1. Hizi harufi moja moja za kutamkwa zinaonyesha kuwa
Qur'ani ni muujiza ulio undwa kwa harufi, na pia ni kuwazindua watu waisikilize.
Rudi kwenye Sura
2. Ewe Mtume! Hizi ni hadithi za Mola wako Mlezi kwa rehema yake
kueleza kisa cha mja wake na Nabii wake, Zakariya.
Rudi kwenye Sura
3. Pale alipo muelekea Mwenyezi Mungu na akamwomba kwa siri wasijue
watu.
Rudi kwenye Sura
4. Akasema: Mola wangu Mlezi! Mimi nimekwisha dhoofika, na kichwa
changu kimejaa mvi. Na mimi sikuwa na bahati mbaya pale ninapo kuomba,
bali bahati yangu siku zote ni nzuri, unaniitikia ninapo kuomba.
Rudi kwenye Sura
5. Na mimi ninaogopa kuwa jamaa zangu hawatashika vyema amri za Dini
baada ya kufa kwangu. Na mke wangu bado ni tasa, hazai. Basi niruzuku mwana,
kwa fadhila yako, atakaye shika pahala pangu kwa watu wangu baada yangu.
Rudi kwenye Sura
6. Anirithi ilimu na Dini. Na awarithi Ukoo wa Yaaqub ufalme. Ewe
Mola wangu Mlezi! Na mjaalie awe maridhia kwako na kwa watu.
Rudi kwenye Sura
7. Akaitwa: Ewe Zakariya! Sisi tunakubashiria khabari nzuri kuwa
utapata mwana, na jina tumemwita: Yahya. Hatujapata kumwita mtu yeyote
kwa jina hilo kabla yake.
Rudi kwenye Sura
8. Zakariya akasema kwa mastaajabu: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi nipate
mwana, na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimo katika miaka ya ukongwe?
Rudi kwenye Sura
9. Mwenyezi Mungu akamfunulia mja wake, Zakariya: Mambo ni kama ulivyo
bashiriwa, na kwamba kupewa wewe mtoto juu ya ukongwe wako na utasa wa
mkeo ni jambo jepesi kwangu Mimi. Wala usiyaone hayo kuwa ni ya mbali hayawezi
kuwa. Kwani Mimi nilikuumba wewe kabla yake, na hali hukuwa kitu chochote.
Rudi kwenye Sura
10. Zakariya akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nijaalie alama ya kuonyesha
kuwa nitapata hayo uliyo nibashiria. Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:
Alama yako ni kuwa hutaweza kusema muda wa masiku matatu, nawe ni mzima
wa hisiya na ulimi.
Rudi kwenye Sura
11. Zakariya akawatokea watu wake kutoka kwenye msala, na akawaashiria
wamtakase Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni.
Rudi kwenye Sura
12. Yahya akazaliwa, akakua, na kisha akapata wito, na akaamrishwa
ayatende yaliomo katika Taurati kwa juhudi na kuazimia. Na Mwenyezi Mungu
alimpa utotoni mwake ilimu ya Dini na kufahamu hukumu za sharia.
Rudi kwenye Sura
13. Mwenyezi Mungu akampa tabia ya huruma, na utukufu wa nafsi, na
akamjenga katika uchamungu.
Rudi kwenye Sura
14. Na Mwenyezi Mungu alimjaalia mwema mno kwa wazazi wake wote wawili,
na akiwafanyia hisani. Wala hakumfanya awe jeuri kwa watu, wala awe mwenye
kumuasi Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
15. Na salama na amani iwe kwake, asipatikane na madhara wala maudhi
siku ya kuzaliwa kwake, na siku ya kufa kwake, na siku atapo fufuliwa kuwa
hai tena.
Rudi kwenye Sura
16. Ewe Mtume! Taja katika Qur'ani hadithi ya Maryamu, pale alipo
jitenga na jamaa zake na watu wote, akenda upande wa mashariki ya pale
alipo kuwepo.
Rudi kwenye Sura
17. Akafunga pazia baina yake na hao watu. Mwenyezi Mungu akamtuma
Jibril amwendee kwa sura ya mwanaadamu kaamili, ili asishituke kumwona
kwa sura yake ya Malaika ambayo hakuizoea.
Rudi kwenye Sura
18. Maryamu akasema: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa
Rehema, anikinge nawe, ikiwa unatarajiwa umche Mwenyezi Mungu, na umwogope.
