1. Mwenyezi Mungu aliye takasika na kila ambalo lisio
laiki naye. Yeye ndiye aliye mchukua mja wake Muhammad wakati wa usiku
kutoka Msikiti Mtakatifu wa Makka kwendea Msikiti wa Mbali wa Baitul Muqaddas,
ambao tuliwabarikia wakaazi majirani wa Msikiti huo katika mahitaji yao,
ili tumwonyeshe baadhi ya Ishara zetu zenye ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha
kuwa Mimi ni Mungu Mmoja peke yangu, na ukubwa wa uwezo wangu! Hakika Mwenyezi
Mungu peke yake ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Rudi kwenye Sura
2. Na hakika hiyo Baitul Muqadda ilikuwa inakaliwa na Wana wa Israili
baada ya Musa, mpaka walipo fanya fisadi yao humo, wakafukuzwa hapo zamani.
Haya ijapo kuwa Sisi tulimpa Musa Taurati, na tukatia ndani yake uwongofu,
na tukawaambia: Msimfanye yeyote wa kumtegemezea mambo yenu isipo kuwa
Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
3. Nyinyi Wana wa Israili mmezalikana kutokana na wale watu safi
wema walio kuwa na Nuhu katika safina baada ya kuwa wameamini. Nasi tukawaokoa
wasizame. Basi mfanyeni Nuhu kuwa ndiye mwongozi wenu wa kumfuata, kama
walivyo mfanya wazee wenu walio tangulia. Kwani hakika yeye alikuwa mja
wa wingi wa shukrani kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake.
Rudi kwenye Sura
4. Na tukatekeleza hukumu yetu kwa Wana wa Israili katika tuliyo
yaandika katika Lauhun Mahfuudh, Ubao Ulio Hifadhiwa, ya kwamba watafanya
ufisadi katika Nyumba Takatifu (Baitul Muqaddas) bila ya shaka yoyote mara
mbili. Kila mara katika hizo itakuwa ni udhaalimu na uasi, na kuacha
hukumu za Taurati, na kuwauwa Manabii, na mtasaidiana katika madhambi,
na kwamba utawala wenu utaenea, na kutukuka na kupanda kichwa na kiburi
kwa dhulma zenu.
Rudi kwenye Sura
5. Na ulipo fika wakati wa kukuleteeni adhabu mara ya kwanza, tulikupatilizeni,
kwa sababu ya fisadi yenu, kwa kukusalitishieni watu wa kali kupigana.
Wakakuingilieni mpaka ndani ya majumba, hapana walicho kiacha, ili wakuuweni.
Na ahadi ya kukuadhibuni ilikuwa ni ahadi haina budi kutimizwa.
Rudi kwenye Sura
6. Kisha mambo yenu yalipo kaa sawa, na mkaongoka, na mkatengeneza
umoja wenu, na mkaacha ufisadi, tukakurejezeeni ushindi juu ya wale makhasimu
zenu. Nasi tukakuruzukuni mali na wana, na mkazidi kuwa wingi kwa idadi.
Rudi kwenye Sura
7. Na tukawambia: Mkifanya wema na mkamt'ii Mwenyezi Mungu, wema
wenu utakufaeni nafsi zenu duniani na Akhera. Na mkifanya uovu kwa maasi,
basi mnajiharibia nafsi zenu vile vile. Na utapo kuja wakati wa adhabu
pale mara ya mwisho katika zile mara mbili za ufisadi wenu katika nchi,
tutakupelekeeni maadui zenu, wafanye athari za uovu na madhila na huzuni
zidhihiri nyusoni mwenu. Na matokeo yake ni kuingia katika Msikiti wa Baitul
Muqaddas, wakauharibu kama walivyo ingia na wakauharibu mara ya kwanza,
wakateketeza watacho kipata kwa uteketezi mkubwa.
Rudi kwenye Sura
8. Asaa Mola wenu Mlezi akakurehemuni baada ya hiyo mara ya pili
pindi mkitubu. Na mkirejea kwenye ufisadi Nasi tutarejea kukuadhibuni.
Na tumeifanya Jahannam kuwa ndiyo gereza la kuwafungia makafiri!
Rudi kwenye Sura
9. Hakika hii Qur'ani inawaongoza watu kwenye njia ambayo ndiyo njia
iliyo kaa sawa kabisa kuliko njia zote, na ndiyo njia ya salama kabisa
ya kufikilia kwenye furaha ya kweli katika dunia. Na wabashirie wenye kumuamini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wenye kuit'ii Haki na wanatenda vitendo vyema,
kuwa watapata ujira mkubwa Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
10. Na hakika wale ambao hawaiamini Akhera tumewatengenezea adhabu
ya machungu makali.
Rudi kwenye Sura
11. Ni katika tabia ya mwanaadamu kufanya haraka katika kuwahukumia
watu kwa yanayo wapata, na katika kauli zake na vitendo vyake. Naye hukimbilia
kulingania shari kama anavyo lingania kheri. Naye hufanya haraka kumuapiza
kwa Mwenyezi Mungu amteremshia shari yule aliye mkasirisha, kama anavyo
fanya haraka kuomba kheri.
Rudi kwenye Sura
12. Na Sisi tumejaalia usiku na mchana, kwa namna yao na kupishana
kwao, kuwa ni alama zenye kuonyesha Upweke wetu na Uwezo wetu. Tukauondoa
mwangaza kwenye usiku, na kisionekane kitu. Na alama yake ni giza liso
kuwa na jua. Hiyo ni ishara kubwa. Na mchana tukaufanya wa kuangaza. Hapo
laonekana jua, ile ishara kuu, ili mpate kwenda mtakako wakati huo katika
kutafuta maisha yenu. Na katika kuja usiku na mchana mpate kujua idadi
ya miaka na hisabu za miezi na siku. Na Sisi tumekubainishieni kila kitu
kwa uwazi kwa sababu ya maslaha yenu, ili isimame hoja juu yenu baada kutimia
neema.
Rudi kwenye Sura
13. Na kila mtu tumemfungamanisha na a'mali yake, vitendo vyake,
kama koja lilioko shingoni. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu kilicho
andikwa vitendo vyake vyote. Atakiona kitabu hicho kiwazi iwe wepesi kwake
kukisoma.
