindi wa mwisho
daima unakuwa kwa walio wema, hoja kuvumilia na kuendelea na kazi ya Mungu).
Rudi kwenye Sura
16. Kushindwa kwa hao madhaalimu kunatangulia hapa duniani, na baada
yake Akhera ipo adhabu ya Jahannamu. Huko watanyweshwa maji yanayo kirihi
kama usaha unao toka kwa watu wa Motoni!
Rudi kwenye Sura
17. Kunywa kwake ni taklifu, ni kama wanayagugumia, na wala hayeshi
kiu, kwani hayumkini kuyaonea tamu kwa ukarihi wake na uchafu wake! Na
mtu anakuwa ni kama amezungukwa na mauti kila upande kwa shida ziliopo,
na wala huko katika Jahannamu hafi akapumzika na yanayo mfika, bali kila
wakati anakuta adhabu nyengine kali zaidi.
Rudi kwenye Sura
18. Hakika hali za vitendo vya kheri wavifanyavyo makafiri duniani
na pato lake, kwa kuwa havikujengwa juu ya msingi wa Imani, hali yake ni
kama jivu. Ukaja upepo mkali ukalipeperusha siku ya kimbunga kilipo kaza.
Siku ya Kiyama hawapati chochote kutokana na vitendo vyao vya namna hivyo
vya duniani. Hayumkini wao kunafiika na chochote kutokana navyo, kwani
hivyo havina thawabu, kama mtu mwenye vumbi linalo peperuka katika upepo
asilo weza kulikamata. Na watu hawa wapotovu hujiona wenyewe ati kuwa ndio
wanafanya mema, na ilhali vitendo vyao viko mbali kabisa na Njia ya Haki.
Rudi kwenye Sura
19. Ewe unae semezwa! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu
na ardhi zisimame juu ya Haki kwa mujibu wa hikima yake? Na Mwenye kuweza
haya basi anaweza kukuteketezeni, enyi makafiri, na akitaka akaleta viumbe
wengine badala yenu nyinyi, ambao watakubali kuwepo kwake, na kwamba Yeye
ni Mmoja wa pekee.
Rudi kwenye Sura
20. Na kuondoa huko na kuleta si muhali wala si uzito kwa Mwenyezi
Mungu.
Rudi kwenye Sura
21. Makafiri wote watadhihiri kutoka makaburini kwao, waonekane kwa
ajili ya kuhisabiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kudhihiri huko hakuna
shaka, ni kama kwamba yametokea hivi sasa. Hapo wale wenye maoni ya kinyonge
miongoni mwa wafwasi watawaambia waongozi wenye kiburi: Sisi tulikuwa wafwasi
wenu katika kuwakanusha Mitume na kuwapiga vita, na kuzipuuza nasaha zao.
Basi je, hii leo, hamtuondolei kidogo baadhi ya adhabu? Wakubwa walio takabari
watasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu ametuongoa kwenye njia ya kuokoka,
na akatuwafikia, basi nasi tungeli kuongozeni na tungeli kuitieni muifuate
hiyo njia. Walakini sisi tumepotea na kwa hivyo tukakupotezeni nyinyi,
yaani tumekuchagulieni tuliyo jichagulia nafsi zetu. Na leo hii sisi na
nyinyi ni sawa sawa, tukisikitika au tukastahamili. Hapana pa kuikimbilia
adhabu hii!
Rudi kwenye Sura
22. Mwenyezi Mungu atapo pitisha amri yake ya kuwaneemesha wat'iifu
na kuwaadhibu wenye kuasi, Iblisi atawaambia wanao mfuata: Hakika Mwenyezi
Mungu amekuahidini ahadi ya kweli kukhusu kufufuliwa na malipo, na ameitimiza.
Na mimi nimekuahidini ahadi ya uwongo ya kwamba hakuna kufufuliwa, wala
malipo, nami nimekwenda kinyume na ahadi yangu. Nami sikuwa na nguvu nanyi
hata nikulazimisheni kunifuata. Lakini nimekuiteni kwa ushawishi wangu
wa upotovu, nanyi mkaja mbio kunit'ii. Basi msinilaumu kwa sababu ya ushawishi
wangu. Na zilaumuni nafsi zenu kwa kuniitikia. Wala mimi hii leo si wa
kukuokoeni na adhabu. Na nyinyi hamwezi kuniokoa mimi! Mimi leo nakataa
huko kunishirikisha mimi na Mwenyezi Mungu huko duniani mlipo kuwa mkinit'ii
kama mtumwa anavyo mt'ii bwana wake. Hakika makafiri watapata adhabu chungu.