Rudi kwenye Sura
19. Malaika akasema: Mimi si lolote ila nimetumwa na Mola wako Mlezi
niwe ni sababu ya kuwa wewe upate mwana aliye safi wa kheri.
Rudi kwenye Sura
20. Maryamu akasema: Vipi nipate mwana na hajanikaribia mwanamume
yeyote, na mimi si kahaba?
Rudi kwenye Sura
21. Malaika akasema: Mambo ni kama unavyo sema: Hakukugusa mwanamume.
Mola wako Mlezi amesema: Kukupa mwana bila ya baba ni jambo jepesi kwangu,
na hilo liwe ni Ishara kwa watu ya kuonyesha ubora wa uwezo wetu, kama
ilivyo kuwa ni rehema kwa mwenye kufuata uwongofu wake. Na huku kuumbwa
kwa Isa ni amri iliyo kwisha kadiriwa, ni lazima iwe.
Rudi kwenye Sura
22. Matakwa ya Mwenyezi Mungu yakatimia. Maryamu akachukua mimba
ya Isa kwa namna alivyo itaka Mwenyezi Mungu. Akatoka na mimba yake akenda
pahala mbali na watu.
Rudi kwenye Sura
23. Machungu ya uzazi yakamchukua mpaka kwenye shina la mtende
alitegemee, na apate kujisitiri. Akawaza vipi watavyo udhika watu wake
naye kwa haya; akatamani afilie mbali, asahaulike kabisa, wala asitajike.
Rudi kwenye Sura
24. Malaika akamtangazia kutoka pahala kwa chini yake: Usihuzunike
kwa upweke wako, na kukosa chakula na cha kukinywa, na maneno ya watu.
Mwenyezi Mungu kesha jaalia karibu nawe kijito kidogo.
Rudi kwenye Sura
25. Na hebu tikisa huo mtende, zitakuangukia tende mbivu nzuri.
"Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende
nzuri zilizo mbivu." Imethibiti kuwa tende, khasa zile rat'ab, yaani "fresh"
zina faida kubwa sana katika mwili, na nyepesi katika tumbo.
Rudi kwenye Sura
26. Basi kula hizo tende na kunywa maji hayo, na tua roho yako. Na
ukikutana na mtu yeyote ambaye hakupendezewa na hali yako hii, basi muashirie
kuwa wewe umo katika saumu, na husemi na mtu.
Rudi kwenye Sura
27. Maryamu akenda kwa watu wake naye kambeba Isa. Wakamwambia kwa
mastaajabu na kuudhika: Umefanya kitendo kiovu!
Rudi kwenye Sura
28. Ewe wa kizazi cha Harun, aliye kuwa Nabii Mchamngu Mahashumu!
Vipi umefanya uliyo yafanya na baba yako hakuwa na tabia mbovu, wala mama
yako hakuwa kahaba!
"Ewe dada wa Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa
kahaba." Imeandikwa katika Encyclopaedia Britannica kuwa Qur'ani imekosea
kosa la kihistoria ilipo mwita Maryamu "Dada wa Harun," ilihali baina ya
Maryamu huyu na Harun nduguye Musa ni karne nyingi. Wamesahau hawa kuwa
Udugu kwa Kiarabu upo kwa kushabihiana. Makusudio ya hapa ni kushabihiana
kwa wema na kuchamngu, yaani ewe uliye mshabihi Harun kwa wema na uchamngu,
nini kilicho kugeuza hali yako njema ukawa hivyo? Wala baba yako hakuwa
mtu muovu wa kutenda mabaya, wala mama yako kufanya uchafu. (Kadhaalika
Maryamu ni ukoo wa Harun, na pengine huitwa "Binti wa Imran", na Imran
ni baba yake Harun.)
Rudi kwenye Sura
29. Akawaashiria yule mtoto waseme naye. Wakasema: Vipi tuzungumze
na mtoto mchanga ambaye bado yumo katika ubeleko?
Rudi kwenye Sura
30. Isa alipo sikia maneno yao Mwenyezi Mungu alimtamkisha akasema:
Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Atanipa Injili, na ataniteuwa
niwe Nabii.
Rudi kwenye Sura
31. Atanijaalia na baraka, nikifunza kheri, na nikiwafaa watu, na
ananiamrisha nishike Sala, na nitoe Zaka muda wa uhai wangu.