Rudi kwenye Sura
14. Ataambiwa: Soma kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa duniani
alikuwa hajui kusoma. Soma kitabu cha a'mali zako. Hicho leo kinatosha
kukuhisabia na kukudhibitia vitendo vyako.
Rudi kwenye Sura
15. Mwenye kufuata njia ya Haki basi anajifaa mwenyewe, na mwenye
kuiacha basi anajipoteza mwenyewe. Wala hapana mwenye kubeba dhambi zake
akambebea dhambi za mwenginewe. Wala haitufalii kumuadhibu yeyote kwa kutenda
kitu kabla hatujampelekea Mtume kutoka kwetu amwonyeshe njia ya Haki na
kumkataza maovu.
Rudi kwenye Sura
16. Na pindi tukikadiria tangu azali katika Lauhun-mahfuudh kuwateketeza
watu wa mji fulani kwa mujibu wa hikima yetu, basi Sisi huwasalitisha wale
walio jidekeza kwa taanusi katika huo mji, wakafanya fisadi zao, wakaacha
njia ya Haki, na wakawafuata wenginewe bila ya kutambua, na kwa hivyo huo
mji wote tena hapo hustahiki kuangamizwa. Nasi huuangamiza vikubwa mno!
Rudi kwenye Sura
17. Na kaumu nyingi zilizo kuja baada ya Nuhu tuliziangamiza kwa
kuwaasi Manabii wao. Na yakutosha kuwa ni ishara ya Mola wako Mlezi kwamba
Yeye ni Mjuzi wa kila kitu kama kilivyo, kwa ujuzi wa Mwenye kuona. Naye
anazo khabari za dhambi za waja wake, na Mwenye kuziona. Hapana chochote
katika vitendo vya waja wake asicho kijua, na Yeye atawalipa kama wanavyo
stahiki.
Rudi kwenye Sura
18. Mwenye kutaka starehe za dunia hii ipitayo na akazitumikia kwa
kutafutia kisingizio, wala asiwe na yakini na miadi, na wala asingojee
malipo ya Akhera, tutamletea haraka haraka tuyatakayo ya duniani kwa ukunjufu
na wasaa. Haya ni kwa tumtakaye kumletea haraka. Kisha tutamuandalia kwa
Akhera Jahannamu ahilikike kwa joto lake, naye hali awe ni mwenye kushutumiwa
kwa aliyo yatenda, mwenye kutengwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
19. Na mwenye kuitaka Akhera kwa vitendo vyake, naye akawa navyo
hivyo vitendo, na akawa anamuamini Mwenyezi Mungu na malipo yake, basi
watu kama hao vitendo vyao vitakubaliwa na Mwenyezi Mungu na watapata malipo
kwa ajili yake.
Rudi kwenye Sura
20. Na Sisi tutawakunjulia neema za Mola wako Mlezi hapa duniani
makundi yote mawili, pindi wakichukua khatua ya kufikia hayo. Wala neema
za Mola wako Mlezi hatonyimwa yeyote, akiwa Muumini au akiwa kafiri, maadamu
wakishika njia za kuzitafuta.
Rudi kwenye Sura
21. Hebu angalia kwa kuzingatia vipi tulivyo wafadhilisha baadhi
ya waja wetu kuliko wengine, kwa kuwapa mali na vyeo na nafasi, pindi wakishika
njia za kuyapata hayo katika dunia. Na hayo ni kwa hikima tunayo ijua Sisi.
Na tafauti zao katika Akhera ni kubwa zaidi kuliko tafauti zao za duniani.
Kwa hivyo yatakikana waishughulikie Akhera, kwani huko ndiko kwenye kutukuka
kwa kweli na kuzidiana kwa hakika.
Rudi kwenye Sura
22. Ewe mwenye jukumu! Usimfanyie Mwenyezi Mungu kuwa na mshirika,
utakuja fedheheka kwa kudharauliwa, na utajaaliwa uwe mwenye kutupika.
Rudi kwenye Sura
23. Na Mola wako Mlezi amehukumu kuwa msimuabudu yeyote isipo kuwa
Yeye. Na pia muwafanyie wema kwa ukamilifu wazazi wenu wawili. Na hao,
au mmoja wao, wakifikilia kwako hali ya unyonge na mwisho wa umri wao,
basi lisikutoke tamko la kuchoka nao au kuudhika kwa yanayo kupata kutokana
nao. Wala usiwahamakie. Na nena nao maneno mazuri, laini, yenye kuwaonyesha
ihsani na kuwahishimu.
Rudi kwenye Sura
24. Na wafanyie upole, na wanyenyekee kwa kuwaonea huruma, na uwaombee:
Ewe Mola Mlezi! Warehemu wote wawili, kama walivyo nifanyia huruma walipo
nilea utotoni.
Rudi kwenye Sura
25. Enyi watu! Mola wenu Mlezi anajua kuliko nyinyi yaliyomo katika
dhamiri zenu, na atakuhasibuni kwayo kwa thawabu na i'kabu. Na mkiwa mnakusudia
wema na mkautenda, tena mkatokea baadhi yenu mkateleza, na kisha mkarejea
kwa Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Subhanahu atakusameheni. Kwani
Yeye ni Mwenye kusamehe daima kwa wale wanao rejea kwake.
Rudi kwenye Sura
26. Na wape jamaa zako haki yao kwa kuwafanyia wema na kuwaunga;
na kadhaalika masikini mwenye haja, na msafiri aliye katikana na mali yake.
Wape hao haki yao katika Zaka na sadaka, wala usiyavuruge mali yako kwa
utumiaji ovyo usio na maslaha.
Rudi kwenye Sura
27. Kwani wabadhirifu (watumiaji ovyo) wenzao ni Mashetani, wanapokea
minong'ono yao wanapo wachochea wafanye ufisadi na watumie kwa uharibifu.
Na ni mtindo wa Shetani daima kukufuru neema ya Mola wake Mlezi. Na sahibu
yake ni hali kadhaalika.
Rudi kwenye Sura
28. Ukilazimika kujikurupusha na hao walio tajwa wenye haja, kwa
sababu ya shida uliyo nayo, na ukawa hukuwapa kwa kuto kuwa nacho cha kuwapa
sasa, na ilhali unataraji Mwenyezi Mungu atakufungulia baadae, basi nena
nao kwa maneno mema ya kuwapa imani nawe.
