1. Enyi watu! Tahadharini na adhabu ya Mola wenu Mlezi,
na wekeni katika nyoyo zenu makumbusho ya Siku ya Kiyama. Kwani mtingishiko
utao tokea hapo ni mkubwa, wenye kuhangaisha na kutikisa viumbe.
Rudi kwenye Sura
2. Siku mtapo kiona Kiyama mtaona kitisho chake kinafikilia ukubwa
wake hata kama yupo mwanamke anaye nyonyesha na ziwa lake limo katika mdomo
wa mwanawe, basi hapana shaka atamsahau na amwachilie mbali. Na kama yupo
mwanamke ana mimba basi ataiharibu mimba kabla ya kufika wakati wake wa
kuzaa kwa ajili ya fazaa na kitisho. Na ewe mwenye kuangalia! Ukiona hali
ya watu Siku hiyo namna wanavyo onekana hawanazo, na wanapo kwenda wanayumba,
utadhani wamelewa, na ilhali hawakulewa. Lakini kitisho walicho kishuhudia,
na khofu ya adhabu kuu ya Mwenyezi Mungu ndiyo iliyo waondoshea utulivu
wao.
Rudi kwenye Sura
3. Na juu ya onyo hili kali na la kweli bado wapo baadhi ya watu
inadi yao au kufuata kwao kijinga huwapelekea katika mambo ya kubishana
juu ya Mwenyezi Mungu na sifa zake, wakamsingizia kuwa ati ana washirika,
au wakaukataa uweza wake wa kufufua na kuwalipa watu kwa vitendo vyao.
Na kwa huo ubishi wao na kukataa kwao hawategemei ilimu sahihi, au hoja
ya kweli; lakini wao hufuata tu nyayo za kila shetani aliye muasi Mola
wake Mlezi, aliye baidika na uwongofu.
Rudi kwenye Sura
4. Mwenyezi Mungu amehukumu kuwa anaye mfuata Shetani na akamfanya
kuwa ni rafiki yake na mlinzi wake, na mwongozi wake, basi humpotoa na
njia ya Haki, na akamuelekeza kwenye upotovu unao pelekea kwenye Moto unao
waka na kuripuka.
Rudi kwenye Sura
5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kukufufueni baada ya kufa,
basi katika kuumbwa kwenu ipo dalili ya kuweza kwetu kufufua. Tulikuumbeni
asili yenu kutokana na udongo, kisha tukaufanya tone ya manii, kisha baada
ya muda tukaigeuza ikawa kipande cha damu iliyo gandana.(1) Kisha
tukaifanya kipande cha nyama yenye sura ya kibinaadamu, au isiyo kuwa na
sura, ili tukubainishieni uweza wetu wa kuanza uumbaji na kuendeleza kukuza
kwa viwango na madaraja, na kugeuza kutoka hali hii na kuingia nyengine.
Na katika viliomo katika matumbo ya mzazi vipo tunavyo viharibu tuvitakavyo
na tunaviweka imara na madhubuti tuvitakavyo, mpaka utimie muda wa
kuzaliwa. Kisha tunakutoeni kwenye matumbo ya mama zenu muwe watoto wachanga.
Kisha tunakuleeni mpaka mkamilike akili na nguvu. Na baada ya hayo wapo
katika nyinyi ambao Mwenyezi Mungu huwafisha, na wapo ambao umri wao hurefushwa
mpaka wakafikia ukongwe wa kupiswa, ujuzi wao na kufahamu kwao mambo kukasita.
Na aliye kuumbeni kwa sura hii tangu mwanzo hashindwi kukurudisheni tena.
Na jambo jengine la kukuonyesha kudra ya Mwenezi Mungu kufufua ni kuwa
wewe unaiona ardhi kavu yabisi; tukiiteremshia maji uhai unaitambalia,
na hiyo ardhi hugutuka, na huzidi na hututumka kwa maji na hewa iliyo ingia
ndani yake, na hapo tena hutokeza namna mbali mbali za mimea inayo furahisha
kuiona, na uzuri wake ukazagaa, na mwenye kuiona roho yake ikakunjuka.
(1)(Maurice Bucaille, mtaalamu wa Kifaransa maarufu aliye silimu,
amelifasiri neno A'laqa kwa maana ya "kitu kilicho tundikwa". Na hivyo
ndivyo inavyo thibitisha Sayansi ya hivi sasa, kuwa mbegu ya uzazi ikisha
pandikizwa huja ikaning'inia kama iliyo tundikwa kwenye tumbo la uzazi.
Tazama pia 23.14, 40.67, 75.37-38 na kadhaalika Sura ya 5 ya Annisaa
Aya 129, inayo eleza kuwa msimwache mke "kama aliye tundikwa")
Rudi kwenye Sura
6, 7. Hayo yaliyo tangulia ya kuumbwa binaadamu, na mimea ya kupanda,
ni ushahidi ya kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wa Haki. Na
kwamba hakika Yeye ndiye anaye huisha maiti wakati wa kufufuliwa kama vile
alivyo anza kuwaumba. Na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu, na
kwamba hakika Kiyama kinakuja tu bila ya shaka kuhakikisha ahadi yake.
Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawahuisha waliomo makaburini kwa kuwafufua
kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
8. Na juu ya yaliyo tangulia bado wapo baadhi ya watu wanao jadili
juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu, na wanakanya kufufuka bila ya msingi wowote
wa ki-ilimu, wala uwongozi wa kweli, au Kitabu kilicho toka kwa Mwenyezi
Mungu cha kumwonyesha. Basi ubishi wake ni wa pumbao na inda tu.
Rudi kwenye Sura
9. Na pamoja na hayo hugeuka upande kwa kiburi na kukataa kuikubali
Haki. Na watu wa namna hii itakuja wapata hizaya na udhalili duniani kwa
ushindi wa Neno la Haki, na Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa
Moto wa kuunguza.