Rudi kwenye Sura
32. Kama alivyo niamrisha niwe mwema kwa mama yangu, wala hakunifanya
niwe jabari kwa watu, wala mwenye kumuasi Yeye.
Rudi kwenye Sura
33. Na amani iwe juu yangu kutokana na Mwenyezi Mungu siku ya kuzaliwa
kwangu, na siku ya kufa kwangu, na siku ya kufufuliwa kwangu nikawa hai
tena.
Rudi kwenye Sura
34. Huyo mwenye kusifiwa kwa sifa hizo ndiye Isa bin Maryamu. Na
hii ndiyo kauli ya kweli iliyo mkhusu yeye wanayo ipinga wapotovu
na wakamtilia shaka unabii wake hao wenye kutia shaka.
Rudi kwenye Sura
35. Wala haifai wala haingii akilini kuwa Mwenyezi Mungu awe na mwana.
Yeye ametakasika na hayo! Shani yake Subhanahu ni akipitisha hukumu ya
jambo lolote basi alitakalo huwa bila ya muhali, kwa tamko tu la kusema:
Kuwa! Na hilo jambo huwa.
Rudi kwenye Sura
36. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wangu, na ndiye Bwana wenu.
Basi muabuduni Yeye. Wala msimshirikishe na yeyote. Hii ninayo kuitieni
ndiyo Njia itakayo kufikishieni kwenye mafanikio.
Rudi kwenye Sura
37. Na juu ya iliyo kwisha tangulia katika kauli ya haki iliyo mkhusu
Isa, watu wa Biblia wamekhitalifiana wao kwa wao, na wakazua madhehebu
mbali mbali. Na makafiri watapata adhabu kali watapo hudhurishwa Siku ya
Hisabu, na wakashuhudia msimamo wa Kiyama, na wakakuta malipo maovu kabisa.
Rudi kwenye Sura
38. Watakuwa na masikio makali, na macho yenye nguvu siku watakayo
kutana na Mwenyezi Mungu! Lakini wao hii leo duniani kwa kujidhulumu nafsi
zao, na kuacha kwao kunafiika kwa kusikia na kuona, wamo katika upotovu
wa kuiacha haki, na hayo ni dhaahiri isiyo na uficho.
Rudi kwenye Sura
39. Ewe Mtume! Wahadharishe hawa wenye kudhulumu na siku watakayo
juta kwa kupindukia kwao mipaka katika haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya
nafsi zao wenyewe! Na hapo hisabu yao itakuwa imekwisha, na malipo wamekwisha
yapata! Na hali huko duniani walikuwa wameghafilika na Siku hiyo, hawakusadiki
kuwa kutakuwako kufufuliwa na kulipwa.
Rudi kwenye Sura
40. Hebu jamani! Nawajue watu kuwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye mrithi
wa kuurithi ulimwengu wote na kila kiliomo ndani yake. Na hisabu yao wote
ni juu ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
41. Ewe Mtume! Watajie watu katika Qur'ani hadithi ya Ibrahim. Hakika
yeye alikuwa mtu mkweli kabisa, katika kauli yake na vitendo vyake, na
mwenye kueleza vilivyo khabari za Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
42. Na taja pale Ibrahim alipo msemeza baba yake kwa upole akimwambia:
Ewe baba yangu! Vipi unayaabudu masanamu yasiyo sikia wala hayaoni, wala
hayawezi kukuletea kheri wala kukukinga na shari?
Rudi kwenye Sura
43. Ewe baba yangu! Mimi yamenijia kwa njia ya ufunuo (wahyi) wa
Mwenyezi Mungu ambayo wewe hukuyapata, ya kumjua Mwenyezi Mungu, na kujua
yanayo mlazimu mwanaadamu kwa Mola wake Mlezi. Basi nifuate mimi kwa hayo
ninayo kuitia ya Imani, nitakuonyesha Njia Iliyo Nyooka itakayo kufikisha
kwenye haki na mafanikio.
Rudi kwenye Sura
44. Ewe baba yangu! Usimt'ii Shetani anaye kuzaini uabudu masanamu.
Ni mtindo wa Shetani kumuasi Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na kuikhalifu
amri yake.
Rudi kwenye Sura
45. Ewe baba yangu! Mimi nakuogopea ukiendelea na ukafiri utapatilizwa
kwa adhabu kali kutokana na Mwingi wa Rehema, ukawa mwenzio ni Shetani
Motoni, wewe unamkaribia, na yeye anakukaribia.