Rudi kwenye Sura
29. Wala usiuzuilie mkono wako kutoa katika mambo ya kheri, ukaufanya
kama ulio fungwa pingu za chuma shingoni mwako ukawa huwezi kuukunjua.
Wala usiukunjue wote kabisa kwa kutumia ovyo. Utakuja tukanika kwa ubakhili
na majuto, au utabaki huna kitu umefilisika kwa sababu ya ubadhirifu na
israfu.
Rudi kwenye Sura
30. Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye katika waja
wake, na humdhikisha katika wao amtakaye. Kwani Yeye anawajua vyema tabia
zao, na anaziona hali zao. Basi Yeye humpa kila mmoja wao, pindi akishika
njia zake, kwa inavyo wafikiana na hikima yake Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
31. Ikiwa yaliyo khusiana na riziki yamo mikononi mwa Mwenyezi Mungu,
basi haikufaliini kuwauwa watoto wenu kwa kukhofu ufakiri utao weza kutokea.
Kwani Sisi ni Wenye kudhamini riziki zao na riziki zenu. Hakika kuwauwa
hao ni dhambi kubwa.
Rudi kwenye Sura
32. Wala msiukaribie uzinzi, kwa kuziingilia sababu zinazo pelekea
uzinzi. Jambo hilo ni jambo la aibu na uovu usio fichikana, na hapana njia
mbovu kama hiyo.
Rudi kwenye Sura
33. Wala msiuwe nafsi yoyote ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa
ila kuuwa huko kukiwa kwa haki, kwa kuwa nafsi hiyo inastahiki kuuwawa
kwa ajili ya kisasi au kuwa ni adhabu ya sharia. Na mwenye kuuliwa kwa
kudhulumiwa Sisi tumempa jamaa yake wa karibu haki juu ya yule muuwaji,
kwa kutaka kwa Qadhi auliwe kwa kisasi. Lakini naye asipite mpaka katika
kuuwa, akataka kumuuwa mtu mwengine asiye kuwa muuwaji, au kwa kuwauwa
wawili badala ya mmoja. Kwani Mwenyezi Mungu amemsaidia huyo kwa kumpa
haki ya kisasi au kulipwa fidiya. Basi haimfalii kukiuka mipaka iliyo wekwa.
Rudi kwenye Sura
34. Wala msiyatumie mali ya yatima ila kwa njia iliyo bora kabisa,
ya kuiamirisha na kuikuza. Na endeleeni hivyo mpaka huyo mtoto afike umri
wa utambuzi kuweza kuendesha mambo yake. Na akisha fika hivyo basi mkabidhini
mali yake, na timizeni ahadi zote mlizo chukua. Kwani Mwenyezi Mungu atamsaili
aliye vunja ahadi kwa kuvunja kwake, na atamhisabia kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
35. Na mnapo mpimia mushtiri mpimieni vilivyo, na pimeni mizani kwa
uadilifu. Kwani kuweka sawa vipimo na mizani ni bora kwenu kwa hapa duniani,
kwa sababu huwaraghibisha watu kufanya nanyi biashara. Na malipo mazuri
zaidi ni ya Akhera.
Rudi kwenye Sura
36. Ewe mtu! Usifuate maneno wala vitendo usivyo vijua. Basi usiseme:
Nimesikia...na hali hukusikia. Au: Najua...na hali hujui. Kwani masikio,
macho na moyo, vyote hivyo Siku ya Kiyama vitamuuliza mtu kwa alivyo tenda
kwavyo.
Rudi kwenye Sura
37. Wala usitembee katika ardhi kwa kiburi na majivuno. Kwani vyovyote
utavyo fanya huwezi kuipasua ardhi kwa nguvu za mkanyago wako, na kama
utavyo kuwa mrefu huwezi kuipita urefu milima.
Rudi kwenye Sura
38. Yote hayo yaliyo tajwa katika mausio ni mambo mabaya yaliyo katazwa
na yanayo chusha na kuchukiza kwa Mola wako Mlezi.
Rudi kwenye Sura
39. Na hayo ni katika aliyo kufunulia Mola wako Mlezi, katika kuijua
haki kwa dhati yake, na kheri ipate kutendwa. Wala usimfanyie Mwenyezi
Mungu kuwa na mungu mwengine, usije kutupwa katika Jahannamu ukijilaumu
na ukilaumiwa, umeangamia na umefurushwa mbali na rehema za Mola wako Mlezi.
Rudi kwenye Sura
40. Subhanahu anayachukia wayasemayo makafiri kwamba Malaika ni mabinti
wa Mwenyezi Mungu. Anasema: Mola wenu Mlezi amekufadhilisheni kuliko Mwenyewe
kwa kukupeni nyinyi watoto wanaume wenye nguvu, na Yeye akawafanya Malaika
ni banati zake kwa mnavyo dai? Kwa maneno yenu haya mnazua matusi
makubwa.
Rudi kwenye Sura
41. Sisi tumebainisha katika Qur'ani hii kwa uwazi mzuri, tukipiga
mifano na kutoa mawaidha na hukumu, ili wapate kwaidhika hawa washirikina.
Lakini nyoyo zao zimekuwa kama mawe. Kubainisha huku hakukuwazidishia ila
kuzidi kuwakimbiza na Haki.
Rudi kwenye Sura
42. Ewe Nabii! Ili kudhihirisha upotovu wa madai yao wanao mshirikisha
Mwenyezi Mungu, sema: Lau kuwa wapo miungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu
kama wasemavyo, hao miungu wangeli tafuta njia kumfikilia huyo Mwenye Ufalme
wa mwisho ili wapate kushindana naye.
Rudi kwenye Sura
43. Mwenyezi Mungu ametakasika kabisa kama anavyo stahiki, na ametukuka
aliye mkuu shani yake na yote wanayo dai kuwa wapo pamoja na Yeye
miungu wengine.