Rudi kwenye Sura
10. Na ataambiwa: Hayo unayo yapata ya hizaya na adhabu ni kwa sababu
ya uzushi wako na kiburi chako; kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Muadilifu,
hadhulumu. Wala hawaweki sawa Muumini na kafiri, na mwema na muovu; bali
kila mmoja wao atamlipa kwa mujibu wa vitendo vyake.
Rudi kwenye Sura
11. Na miongoni mwa watu wapo wa namna ya tatu, ambao Imani
bado haijatulia katika nyoyo zao, bali itikadi yao inayumba yumba. Maslaha
ya nafsi zao ndiyo yanatawala katika Imani yao. Wakipata kheri hufurahi
na hutulizana. Na wakipata shida yoyote katika nafsi zao, au mali zao,
au wana wao, hurejea ukafirini. Hao huwa wamekosa duniani raha ya utulivu
kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu na nusura yake, kama Akhera walivyo kosa neema
ambayo Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini walio thibiti na wakasubiri. Hiyo
khasara ya mara mbili ndiyo khasara ya kweli kweli iliyo wazi.
Rudi kwenye Sura
12. Mwenye kukhasiri hivi humuacha Mwenyezi Mungu na akayaabudu masanamu
yasiyo weza kumdhuru pindi akito yaabudu, wala hayamfai kitu pindi akiyaabudu.
Kitendo chake huyo ndio kupotelea mbali na haki na uwongofu.
Rudi kwenye Sura
13. Badala ya Mwenyezi Mungu anamwomba ambaye madhara yake kwa kuharibu
akili na kutawala mawazo ovyo ni karibu zaidi kwa nafsi kuliko kuitakidi
msaada wake. Muabudiwa huyo ni muovu mno wa kumtaraji msaada, na muovu
mno kumfanya rafiki.
Rudi kwenye Sura
14. Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake kwa Imani
yenye kuambatana na vitendo vyema, Mola wao Mlezi atawatia Siku ya Kiyama
katika Bustani zipitwazo chini ya miti yake na mito. Hakika Mwenyezi Mungu
hutenda apendavyo kumuadhibu mharibifu na kumlipa mema mtenda mema.
Rudi kwenye Sura
15. Ikiwa miongoni mwa makafiri yupo anaye dhani kwamba Mwenyezi
Mungu hatamsaidia Nabii wake, basi na anyooshe kamba mpaka kwenye dari
ya nyumba yake. Kisha ajinyonge, na akadirie katika nafsi yake na atazame,
je, kitendo chake hicho kitaondoa hayo yanayo muudhi ya kuwa Mwenyezi Mungu
anamnusuru Mtume wake?
Rudi kwenye Sura
16. Mfano wa tulivyo bainisha hoja zetu zi wazi katika tuliyo kwisha
wateremshia Mitume. Tumemteremshia Muhammad Qur'ani yote, nayo ni Aya zilizo
wazi ili ziwe ni hoja juu ya watu. Na hakika Mwenyezi Mungu humuongoa amtakaye
kuwaongoa ili isalimike tabia yake na abaidike mbali na inadi na yanayo
sabibisha hayo.
Rudi kwenye Sura
17. Hakika wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wote, na Mayahudi
wanao nasibika na Musa, na waabuduo nyota na Malaika, na Wakristo wanao
nasibika na Isa, na Majusi wanao abudu moto, na washirikina wanao abudu
masanamu..hakika wote hawa Mwenyezi Mungu atakuja wapambanua mbali mbali
Siku ya Kiyama kwa kumdhihirisha mwenye haki na aliye potea kati yao. Kwani
Yeye anajua vyema vitendo vyote vya viumbe vyake. Na atawalipa kwa vitendo
vyao.
Rudi kwenye Sura
18. Ewe mwenye akili! Hujui kwamba hakika Mwenyezi Mungu vinamnyenyekea
na kumt'ii vyote viliomo mbinguni na katika ardhi, na jua, na mwezi, na
nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi katika watu wanamuamini
Mwenyezi Mungu na wanafuata maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki Pepo?
Na wapo wengi miongoni mwao wanao puuza na wala hawamuamini, wala hawayatendi
maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki adhabu na hizaya. Na anaye fukuzwa
na Mwenyezi Mungu kutokana na rehema yake basi hawezi yeyote kumhishimu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. Kwani Yeye hutenda ayapendayo.
Rudi kwenye Sura
19. Haya ni makundi mawili walio zozana kwa mambo yaliyo mkhusu Mola
wao Mlezi, na yanayo mstahiki na yasio mstahiki. Kikundi kimoja kikamuamini
na kikundi kingine kikakataa. Basi wale walio kataa na kukufuru Mwenyezi
Mungu amewaandalia Siku ya Kiyama moto utao wazunguka na kuwapamba kila
upande, kama nguo inavyo upamba mwili. Na kuzidi kuwaadhibu Malaika watawamiminia
maji ya moto mno juu ya vichwa vyao!
Rudi kwenye Sura
20. Yatawapenya mpaka kwenye matumbo yao, viliomo ndani viyayuke
kama zitavyo yayuka ngozi zao!
Rudi kwenye Sura
21. Na pia wataandaliwa marungu ya chuma.
Rudi kwenye Sura
22. Kila wakijaribu kutoka Motoni kwa wingi wa machungu na dhiki
Malaika watawapiga nayo hayo marungu, na watarudishwa huko huko waliko
kuwako. Na watawaambia: Onjeni adhabu ya Moto unao unguza kuwa ni malipo
ya ukafiri wenu.
Rudi kwenye Sura
23. Ama walio amini na wakatenda vitendo vyema, hao bila ya shaka
Mwenyezi Mungu atawaingiza kwenye Mabustani yanayo pita mito kati ya majumba
yake na miti yake. Humo watastarehe kwa kila namna ya starehe, na Malaika
watawapamba vikuku vya mikono vya dhahabu na watawapamba kwa lulu. Ama
nguo zao za kawaida zitakuwa za hariri.