Rudi kwenye Sura
23. Na Akhera wataingizwa wenye kuamini, na wakatenda vitendo vyema,
katika Mabustani yanayo pitiwa na mito chini ya majumba yake, kwa idhini
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na amri yake. Maamkio yao humo kutokana na Malaika
ni kufahamisha amani na utulivu.
Rudi kwenye Sura
24. Je, ewe mtu! Hujui vipi Mwenyezi Mungu alivyo fananisha neno
la Haki lilio zuri, na neno la uwongo lilio baya? Amelimathili neno
zuri lenye faida kuwa ni kama mti wenye manufaa. Asili yake ni mizizi iliyo
shikilia baraabara kwenye ardhi na matawi yake yamenyanyuka kuelekea mbinguni.
Rudi kwenye Sura
25. Hutoa matunda yake kila wakati aliyo uweka Mwenyezi Mungu yazae
kwa mapendekezo ya aliye yaumba. Hivyo hivyo ndio tamshi la Tawhid,
Upweke wa Mwenyezi Mungu, ni lenye kuthibiti katika moyo wa Muumini. A'mali
yake inapanda kwa Mwenyezi Mungu, na inamfikilia baraka zake na thawabu
zake kila wakati. Na Mwenyezi Mungu anawabainishia watu kwa mifano, anashabihisha
maana kwa vitu wavijuavyo ili Waumini wawaidhike.
Rudi kwenye Sura
26. Neno la uwongo baya mfano wake ni kama mti mbaya ulio ng'olewa,
umetupwa juu ya ardhi. Haukusimama imara. Hali kadhaalika neno la uwongo
lilio kataliwa halina uthabiti, kwa kuwa halikuungwa mkono na hoja.
Rudi kwenye Sura
27. Mwenyezi Mungu anawathibitisha imara wanao amini juu ya neno
la Haki katika uhai wa duniani na Siku ya Kiyama pia. Na Mwenyezi Mungu
huwabaidisha nalo neno hilo makafiri kwa kutojitengenezea wenyewe. Mwenyezi
Mungu hutenda atakavyo, akiwathibitisha baadhi na kuwaacha kupotea wenginewe.
Hapana wa kumtoa kombo kwa hukumu yake, wala mwenye kuurudisha uamuzi wake!
Rudi kwenye Sura
28. Ewe msikilizaji! Hebu huwaangalii hao washirikina ambao, badala
ya kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu ya kumleta Muhammad na Dini yake,
wakaingia kumkataa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wakawasabibisha wafwasi wao
kutumbukia katika nyumba ya hilaki kwa upotovu wao.
Rudi kwenye Sura
29. Na nyumba hiyo ndiyo Jahannamu wakiteswa kwa uvukuto wake. Na
makaazi maovu mno ni Jahannamu.
Rudi kwenye Sura
30. Na wakamfanyia Mwenyezi Mungu Mmoja wa pekee mifano ya masanamu
wakiyaabudu, kwa ajili ya kuwa natija ya vitendo vyao iwe kuwapoteza watu
wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu! Ewe Nabii! Waambie hao walio potea: Stareheni
na matamanio yenu, kwani marejeo yenu ni Motoni!
Rudi kwenye Sura
31. Ewe Muhammad! Waambie waja wangu walio sadiki, wakaamini, na
wakatenda mema: Shikeni Sala, na toeni baadhi ya tuliyo kuruzukuni katika
njia za kheri, kwa siri na kwa dhaahiri, kabla ya kufika siku ambayo haifai
kitu kupatana kibiashara wala hisani ya urafiki.