Rudi kwenye Sura
44. Hakika mbingu saba na ardhi, na viumbe vyote viliomo humo, vinamtakasa
na kumtukuza, na vinaonyesha uzuri wa kuumba kwake, na kutakasika kwake
Subhanahu na kila upungufu, na kukamilika ufalme wake, na kwamba Yeye hana
mshirika na yeyote katika viumbe wa Ufalme wake uliyo enea. Vyote hivyo
vinamtakasa na kumsifu. Lakini makafiri hawafahamu hoja hizi kwa kutawaliwa
nyoyo zao na mghafala. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwao, na Mwenye kuwasamehe
wanao tubu. Kwa hivyo hawafanyii haraka kuwapa adhabu.
Rudi kwenye Sura
45. Ewe Nabii! Unapo soma Qur'ani inayo taja dalili za Haki, Sisi
huweka pazia, lenye kukuficha baina yako na wale wasio amini kufufuliwa
na malipo, pale wanapo taka kukushambulia. Kwa hivyo hawakuoni.
Rudi kwenye Sura
46. Na kwa mujibu wa hikima yetu ya kupotoa na kuongoa huweka vifuniko
juu ya nyoyo zao, wasipate kuifahamu Qur'ani ilivyo. Na katika masikio
yao hutia uziwi basi hawasikii lenye manufaa kwao. Hayo ni kwa sababu ya
kupindukia katika inda yao na majivuno yao. Na pale unapo mtaja Mola wako
Mlezi katika Qur'ani peke yake bila ya kuwataja miungu yao, wao basi hurejea
nyuma wakaacha kukusikiliza.
Rudi kwenye Sura
47. Sisi tunajua vyema vile wanavyo isikiliza Qur'ani nao ilhali
wanaikejeli na kuifanyia maskhara na huku wanakusikiliza. Nao wanayaficha
yaliyo semwa. Na hiyo ndiyo kauli ya wenye kudhulumu katika siri zao, wakisema:
Ikiwa mtamfuata huyu basi hamumfuati ila mtu aliye geuzwa akili yake.
Rudi kwenye Sura
48. Hebu angalia vipi walivyo kushabihisha; wamekushabihisha na mtu
aliye rogwa, na wakakuita kohani, mtunga mashairi, wakaipotea njia ya hoja.
Kwa hivyo wasiweze kupata njia ya kuzua tusi linalo kubalika, au kwa hivyo
wakaukosa uwongofu, na wasiipate njia ya kuufikilia.
Rudi kwenye Sura
49. Wanao kataa kuwa watafufuliwa wanasema: Hivyo tutafuliwa
baada ya kwisha kuwa mafupa yaliyo bunguliwa, na mapande mbali mbali, tukawa
hai na umbo jipya? Haya hayaingii akilini.
Rudi kwenye Sura
50. Ewe Nabii! Waambie: Hata mkiwa mawe yasiyo na uhai, au
chuma, ambacho ni kigumu kuliko jiwe,
Rudi kwenye Sura
51. Au umbo jingenelo lolote ambalo mnaona kwa mawazo yenu haliwezi
kuwa hai, basi hapana shaka yoyote mtafufuliwa! Watasema kwa kuona ni muhali:
Nani atakaye turejesha hivyo? Waambie: Atakurjesheeni Mwenyezi Mungu, yule
yule aliye kuumbeni mara ya kwanza. Watakutikisia vichwa vyao kwa mastaajabu,
nao wakisema kwa kejeli: Huko kufufuliwa unako tuahidi kutakuwa lini? Waambie:
Nataraji kutakuwa karibu!
Rudi kwenye Sura
52. Na siku atapo kufufueni Mwenyezi Mungu kutoka makaburini kwenu,
mtafufuliwa nanyi mkimshukuru na kumsifu Mola wenu Mlezi kwa ukamilifu
wa uwezo wake. Na mtadhani kuwa hamkukaa makaburni kwenu ila muda mchache
tu. Mtaona muda ni mfupi kwa mnasaba ya hayo mnayo yaendea.
Rudi kwenye Sura
53. Ewe Nabii! Waambie waja wangu Waumini wanapo pambana na washirikina
waseme maneno yaliyo bora ya kukinaisha, na waachilie mbali kutumia maneno
makali makali yanayo sabibisha shari na uharibifu. Kwani Shetani huleta
fisadi baina ya Waumini na makafiri, kwa kuwa yeye ni adui aliye wazi wa
binaadamu.
Rudi kwenye Sura
54. Mola wenu Mlezi ndiye anaye jua vyema mwisho wa mambo yenu. Akipenda
atakurehemuni kwa kukupeni tawfiki ya Imani, (uwezo wa kuamini) au akipenda
atakupeni adhabu kwa kuikosa hiyo Imani. Wala Sisi hatukukupeleka wewe
uwe ni mwakilishi wao kwa mambo yao, hata uwalazimishe kuamini. Bali tumekutuma
uwe ni mbashiri kuwapa khabari njema wenye kusadiki, na mwonyaji kuwaonya
wanao kanusha. Waachilie mbali, na waamrishe sahaba zako wawastahamilie.
Rudi kwenye Sura
55. Na Mola wako Mlezi anajua vilivyo vyote viliomo mbinguni na ardhini,
na anajua hali zao. Basi anawakhiari miongoni mwao kwa kuwapa Unabii awatakao.
Naye amekukhiari wewe kwa kukupa Utume wake. Basi haiwafalii wao kuudhika
na Unabii wako. Na hao Manabii si wote sawa sawa kwa daraja mbele yake
Aliye tukuka shani yake. Bali baadhi yao ni bora kuliko wenginewe. Naye
amewatukuza baadhi ya Manabii juu ya wengine kwa miujiza, na wingi wa wafwasi,
si kwa ufalme. Basi alitukuzwa Daudi kwa kuwa kapewa Zaburi, si kwa kuwa
kapewa ufalme. Basi hapana ajabu kuwa wewe, Muhammad, ukapata fadhila kubwa
kabisa kwa kuwa umepewa Qur'ani.
Rudi kwenye Sura
56. Waambie hawa wanao abudu viumbe na wanadai kuwa hao ni miungu
badala ya Mwenyezi Mungu: Waombeni hao mnao waabudu inapo kuteremkieni
shida, au mkakhofu kuwa itakushukieni. Hamtopata kwao chochote cha kukuondoleeni
madhara yenu, wala kuyahamisha akapewa mwinginewe.