Rudi kwenye Sura
24. Na ziada ya starehe yao humo Peponi ni kuwa Mwenyezi Mungu atawajaalia
wawe na kauli njema, na vitendo vizuri vya kusifika. Basi watakuwa wakimtakasa
Mwenyezi Mungu na kumtukuza, na watakuwa wenyewe kwa wenyewe wakiamiliana
kwa mapenzi na amani.
Rudi kwenye Sura
25. Hakika wale walio kufuru, yaani walio mkataa Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, na pamoja na hayo wakawa mtindo wao kuwazuia watu wasiingie
katika Uislamu, na kuwafanyia pingamizi Waumini kuingia kwenye Msikiti
Mtakatifu wa Makka - na ilhali Mwenyezi Mungu ameufanya huo ni pahala pa
amani kwa watu wote, mkaazi na mpita njia - atawapa watu hao adhabu kali.
Na hali kadhaalika kila atakaye kengeuka na Haki, na akatenda udhalimu
wowote katika pahala patakatifu, Mwenyezi Mungu atamuadhibu adhabu ya kutia
uchungu.
Rudi kwenye Sura
26. Ewe Nabii! Watajie hawa washirikina wanao dai kuwa ati wanamfuata
Ibrahim a.s. na wakaifanya Nyumba Takatifu kuwa ni pahala pa kuwekea masanamu
yao; watajie kisa cha Ibrahim na Nyumba Takatifu tulipo mwongoza mpaka
pahala pake, na tukamuamrisha aijenge, na tukamwambia: Usinishirikishe
Mimi na kitu chochote katika ibada. Na isafishe Nyumba yangu na masanamu
na uchafu, ili iwe ni pahala pa makusudi ya mwenye kuizunguka kwa kut'ufu,
na mwenye kukaa hapo na akafanya ibada.
Rudi kwenye Sura
27. Ewe Nabii! Wajuvye watu kwamba hakika Mwenyezi Mungu amewalazimisha
wawezao miongoni mwao waijie hii Nyumba. Basi waitikie wito wako, watakujia
kwa miguu na kwa kupanda ngamia aliye konda kwa ajili ya safari ya kutoka
mbali.
Rudi kwenye Sura
28. Ili wapate manufaa yao ya Kidini kwa kutekeleza Hija na manufaa
ya kiduniani kwa kujuana na ndugu zao Waislamu na kushauriana nao katika
mambo ya Dini yao na dunia yao. Nao wataje jina la Mwenyezi Mungu katika
Siku ya Idi Kubwa na siku tatu zifwatazo, pale wanapo chinja walio jaaliwa,
ikiwa ngamia, au ng'ombe au kondoo na mbuzi. Kuleni mpendacho katika hao,
na muwalishe walio patwa na shida na ufakiri.
Rudi kwenye Sura
29. Tena baada ya hao yawapasa waondoe takataka na uchafu ulio wapata
wakati ule wa Ih'ram (yaani kuharimia Hija), nao ni majasho na safari ndefu.
Pia waondoe nadhiri walizo mwekea Mwenyezi Mungu, ikiwa wameweka nadhiri
yoyote. Na waizunguke kwa kwenda kwa miguu ile Nyumba iliyo jengwa kwa
ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu duniani.
Rudi kwenye Sura
30. Na mwenye kuzishika amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake katika
Hija yake kwa kuzitukuza katika nafsi yake, hayo yatakuwa ni kheri yake
katika dunia yake na Akhera yake. Na Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kula
nyama hoa, (mifugo) yaani ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, ila katika
hali mnazo zijua kwa mlivyo kwisha somewa katika Qur'ani, kama vile nyamafu
na nyenginezo. Basi epukaneni na kuabudu masanamu, kwani ibada hiyo ni
uchafu wa kiakili na kiroho, na haimwelekei mwanaadamu kufanya hivyo. Na
epukaneni na kusema uwongo, kumzulia Mwenyezi Mungu au mwanaadamu.
Rudi kwenye Sura
31. Na kuweni wenye kumsafia niya Mwenyezi Mungu, wenye pupa kutaka
kuifuata Haki, bila ya kumfuata mshirika wowote na Mwenyezi Mungu katika
ibada. Kwani mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu ameanguka huyo kutoka
kwenye ngome ya Imani, na amesalitiwa na upotovu, na ameitia nafsi yake
katika hilaki ya kutisha kabisa. Ikawa hali yake kama hali ya mtu aliye
poromoka kutoka mbinguni na midege ikamrarua akakatika mapande mapande,
asibakie hata alama. Au kama aliye peperushwa na upepo mkali, na mwili
ukatawanyika mwahala mbali mbali.
Rudi kwenye Sura
32. Hakika mwenye kuitukuza Dini ya Mwenyezi Mungu na faridha ya
Hija na a'mali zake na mihanga inayo pelekwa kwa ajili mafakiri wa Al-Haram,
na wakachagua walio nona wazima, hawana ila, basi huyo ndio amemcha Mwenyezi
Mungu. Kwani kutukuza kwake hayo ni matokeo ya unyenyekevu wa nyoyo zilizo
amini, na alama katika alama za usafi wa niya.
Rudi kwenye Sura
33. Katika kutoa mihanga hii yapo manufaa ya kidunia. Mnawapanda
na mnakunywa maziwa yake mpaka wakati wa kuwachinja. Kisha mnapata manufaa
ya Kidini vile vile pale mnapo wachinja kwenye Nyumba Takatifu kwa kutafuta
kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
34. Hizi faridha za Hija hazikukhusuni nyinyi peke yenu. Kwani tumewajaalia
jamaa wote walio amini mambo ya kuwakaribisha kwa Mwenyezi Mungu, na wanataja
jina lake, na wanamtukuza wakati wanapo chinja kwa kumshukuru kwa neema
aliyo waneemesha, na kuwasahilishia wanyama wa mifugo, nao ni ngamia, ng'ombe,
mbuzi na kondoo. Na Mwenyezi Mungu aliye kuwekeeni sharia nyinyi na wao
ni Mungu Mmoja. Basi yasalimisheni mambo yenu yote kwake Yeye peke yake.