Rudi kwenye Sura
32. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye zianzisha mbingu na viliomo
ndani yake, na ardhi na viliomo ndani yake. Na akateremsha kutoka mawinguni
maji ya kumiminika. Na kwa sababu yake akakutoleeni riziki ya matunda,
na mazao mengine na miti. Na Yeye akakufanyieni vyombo vya baharini vikufaeni
vinakwenda na kupakia riziki zenu, na bidhaa zenu za biashara, kwa idhini
yake na kutaka kwake. Na akaifanya mito ya maji matamu ikunufaisheni kwa
kunywa nyinyi na kumwagia katika mashamba yenu.
Rudi kwenye Sura
33. Na akalifanya jua na mwezi yakufaeni daima dawamu, kwa mwangaza
na maslaha ya mimea na wanyama. Na akajaalia usiku ukufaeni kwa kupumzika
na mchana kwa kufanya kazi.
Rudi kwenye Sura
34. Na akakutengenezeeni yote mnayo yahitajia katika maisha yenu
ambayo anastahiki kuombwa, sawa sawa ikiwa mmemuomba au la. Na mkizihisabu
neema alizo kuneemesheni Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzidhibiti namna zake,
seuze idadi yake! Hakika huyo mwenye kukanya ambaye akalipa ukafiri kuwa
ni malipo ya neema alizo pewa, basi ni mwingi wa udhalimu na ukafiri!
Rudi kwenye Sura
35. Ewe Nabii! Ili watu wako wapate kuzingatia na waache ushirikina
wao, wakumbushe kauli ya baba yao Ibrahim baada ya kuijenga Alkaaba. Alisema:
Ewe Mola Mlezi! Ujaalie mji huu wenye Alkaaba uwe wa amani, ulindwe na
wenye kudhulumu. Na unibaidishe, niwe mbali, mimi na wanangu na ibada ya
masanamu.
Rudi kwenye Sura
36. Kwani masanamu yamepelekea kupotea watu wengi kwa kuyaabudu.
Basi katika dhuriya zangu, wenye kunifuata mimi na wakakuabudu Wewe
kwa ikhlasi, basi hao ni watu wa Dini yangu. Na wenye kuniasi kwa
kushika ushirikina, basi Wewe ni Muweza wa kuwaongoa, kwani Wewe ni Mwingi
wa maghfira na rehema.
Rudi kwenye Sura
37. Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewafanyia maskani baadhi
ya dhuriya zangu katika bonde la Makka ambalo halioti mimea, kwenye Nyumba
yako uliyo kataza isiingiliwe na kuvunjiwa hishima yake, na ukajaalia sehemu
za jirani yake ziwe na amani. Ewe Mola wetu Mlezi! Wakirimu wapate kushika
Sala karibu na Nyumba hii. Na zijaalie nyoyo za bora ya watu ziwapende
kwa kuizuru Nyumba yako. Na uwaruzuku matunda kwa kuletwa na hao watakao
kuja, ili wapate kushukuru neema yako kwa Sala na Dua.
Rudi kwenye Sura
38. Ewe Mola wetu Mlezi! Ni sawa sawa kwako tunayo fanya siri na
tunayo fanya dhaahiri. Kwani Wewe unajua maslaha yetu, na unatuonea huruma
zaidi kuliko sisi wenyewe. Na hapana lifichikanalo kwako hata likiwa dogo,
katika ardhi na katika mbingu. Basi hapana haja sisi ya kukuomba. Lakini
juu ya hivyo tunaomba kwa kuonyesha kuwa sisi ni waja wako, twanyenyekea
utukufu wako, na tunahitajia uliyo nayo, Wewe!
Rudi kwenye Sura
39. Alhamdulillahi, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu, aliye nipa juu
ya kuwa ni mzee wa miaka mingi, na nimekwisha kata tamaa ya kuzaa, Ismail
na kisha Is-haq! Hakika Mwenyezi Mungu anasikia na ananipokelea maombi
yangu.
Rudi kwenye Sura
40. Ewe Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nitimize Sala kwa inavyo takikana.
Na wawezeshe watimilize kadhaalika wale walio wa kheri katika dhuriya zangu.
Ewe Mola wetu Mlezi ipokee dua yangu kwa mapokezi ya kukubaliwa.