Rudi kwenye Sura
57. Na hakika hawa viumbe wanao waomba wale wanao waabudu, wao wenyewe
wanamuabudu Mwenyezi Mungu, na wanaomba wapate daraja na cheo kwake kwa
ut'iifu, na wana pupa ya kutaka wawe karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, na
wanatumaini kupata kwake rehema, na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu
ya Mwenyezi Mungu inatakikana kutahadhari nayo na kuiogopa!
Rudi kwenye Sura
58. Na ni mazoea yetu kuuteketeza kila mji na watu wake unapo dhulumu
mji huo. Au huwapa adhabu kali watu wake kwa mauwaji au vyenginevyo. Basi
watu wako watahadhari, kwani hukumu yetu imekwisha hukumiwa, na imekwisha
andikwa katika Kitabu chetu.
Rudi kwenye Sura
59. Watu wako wamekutaka uwaletee Ishara na miujiza. Nao hawakukinaika
kwa yaliyo wajia ambayo huwakinaisha wenye akili. Na mwendo wetu
umekwisha wapitia hao wanao taka miujiza, na wanapo kubaliwa wasiamini,
nao ni kuwang'olea mbali kwa adhabu kama tulivyo wafanyia wa kale.
Miongoni mwa hao ni watu wa Thamud. Walitaka miujiza, akawa ngamia mke
ni muujiza wazi kwao wa kuondoa shaka zote. Wakamkanusha, yakatokea kwao
yaliyo tokea! Na imekuwa hikima ya Mwenyezi Mungu kuwa asiwakubalie hayo
waliyo yataka, kwa kuchelea wasiikatae miujiza, kwa kutarajia watakuja
amini miongoni mwao, au watakuja zaa watakao amini. Na miujiza hakika Sisi
huwapelekea watu kwa kuwatia khofu na kitisho.
Rudi kwenye Sura
60. Ewe Nabii! Kumbuka tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amewazunguka
hao watu. Wao wamo wamedhibitiwa na kudra yake. Basi wewe wafikishie Ujumbe
wala usimwogope yeyote katika wao. Mwenyezi Mungu atakulinda nao. Na mambo
ya ajabu uliyo yaona katika Usiku wa Israi (Safari ya Usiku), hatukuyafanya
Sisi ila yawe ni mtihani na majaribio kwa wanaadamu. Kwa hayo ipate kuzidi
Imani ya Muumini, na ukafiri wa kafiri. Na wala hatukuufanya ule mti ulio
subiwa katika Qur'ani, nao ni Mti wa Zaquum, unao mea huko Motoni, isipo
kuwa ni kuwafanyia wao pia mtihani pale walipo sema: Moto unaunguza
mti, basi vipi mti umee katika moto? Pia ni kuzidi kuwahadharisha kwa hayo.
Lakini kuwahadharisha kwetu hakuwazidishii isipo kuwa kupindukia kiwango
kikubwa kabisa.
Rudi kwenye Sura
61. Na Mwenyezi Mungu anakumbusha asli ya kuumba na uadui baina ya
mwanaadamu na Iblisi, pale alipo waambia Malaika: Msujudieni Adam kwa kumuamkia
na kumhishimu kwa kumuinamia. Hapo hapo wakasujudu. Isipo kuwa Iblisi akakataa,
na akasema kwa chuki: Vipi nimsujudie uliye muumba kwa udongo, na hali
mimi umeniumba kwa moto. Mimi ni bora kuliko yeye.
Rudi kwenye Sura
62. Iblisi akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hebu nambie khabari za
huyu uliye mtukuza juu yangu, ukaniamrisha nimsujudie. Kwa nini ukamtukuza
kuliko mimi, na mimi ni bora kuliko yeye? Naapa kwa Utukufu wako! Ukinibakisha
nihai mpaka Siku ya Kiyama, basi nitawahiliki dhuriya zao watao wazaa kwa
kuwaghuri, isipo kuwa wachache tu kati yao utakao walinda na kuwahifadhi.
Rudi kwenye Sura
63. Mola akamwambia kwa kumtisha na kumlegezea kamba: Endelea na
shani yako uliyo jichagulia kuifuata. Atakaye kut'ii wewe katika wana wa
Adam, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yako na yao, malipo ya kutosha
yaliyo kamilika.
Rudi kwenye Sura
64. Na wazuge na wavute kwa kuwaita wamuasi Mwenyezi Mungu hao unao
waweza miongoni mwao. Na fanya kila juhudi yako ya namna zote za udanganyifu.
Na shirikiana nao katika kuchuma mali ya haramu, na kuyatumia kwa haramu,
na kuwakufurisha watoto na kuwaghuri wafanye fisadi. Na wape ahadi za uwongo,
kama kuwa miungu yao itawaombea, na kuwa watapata utukufu kwa Mwenyezi
Mungu kwa sababu ya nasaba zao. Na Shetani hawaahidi wafwasi wake ila kwa
udanganyifu na uficho.
Rudi kwenye Sura
65. Ama waja wangu walio nisafia niya Mimi wewe huna uwezo wa kuwapotoa,
kwa kuwa wao wanamtegemea Mola wao Mlezi. Na Yeye anatosha kabisa kuwa
ni wa kuwanusuru wakimtaka msaada wa kusalimika nawe.
Rudi kwenye Sura
66. Mola wenu Mlezi ni Yeye peke yake ndiye anaye ziendesha marikebu
baharini ambazo kwazo nyinyi mnatafutia manufaa kwa biashara na mengineyo.
Yeye daima ni Mwenye rehema kwenu.
Rudi kwenye Sura
67. Mkisibiwa na madhara na mkakabiliwa na khatari katika bahari,
hukukimbieni wote hao muwaombao kwa haja zenu isipo kuwa Mwenyezi Mungu
peke yake. Kwani nyinyi hapo hamumkumbuki mwenginewe. Lakini akisha kuvueni
na kuzama na akakufikisheni nchi kavu, mnaacha Tawhid, kumuabudu Mwenyezi
Mungu Mmoja, na mnakufuru neema. Ndio mtindo wa binaadamu daima kukataa
neema.