Rudi kwenye Sura
46. Baba akasema kumwambia Ibrahim naye kakasirika naye, akimtolea
ndaro: Yawaje unawawacha miungu yangu, ewe Ibrahim, na unanitaka nimuabudu
Mungu wako? Kama hukusita kuwatukana masanamu basi hapana shaka nitakupiga
kwa mawe. Tahadhari nami! Niondokelee kwa muda mrefu, mpaka nipoe hamaki
zangu.
Rudi kwenye Sura
47. Ibrahim bado akamtwaa pole baba yake akamwaga kwa kusema: Salamun
A'laika! Amani iwe juu yako! Nitamwomba Mola wangu Mlezi akuongoe
na akusamehe. Na Mola wangu Mlezi amenizoeza kuwa na huruma nami, na kuwa
karibu nami.
Rudi kwenye Sura
48. Na hivyo mimi basi nakuondokeeni, na najitenga na hiyo miungu
mnayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Nami namuabudu Mola wangu Mlezi
tu peke yake, kwa kutaraji kuwa apokee ut'iifu wangu, wala yasipotee matarajio
yangu.
Rudi kwenye Sura
49. Ibrahim alipo jitenga na baba yake na kaumu yake na miungu yao,
Mwenyezi Mungu alimkirimu kwa kumpa dhuriya wema, juu ya kuwa alikuwa kesha
kata tamaa ya kupata watoto. Kwani yeye na mkewe walikwisha kuwa ni wakongwe,
si wa kuzaa tena. Mwenyezi Mungu akawatunukia Is-haq, na kutokana na Is-haq
akazaliwa Yaaqub, na akawateuwa wote wawili wawe Manabii.
Rudi kwenye Sura
50. Na tukawapa, juu ya cheo cha Unabii, kheri nyingi za Dini na
dunia kwa rehema zetu. Na tukawarithisha duniani makumbusho mema ya daima
kwa ulimi wa kweli mtukufu wa kutaja sifa zao.
Rudi kwenye Sura
51. Ewe Mtume! Wasomee watu katika Qur'ani hadithi ya Musa. Yeye
alikuwa ni mwenye niya safi kwa nafsi yake, na moyo wake, na mwili wake,
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu alimteuwa kwa kumpa
Unabii na Utume.
Rudi kwenye Sura
52. Nasi tulimtukuza, na tukamwita kwenye Mlima wa T'ur. Musa akasikia
huo wito wa Mwenyezi Mungu kwa upande wa kulia. Nasi tukamkaribisha kwa
kumtukuza, na tukamteuwa ili tunong'one naye.
Rudi kwenye Sura
53. Tukampa rehema yetu na neema yetu, na tukamchagua pamoja naye
nduguye Harun awe Nabii vile vile, ili amsaidie kufikisha ujumbe.
Rudi kwenye Sura
54. Ewe Mtume! Wasomee watu yaliyomo katika Qur'ani katika kisa cha
Ismail. Hakika yeye alikuwa ni mkweli wa kutimiza ahadi yake. Na
alimuahidi baba yake kuwa atasubiri pindi akimchinja kama alivyo amrishwa
na Mwenyezi Mungu. Na akatimiza ahadi yake, na Mwenyezi Mungu akamtolea
fidia kondoo badala yake na akamtukuza kwa kumpa Utume na Unabii.
Rudi kwenye Sura
55. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake kushika Sala na kutoa Zaka,
na akawa katika makamo matukufu katika kumridhi Mola wake Mlezi.
Rudi kwenye Sura
56. Ewe Mtume! Wasomee watu yaliyomo katika Qur'ani hadithi ya Idris.
Dasturi yake ilikuwa ni ukweli wa kauli, na vitendo, na a'mali. Na Mwenyezi
Mungu alimpa utukufu wa Unabii.
Rudi kwenye Sura
57. Na kwa hayo Mwenyezi Mungu alimnyanyua cheo cha juu.
Rudi kwenye Sura
58. Hao walio kwisha tajwa, ni miongoni alio waneemesha Mwenyezi
Mungu katika Manabii, katika dhuriya wa Adam na dhuriya wa tulio waokoa
pamoja na Nuhu na dhuriya wa Ibrahim kama Ismail; na katika dhuriya wa
Yaaqub, kama Manabii wa Wana wa Israil; na miongoni tulio waongoa kwenye
Haki na tukawachagua walinyanyue Neno la Mwenyezi Mungu.. Hawa pindi wakisikia
Aya za Mwenyezi Mungu wanasomewa huingia khofu, na huanguka mpaka chini
wakimsujudia Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu.