Na vitendo vyenu visafisheni kwake, wala msimshirikishe na yeyote. Na ewe
Nabii! Wape bishara ya Pepo na thawabu nyingi wale walio safisha niya zao
kwa Mwenyezi Mungu na wakawa wanamnyenyekea Yeye miongoni mwa waja wake,
Rudi kwenye Sura
35. Wale ambao akitajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hupapatika kwa kumkhofu,
na hunyenyekea kwa kutajwa kwake, na ambao wanasubiri kwa masaibu ya karaha
na shida yanayo wapata kwa kujisalimisha mbele ya amri yake na hukumu yake,
na wakashika Sala kwa ukamilifu wake, na wakatoa baadhi ya mali aliyo waruzuku
Mwenyezi Mungu katika njia za kheri.
Rudi kwenye Sura
36. Nasi tumefanya uchinjaji ngamia na ng'ombe n.k. katika Hija kuwa
ni katika matukuzo ya Dini yalio dhaahiri. Na nyinyi kwa hayo mnajileta
karibu na watu. Nanyi katika hao mnapata kheri nyingi katika dunia kwa
kuwapanda, na kunywa maziwa yake. Na Akhera mnapata malipo na thawabu kwa
kuwachinja na kuwalisha mafakiri. Basi tajeni jina la Mwenyezi Mungu wakati
mnapo wapanga kwa safu kwa ajili ya kuwachinja. Mkisha wachinja kuleni
sehemu mkitaka, na walisheni mafakiri walio kinai hawaombi, na ambao wanalazimika
kuomba kwa haja. Na kama tulivyo fanya kila kitu kiwe kit'iifu kwa tuyatakayo
kwa ajili ya manufaa yenu, na tumedhalilisha hivyo vikut'iini nyinyi ili
mpate kuishukuru neema yetu kubwa iliyo juu yenu.
Rudi kwenye Sura
37. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu haangalii sura zenu wala vitendo
vyenu, lakini anaangalia nyoyo zenu. Wala hataki kwenu mambo ya kujionyesha
tu kwa kuchinja na kumwaga damu. Lakini anataka kwenu moyo wenye kunyenyekea.
Basi hapati radhi yake mwenye kugawa hizo nyama wala damu. Lakini linalo
pata radhi yake ni uchamngu wenu na usafi wa niya zenu. Kuwadhalilisha
hao wanyama tulivyo wadhalilisha ni kwa ajili ya kukunafiisheni, mpate
kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa vile alivyo kuongoeni hata mkatimiza ibada
za Hija. Na ewe Nabii! Wape khabari njema watu wema walio tengeneza a'mali
zao na niya zao kuwa watapata malipo makuu.
Rudi kwenye Sura
38. Hakika Mwenyezi Mungu huwalinda Waumini na huwahami na huwanusuru
kwa Imani yao. Kwani Yeye hawapendi wenye kukhuni dhamana zao, wenye kupita
mipaka katika ukafiri wao kumkataa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu hamsaidii
yule asiye mpenda.
Rudi kwenye Sura
39. Mwenyezi Mungu amewaruhusu Waumini wanao pigwa vita na washirikina
wawarejezee uadui wao, kwa sababu ya dhulma iliyo wapata nao wakasubiri
kwa muda mrefu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuweza kuwanusuru vipenzi
vyake Waumini.
" Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa
- na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia" Yaliyo tajwa na
Qur'ani Tukufu kukhusu hukumu iliomo katika Aya 39 yamezitangulia kanuni
zilizo kuja kuwekwa na madola baada yake, nayo ni kuwa mtu kujitetea nafsi
yake ni sharia vyovyote vile itavyo kuwa matokeo yake. Na kwamba mwenye
kuitetea nafsi yake, na mali yake, na nchi yake, hawi ni mkosa mbele ya
Mwenyezi Mungu na mbele ya uadilifu, ijapo kuwa ameuwa mtu au ameteketeza
roho nyingi. Aya hii imepasisha kuwa Waislamu wanayo ruhusa kujitetea pindi
wakivamiwa. Na kwa hivyo tunafahamu kuwa vita vya Waislamu vilikuwa vita
vya utetezi na kujilinda si vita vya kushambulia na kuvamia. Na kwamba
Waislamu waliusimamisha Uislamu na wakaupa nguvu kwa hoja zilizo wazi,
na dalili zilizo dhaahiri.
Rudi kwenye Sura
40. Hao ambao makafiri wamewadhulumu na wakawalazimisha waache mji
wao wa Makka wauhame. Na wao hawakuwa na kosa lolote ila ni kuwa walimjua
Mwenyezi Mungu na wakamuabudu Yeye pekee. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwatumilia
kwa ajili ya Haki wasaidizi wa kumnusuru Yeye na wakamtetea kupinga jeuri
za madhaalimu, basi hapana shaka upotovu ungeli enea, na majeuri wangeli
endelea katika jeuri zao, na sauti ya haki wangeli inyamazisha. Wala
wasingeli achiliwa Wakristo makanisa yao, wala mamonaki (wat'awa wa Kikristo)
wasinge baki na monastari zao (nyumba zao za ibada), wala Mayahudi wansinge
kuwa na masinagogi yao, wala Waislamu wasinge kuwa na misikiti yao, ambamo
mote humo hutajwa kwa wingi jina la Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
amechukua juu ya nafsi yake ahadi ya nguvu ya kwamba atamsaidia na kumnusuru
kila anaye isaidia Dini yake, na atamtukuza kila mwenye kulitukuza Neno
la Haki katika ulimwengu. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haiendi kinyume. Kwani
Yeye ni Mwenye nguvu wa kutimiza alitakalo, Mtukufu hashindwi na yeyote.