Rudi kwenye Sura
68. Na hapo tukisha kuvueni mkafika nchi kavu, kwani ndio mmeaminisha
kuwa basi haikupateni adhabu ya Mwenyezi Mungu? Hasha! Akitaka anaweza
akaipindua ardhi ikakuteketezeni chini yake. Na akitaka atakupelekeeni
upepo mkali ukutupieni kokoto na mawe, na wala msipate wa kukulindeni na
yanayo kupateni.
Rudi kwenye Sura
69. Au nyinyi mmeaminisha kuwa Mola wenu Mlezi hatakurejesheni tena
baharini, na akuleteeni tufani la upepo livunjilie mbali hicho chombo chenu?
Akakuzamisheni kwa sababu ya kuto thamini neema yake pale alipo kuokoeni
mara ya kwanza? Tena hapo hamtapata wa kukuteteeni kwetu kwa tuliyo kufanyieni
ili mpate kusalimika.
Rudi kwenye Sura
70. Na hakika Sisi tumewatukuza wana wa Adam kwa kuwapa umbo zuri
lilio nyooka, na matamshi, na uwezo wa kukhiari mambo. Na tukawapa hishima
na utukufu pindi wakit'ii. Na tukawapakia nchi kavu juu ya wanyama, na
baharini katika marikebu, na tukawaruzuku vitu vitamu, na tukawafadhilisha
fadhila kubwa kuliko viumbe vingi kwa kuwapa akili na kuweza kufikiri.
Rudi kwenye Sura
71. Ewe Nabii! Waambie watu wako: Siku tutapo waita kila kikundi
kwa alama zao wanazo zijua, au mwongozi wao wanaye mfuata, au Nabii, au
Kitabu wakaambiwa: Enyi watu wa Musa! Au Enyi watu wa Qur'ani! Na kadhaalika,
ili wapokee vitabu vya a'mali zao. Basi atakaye pokea kitabu cha a'mali
zake kwa mkono wake wa kulia, na hao ndio wenye bahati njema, hao watasoma
kitabu chao kwa furaha. Na wala hawatapunguziwa katika ujira wao
duni ya kitu.
Rudi kwenye Sura
72. Ama yule wa kikundi kingine yatamhuzunisha atayo yaona. Na atazibiwa
njia za kuokoka. Na atakuwa kipofu asione pa kuepuka adhabu yake, kama
alivyo kuwa duniani kipofu haioni Njia ya Haki na Uwongofu! Na anaye kuwa
duniani kipofu (wa moyo) basi Akhera ni kipofu zaidi, na yu mbali zaidi
na Njia ya Kheri.
Rudi kwenye Sura
73. Hakika washirikina wanatafuta kila njia wakuachishe Qur'ani utafute
miujiza myengineyo, ili uwe kama uliye tuzulia Sisi uwongo. Na hapo ndio
watakufanya uwe rafiki yao! Na hila hizi zimekaririwa na zimekuwa nyingi.
Na kwa hivyo ungeli karibia kuyafuata wayatakayo, ila kwa kuwa wewe ni
Mtume wetu uliye muaminifu, hayakuwa hayo.
Rudi kwenye Sura
74. Upole wetu umekugubika wewe, tukakulinda usiwakubalie matakwa
yao, na tukakupa nguvu usimame juu ya Haki. Na lau kuwa si hayo ungeli
karibia kuwakubalia kwa tamaa ya kuwa huenda ikafika siku imani yao ikakamilika
baadae wakisha anza kuingia katika Uislamu.
Rudi kwenye Sura
75. Na lau ungeli karibia kuwaelekea hao, basi tungeli kukusanyia
adhabu za duniani tukazifanya mardufu, na adhabu za Akhera nazo tukaziongeza
mara mbili vile vile. Na wala usingeli pata yeyote wa kukunusuru na adhabu.
Lakini hayo hayawi kabisa, hayawezi kumfikilia Mtume wetu Muaminifu.
Rudi kwenye Sura
76. Na makafiri wa Makka wamejaribu, na walikaribia kukuudhi mpaka
wakutoe kwenye ardhi ya Makka kwa uadui wao na chuki zao. Na lau yangeli
kuwa hayo, basi wao nao wasingeli baki humo ila muda mchache tu, kisha
washindwe katika hayo mambo yao, na hukumu iwe ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
77. Na huo ndio mwendo wetu kwa Mitume wa kabla yako - huwahiliki
wale wanao wafukuza Manabii wao. Na wala hapana mabadiliko katika mwendo
wetu.
Rudi kwenye Sura
78. Shika Sala zilizo faridhiwa, tangu kupinduka jua kati ya mbingu
kuelekea upande wa machwea jua, mpaka kiza cha usiku. Na hizi ndizo Sala
za Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha. Na pia shika Sala ya Alfajiri
ambayo wanaishuhudia Malaika.
Rudi kwenye Sura
79. Na katika wakati wa usiku amka, kwa kusali Sala ya Tahajjud.
Hiyo ni ibada ya zaidi juu ya zile Sala Tano. Hii imekukhusu wewe tu, kwa
kutaraji kuwa Mola wako Mlezi atakuweka Siku ya Kiyama makamo watakao kusifia
viumbe.
Rudi kwenye Sura
80. Na sema: Ewe Mola Mlezi! Niingize maingizo ya kuridhisha matukufu
katika kila unapo niingiza katika jambo au pahala. Na unitoe kwa kutoka
kunako ridhisha kutukufu. Na kwa fadhila yako nijaalie nguvu za kunisaidia
niwashinde maadui zangu.
Rudi kwenye Sura
81. Na sema ukiwaonya watu wako washirikina: Haki ya Tawhid, Imani
ya Mungu Mmoja, na Dini ya Kweli na Uadilifu, imekwisha fika. Na uwongo,
na ushirikina, na dini ya ufisadi na dhulma, yote hayo yameondoka. Kwani
uwongo daima hauna dawamu.
Rudi kwenye Sura
82. Na vipi Haki isiwe na nguvu na hali Sisi tunateremsha katika
Qur'ani dawa ya kuponyesha maradhi ya shaka katika vifua vya watu, na sababu
za kuwapatia rehema wanao iamini! Na madhaalimu hawana linao wazidia ila
khasara tu kwa kuikataa kwao.