Rudi kwenye Sura
59. Tena baada ya wateuliwa hawa wakatokea wa vizazi vingine wasio
kuwa waongofu kama hao. Wakaacha Sala, wakapuuza kunafiika na uwongofu
wake, na wakashughulikia maasi. Hawa, basi, watakuja kuta malipo ya maasi
yao na upotovu wao duniani na akhera.
Rudi kwenye Sura
60. Lakini watao zidiriki nafsi zao kwa kutubia, na kwa Imani ya
kweli, na vitendo vyema, basi Mwenyezi Mungu ataipokea toba yao na atawaingiza
Peponi, na atawalipa sawa ujira wao.
Rudi kwenye Sura
61. Bustani hizo za Peponi ni makaazi ya milele kwa mujibu wa ahadi
ya Arrahmani, Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, kuwaahidi waja wake walio
tubia, na wakamuamini kwa ghaibu, bila ya kumwona. Basi wao wataingia humo
bila ya shaka yoyote, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu haina kinyume.
Rudi kwenye Sura
62. Na hao katika Bustani hizo za Peponi hawatakuwa na mazungumzo
ya upuuzi, wala hawatasikia ila kheri na amani. Na riziki yao ni tele na
imedhaminiwa haina ukomo.
Rudi kwenye Sura
63. Na hakika Mwenyezi Mungu huwapa Pepo hiyo iwe yao wale ambao
duniani walikuwa ni wachamngu, wakaacha maasi na wakatenda mema yanayo
stahiki.
Rudi kwenye Sura
64. Na wakati wanapo ingia wakatulia humo husema kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu: Hatukuingia Peponi, wala hatuondoki kutoka hapa kwenda penginepo,
ila kwa amri ya Mwenyezi Mungu na fadhila yake. Kwani Yeye, Subhanahu,
ndiye Mwenye kumiliki, Mwenye kudabiri, na Mwenye kujua ya mbele yetu na
ya nyuma yetu. Wala Yeye Mwenyezi Mungu hasahau kutimiza ahadi yake aliyo
waahidi waja wake wachamngu.
Rudi kwenye Sura
65. Kwani Yeye, Subhanahu, ndiye Muumba, na Mwenye kumiliki mbingu
na ardhi na viliomo baina yake; na ndiye Mwenye kuyaendesha mambo yao yote;
na ndiye peke yake Mwenye kustahiki kuabudiwa. Basi muabudu Yeye tu; na
ushikilie kumuabudu, nawe hali umesubiri na umetua. Kwani Yeye, Subhanahu,
ndiye Mwenye kustahiki peke yake kuabudiwa, wala hana mwenzie anaye stahiki
kuabudiwa, au kuitwa kwa jina lake.
Rudi kwenye Sura
66. Na mwanaadamu kwa mastaajabu kuwa atafufuliwa husema: Vipi nitafufuliwa
niwe hai tena, baada ya kwisha kufa na kuteketea?
Rudi kwenye Sura
67. Vipi huyu binaadamu anamstaajabia Mwenyezi Mungu kuweza kumfufua
Akhera, na hakumbuki kwamba Yeye Mtukufu alimuumba duniani naye hakuwa
chochote, na hali kurejesha kuumba ni jambo jepesi kuliko kuanza kuumba
hapo mwanzo, ukipima kwa akili.
Rudi kwenye Sura
68. Ikiwa hili jambo la kufufuliwa linaonekana ni geni, wanalikataa
makafiri, basi naapa kwa Aliye kuumba na akakulea, na akakukuza, Siku ya
Kiyama tutawakusanya makafiri pamoja na mashetani wao, walio wazaini hata
wakauona ukafiri mzuri, tutawakusanya wote kuizunguka Jahannamu, nao wamepiga
magoti kwa udhalili na wingi wa kitisho na kufazaika.
Rudi kwenye Sura
69. Kisha kwa yakini kutoka kila kikundi tutawatoa wale walio shadidi
ya ukafiri kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumuasi, tutawapeleka wao mbele
kwenye adhabu iliyo kali kabisa.