Rudi kwenye Sura
41. Hao Waumini tulio waahidi kuwanusuru ndio hao ambao tukiwapa
madaraka katika nchi wanalinda makhusiano yao na Mwenyezi Mungu na pia
na wanaadamu wenzao. Kwa hivyo hushika Sala kwa utimilifu wake, na huwapa
Zaka wanao stahiki kupewa, na huamrisha kila lenye kheri, na hukataza kila
lenye shari. Na mambo yote hurejea kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Basi Yeye
humtukuza amtakaye, na humdhalilisha amtakaye.
Rudi kwenye Sura
42. Ewe Nabii! Ukiwa unapata makanusho, kuambiwa mwongo, na maudhi
kutokana na watu wako, basi usisikitike. Zingatia taarikh kwa yaliyo wapata
Mitume wa kabla yako, utaona kwamba wewe si Mtume wa kwanza aliye kanushwa
na kuudhiwa na watu wake. Kwani kabla ya hawa walio kukanusha wewe, kaumu
Nuhu walimkadhibisha Mtume wao Nuhu, na kaumu ya A'ad walimkadhibisha Mtume
wao Huud, na kina Thamud walimkanusha Mtume wao Saleh.
Rudi kwenye Sura
43. Na kaumu ya Ibrahim walimkanusha Mtume wao Ibrahim, na kaumu
Lut'i walimfanyia hayo hayo Mtume wao Lut'i.
Rudi kwenye Sura
44. Na watu wa Madiana walimkanusha Mtume wao Shua'ib. Na Firauni
na watu wake walimkanusha Mtume wa Mwenyezi Mungu Musa. Mitume hao wote
yaliwapata yanayo kupata wewe. Na Mimi niliwapa muhula hao wakanushao ili
wapate kutubia waongoke, na waitikie Wito wa Haki. Lakini wakazua na wakaendelea
na kuwakadhibisha Mitume wao na kuwaudhi. Wakazidisha madhambi juu ya madhambi
yao. Basi nikawaadhibu ukomo wa kuwaadhibu. Angalia taarikhi yao utaona
kuwa adhabu yangu ilikuwa kali mno, pale nilipo ibadilisha neema ikawa
nakama, na uzima ukawa ni maangamizo, na badala ya ujenzi ukawa uharibifu.
Rudi kwenye Sura
45. Basi tuliwatekeza watu wengi wa miji ambayo waliiamirisha, kwa
sababu ya udhalimu wao na kukanusha kwao Mitume wao. Zikawa paa za nyumba
zao zimeangukia kuta zake, hazina wakaazi. Kama kwamba jana hazikuwapo.
Visima vingapi vilivyo bomoka na maji yake yakapotea, na majumba mangapi
madhubuti yaliyo jengwa kwa mawe na saruji na chokaa, yamekuwa magofu hayana
wakaazi!
Rudi kwenye Sura
46. Hivyo wao wanasema wayasemayo na wanahimiza waletewe adhabu,
nao hawatembei ulimwenguni wakaona kwa macho yao walivyo teketea hao madhaalimu
wakanushao? Huenda hapo nyoyo zao zikagutuka kutokana na ghafla iliyo wapamba,
na wakatia akilini yanao wapasa wakafuata hayo ya wito wa Haki unao waitia.
Na masikio yao yakisikia vifo vya hao makafiri huenda wao wakazingatia.
Lakini wapi! Ya mbali hayo kuwa watu hawa waweze kuzingatia kwa wanayo
yaona au kuyasikia maadamu nyoyo zao zimekuwa kama mawe. Kwani kipofu wa
kweli siye yule aliye pofuka macho, lakini ni yule aliye pofuka moyo na
hatambui kitu.
Rudi kwenye Sura
47. Na makafiri wa Makka wameshikwa na udanganyifu, na hawana wanalo
litambua juu ya kuwepo dalili zote hizi. Kwa hivyo ndio wanakuhimiza, wewe
Nabii, uwaletee adhabu ulio waahidi. Wanasema hayo kwa upinzani na kejeli.
Na hayo hapana shaka yoyote yatawapata, lakini kwa wakati alio uweka Mwenyezi
Mungu, ama duniani au Akhera. Naye hendi kinyume na ahadi yake, hata ikipita
miaka. Kwani siku moja kwake ni kama miaka elfu mnayo ikadiria na kuihisabu.
"Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda
kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni
kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Qur'ani kwa Aya hii tukufu imeutangulia
msafara wa wana sayansi kwa kueleza kuwa zama ni kipimo cha mnasaba, na
kwamba fikra ya kuwa zama kwa ulimwengu ni moja kama watu wa zamani walivyo
kuwa wakifikiri ni makosa.
Rudi kwenye Sura
48. Na wengi katika watu wa mijini walikuwa madhaalimu kama wao.
Nami nikawapa muhula wala sikuwafanyia haraka kuwaadhibu. Na kisha nikawateremshia
hiyo adhabu. Na ni kwangu Mimi tu ndio marejeo ya wote Siku ya Kiyama;
na hapo nitawalipa kwa wanayo stahiki. Basi enyi makafiri! Msighurike kwa
kuchelewa adhabu kukufikieni.
Rudi kwenye Sura
49. Ewe Nabii! Waambie hao wanao kanusha, wanao kuhimiza waletewe
adhabu: Sio kazi yangu mimi kukulipeni kwa vitendo vyenu. Bali hakika mimi
ni mwenye kukuhadharisheni kwa hadhari iliyo wazi kwamba kuna adhabu. Na
Mwenyezi Mungu ndiye wa kukuhisabuni na kukulipeni.
Rudi kwenye Sura
50. Na wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda
vitendo vyema, watapata kutokana na Mwenyezi Mungu kusamehewa dhambi zao
walizo ziingia, kama kadhaalika watavyo pata riziki ya ukarimu huko Peponi.