Rudi kwenye Sura
83. Na hakika katika maumbile ya mwanaadamu ni kujidanganya na kukata
tamaa. Tukimneemesha kwa kumpa uzima na ukunjufu wa mali, hupuuza kutukumbuka
na kutuomba, na hujitenga nasi kwa kiburi na majivuno! Na akiguswa na shari,
kama ugonjwa na ufakiri, huwa mwingi wa kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi
Mungu.
Rudi kwenye Sura
84. Ewe Nabii! Waambie makafiri wa Kikureshi kwa kuepuka kuchochea
ugomvi na makindano: Kila mmoja wetu na mmoja wenu anatenda na anakwenda
kwa kufuata njia yake. Na Mola wenu Mlezi ni Mjuzi mno, wala hana ajuaye
kuliko Yeye kumjua nani aliye shika njia sawa na kufuata Haki. Na huyo
humlipa ujira wake kaamili. Na kumjua aliye potea njia, na huyo humpa adhabu
kama anayo stahiki.
Rudi kwenye Sura
85. Ewe Muhammad! Watu wako wanakuuliza kwa kutomezwa na Mayahudi:
Nini hakika ya Roho? Waambie: Roho ni katika ilimu yake Mwenyewe Mola wangu
Mlezi aliyo jikhusisha nayo Yeye. Na nyinyi hamkupewa ilimu ila chache
tu ukilinganisha na ilimu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Rudi kwenye Sura
86. Na lau tungeli taka kuifuta kabisa kifuani mwako hiyo Qur'ani
tuliyo kufunulia tungeli fanya hivyo, na kisha usingeli mpata yeyote wa
kukunusuru katika watu wako.
Rudi kwenye Sura
87. Lakini tumeiacha Qur'ani ibaki vile vile kifuani mwako kwa rehema
kutoka kwa Mola wako Mlezi, kwani fadhila zake kwako wewe ni kubwa mno
katika muujiza huu.
Rudi kwenye Sura
88. Waambie, kwa kushindana nao, kama wanaweza walete mfano wake.
Nao hawawezi! Hata wakikusanyika watu na majini wakasaidiana kuleta mfano
wa hii Qur'ani kwa mpango wake na maana yake, hawawezi; na wanga saidiana
wao kwa wao.
Rudi kwenye Sura
89. Na katika Qur'ani hii tumewaeleza watu kwa namna mbali mbali
kila maana kama ni mifano katika maajabu yake. Lakini watu wengi walikataa
ila kupinga na kuchukia.
Rudi kwenye Sura
90. Ilipo dhihiri kushindwa kwao na Qur'ani, na wakabanwa kwa hoja,
wakataka waletewe ishara nyingine na miujiza mingine. Hicho ni kitendo
cha mwenye kushindwa hoja, aliye emewa na kutahayari. Ndio wakasema: Hatutokuamini
mpaka ututimbulie katika ardhi ya Makka chemchem ambayo maji yake hayakatiki.
Rudi kwenye Sura
91. Au uwe nacho kitalu Makka cha mitende na mizabibu chenye kupita
mito kati yake! (Kwa kujua kuwa ardhi ya Makka ni kavu haioti kitu.)
Rudi kwenye Sura
92. Au mbingu ituangukie vichwani mwetu kwa mapande kama ulivyo dai
kuwa Mwenyezi Mungu anatuahidi hayo. Au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika
tukabiliane nao macho kwa macho!
Rudi kwenye Sura
93. Au uwe na nyumba iliyo pambwa kwa dhahabu, au upae mbinguni.
Na hata hivyo hatukusadiki mpaka ukituletea kitabu kutoka kwa Mwenyezi
Mungu kinacho thibitisha ukweli wako tukisome! Waambie: Mola wangu
Mlezi ametakasika kabisa na kuhukumiwa na yeyote, au yeyote kushirikiana
naye katika kudra yake! Mimi si chochote ila ni mwanaadamu kama Mitume
wote wengineo. Na wala wao hawakuwaletea watu wao muujiza ila kwa idhini
ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
94. Na nini kilicho wazuilia washirikina wa Makka kuifuata
Haki ulipo wajia wahyi (ufunuo) pamoja na miujiza isipo kuwa madai yao
kwa ujinga wao ya kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hatumi Mitume wanaadamu,
ila huwa ni Malaika!
Rudi kwenye Sura
95. Sema kwa kuwarudi: Lau kuwa duniani badala ya wanaadamu wapo
Malaika wanatembea kama wanaadamu na wamekaa humo, basi tungeli wateremshia
kutoka mbinguni Malaika kuwa ni Mitume wao katika jinsi yao. Lakini Malaika
si kama binaadamu; na wangeli kuja basi wange kuja kwa sura za watu.
*
Rudi kwenye Sura
96. Sema: Kama mnaukataa Utume wangu, basi Mwenyezi Mungu anatosha
kuwa ni wa kutuhukumu baina yangu na nyinyi, akathibitisha ukweli wa Ujumbe
wangu kwenu. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kujua hali zenu, na Mwenye
kuviona vitendo vyenu. Naye ni Mwenye kukulipeni kwa hivyo.
Rudi kwenye Sura
97. Waambie: Yule ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa kwa kuwa yu tayari
kufuata uwongofu, basi huyo ni mwongofu. Na anaye mpotoa kwa kufisidika
khulka yake, hutopata wa kuwanusuru asiye kuwa Yeye wa kuwaongoa duniani.
Na Akhera tutawakusanya wakikokotwa juu ya nyuso zao, hawaoni, wala hawasemi,
wala hawasikii. Na mahali pao wanapo pelekwa kukaa ni Jahannamu. Kula moto
ukipungua ukali wake Mwenyezi Mungu anazidi kuuchochea uwake kwa nguvu
zaidi.
Rudi kwenye Sura
98. Adhabu hiyo ndiyo malipo yao kwa sababu ya kuzikataa dalili tulizo
waletea za kuthibitisha Haki, na kwa ile kauli yao kusema: Hivyo sisi tutafufuliwa
kwa umbo jipya baada ya kwisha kuwa mifupa na vumbi?