Rudi kwenye Sura
70. Na Sisi tunawajua vyema zaidi kati yao wanao stahiki kuingia
Motoni na kuungua humo.
Rudi kwenye Sura
71. Na enyi viumbe! Hapana yeyote kati yenu ila atahudhuria hapo.
Muumini atauona Moto na atapita, na kafiri atatumbukia. Amri hii lazima
itimizwe, hukumu ya Mwenyezi Mungu imekwisha pita.
Rudi kwenye Sura
72. Tena kwa rehema yetu, tutawakusanya wachamngu na tutawaokoa na
Jahannamu. Na tutawaacha humo wale walio dhulumu nafsi zao, wakipiga magoti,
kwa kuwaadhibu.
Rudi kwenye Sura
73. Na walikuwa makafiri duniani pindi wakisomewa Aya za Mwenyezi
Mungu zenye kueleza wazi, wakizipuuza, na wakiwaambia Waumini kwa majivuno
ya mali yao na watu wao: Nyinyi si kama sisi katika dunia. Sisi tuna cheo
bora zaidi kuliko nyinyi, na hadhi zetu mabarazani ni kubwa zaidi. Hali
kadhaalika itakuwa hali yetu Akhera mnayo iamini nyinyi.
Rudi kwenye Sura
74. Ingeli wafalia hawa makafiri wange waidhika kwa yaliyo wapata
watu wengi walio watangulia. Wao walimkufuru Mwenyezi Mungu, na wakawa
na cheo bora zaidi katika dunia, na starehe nyingi zaidi, na wakipendeza
kuwaangalia. Na Mwenyezi Mungu akawateketeza kwa ukafiri wao - nao ni wengi.
Na katika mabaki yao pana mafunzo kwa mwenye kuzingatia.
Rudi kwenye Sura
75. Ewe Mtume! Waambie hawa: Aliomo katika upotovu na ukafiri Arrahmani,
Mwingi wa Rehema, humpa muhula, akamkunjulia umri, azidi ujabari wake na
upotovu wake. Na makafiri huwakariria Waumini kauli kwa kusema: Kundi gani,
baina yetu na nyinyi, lenye hadhi zaidi na bora katika mabaraza na majlisi?
Mpaka watakapo ona yale walio ahidiwa, nayo ama kuadhibiwa na Waislamu
duniani kwa kuuwawa na kutekwa, au kupata hizaya ya Siku ya Kiyama. Hapo
tena watajijua kuwa hadhi yao ni duni, na msaada wao ni dhaifu.
Rudi kwenye Sura
76. Ama wenye kuamini Ishara za Mwenyezi Mungu, pindi wakizisikia
tu wanazikubali. Na Mwenyezi Mungu huwazidishia tawfiki kwa vitendo vyao
vizuri. Na vitendo vyema ni bora na vinadumu zaidi kwa Mwenyezi Mungu kwa
malipo, na kuwa mwisho wake ni mwema.
Rudi kwenye Sura
77. Yafaa ustaajabu, ewe Mtume, huu mtindo wa anaye kanya Ishara
za Mwenyezi Mungu. Mtu huyu amefitinika na dunia yake, akakanya kufufuliwa,
akasema, kwa maskhara: Hakika Mwenyezi Mungu atanipa Akhera hiyo mnayo
dai mali na wana nitafakhari nayo huko. Naye anadhani kuwa Akhera ni kama
dunia, hukisiwa ya huko kama yalivyo huku. Amesahau kuwa huko ni malipo
ya mema na mabaya, na kwamba kuzidiana huko ni kwa vitendo vyema.
Rudi kwenye Sura
78. Kwani huyo kafiri ameijua siri ya ghaibu, hata aieleze kwa ukweli?
Na kwani amechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwa hayo hata awe na tamaa?
Rudi kwenye Sura
79. Basi na ayaache hayo anayo yazua. Kwani Sisi tunamhisabia uzushi
wake, na atakuta adhabu yake imekunjuliwa muda mrefu kuliko anavyo fikiri.
Rudi kwenye Sura
80. Mwenyezi Mungu atampokonya yote anayo tafakhari nayo duniani,
mali na wana; na atamteketeza. Na atakuja Akhera, peke yake, mtupu, hana
mali wala mwana wala msaidizi.