Rudi kwenye Sura
51. Na wale walio jikukusa nafsi zao katika kuipiga vita Qur'ani
kushindana na Waumini na kuwapinga, wakitamani na kudai kwa uwongo, kwamba
wao watapata wayatakayo - watu hao watabaki milele katika adhabu ya Motoni.
Rudi kwenye Sura
52. Ewe Nabii! Usihuzunike kwa hizi hila za makafiri. Yalimpata kama
haya kila Mtume katika Mitume wetu, na kila Nabii katika Manabii wetu.
Nayo ni kuwa kila wakiwasomea kitu kwa kuwaita waifuate Haki Mashetani
wa kibinaadamu walio asi wakiyapinga ili waubat'ilishe Wito, na wawatie
shaka watu kwa yale wanayo somewa. Makusudio yao ni kujiingiza kati baina
ya Nabii na matamanio yake ya kutaka Wito wake uitikiwe. Lakini Mwenyezi
Mungu huyaondoa wayatakayo. Na mwishoe Haki ndiyo inayo shinda anapo isimamisha
Mwenyezi Mungu sharia yake, na akamnusuru Mtume wake. Na Yeye ndiye Mwenye
kuzijua hali za watu na vitimbi vyao, Mwenye hikima katika vitendo vyake.
Anaweka kila kitu pahala pake.
Rudi kwenye Sura
53. Na hakika Mwenyezi Mungu amewawezesha waasi wanao kataa Haki
waweze kutumbukiza shakashaka na vikwazo katika Njia ya Wito ili uwe ni
mtihani na majaribio kwa watu. Makafiri ambao nyoyo zao zimegeuka mawe,
na wanaafiki ambao nyoyo zao zina maradhi, huzidi upotovu kwa kueneza shakashaka
hizi na kuziunga mkono. Na si ajabu madhaalimu hawa kusimama msimamo huu,
kwani wao wamezama katika upotovu na wamevuka mpaka katika inadi na mfarakano.
Rudi kwenye Sura
54. Na ili walio pewa ilimu ya sharia na Imani wazidi Imani na kujua
kwamba wayasemayo Mitume na Manabii hakika ni kweli iliyo teremka kutokana
na Mwenyezi Mungu. Na kwamba Mwenyezi Mungu hakika anawalinda Waumini kwa
hima yake kutokana na matatizo yote yanayo wapitikia. Na huwaongoa kwenye
maarifa ya Njia Iliyo Nyooka nao wakaifuata.
Rudi kwenye Sura
55. Na walio kufuru hawatengenei. Bali wanaendelea kuitilia shaka
Qur'ani mpaka wafikiwe na mauti, iwafikie adhabu ya Siku isiyo kuwa na
kheri kwao wala rehema; nayo ni Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
56. Siku ambayo madaraka ya nguvu, na uendeshaji mambo usio na ukomo
wote, ni wa Mwenyezi Mungu pekee. Siku hiyo ndipo atapo hukumu baina ya
waja wake. Walio amini na wakatenda mema watadumu katika Bustani zilizo
jaa kila namna ya neema.
Rudi kwenye Sura
57. Na walio kufuru na wakazikanusha Aya za Qur'ani tulizo mteremshia
Muhammad, hao watakuta adhabu ya madhila na fedheha.
Rudi kwenye Sura
58. Na wenye kuacha nchi zao kwa ajili ya kutukuza shani ya Dini
yao wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, kisha wakauliwa katika uwanja wa
Jihadi, au wakafa vitandani mwao, Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mazuri
kabisa. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kutoa thawabu za ukarimu.
Rudi kwenye Sura
59. Na hakika atawatia katika Pepo kwenye vyeo watavyo ridhika navyo
na vitawafurahisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua vyema hali
zao, basi atawalipa malipo bora, naye ni Mpole huyasamehe makosa yao madogo
madogo ya kuteleza.
Rudi kwenye Sura
60. Huo ndio mwendo wetu katika kuwalipa watu. Hatuwadhulumu. Na
Muumini mwenye kulipiza kisasi kwa aliye mfanyia uovu, na akalipiza kwa
kadri ya alivyo tendewa bila ya kuzidisha, kisha yule mkosa akaja kumfanyia
uadui tena baada yake, basi hakika Mwenyezi Mungu anatoa ahadi ya nguvu
kuwa atamnusuru na kumsaidia yule aliye dhulumiwa. Na hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwingi wa kumsamehe mwenye kulipiza kama alivyo dhulumiwa. Hamtii makosani
kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, basi huyasitiri makosa
ya kuteleza ya mja wake mt'iifu, wala hamfedhehi Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
61. Msaada huo ni mwepesi kwa Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni Muweza
wa kila kitu. Na katika Ishara za uwezo wake zilio wazi mbele yenu ni utawala
wake juu ya ulimwengu wote. Huzungusha usiku na mchana, pengine huzidi
huu au huzidi huu. Inakuwa baadhi ya kiza cha usiku pahala pa mwanga wa
mchana. Na pengine huwa kinyume cha hivyo. Naye Subhanahu juu ya uwezo
wake husikiliza kauli ya aliye dhulumiwa, na anaviona vitendo vya mwenye
kudhulumu. Basi humtia adhabuni.
Rudi kwenye Sura
62. Huo ndio msaada wa wenye kudhulumiwa unao tokana na Mwenyezi
Mungu Mtukufu. Na kutenda kwake katika ulimwengu kama atakavyo bila ya
kiwango ni kama muonavyo matokeo yake; na kwa hakika Yeye ndiye Mungu wa
Haki ambaye hapana mungu mwenginewe pamoja naye. Na kwamba masanamu wanayo
yaabudu washirikina ni uwongo, hayana ukweli, na Mwenyezi Mungu peke yake
ndiye aliye tukuka juu ya vyote isipo kuwa Yeye Mwenyewe kwa shani yake,
na ni Mkuu wa madaraka.