Rudi kwenye Sura
41. Ewe Mola wetu Mlezi! Nisamehe madhambi yaliyo niponyoka, na wasamehe
wazazi wangu, na Waumini wote, Siku itapo hakikishwa hisabu, na baadae
ikawa malipo.
Rudi kwenye Sura
42. Ewe Mtume! Wala usidhani kabisa kuwa Mola wako Mlezi ameghafilika
na vitendo wafanyavyo wenye kudhulumu, kuupiga vita Uislamu na Waislamu
wenyewe. Bali Yeye anaujua ukhalifu wao. Na amekadiria kuakhirisha kuwaadhibu
mpaka Siku nzito. Macho yao yatabaki yamekodoka, hawawezi kuyafumba, wala
kupepesa kwa kitisho watacho kiona.
Rudi kwenye Sura
43. Nao wako mbioni kumwendea anaye wita, vichwa vyao vimeelekea
juu mbinguni, macho yao hayapepesi hata wakitaka, na nyoyo zao tupu hazina
wazo lolote kwa wingi wa khofu.
Rudi kwenye Sura
44. Ewe Nabii! Waeleze watu khabari za vitisho vya Siku ya Kiyama
watapo sema walio zidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi: Mola wetu Mlezi,
tuakhirishie adhabu, uturejeshe duniani, na utupe muhula kwa muda mdogo,
walau tudiriki kuitikia wito wako wa Tawhidi na kuwafuata Mitume. Nao wataambiwa:
Leo ndio mwasema haya? Na mmesahau ya kwamba mliapa nyinyi ya kuwa
mkifa neema hizi hazitokuondokeeni mtapo fufuliwa Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
45. Na mkakaa duniani katika maskani zile zile za wale walio tangulia
kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi miongoni mwa kaumu zilizo kuwa
kabla yenu. Na ikadhihiri kwenu kwa kuona mabaki ya vile tulivyo waadhibu
wao, na nyinyi msiwaidhike. Na tukakuelezeni waliyo yafanya wao, na nini
kilicho wafika. Nanyi msizingatie.
Rudi kwenye Sura
46. Na wakapanga hao washirikina njama zao kutaka kuvunja Daa'wa,
yaani Wito. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hila zao. Wala vitimbi
vyao haviwezi kuiondoa Sharia iliyo thibiti imara kama milima.
Rudi kwenye Sura
47. Ewe Mtume! Usidhani kuwa Mwenyezi Mungu atawatupa Mitume wake
kwa kwenda kinyume na ahadi aliyo wapa kuwa atawanusuru. Kwani Yeye daima
ni Mwenye kushinda, hapana mmoja awezaye kumzuia kwa alitakalo, ni Mkali
wa kulipiza kwa anaye mkanya na kumuasi.
Rudi kwenye Sura
48. Basi Mwenyezi Mungu atalipizia Siku ya Kiyama itapo geuzwa ardhi
iwe ardhi nyengine sio hii ya sasa, na mbingu hali kadhaalika zigeuzwe
ziwe nyengine, na viumbe watolewe makaburini mwao kwa hukumu ya Mwenyezi
Mungu asiye na mshirika, wala wa kumshinda.
Rudi kwenye Sura
49. Utawaona makafiri Siku ya Kiyama wamefungwa pingu pamoja na mashetani
wao.
Rudi kwenye Sura
50. Ngozi zao zimepakwa lami inayo chiririka, imekuwa kama ndio nguo
juu ya ngozi zao. Na moto umewapamba na kuwagubika nyuso zao.
Rudi kwenye Sura
51. Wanafanyiwa hayo ili Mwenyezi Mungu apate kumlipa kila mmoja
wao kwa aliyo yachuma katika dunia. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu
Siku ya Kiyama, wala hapana kitu cha kumshughulisha.
Rudi kwenye Sura
52. Hii Qur'ani ni Tangazo la kuwanasihi na kuwaonya na kuwakhofisha
adhabu ya Mwenyezi Mungu, na ili wajue ya kwamba wakikhofu wakazingatia
kuwa hakika hapana mungu ila Mungu Mmoja, na ili wenye akili wakumbuke
utukufu wa Mola wao Mlezi, na kwa hivyo wajitenge mbali na yale yatayo
waletea hilaki.
Rudi kwenye Sura