Rudi kwenye Sura
81. Hao makafiri wamewafanya miungu mingine mbali mbali badala ya
Mwenyezi Mungu wakaiabudu, ili wawe ndio waombezi wao Akhera.
Rudi kwenye Sura
82. Yawapasa waachilie mbali hayo wanayo yadhani. Hiyo miungu itakuja
wapinga ibada yao na wataikanya. Na hiyo miungu itakuwa ndio makhasimu
wa washirikina, na itaomba waadhibiwe.
Rudi kwenye Sura
83. Ewe Mtume! Hujui kama Sisi tumewapa madaraka mashetani juu ya
makafiri - nao wamewazuga hawa makafiri - wanawaghuri na huwapelekea kwenye
maasi waiache haki na wawafuate wao.
Rudi kwenye Sura
84. Basi ewe Mtume! Usiingie dhiki moyo wako kwa ukafiri wao, wala
usiwatakie adhabu ya haraka. Kwani Sisi tunawawacha hivi duniani kwa muda
wenye kiwango maalumu, na tunawadhibitia a'mali zao na madhambi yao,
ili Akhera tuwahisabie.
Rudi kwenye Sura
85. Ewe Mtume! Itaje Siku tutapo wakusanya wachamngu kuwapeleka Peponi
makundi kwa makundi yaliyo tukuzwa.
Rudi kwenye Sura
86. Na tutawachunga wakosefu kuwasukumia Jahannamu nao wamebanwa
na kiu, kama wanavyo chungwa wanyama kwenda kwenye maji.
Rudi kwenye Sura
87. Na hapana ataye kuwa na mamlaka ya uombezi Siku hiyo yeyote isipo
kuwa aliye pata ruhusa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ahadi aliyo mpa.
Rudi kwenye Sura
88. Washirikina, na Mayahudi, na Wakristo wamesema: Mwenyezi Mungu
amejifanyia mwana kutokana na Malaika au kutokana na watu.
Rudi kwenye Sura
89. Enyi mlio sema hivyo, mmeleta jambo linalo chusha mno! Linalo
chusha katika akili iliyo kaa sawa.
Rudi kwenye Sura
90. Mbingu zakaribia kupasuka kwa hayo, na ardhi kudidimia, na milima
kuanguka mapande mapande!
Rudi kwenye Sura
91. Vituko hivyo vya mbingu, na ardhi, na milima, vyakaribia kutokea
kwa sababu ya kumbandikiza Mwenyezi Mungu mwana!
Rudi kwenye Sura
92. Wala hayaingii akilini kuwa Mwenyezi Mungu awe na mwana; kwani
kuthibiti kuwa na mwana Yeye inahitajia awe Yeye ni mwenye kuzuka, mwenye
mwanzo na mwisho, na kuwa Yeye awe na haja ya mwana.
Rudi kwenye Sura
93. Hapana yeyote aliomo mbinguni na kwenye ardhi ila atamjia
Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Siku ya Kiyama hali naye ni mtumwa wake mwenye
kuunyenyekea Ungu wake.
Rudi kwenye Sura
94. Ujuzi wake umewaenea wao wote na wanayo yatenda. Hapana aliye
fichikana kwake, wala chochote katika vitendo vyao.
Rudi kwenye Sura
95. Na wote hao watamjia Siku ya Kiyama hali ni wapweke, hawana wasaidizi
wa kuwasaidia, wala wana, wala mali.
Rudi kwenye Sura
96. Hakika Waumini wenye kutenda mema Mwenyezi Mungu anawapenda,
na anawapendezesha kwa watu.
Rudi kwenye Sura
97. Na hakika Sisi tumeifanya hii Qur'ani kuwa ni nyepesi, kwa lugha
yako, ili kwa radhi ya Mwenyezi Mungu na neema zake uwape bishara nzuri
wanao fuata amri zake, na wakaepuka makatazo yake. Na pia upate kuwaonya
kwa hii Qur'ani wale wanao ipinga na wakakazana kuifanyia khasama,
kuwa watapata ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu zake.
Rudi kwenye Sura
98. Ewe Mtume! Isikuhuzunishe inadi yao kwako. Kwani Mwenyezi
Mungu amekwisha wahiliki kabla yao kaumu kadhaa wa kadhaa katika vizazi
vilivyo tangulia. Wote wamemalizika. Huwaoni hata mmoja wao, wala huwasikii
sauti yao.
Rudi kwenye Sura