Rudi kwenye Sura
99. Jee wameghafilika na hawakujua kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba
mbingu na ardhi, juu ya ukubwa wao, ni Mwenye kuweza kuumba watu na majini
kama wao? Na Mwenye kuweza hayo, vipi awe hawezi kuwarejesha wao upya,
na hilo ni jepesi zaidi kwake! Na Yeye Subhanahu ameweka muda maalumu wa
kuwarejesha tena baada ya kwisha kufa, na huo hauna shaka kuwa. Na muda
huo ndio Siku ya Kiyama. Na juu ya hivyo walio zidhulumu nafsi zao kwa
ukafiri wanakataa baada ya kuletewa hoja hizi. Na hayo si kwa lolote ila
kwa ukafiri tu.
Rudi kwenye Sura
100. Waambie hawa washirikina: Lau kuwa mnazimiliki riziki za Mola
wangu Mlezi, mngeli zifanyia ubakhili kwa kuogopa ufakiri. Kwani ni tabia
ya watu kuwa na pupa na ubakhili. Na Mwenyezi Mungu, Mkwasi na Karimu,
humpa anacho taka amtakaye, na huteremsha miujiza aitakayo Yeye, sio waitakayo
watu. Na Yeye katika yote hayo ni Mwenye hikima na Mjuzi.
Rudi kwenye Sura
101. Na lau hawa watu wangeli letewa hizo ishara wazitakazo, wange
zigeuzia uso, wala wasinge ziamini! Na Sisi tulimpa Musa Ishara tisa wazi
(1). Na juu ya hivyo wakakufuru. Na Firauni akasema: Hakika mimi nakuona
wewe, Musa, ni mtu uliye rogwa!
(1) Hizo ishara tisa ni: 1. Fimbo, 2. Mkono Mweupe, 3. Tufani, 4.
Nzige na vyura na chawa na damu, 5. Ukame na upungufu wa mazao, 6. Kupasuka
bahari, 7. Kutimbuka maji baharini, 8. Kuning'inia mlima kama kivuli, 9.
Kusemezwa na Mola wake Mlezi.
Rudi kwenye Sura
102. Musa akasema: Ewe Firauni! Unajua vyema kuwa aliye ziteremsha
Ishara hizi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Kwani ni Yeye ndiye Mwenye
kuweza hayo. Nazo Ishara hizo zi wazi, zinakuonyesha ukweli wangu. Lakini
wewe unafanya kiburi na inadi tu. Na hakika mimi nakuona wewe, Firauni,
kuwa ni mwenye kuangamia ikiwa hutoacha inadi yako.
Rudi kwenye Sura
103. Firauni akashikilia uasi wake, akataka kumtoa Musa na Wana wa
Israili katika nchi ya Misri. Tukamzamisha yeye na askari wake wote.
Rudi kwenye Sura
104. Tukamvua Musa na kaumu yake, na baada ya kumzamisha Firauni
tukasema kuwaambia
Wana wa Israili: Kaeni katika nchi takatifu ilioko Sham. Ukija wakati
wa uhai wa pili tutakutoeni makaburini kwenu kwa mchanganyiko. Kisha tutakuhukumuni
kwa uadilifu.
Rudi kwenye Sura
105. Na hatukuiteremsha Qur'ani ila kwa kuunga mkono hikima ya Mwenyezi
Muungu, iliyo pelekea kuteremshwa kwake. Nayo hiyo Qur'ani kwa dhati yake
haikuteremka ila kuwa imekusanya Ukweli wote. Kwani itikadi zake ndizo
zilizo sawa, na hukumu zake ndizo zilizo nyooka. Na wewe, ewe Nabii, hatukukutuma
ila uwe mbashiri wa kuwabashiria Pepo wenye kuamini, na mwonyaji kuwaonya
wanao ukanya Moto. Basi wewe huna jukumu lolote ikiwa wao hawaamini.
Rudi kwenye Sura
106. Na hii Qur'ani tumeigawa na tumeiteremsha kipande kipande kwa
muda mrefu, ili uwasomee watu kwa taratibu wapate kuifahamu. Tumeiteremsha
kidogo kidogo kwa utulivu bila ya matatanisho.
Rudi kwenye Sura
107. Waambie makafiri wa Makka kwa kuwatisha: Jichagulieni nafsi
zenu mlitakalo - kuiamini Qur'ani au la! Kwani hakika walio pewa ilimu
sawa na fahamu baraabara kabla ya kuteremka kwake, wakisomewa Qur'ani huangukia
kwenye nyuso zao kwa kusujudu na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Rudi kwenye Sura
108. Na wao husema: Mola wetu Mlezi ametakasika na ila ya kwenda
kinyume na ahadi yake ya kuneemesha na kuadhibu alio ahidi. Kwani ahadi
yake lazima itimie bila ya shaka yoyote.
Rudi kwenye Sura
109. Na huangukia tena kwenye nyuso zao mara ya pili wakilia kwa
kumkhofu Mwenyezi Mungu, na Qur'ani inawazidisha unyenyekevu kwa Mwenyezi
Mungu.
Rudi kwenye Sura
110. Waambie hawa washirikina: Mwiteni Mwenyezi Mungu kwa jina la
Allah, au jina la Rahman; kwani jina lolote mtalo mwitia ni zuri. Yeye
Mtukufu ana majina mengi mazuri mazuri. Wala hamdanganyikiwi kwa kutumia
majina mengi kuwa kwa hivyo mwenye kuitwa ni zaidi ya Mmoja. Na unapo soma
Qur'ani katika Sala zako, basi usipaze sauti yako wakasikia washirikina
wakakusibabi na wakakuudhi. Wala usifanye kwa siri hata Waumini wakawa
hawasikii. Kuwa kati kati katika kusoma kwako.
Rudi kwenye Sura
111. Nasema Alhamdulillah, Himdi zote, yaani sifa na shukrani, ni
za Mwenyezi Mungu ambaye hakuzaa mwana, kwani hamhitajii; wala hana mshirika
katika ufalme, kwani Yeye peke yake ndiye aliye uanzisha; wala hana msaidizi
wa kumtia nguvu kwa udhaifu fulani unao mpata. Na mtukuze Mola wako Mlezi
kwa utukufu mkubwa ulio laiki naye.
Rudi kwenye Sura