Rudi kwenye Sura
63. Ewe mwenye akili! Huzingatii haya yalio kuzunguka uyaonayo kwa
macho yenye kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukamuabudu Yeye peke yake?
Yeye ndiye anaye iteremsha mvua kutoka mawinguni, na ardhi ikageuka rangi
ya kijani kibichi kwa mimea inayo chipuka, baada ya kuwa na ukame.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole mno kwa waja wake, na anajua vyema yanayo
wanufaisha na kwa hivyo akawatengenezea kwa kudra yake.
Rudi kwenye Sura
64. Kila kiliomo mbinguni na katika ardhi ni chake Yeye, na kinamtumikia
Yeye peke yake, na anakiendesha kama apendavyo. Na Yeye hawahitajii waja
wake, bali wao ndio wanao mhitajia Yeye. Na Yeye ndiye anaye stahiki peke
yake kuhimidiwa na kusifiwa na viumbe vyote.
Rudi kwenye Sura
65. Ewe mwenye akili! Huyaangalii yaonekanayo kwa macho ya uwezo
wa Mwenyezi Mungu, ukaona anavyo wasahilishia watu wote kunafiika na ardhi
na viliomo ndani yake? Na akawatengenezea bahari za kwendea ndani yake
marikebu kwa mujibu apendavyo Yeye? Na akazishika sayari zote ziliomo angani
kwa kudra yake hata zisikosee mpango wake, au zikaangukia kwenye ardhi,
isipo kuwa akitaka kwa mapenzi yake. Hakika Mwenyezi Mungu Aliye
takasika ni Mwingi wa huruma na rehema kwa waja wake. Kwa hivyo amewatengenezea
kila njia za maisha mema. Huwaje basi baada ya haya yote hamumsafii niya
Yeye kwa kumshukuru na kumuabudu?
"Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo
katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika
mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu." Aya hii tukufu inakusanya
maana za kisayansi za ndani. Mbingu, nayo ni kila kilicho juu yetu, inaanza
kwa kuifunika ardhi kwa hewa, tena kwa anga, tena kwa vyombo vya mbinguni
vinavyo toa mwanga kama nyota n.k. na visio toa mwanga wake mwenyewe kama
mwezi, na sayari nyengine, na nyota mkia, na vumbi la ulimwengu, n.k. Vyote
hivi vinakuwa vilivyo na vinashikana kwa athari ya nguvu mbali mbali. Muhimu
wa hizo ni mvuto na nguvu inayo tokana na kule kuzunguka kwao.
Yamedhihiri mapenzi ya Mwenyezi Mungu na huruma zake kwa waja wake
kuwa katengeneza kifuniko cha angani kina namna za gasi mbali mbali ambazo
ni dharura kwa uhai. Kama pia anawalinda wakaazi wa duniani na mianga na
vimondo n.k. vinavyo zunguka angani na ambavyo vinapo karibia kwenye ardhi
huungua kabla havijafika chini.
Na katika mapenzi yake na rehema yake Mwenyezi Mungu ni kuwa hivyo
vimondo vinavyo anguka kwenye ardhi ni nadra sana kutokea, na hutokea mwahala
wasipo kaa watu. Jambo hili la dhaahiri laonyesha huruma na rehema ya Mwenyezi
Mungu kwa waja wake. Na haya yanatilia nguvu na kusadikisha kauli yake
Mwenyezi Mungu: " na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa
idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu."
Rudi kwenye Sura
66. Na Yeye ndiye aliye kupeni uhai. Kisha anakufisheni unapo malizika
muda wenu. Kisha tena atakufufueni Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na
malipo. Hakika mwanaadamu baada ya neema zote hizi na ushahidi wote huu
ni mwingi wa kumkataa Mwenyezi Mungu na kuzikataa neema zake alizo mpa.
Rudi kwenye Sura
67. Tumewajaalia katika kila umma walio kwisha tangulia wawe na sharia
zao makhsusi zinazo ambatana na zama zao, za kumuabudia Mwenyezi Mungu,
mpaka zinapo kuja futwa na zijazo baadae. Na kwa hivyo tumewajaalia watu
wako, ewe Nabii, wawe na Sharia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka Siku
ya Kiyama. Ilivyo kuwa hivi ndio amri yetu na mpango wetu, basi hao wanao
jiabudia kwa dini zao zilizo pita, haiwafalii wao kutia mkazo katika kukupinga
wewe. Kwani hakika sharia yako wewe imefuta sharia zao. Basi usijishughulishe
na kujadiliana nao. Nawe endelea kuwaita watu wende kwa Mola wako Mlezi
kwa mujibu wa unavyo pewa wahyi (ufunuo). Hakika wewe unafuata Uwongofu
Ulio Nyooka wa Mola wako Mlezi.
Rudi kwenye Sura
68. Na wakishikilia kuendea kukujadili basi waachilie mbali, na waambie:
Mwenyezi Mungu anajua zaidi vitendo vyenu, na malipo mnayo yastahiki.
Rudi kwenye Sura
69. Mwenyezi Mungu atahukumu baina yangu na nyinyi Siku ya Kiyama
katika hayo mnayo khitalifiana nami. Atamlipa thawabu aliye ongoka na atamuadhibu
aliye potoka.
Rudi kwenye Sura
70. Ewe mwenye akili! Jua kuwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu umekusanya
kila kiliomo mbinguni na duniani. Hapana kitendo cha hawa washindani kinacho
fichika kwake. Vyote hivyo vimekwisha andikwa katika Ubao ulio hifadhiwa
(Lauhun Mahfuudh). Kwani kujua kwake Mwenyezi Mungu na kuvithibiti kwake
ni kazi nyepesi kabisa kwake.
Rudi kwenye Sura
71. Na washirikina huabudu badala ya Mwenyezi Mungu masanamu na watu
ambao haikuteremka hoja yoyote ya kuwaabudu hao katika Kitabu cha mbinguni
chochote. Wala wao hawana ushahidi wowote wa kuingia akilini. Lakini
wanafanya yote hayo kufuata pumbao na mila tu. Wala hao washirikina walio
zidhulumu nafsi zao na wakazidharaulisha akili zao hawato pata msaidizi
wa kuwanusuru, na kuwakinga na adhabu ya Moto Siku ya Kiyama, kama wanavyo
jidai.
Rudi kwenye Sura
72. Ewe Nabii! Hawa washirikina mtu akiwasomea Aya zetu zilizo wazi,
na ambazo ndani yake mna ushahidi wa ukweli wa hayo unao waitia, na ubaya
wa ibada zao, utaona katika nyuso zao ghadhabu na chuki inayo wajaa, hata
inakaribia kuwapelekea kutaka kumuuwa huyo anaye wasomea. Ewe Nabii! Waambie
kwa kuwazindua na kuwaonya: Je! Mtanisikiliza nikwambieni yaliyo kuwa mabaya
zaidi kuliko hiyo chuki inayo kuunguzeni roho? Ni Moto ambao Mwenyezi Mungu
amewaahidi walio kufuru kama nyinyi Siku ya Kiyama. Na hapana mwisho mbaya
na makaazi maovu kuliko hayo.
Rudi kwenye Sura
73. Enyi watu! Sisi tunakufahamisheni ukweli wa ajabu, basi hebu
usikilizeni na muuzingatie. Haya masanamu hayataweza kabisa kuumba chochote
hata kikiwa kitu duni kabisa kama nzi; hata ikiwa yote yakisaidiana
katika kuumba huko. Bali huyu makhluku duni kabisa akiwanyang'anya chochote
katika hizo sadaka wanazo pewa masanamu hawawezi kumzuia au kumfukuza.
Unyonge gani basi huo wa kushindwa na nzi kutoweza kurejesha alicho pokonya.
Na nzi ni kitu dhaifu mno! Wote wawili ni wanyonge. Bali hayo masanamu
ambayo kama mnavyo ona ni dhaifu zaidi, basi huwaje mwanaadamu mwenye akili
akenda kuyaabudu na kutaka yamnafiishe.
Rudi kwenye Sura
74. Hawa washirikina hawamjui Mwenyezi Mungu kama anavyo faa
kujuulikana, wala hawamtukuzi kama anavyo stahiki kutukuzwa, walipo kwenda
kumshirikisha katika ibada na vitu visio kuwa na maana kabisa. Na hali
kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muweza wa kila kitu, Asiye shindika na yeyote.
Rudi kwenye Sura
75. Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na hikima yake yamempelekea kuteuwa
Wajumbe kutokana na Malaika, na kutokana na wanaadamu, ili wafikishe sharia
yake kwa viumbe vyake. Basi huwaje mkampinga aliye mchagua Mwenyewe kuwa
ni Mjumbe wake kwenu? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia wayanenayo
waja wake, Mwenye kuviona vitendo wavitendavyo. Naye atawalipa kwavyo.
Rudi kwenye Sura
76. Na Yeye Subhanahu anajua hali zao zilizo dhaahiri na za ndani.
Hapana kinacho fichika kwake. Na kwake Yeye pekee ndiyo yanarejea mambo
yote.
Rudi kwenye Sura
77. Enyi mlio amini! Msishughulikie upotovu wa makafiri. Nyinyi endeleeni
na kutimiza Sala zenu kwa ukamilifu kwa kurukuu na kusujudu. Na muabuduni
Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni na akakuruzukuni. Wala msimshirikishe naye
na yeyote. Na tendeni kila lenye kheri na manufaa, ili mpate kuwa watu
wema, walio bahatika katika Akhera yenu na dunia yenu.
Rudi kwenye Sura
78. Na wanieni katika Jihadi ya kunyanyua Neno la Mwenyezi Mungu
na kutafuta radhi zake mpaka mwashinde maadui zenu na myashinde matamanio
yenu. Kwani Yeye Subhanahu amekukaribisheni kwake, na amekuteueni muinusuru
Dini yake, na amekujaalieni muwe Umma wa katikati. Wala hakukulazimisheni
katika aliyo kuwekeeni Sharia lolote lenye mashaka juu yenu msilo weza
kulichukua. Na amekufanyieni mepesi katika yanayo kuleteeni mashaka,
na katika msiyo yaweza amekufanyieni ruhusa namna mbali mbali. Basi ishikeni
Dini hii, kwani hii ndiyo Dini ya baba yenu Ibrahim katika misingi yake.
Na Yeye Subhanahu ndiye aliye kuiteni Waislamu, (yaani Wanyenyekevu) katika
Vitabu vya mbinguni vilivyo tangulia, na pia katika hii Qur'ani kwa ut'iifu
wenu kwa yale aliyo kutungieni sharia. Basi kueni kama alivyo kuiteni Mwenyezi
Mungu ili muwe mwisho wenu mnamshuhudia Mtume kama amekufikishieni ujumbe
nanyi mkatenda aliyo kufikishieni, mpate kufanikiwa, na muwe mashahidi
kwa kaumu zilizo tangulia kwa yaliyo kuja katika Qur'ani kwamba Mitume
wao nao walifikisha ujumbe. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu amekuchagueni
nyinyi khasa kuwa ni wat'iifu kwake, mkashika Sala kwa ukomo wa ukamilifu
wake, basi ni waajibu wenu kulipa hayo kwa kumshukuru na kumt'ii, mshike
Sala kwa utimilifu wake, na mwape Zaka wanao stahiki, na mumtegemee Mwenyezi
Mungu katika mambo yenu yote, na mchukue kwake msaada, kwani Yeye ndiye
Msaidizi wenu na ndiye wa kuwanusuru.
Yeye ndiye Mbora wa ulinzi na Mbora wa kunusuru.
Rudi kwenye Sura